Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuhusu Suala la Kupro

March 20, 2012
2070

Swali:

Mnamo tarehe 3/3/2012, Waziri wa Masuala ya Umoja wa Ulaya katika serikali ya Uturuki na mpatanishi mkuu, Egemen Bağış, alimweleza mwandishi wa gazeti la "Kıbrıs" wakati wa ziara yake nchini Uingereza kukutana na maafisa wa huko kuhusu suala la Kupro akisema: "Chaguo zote zipo mezani kwa ajili ya suluhu nchini Kupro. Suluhu inaweza kuwa katika mfumo wa umoja (dola iliyoungana) kwa makubaliano kati ya viongozi wawili. Inaweza pia kuwa katika mfumo wa nchi mbili (ndani ya dola moja) kwa makubaliano yatakayofikiwa kati ya viongozi hao wawili, na inaweza kuwa kwa kuiunganisha Kupro ya Kaskazini na Uturuki. Chaguo zote zipo mezani. Lakini tunachotumaini na kilicho akilini mwetu ni kuwa na shirikisho la nchi mbili katika dola moja nchini Kupro." Lakini waziri huyo wa Uturuki hakutaja asili ya suluhu ambayo ni kuiunganisha Kupro yote na Uturuki, kwani ilikuwa sehemu yake. Je, nini ukweli wa matamshi haya? Na Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

1- Waziri huyo wa Uturuki amewasilisha miradi ya zamani ya Marekani, kwani Marekani imekuwa ikiwasilisha mipango hii tangu miaka ya sabini ya karne iliyopita; ama kuigawa kisiwa hicho katika nchi mbili tofauti, au sehemu hizo mbili ziwe kama nchi mbili ndani ya dola moja, yaani shirikisho la federation au confederation, au Kupro ya Kaskazini iunganishwe na Uturuki na ya Kusini iunganishwe na Ugiriki.

Lakini baada ya Kupro ya Kusini kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ni jambo lisilowezekana kuwa na fikra yoyote ya kuiunganisha sehemu ya kusini na Ugiriki, kwani yenyewe, kama ilivyo Ugiriki, inafurahia uanachama kamili katika Umoja huo na ina uhuru wake na inapewa umuhimu; ambapo itashikilia kiti cha urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya mnamo Julai ijayo. Hali ya Ugiriki ni mbaya, hasa kiuchumi, hivyo watu wa kusini hawapendelei kuungana nayo, ingawa wana hisia za utaifa wa Kigiriki zilizochanganyika na ushabiki wa kidini.

Kwa hivyo, tishio la Uturuki linakuja upande mmoja. Na hii ni mara ya kwanza kwa afisa wa Uturuki kutamka hili tangu kuanza kudhihirika kwa kadhia ya Kupro kiuhalisia, yaani tangu Marekani ilipoanza katika miaka ya hamsini ya karne iliyopita kufanya harakati nchini Kupro ili kuathiri ushawishi wa Uingereza huko na hatimaye kuifukuza ili kuchukua nafasi yake. Mpaka Uingereza ililazimika kutoa uhuru wa kijuujuu kwa Kupro mnamo 1960 na kumsimika kiongozi wa kidini wa Kikristo, Askofu Makarios, na kumfanya wakala wake, Rauf Denktaş, kuwa mwakilishi wa Waislamu na makamu wake. Kwa njia hiyo, kisiwa kilibaki kimeungana chini ya udhibiti wa Uingereza.

Inaonekana kuwa tishio la Uturuki limekuja baada ya kukwama kwa mazungumzo yanayohusu Kupro na Waingereza, ambapo waziri Egemen Bağış aliongeza katika matamshi yake kwa gazeti hilo mnamo 3/3/2012 alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, akisema: "Uingereza inafuatilia pande zote mbili kwa umakini, lakini siioni ikichukua hatua kwa hamu kubwa kuhusiana na kutumia ushawishi wake. Tumefanya kazi ya kuishawishi katika suala hili. Kwa kuwa Uingereza ni moja ya nchi dhamana nchini Kupro, tunaamini kuwa inapaswa kutekeleza siasa yenye ufanisi zaidi na kucheza dori ya ujenzi kwa nguvu zaidi."

2- Kutokana na hapa, inadhihirika kuwa Waingereza hawataki suluhu zinazopendekezwa na Marekani ambazo waziri wa Uturuki amezikariri, hata kama wanajifanya kuunga mkono utatuzi wa kadhia hiyo. Kwani wao, yaani Waingereza, wana vituo viwili muhimu vya kijeshi nchini Kupro vinavyohifadhi zaidi ya wanajeshi 24,000 wa Uingereza, mbali na vifaa vya kunasa mawasiliano na ujasusi kwa ajili ya kufanyia ujasusi eneo hilo na kulifuatilia. Nayo ni moja ya nchi dhamana kulingana na mkataba uliotiwa saini mnamo 1964, ambapo yenyewe, Uturuki, na Ugiriki ziwe nchi dhamana kwa hali iliyochorwa na Uingereza kisiwani humo baada ya matukio yaliyofanywa na Wagiriki wa Kupro dhidi ya Waturuki wa Kiislamu. Kwa njia hiyo, Uingereza ililinda uwepo na ushawishi wake huko kulingana na mkataba huu.

Sehemu ya kusini ya Kupro inatambulika kimataifa na kiulaya na ni sehemu ya Umoja wa Ulaya, na Uingereza ni sehemu ya Umoja wa Ulaya, hivyo uwepo wa Uingereza nchini Kupro umekuwa kama uwepo wa ndani na si wa nje, na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya hazichukizwi na uwepo huu. Bali zinaunga mkono msimamo wa Uingereza kwa siri, hata kama zilitangaza kuunga mkono mpango wa Annan; kwa sababu unahakikisha udhibiti wa Wagiriki katika utawala wa kisiwa hicho na kukomesha uwepo wa dola ya Uturuki ndani yake. Kwa sababu hiyo, Uingereza haitaacha uwepo na ushawishi wake nchini Kupro.

3- Wazungu wanatumia shinikizo dhidi ya Uturuki ili kutimiza matakwa yao chini ya jina la "Faili la Kupro", ambalo ni moja ya mafaili ambayo hayajafungwa kati yao na Uturuki, na kisha kulihitimisha. Hilo ni miongoni mwa mafaili yaliyokwama yanayozuia Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, ambapo idadi ya mafaili haya inafikia takriban 35, yakiwemo masuala ya ndani kama vile lile linaloitwa "walio wachache" (minorities) kuanzia faili la Wakurdi, faili la Waalawi, faili la Waarmenia, mpaka faili la demokrasia na haki za binadamu, faili la marekebisho ya katiba, kukubali usimamizi wa kimataifa wa uchaguzi, na yale yanayohusu kupunguza dori ya jeshi katika utawala na mafaili mengineyo.

Miongoni mwa matakwa yao kuhusiana na faili la Kupro ni kufungua bandari na viwanja vya ndege vya Uturuki kwa Wagiriki wa Kupro. Hata hivyo, Uturuki haikutekeleza makubaliano yanayohusu hilo kwa sababu Wazungu hawakutimiza ahadi yao ya kuondoa vikwazo walivyowekewa Waturuki wa Kupro kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili. Hivyo, faili la Kupro pamoja na mafaili mengine saba yamegandishwa na hayajatatuliwa. Vilevile, Uturuki inakataa kuitambua nchi ya Kupro ya Kusini inayodhibitiwa na Wagiriki mpaka kadhia hiyo itatuliwe. Uingereza, kupitia mawakala wake, ilifanya kazi ya kukwamisha mpango wa Marekani ulioitwa "Mpango wa Kofi Annan", Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, wakati walio wengi katika sehemu ya kusini ya kisiwa walipopiga kura dhidi yake mnamo 2004.

Waturuki katika sehemu ya kaskazini waliupigia kura mpango huo wakati serikali ya sehemu ya kaskazini chini ya uongozi wa Mehmet Ali Talat ilikuwa wakala wa Marekani, na serikali ya Erdogan iliunga mkono kwa nguvu na kuweka uzito wake wote kupigia kura mpango huu. Rauf Denktaş aliupinga vikali siku hiyo na kulingania kuukataliwa, bali alikuja mpaka Uturuki na kuishtaki serikali ya Erdogan kwa uongozi wa kijeshi wa Uturuki ambao ulikuwa ukiipinga serikali hiyo na wakati huo haukuwa ukiunga mkono mpango wa Annan, jambo lililodhihirisha mapambano kati ya mawakala wa Waingereza na Waamerika nchini Uturuki na Kupro ya Kaskazini. Mpango huo ulikuwa unalenga kuunganisha kisiwa kwa kuwashirikisha Waturuki katika utawala kwa viwango fulani, huku Wagiriki wa Kupro wakiwa na fungu kubwa zaidi katika utawala, na Waturuki waachie sehemu ya ardhi yao kwa Wagiriki kwa kiasi cha 7%.

4- Marekani haitaridhika na kadhia hiyo kutatuliwa kwa kuunganisha sehemu ya kaskazini ya kisiwa na Uturuki kisha sehemu ya kusini ibaki kama ilivyo na Waingereza wabaki humo kwa starehe. Kwani Waingereza ikiwa hilo litatokea na uwepo wao na ushawishi wao usiguswe, basi watastarehe na kulikubali hilo. Lakini Marekani haitaridhika na hilo mpaka iondoe ushawishi wa Waingereza na kuchukua nafasi yao na kuondoa vituo vyao na kuweka kambi zake humo; kwani kwa zaidi ya miaka hamsini imekuwa ikipambana nao huko, hivyo hairidhiki na kupanua ushawishi wake katika kaskazini ya kisiwa pekee na kuwaacha Waingereza wakistarehe katika kusini yake! Waingereza kupitia vyombo vyao vya habari walikuwa wakiipendekezea Marekani ijenge vituo vyake katika sehemu ya kaskazini ya kisiwa, lakini Waamerika hawakuchukua hatua hiyo kwa sababu kufanya hivyo ni kukiri uwepo wa Uingereza huko. Marekani iliwasilisha mpango wa Annan ili kudhibiti sehemu zote mbili itakapounda mfumo mpya wa kisiasa kisiwani humo utakaoiwezesha kudhibiti serikali na kuilazimisha kutekeleza amri zake.

5- Tamshi la waziri wa Uturuki kuhusu chaguo la kuiunganisha Kupro ya Kaskazini na Uturuki, ingawa ni moja ya miradi ya zamani ya Marekani, kwa sasa linaonekana kama tishio linalotumiwa kama karata ya shinikizo dhidi ya Waingereza, Wazungu, na Wagiriki wa Kupro; kwa sababu Waingereza wameridhika na hali yao nchini Kupro na kwa hivyo hawaonyeshi hamu ya kutatua kadhia hii, na wanakwamisha miradi ya Marekani kupitia mawakala wao kisiwani humo. Waziri wa Uturuki alitamka hayo akiwa ndani ya Uingereza, na kuelekeza lawama moja kwa moja kwa Uingereza inayokwamisha suluhu kwamba haichukui hatua kwa hamu kubwa kuhusiana na kutumia ushawishi wake na haitekelezi siasa yenye ufanisi zaidi wala kucheza dori ya ujenzi kwa nguvu zaidi. Hizi ni lugha za kidiplomasia lakini ni tuhuma za siri kwa Uingereza kwamba inakwamisha suluhu, bali haifanyi kazi kuileta suluhu.

Kuiunganisha Kupro ya Kaskazini na Uturuki kutazidisha ukwamishaji wa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya, kwani Wazungu hawaridhii hilo. Kwa hivyo, ni jambo lisilowezekana kwa Uturuki kwa wakati huu kufanya hivyo hali ya kuwa inajitahidi kuingia katika Umoja wa Ulaya na Marekani inaiunga mkono katika jitihada hizi na kupiga shinikizo kwa Wazungu ili wakubali ombi lake kwa ajili ya kutimiza malengo yake dhidi ya Umoja wa Ulaya. Wakati huo huo, hilo halitimizi kwa Marekani kile inachokilenga cha kuondoa uwepo wa Uingereza na ushawishi wake kutoka kisiwani humo, kwa sababu litabakisha hali ya Kupro ya Kusini kama ilivyo na Marekani haiwezi kupenya humo kwa mfumo huu. Kwa hivyo, maneno ya waziri wa Uturuki si zaidi ya karata ya shinikizo.

Hii ni pamoja na kufahamu kuwa kuiunganisha sehemu ya kaskazini ya kisiwa si jambo gumu kwa Uturuki kwa sababu inachukuliwa kuwa chini ya udhibiti wake ambapo kuna zaidi ya wanajeshi wake 30,000 huko, na uongozi wa sasa wa jeshi la Uturuki umekuwa ukiisaidia serikali na kusimama upande wake. Hatua hii haitakasirisha jeshi na italinda uwepo wake huko. Ulinzi wa sehemu ya kaskazini, usalama wake, na maslahi yake yote yamefungamana na Uturuki, na hakuna anayeitambua nchi ya sehemu hii na serikali yake isipokuwa yenyewe. Hivyo hatima yake iko mikononi mwa Uturuki. Kuiunganisha ni jambo rahisi sana, lakini mfumo nchini Uturuki haujitegemei na unafuata mzunguko wa Marekani, hivyo hauchukui hatua hii isipokuwa kwa amri kutoka kwake. Hivyo basi, kuashiria kuiunganisha Kupro ya Kaskazini kwayo ni kwa ajili ya kuwashinikiza Waingereza na Wagiriki nchini Kupro ili wakubali mipango ya Marekani.

6- Jambo hili litabainika zaidi baada ya mwezi Julai ujao wakati mfumo katika sehemu ya kusini ya Kupro utakaposhika urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya na kudhihirika kwa ugumu wa Uturuki kushirikiana na Umoja huu. Waziri wa Uturuki Bağış, anayehusika na mahusiano na Wazungu na mpatanishi mkuu nao, aliliambia gazeti la Kupro lililotajwa hapo awali akisema: "Hatutazungumza na mfumo wa Warumi katika kusini ya Kupro utakapochukua urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya mnamo Julai... lakini tutashirikiana na Umoja huo kana kwamba hatuoni mfumo wa Warumi kama rais wa Umoja huo... na kwamba mfumo wa Warumi katika kusini ya Kupro unafanya mambo kwa utukutu. Na kuna uwezekano kuwa hatutashiriki katika mikutano ya Brussels chini ya urais wa mfumo huu." Yaani hali hiyo itatumiwa, na hii ni fursa kwa Marekani kuleta vurugu na hofu kwa Wazungu na Wagiriki kutokana na hilo ikiwa Waingereza na mawakala wao katika sehemu ya kusini ya Kupro hawatalegeza msimamo na kukubali mpango wa Marekani uitwao mpango wa Annan. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alisisitiza hilo mwaka jana baada ya kukutana na mwenzake wa Uturuki, Davutoğlu, akisema: "Hatuaamini kwamba hali iliyopo nchini Kupro ni kwa maslahi ya yeyote. Tunataka kuona shirikisho la kanda mbili na makundi mawili (nchini Kupro) na tunataka kuliona haraka iwezekanavyo" (16/7/2011 AFP), yaani Marekani hairidhii hali iliyopo nchini Kupro na inataka kuifanya kulingana na dira yake.

7- Ama suluhu sahihi ambayo Uislamu unaamrisha kwa tatizo la Kupro ni kwamba iunganishwe yote na Uturuki, kwani Kupro ni nchi ya Kiislamu, na ni lazima iunganishwe na asili yake, Uturuki. Kisiwa cha Kupro ni kisiwa cha Kiislamu kilichofunguliwa na Waislamu wakati wa zama za bwana wetu Uthman, Khalifa Mwongofu wa tatu. Na Wapiganaji wa msalaba wa Ulaya walikivamia katika vita vyao vya kwanza vya msalaba walivyovianzisha dhidi ya nchi za Kiislamu, lakini Waislamu walikikomboa baadaye na kukirejesha katika asili yake ya nchi za Waislamu. Na kilikuwa chini ya utawala wa Dola ya Osmania (Ottoman) kama zilivyo nchi nyingine za Waislamu kwa sababu Khilafah ilihamia kwao. Waingereza walitangaza udhibiti wao juu yake katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutangaza kukiunganisha na Uingereza, na wakala wao Mustafa Kemal alikiri hilo katika Mkataba wa Lausanne. Pamoja na hayo, Waislamu nchini Uturuki wanaichukulia Kupro kama sehemu ya ardhi yao na wamefanya kazi ya kuwanusuru ndugu zao huko katika miaka ya sitini na sabini walipofanyiwa mauaji na Warumi kwa msaada wa Uingereza na Marekani kwa njia mbalimbali. Na jeshi lao bado liko huko kulinda zaidi ya Waislamu 300,000.

Pamoja na yote yaliyotajwa, mradi wa kuiunganisha sehemu ya kaskazini ya Kupro na Uturuki bila sehemu ya kusini ili kuitikia miradi ya Marekani, ingawa ni jambo lisilowezekana na Uturuki haifanyi kazi ya kulitekeleza kiuhalisia, lakini unachukuliwa kuwa ni kuachia theluthi mbili ya kisiwa kwa Warumi, yaani kwa makafiri; kwani Waturuki rasmi, kiraia, na vyombo vya habari huwaita Wagiriki nchini Kupro kwa majina haya, husema: Warumi, sehemu ya Warumi ya Kusini, na mfumo wa Warumi. Na kutosheka na theluthi moja ya kisiwa ambayo ni sehemu ya kaskazini, ni kinyume na Uislamu na dhambi yake itampata kila anayekubaliana nayo, kwa sababu asili ni kuiunganisha kisiwa chote cha Kupro na Uturuki na kukiambatanisha na asili yake.

Serikali chini ya uongozi wa Erdogan na chama chake inafanya kazi ya kuipoteza kadhia hii kabisa na kubadilisha mtazamo wa Waislamu kwayo mpaka mtazamo wao uwe si kama kisiwa chao! Shirika la habari la KUNA la Kuwait lilinukuu kutoka kwa gazeti la Uturuki la "Akşam" mnamo 9/3/2012 likimnukuu afisa mmoja katika chama tawala cha Adalet ve Kalkınma Partisi (AKP) akisema: "Serikali ya Erdogan inaamini kuwa mpango wa amani wa Annan unaweza kuunda msingi muhimu wa kufikia amani ya kudumu na ya haki nchini Kupro hasa kwa kuwa Marekani na nchi zote za Umoja wa Ulaya zinaunga mkono mpango huu." Aliongeza: "Chama cha AKP kinajitahidi kuanzisha mtazamo mpya kwa suala la Kupro na kushawishi duru nyingi nchini Uturuki kutoichukulia kadhia hii kama suala la utaifa wa Kituruki pekee, bali inapaswa kutazamwa kwa msingi wa kuwa ni suala la haki za binadamu katika daraja la kwanza, na kile kinachotuhusu katika jambo hili ni kulinda haki za Waturuki wa Kupro kupitia dhamana za kimataifa za Marekani na Ulaya."

Kuichukulia Kupro kama suala la haki za binadamu sawa na suala lolote la nje katika pembe za dunia, na si kadhia ya nchi ya Kiislamu iliyotenganishwa na asili yake, mtazamo huu kwa namna hii ni kuipoteza Kupro. Na dhambi ya upotezaji huu itampata kila aliyeshiriki ndani yake au kuridhia, mpaka Siku ya Kiyama. Waislamu hawataiacha Kupro, wala sehemu yoyote ya nchi za Waislamu iliyopotezwa na watawala madhalimu, bali watairejesha kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ikiwa si sasa hivi basi ni baadaye, na hakika kesho iko karibu kwa anayeisubiri.

Share Article

Share this article with your network