Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Ziara ya Blinken Nchini China

July 04, 2023
1957

Jibu la Swali

Swali:

Mtandao wa Televisheni wa Kimataifa wa China (CGTN) ulichapisha mnamo tarehe 30/06/2023: (Wizara ya Mambo ya Nje ya China iliikosoa Marekani kwa kutoa matamshi yasiyo ya kimaslahi kuhusu uhusiano wa nchi mbili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema katika mahojiano mapema kwamba Washington itaendelea kutetea maslahi yake, na itaendelea kufanya vitendo na kutoa matamshi ambayo China haiyapendi bila kujali tofauti kati ya pande hizo mbili. Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilipinga matamshi hayo...) Ikumbukwe kuwa (Al-Arabiya) ilikuwa imechapisha wiki moja kabla ya hapo mnamo tarehe 23/06/2023: (Na moja ya matarajio ya ziara ya Blinken ni kwamba Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen atafanya ziara rasmi nchini China hivi karibuni. Waziri wa Biashara Gina Raimondo, na pia John Kerry "mjumbe wa Biden kuhusu hali ya hewa" wanaweza pia kwenda katika ziara... Inatarajiwa pia kuwa Rais Xi atatembelea "San Francisco" mwezi Novemba ujao kuhudhuria mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki, ambapo anaweza kukutana na Biden).

Hivyo, ilitegemewa kuwa uhusiano kati ya China na Marekani baada ya ziara ya Blinken nchini China mnamo tarehe 18-19 Juni 2023 ungekuwa wa kutuliza hali na siyo hali ya mvutano kurejea upya! Je, ziara ya Blinken nchini China haikuwa na tija au ilikuwa ya kishughuli tu? Naomba radhi kwa urefu wa swali.. na Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:

Kwanza: Historia ya hali ilivyo kuhusiana na ziara ya Blinken nchini China:

  1. Hali ya uhusiano kati ya Marekani na China ina mivutano kwa kiasi fulani. Hii imekuwa hivyo tangu vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, kwani serikali ya Marekani iliweka vizuizi mbalimbali kwa biashara na bidhaa za China, na kuweka ushuru mkubwa wa forodha kwa baadhi ya bidhaa za China, pamoja na kuweka vikwazo dhidi ya kampuni za China kama vile Huawei na viongozi wake. Sera hii haikufutwa na serikali ya Biden. Serikali ya China imejibu kwa sera zinazofanana na hizo. Hii pekee inatosha kuleta mvutano katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

  2. Wachina wamefanya kazi kwa muda mrefu kuwa huru katika uwanja wa teknolojia chini ya mpango wa China 2025, na jambo lililozidisha hayo ni jinsi Waamerika walivyoshughulika na kampuni ya Huawei na kampuni zingine za China jambo ambalo liliunda mvutano ulioifanya China kupanga kutengeneza chipsi zake za silikoni (silicon chips). Wachambuzi wa Marekani wanatarajia kuwa China itafikia uhuru katika tasnia ya chipsi ndani ya miaka mitano hadi saba... Na haya yote yanazalisha ushindani ulio karibu na mgongano kati ya nchi hizo mbili.

  3. Katika ngazi ya kijeshi na usalama, mnamo mwezi Februari uliopita, puto iliyodhaniwa kuwa ya ujasusi ya China iliruka katika anga ya Marekani, na ingawa China ilikanusha hilo, jambo hili lilisababisha kufutwa kwa ziara ya Blinken mjini Beijing ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi Februari ujao... Kisha kulikuwa na maneva ya meli za kivita za China katika Mlango-bahari wa Taiwan, na Marekani ikajibu kwa maneva ya manowari ya Marekani katika Mlango-bahari wa Taiwan mwezi uliopita ikizingatia Bahari ya Kusini ya China kama maji huru ya kimataifa... Katika mwezi wa mwisho, ndege ya kivita ya China ilikaribia ndege za Marekani, na hivyo hali ya anga ikawa ya wasiwasi kati ya nchi hizo mbili... Na hivyo ziara ya Blinken haikufanyika wakati huo...

  4. Marekani imeingia mikataba mbalimbali ya kijeshi na usalama ili kuibana China, na utawala wa Biden umechukua mfululizo wa sera katika mwelekeo huu, ikijumuisha mipango inayolenga kuikabili China kijeshi, hususan makubaliano ya AUKUS na Australia na Uingereza, na mazungumzo ya usalama ya pande nne "Quad" na Australia, India na Japan, pamoja na majaribio ya kupanua jukumu la NATO barani Asia. Marekani pia imeingia mkataba na Ufilipino kutumia vituo vitano vya kijeshi vya ziada ili kuwa na jumla ya vituo tisa nchini Ufilipino, na mengineyo.

Pili: Kuhusu ziara ya Blinken nchini China, haikuwa ya kishughuli tu bali ilikuwa na malengo:

  1. Jaribio la kupunguza mvutano unaotokana na mambo yaliyotajwa hapo awali, kwani taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitolewa ikieleza kuwa lengo la ziara hii ni kufungua tena njia ya mawasiliano kati ya nchi hizo mbili ili kupata maelewano kati yao, na njia ya mawasiliano kati ya wanajeshi, na kufungua nafasi ya ushirikiano zaidi na kuuimarisha kati ya nchi hizo mbili... Pia inabainika kutokana na taarifa hiyo kuwa ziara ya Blinken ilifanikisha malengo lakini haikufanikiwa kufanikisha mawasiliano kati ya wanajeshi...

  2. Gazeti la Asharq Al-Awsat lilichapisha mnamo tarehe 19 Juni 2023: (Ingawa lugha chanya ilitumiwa na kiongozi wa China, akielezea kuridhika kwake baada ya mkutano uliodumu kwa dakika 35 na Blinken, huyu wa mwisho aliweka wazi kuwa Beijing ilikataa kufungua tena njia za kijeshi na Washington, ikumbukwe kuwa suala hili ni kipaumbele kwa utawala wa Rais Joe Biden, na lilikuwa miongoni mwa malengo makuu ya ziara hii. Hata hivyo, mkutano uliofanyika katika Ukumbi Mkuu wa Watu ulikuwa ishara kwamba nchi hizo mbili hazitaki uhusiano wao ufikie uadui wa wazi, na kwamba wanatambua kuwa ushindani wao na juhudi zao za kidiplomasia zina hatari kubwa).

  3. Gazeti hilo liliongeza, (Baada ya siku mbili za mikutano na maafisa wa ngazi ya juu wa China, Blinken alisema kuwa Marekani iliweka malengo maalum ya safari hiyo na kuyafikia, akibainisha kuwa aliibua mada ya mawasiliano ya kijeshi "mara kwa mara". Aliongeza "Ni muhimu sana kuwa na aina hizi za mawasiliano (...) hili ni jambo tutaendelea kulifanyia kazi", katika juhudi zilizoanza tangu mwaka 2021 wakati China ilipokataa zaidi ya maombi kumi kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na upande wa China. Hata hivyo, Blinken alielezea majadiliano yake ya awali na maafisa wa ngazi ya juu wa China kuwa yalikuwa ya "uwazi na yenye kujenga")... Gazeti la Asharq Al-Awsat, 19/06/2023).

  4. Hivyo, moja ya masuala makuu ambayo hayakutatuliwa ilikuwa ni kurejesha mawasiliano ya kijeshi kati ya Marekani na China. Mawasiliano kati ya maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili bado yamegandishwa, na matukio mawili ya hivi karibuni yameibua hofu kuwa uhusiano huo wenye msukosuko unaweza kugeuka kuwa mzozo. Hivi karibuni China ilikataa mkutano kati ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Ulinzi wa China Li Shangfu nchini Singapore... Blinken alisema kuwa ingawa aliibua hitaji la njia hizo "mara kwa mara" katika mikutano yake, lakini "hakukuwa na maendeleo ya haraka". Aliongeza "Katika wakati huu, China haijakubali kusonga mbele na hilo. Naona hili ni tatizo ambalo lazima tuendelee kulifanyia kazi". Alisema "Ni muhimu sana kurejesha njia hizo" (CNN, 19/06/2023).

  5. Hapana shaka kuwa ziara ya Blinken ilipiga hatua kwa kiasi fulani. Lakini kama Blinken alivyosema, maendeleo hayakuwa rahisi. Blinken alisema kabla ya kuondoka China: ("Uhusiano ulikuwa katika hatua ya kutokuwa na utulivu, na pande zote mbili zilitambua hitaji la kufanya kazi ili kuuweka sawa". Aliongeza "Lakini maendeleo ni magumu. Inachukua muda. Na siyo matokeo ya ziara moja, au safari moja, au mazungumzo moja. Matumaini yangu na matarajio yangu ni: tutakuwa na mawasiliano bora, na ushiriki bora katika siku zijazo"... Aliongeza "Maafisa wa Marekani walikuwa wakipunguza umuhimu wa uwezekano wa kutokea mafanikio makubwa, lakini wanatumai kuwa ziara ya Blinken itaweka njia kwa mikutano zaidi ya nchi mbili, ikiwa ni pamoja na safari zinazowezekana za Waziri wa Fedha Janet Yellen na Waziri wa Biashara Gina Raimondo". Ilikuwa inatumainiwa kuwa hiyo itaweka njia ya kufanya mkutano wa kilele kati ya Xi Jinping na Biden baadaye mwaka huu"... Reuters, 20/06/2023).

  6. Kuhusu suala la vita vya Ukraine, Al Jazeera Net ilichapisha kuwa (Blinken alikaribisha mapendekezo ya China kwa ajili ya kuleta amani ya kudumu nchini Ukraine, na kusema kuwa China ilithibitisha kutotoa msaada wowote kwa Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine, akibainisha pamoja na hayo hofu yake "ya kuhusika kwa kampuni za China katika hilo"... Al Jazeera Net, 19/06/2023). Blinken alisema (kuwa China iliithibitishia Marekani na nchi zingine kuwa haitatoa msaada wa kijeshi hatari kwa Urusi na "hatujaona ushahidi wowote unaopingana na hilo", ingawa alibainisha kuwa uhakikisho wa China unaendana na matamshi ya mara kwa mara yaliyotolewa katika wiki za hivi karibuni... CNN, 19/06/2023).

  7. Na katika suala la Taiwan, gazeti la Asharq Al-Awsat lilichapisha kuwa Waziri wa China (alisisitiza tena msimamo wa nchi yake kuhusu faili la Taiwan, na dhidi ya kile ambacho Beijing inakiona kama ukaribu unaoendelea katika miaka ya hivi karibuni kati ya Washington na mamlaka za Taiwan zinazotokana na chama kinachounga mkono uhuru wa kisiwa hicho. Qin Gang alisema, kama wizara yake ilivyoeleza: "Suala la Taiwan liko katika kiini cha maslahi ya msingi ya China, na suala muhimu zaidi katika uhusiano wa China na Marekani na hatari kubwa zaidi". Alisisitiza kuwa "China inaihimiza Marekani kuheshimu kanuni ya China moja"; yaani kutokuwa na uhusiano rasmi na Taiwan, "na kuheshimu ahadi yake ya kutounga mkono wataka uhuru wa Taiwan". Kwa upande wake, afisa mkuu wa masuala ya nje wa China Wang Yi, alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba nchi yake haitatoa "makubaliano yoyote" kuhusu Taiwan"... Asharq Al-Awsat, 19/06/2023). Kwa upande wake, Blinken alisema (kuwa nchi yake haiungi mkono uhuru wa Taiwan, na inatarajia suluhisho la amani la suala hilo, akibainisha kuwa makubaliano yao na China "yanajengwa juu ya kufuata suluhisho la amani kuhusu tofauti zozote zinazohusiana na Taiwan, na sisi tunaiunga mkono China moja"... Al Jazeera Net, 19/06/2023). Tovuti ya BBC ilinukuu kauli ya Blinken akisema (kuwa kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu "vitendo vya uchochezi" vya China katika Mlango-bahari wa Taiwan, lakini anakariri kuwa Marekani haiungi mkono uhuru wa Taiwan. Anasema kuwa ikiwa kutakuwa na mgogoro kuhusu Taiwan, kuna uwezekano "hilo likapelekea mgogoro wa kiuchumi ambao unaweza kuathiri ulimwengu mzima". Alieleza kuwa 50% ya harakati za kontena za kibiashara hupita katika Mlango-bahari wa Taiwan kila siku, na 70% ya mauzo ya nje ya nusu-kipitishi (semiconductors) yanatengenezwa Taiwan... BBC, 19/06/2023).

Tatu: Na kutokana na hayo yote, yafuatayo yanabainika:

  1. Hakuna mabadiliko katika msimamo wa Marekani kuelekea Taiwan... Marekani haijatambua uhuru wa Taiwan (ikumbukwe kuwa kuna takriban nchi 15 zinazotambua uhuru wa Taiwan rasmi ikiwemo Vatican). Na ingawa Marekani haijaamua kutambua uhuru wa Taiwan rasmi, lakini inaitendea Taiwan kama nchi huru kwa ushahidi kwamba kuna ofisi ya Marekani mjini Taipei inayofanya kazi kama ubalozi wa Marekani, na Marekani imeingia makubaliano ya ulinzi na Taiwan na kuipatia aina za silaha za kisasa, na misaada mingineyo. Marekani inatangaza kuilinda Taiwan iwapo itatokea shambulio la kijeshi dhidi yake kutoka China, na Biden alithibitisha hilo mwezi Mei mwaka jana, ambapo Rais wa Marekani Joe Biden alionya kuwa (China inacheza na moto katika suala la Taiwan na akaahidi kuingilia kati kijeshi kulinda kisiwa hicho ikiwa kitashambuliwa... BBC 23/05/2022).

  2. Ziara hii na "matokeo yake" hayatoshi kutuliza hali kati ya nchi hizo mbili lakini inaweza kuwa mwanzo wa muda wa mlango wa kutulia hali kati yao na utangulizi wa ziara zingine... Na kama ilivyokuja katika swali kuwa moja ya matarajio ya ziara ya Blinken (ni kwamba Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen atafanya ziara rasmi nchini China hivi karibuni. Waziri wa Biashara Gina Raimondo, na pia John Kerry (mjumbe wa Biden kuhusu hali ya hewa), wanaweza kwenda katika ziara pia, kwa kuzingatia kwamba wote wawili wanawajibika kwa masuala yanayounganisha China na Marekani katika maslahi ya pamoja ya ushirikiano. Inatarajiwa pia kuwa Rais Xi atatembelea "San Francisco" mwezi Novemba ujao kuhudhuria mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki, ambapo anaweza kukutana na Biden). Lakini hiyo haimaanishi kuwa mlango wa mvutano kati ya nchi hizo mbili umefungwa na kufunguliwa mlango mpya wa utulivu wa kudumu kati ya nchi hizo mbili, kwani jambo hilo haliwezekani kwa sababu maslahi yao ni tofauti...

Washirika wa Marekani kuzunguka China kama Japan, Korea Kusini na Ufilipino kisha suala la Taiwan... haya yote yatazuia kufungwa kwa mlango wa mvutano bali utabaki (umeshindikizwa kidogo) ili ufunguke tena kulingana na maslahi ya nchi hizo mbili...

3. Lakini miongoni mwa malengo muhimu ya ziara hii ambayo hayakufikiwa ni kwamba Marekani ilitaka kufungua njia ya mawasiliano kati ya wanajeshi wa China na Waamerika, na hiyo ni kwa madhumuni yanayofanana na ujasusi! Ni kana kwamba China iling’amua hilo ikakataa njia hizi katakata na hili ndilo lililomkasirisha Blinken hata kama hakulionyesha waziwazi lakini lilikuwa likijitokeza katika maneno yake na matamshi yake kama tulivyobainisha hapo juu na narejea kuyakumbusha:

  • (Ingawa lugha chanya ilitumiwa na kiongozi wa China, akielezea kuridhika kwake baada ya mkutano uliodumu kwa dakika 35 na Blinken, huyu wa mwisho aliweka wazi kuwa Beijing ilikataa kufungua tena njia za kijeshi na Washington, ikumbukwe kuwa suala hili ni kipaumbele kwa utawala wa Rais Joe Biden, na lilikuwa miongoni mwa malengo makuu ya ziara hii).

  • (Baada ya siku mbili za mikutano na maafisa wa ngazi ya juu wa China, Blinken alisema kuwa Marekani iliweka malengo maalum ya safari hiyo na kuyafikia, akibainisha kuwa aliibua mada ya mawasiliano ya kijeshi "mara kwa mara". Aliongeza "Ni muhimu sana kuwa na aina hizi za mawasiliano (...) hili ni jambo tutaendelea kulifanyia kazi").

  • (Matukio mawili ya hivi karibuni yameibua hofu kuwa uhusiano huo wenye msukosuko unaweza kugeuka kuwa mzozo. Hivi karibuni China ilikataa mkutano kati ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Ulinzi wa China Li Shangfu nchini Singapore.. Blinken alisema kuwa ingawa aliibua hitaji la njia hizo "mara kwa mara" katika mikutano yake, lakini "hakukuwa na maendeleo ya haraka". Aliongeza "Katika wakati huu, China haijakubali kusonga mbele na hilo. Naona hili ni tatizo ambalo lazima tuendelee kulifanyia kazi". Alisema "Ni muhimu sana kurejesha njia hizo").

4. Huenda misimamo hii ya China ilibaki akilini mwa Blinken kwa sababu hakuweza kufanikisha mawasiliano ya kijeshi, ndiyo maana kukawa na matamshi yake ya hivi karibuni yaliyokuja katika swali... na pia yale yaliyonukuliwa na tovuti ya Saba mnamo tarehe 29/06/2023: (Shirika la habari la China "Xinhua" lilimnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning akijibu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akisema: "Siyo siri kwamba kuna tofauti kati ya Marekani na China".. Aliongeza: "Yale ambayo Marekani iliyasema na yale iliyoyafanya yanakiuka kanuni za msingi zinazoongoza uhusiano wa kimataifa".. akisisitiza upinzani wa nchi yake kwa jambo hili..) Na amesema kweli Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu na Mtukufu:

وَكَذَلِكَ نُوَلِّي بَعْضَ الظَّالِمِينَ بَعْضاً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

"Na namna hivi tunawajalia baadhi ya madhalimu kuwa marafiki wa baadhi yao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma." (Al-An'am: 129)

وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُون

"Na makafiri ndio madhalimu." (Al-Baqarah: 254)

15 Dhul-Hijjah 1444 Hijiria 03/07/2023 Miladi

Share Article

Share this article with your network