Jibu la Swali
Makubaliano ya Kiunzi nchini Sudan
Swali: Vyombo vya habari nchini Sudan mnamo tarehe 05/12/2022 vilirusha matukio ya utiaji saini wa makubaliano ya kiunzi katika Ikulu ya Rais kati ya jeshi, likiwakilishwa na kamanda wa jeshi na mwenyekiti wa Baraza la Uongozi pamoja na naibu wake, na vyama pamoja na makundi ya kisiasa 52. Makubaliano haya yanatayarisha njia ya serikali ya mpito kwa muda wa miaka miwili kuelekea uchaguzi mkuu, chini ya usimamizi wa kimataifa hasa kutoka Marekani, Uingereza, na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambaye alifanya kazi ya kuongoza makubaliano haya katika sura yaliyotiwa saini. Pamoja na hayo, kuna upinzani dhidi ya makubaliano haya na maandamano yalizuka mnamo tarehe 8 na 09/12/2022 dhidi yake. Je, makubaliano haya yanamaanisha nini? Ni nani mnufaika wake? Vipi kuhusu upinzani dhidi yake? Na je, yanatarajiwa kudumu?
Jibu: Ili kubainisha jibu la maswali haya, tunatathmini mambo yafuatayo:
Kwanza: Kutokana na maandishi ya makubaliano:
Makubaliano hayo katika sehemu yake ya kwanza yameeleza kuwa "Sudan ni nchi yenye tamaduni, makabila na dini mbalimbali," ikitambulika kuwa zaidi ya 96% ya watu wa Sudan ni Waislamu, na hivyo dini yao ni moja na utamaduni wao ni mmoja bila kujali wingi wa makabila yao. Hivyo, makubaliano haya ni hila na hadaa ya kuuondoa Uislamu katika maisha na wajibu wa kuutekeleza katika utawala, uchumi, elimu, mfumo wa kijamii, mfumo wa adhabu, siasa za ndani na nje, vita, viwanda na mambo yote ya maisha ya mtu binafsi na jamii. Kwa sababu hii, ilitajwa katika makubaliano hayo kuwa: "Sudan ni nchi ya kiraia, ya kidemokrasia, ya kifederali na ya kiparalamani, ambapo enzi (sovereignty) ni ya watu na wao ndio chanzo cha mamlaka." Haya yote yanapingana na Uislamu kwani yanaifanya Sudan kuwa nchi ya kiraia, yaani nchi ya kisekula inayotenganisha dini na maisha, na ya kidemokrasia inayowapa wanadamu haki ya kutunga sheria, na hivyo kutoifanya enzi kuwa ya Sheria (As-Siyadah lish-Shar') ambapo chanzo chake ni Qur'an na Sunnah. Pia inaifanya nchi kuwa ya kifederali, mfumo ambao unapingana na Uislamu na unaifanya nchi kuwa tayari kugawanyika na majimbo yake kuwa tayari kujitenga kama ilivyotokea Kusini mwa Sudan! Inaonekana makubaliano haya yanalenga kuondoa athari yoyote ya Uislamu nchini Sudan kwani yameeleza: "Dola haitalazimisha dini kwa mtu yeyote, na dola haitafungamana na upande wowote kuhusu masuala ya kidini, imani na dhamiri. Inahakikisha uhuru na kujitolea kwa mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, hasa mikataba ya haki za wanawake," yaani, nguvu hizi zilizounda makubaliano haya zilikusudia kuuondoa Uislamu mbali na Waislamu katika nchi hii ya Kiislamu.
Makubaliano hayo katika sehemu yake ya pili yameeleza: "Kukabidhi mamlaka ya mpito kwa mamlaka kamili ya kiraia... na nchi itakuwa na rais mwenye majukumu ya kisherehe... kisha ngazi ya utendaji inayoongozwa na Waziri Mkuu wa kiraia atakayechaguliwa na nguvu zilizotia saini makubaliano hayo, pamoja na baraza la kutunga sheria na lingine la usalama na ulinzi litakaloongozwa na Waziri Mkuu na kujumuisha viongozi wa vyombo vya usalama na harakati za mapambano ya silaha zilizotia saini amani ya Juba." Pia inaeleza kuwa: "Jeshi lijiepushe na siasa na shughuli za kiuchumi na kibiashara za uwekezaji, na kwamba vikosi vya msaada wa haraka (Rapid Support Forces) na vikosi vya harakati za silaha viunganishwe jeshini kulingana na mipango itakayokubaliwa baadaye katika tume ya uunganishaji na upunguzaji kama sehemu ya mpango wa mageuzi ya kiusalama na kijeshi unaopelekea kuwa na jeshi moja la kitaalamu na la kitaifa." Pia inaeleza juu ya: "Utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Juba... na kukamilisha amani na harakati za silaha ambazo hazikutia saini." Na inaeleza "Kuanzisha mchakato mpana wa kutengeneza katiba, chini ya usimamizi wa tume ya kutengeneza katiba kwa ajili ya mazungumzo na kukubaliana misingi na masuala ya kikatiba kwa ushiriki wa majimbo yote ya Sudan." Na inaeleza: "Kuandaa mchakato kamili wa uchaguzi mwishoni mwa kipindi cha mpito cha miezi 24 kuanzia tarehe ya kuteuliwa kwa Waziri Mkuu."
Pili: Misimamo ya ndani:
Kamanda wa jeshi na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, aliashiria hilo wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo kwa kusema: "Tumejitolea kwa taasisi ya kijeshi kujiondoa katika mchakato wa kisiasa kwa namna ya mwisho na kufanya uchaguzi mwishoni mwa kipindi cha mpito na kutekeleza masuala yaliyopendekezwa katika makubaliano ya kiunzi... Nchi inapitia mazingira ya kipekee. Tumekuwa katika hali ya kutofautiana kati ya nguvu za kisiasa na kijeshi. Na hili limeathiri nchi vibaya. Tunalenga kuligeuza jeshi kuwa taasisi ya kikatiba iliyo mbali na upendeleo wowote wa chama, kikundi au itikadi." Na naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo, alisema: "Utiaji saini wa makubaliano ya kiunzi cha kisiasa unawakilisha mwanzo wa awamu mpya na ya ajabu katika historia ya dola ya Sudan. Utiaji saini huu unatarajiwa kuhitimisha mgogoro wa sasa wa kisiasa na kujiandaa kwa awamu mpya ya mpito ambapo makosa yaliyotokea kipindi kilichopita yataepukwa. Tangu mwanzo wa kipindi cha mpito mnamo Agosti 2019, kulikuwa na tofauti kati ya washirika wa mpito na makosa ya kisiasa yaliyopelekea yaliyotokea tarehe 25 Oktoba. Pia ni kosa la kisiasa lililofungua mlango wa kurejea kwa nguvu za mapinduzi pinzani... Kwa hivyo, vipaumbele vya serikali ijayo ni lazima viwe utekelezaji wa makubaliano ya Juba, na kukamilisha amani na harakati ambazo hazikutia saini na kufanya kazi ya kuwarejesha wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao katika vijiji vyao vya asili na kushughulikia matatizo ya ardhi na masuala ya wafugaji" (Shirika la habari la serikali la Sona, 05/12/2022). Makubaliano haya yanawaokoa viongozi wa kijeshi wakiongozwa na Burhan na naibu wake na walioko pamoja nao kutokana na matatizo yao kwani watu wameanza kukataa utawala wao na hawana uungaji mkono wa ndani, na yanawahakikishia viongozi wa kijeshi kinga na ulinzi dhidi ya kufunguliwa mashtaka kwa uhalifu walioutenda na kuepuka adhabu. Wameshindwa kusimamia mambo ya nchi na kushindwa kutatua matatizo yake, na kila walichofanya ni kulinda ushawishi wa Marekani baada ya kuanguka kwa mwenzao katika utumishi kwa mkoloni, Omar al-Bashir. Ikumbukwe kuwa upande wa pili wa kile kinachoitwa Kikosi cha Uhuru na Mabadiliko (Forces for Freedom and Change) na vyama vilivyounda serikali, nao pia walishindwa kusimamia mambo ya nchi na kutatua matatizo yake na kuhakikisha mahitaji ya kimsingi ya maisha kwa watu, na kila walichofanya ni kulinda ushawishi wa Waingereza nchini humo... na kusimama dhidi ya mabadiliko ya kimsingi ya mfumo.
Kuna upinzani dhidi ya makubaliano haya, na maandamano yalizuka mnamo tarehe 8 na 09/12/2022 ku yakataa. Miongoni mwao ni nguvu ambazo si za kweli katika upinzani, kama vile ambavyo hazina ikhlasi kwa Umma na watu wa Sudan, kama vile harakati ya Haki na Usawa chini ya uongozi wa Gibril Ibrahim na harakati ya Ukombozi wa Sudan chini ya uongozi wa Minni Arko Minnawi na vyama vya kisiasa vilivyoungana na Kikosi cha Uhuru na Mabadiliko ambavyo vinafuata mkoloni Mwingereza. Uingereza imeweka nguvu hizi kama akiba na upinzani sawia, ili kama makubaliano yakifeli, nguvu hizi zionekane kama makundi ya upinzani na kuficha utumishi wao kwa mkoloni ili kuwaongoza watu ambao hawajaweza kujikwamua na utawala wa vibaraka wa Marekani au Waingereza; wakijiondoa kwa mmoja, wanaangukia katika mitego ya mwingine, na hivyo ndivyo mambo yanavyoendelea tangu nchi hiyo kupewa uhuru wa kijuujuu na kuondoka kwa mkoloni kijeshi huku akiendelea kwa sura za kisiasa, kifikra, kiuchumi na nyinginezo.
Makubaliano haya yanaonekana kwa baadhi ya watu kama suluhisho la mgogoro sugu wa utawala nchini humo, ambao ni tofauti kati ya jeshi na makundi ya kisiasa, ili kukabidhi mamlaka kwa nguvu za kisiasa na kuliweka jeshi mbali na utawala na siasa. Lakini huu si chochote isipokuwa ni mzozo kati ya vibaraka juu ya vyeo, na hautatui matatizo ya kiuchumi ya Sudan kwa daraja la kwanza ambayo inateseka kwayo na ambayo watu waliandamana kwa ajili yake. Wala hautatui tatizo la utawala kwa sababu ni mzozo kati ya vibaraka ambao ni zana kwa maslahi ya nchi kubwa zinazovutana juu ya Sudan. Haiwezekani kutatua matatizo haya na mengineyo kwa sababu yamejengwa juu ya msingi batili, ambao ni kutenganisha dini na maisha, dola na jamii, na kwa sababu ni suluhisho la muda la kuridhishana kati ya jeshi na nguvu fulani za kisiasa zisizo na ikhlasi zinazofuata nguvu za kigeni. Pia kwa sababu makubaliano ya awali yalitiwa saini kati ya pande mbili kwa ajili ya awamu ya mpito kisha yakaanguka kwa mapinduzi ya tarehe 25 Oktoba. Swala si kuunda serikali ya kiraia au kutoitengeneza, kwani hilo halileti lolote jipya... kwani hakuna dhamana ya kutimia kwake, kwa sababu kila upande unamvizia mwingine na unapewa amri na nchi kubwa zinazovutana.
Tatu: Misimamo ya kimataifa:
Marekani imeyasifia makubaliano hayo ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kupitia Twitter mnamo tarehe 06/12/2022: "Utiaji saini wa makubaliano ya kiunzi cha kisiasa nchini Sudan ni hatua muhimu kuelekea kuundwa kwa serikali ya kiraia na kuainisha mipango ya kikatiba ya kuiongoza Sudan katika kipindi cha mpito kitakachofikia kilele cha uchaguzi." Na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa taarifa katika tovuti yake mnamo tarehe 07/12/2022 ikieleza kuwa "inaunga mkono pande za kiraia za Sudan na jeshi kufanya mazungumzo jumuishi juu ya masuala yaliyosalia kabla ya kuhitimisha makubaliano ya mwisho na kuhamisha madaraka kwa serikali ya mpito inayoongozwa na raia," na ilionya juu ya kuweka vikwazo kwa mtu yeyote atakayedhoofisha makubaliano hayo ikisema: "Wizara imeamua leo kupanua sera ya kuzuia utoaji wa viza dhidi ya maafisa wa sasa au wa zamani wa Sudan au watu wengine ambao wanaaminika kuhusika au kushirikiana katika kudhoofisha mabadiliko ya kidemokrasia nchini Sudan kupitia ukandamizaji wa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi." Hivyo, makubaliano haya ni hatua muhimu kwa Marekani ili kuhifadhi ushawishi wake nchini Sudan kwa kuzuia kuanguka kwa mamlaka ya kijeshi inayoiunga mkono chini ya uongozi wa vibaraka wake Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake Mohamed Dagalo na mfano wao. Hasa ikizingatiwa kuwa walifanya mapinduzi dhidi ya serikali ya kiraia mwaka mmoja na nusu uliopita mnamo tarehe 25/10/2021 na kusitisha mwendo wa awamu ya mpito iliyotiwa saini kati ya pande mbili katika makubaliano ya tarehe 21/08/2019, ambayo yalieleza wanajeshi kuongoza Baraza la Uongozi kwa miezi 21 na kisha raia kuongoza kwa miezi 18, na iliongezwa hadi kuwa miezi 53 baada ya makubaliano ya Juba mnamo tarehe 03/10/2020. Hivyo mapinduzi ya tarehe 25 Oktoba 2021 yalikuja ili kuwapokonya fursa vibaraka wa Waingereza na kuwazuia wasiongoze Baraza la Uongozi... Hivyo makubaliano haya ya mwisho yanawaokoa vibaraka wa Marekani dhidi ya kuanguka na kufunguliwa mashtaka na hivyo kuhifadhi ushawishi wa Marekani nchini Sudan, na kuzuia kutawaliwa kwa kila kitu na vibaraka wa Waingereza ambapo wanadhibiti mazingira ya kisiasa.
Uingereza ilitangaza kupitia kwa Waziri wake wa masuala ya Afrika na Maendeleo ya Kimataifa, Andrew Mitchell, kukaribisha makubaliano hayo ikisema: "Kundi la nchi nne (Quad) na nchi za Troika zinakaribisha hatua hii muhimu kuelekea makubaliano yanayoongozwa na raia nchini Sudan. Uingereza inatarajia kufanya kazi kwa karibu na serikali kama hiyo pindi itakapoundwa. Tunahimiza watendaji wote kuungana haraka ili kufikia makubaliano ya mwisho" (Sudan Today 06/12/2022). Na Balozi wa Uingereza katika Baraza la Usalama, James Kariuki, alionya juu ya "matokeo mabaya ya kuchelewa kufikia makubaliano ya mwisho nchini Sudan" na alielezea "uungaji mkono wa Uingereza kwa serikali ijayo ya kiraia inayoongozwa na raia kupitia uratibu na washirika wa kimataifa" na akaashiria "hali tete katika maeneo kadhaa ya Sudan, hasa jimbo la Blue Nile na jimbo la West Kordofan" (Sudan News 06/12/2022). Hivyo Uingereza inaingilia kati kama Marekani nchini Sudan kwa njia ya moja kwa moja, na inatangaza uungaji mkono wake kwa makubaliano hayo kwani ilikuwa miongoni mwa wasimamizi wa uandishi na utoaji wake pamoja na Marekani kupitia mjumbe wa Umoja wa Mataifa, na inatangaza uungaji mkono wake kwa serikali ya kiraia ijayo ambayo inatarajiwa kuundwa na wengi wa vibaraka wake, na itakuwa imehifadhi ushawishi wake katika mazingira ya kisiasa kama maandalizi ya kushika madaraka na kujaribu kuyumbisha ushawishi wa jeshi katika utawala na siasa.
Nne: Hitimisho
Kwa kuzingatia matukio haya yanayoendelea nchini Sudan, inabainika kuwa mzozo wa kimataifa humo haujabadilika, bali ni mzozo ambao hauko kwa siri bali ni wa wazi kati ya Marekani inayomdhibiti Burhan, naibu wake na kundi lake upande mmoja, na Kikosi cha Uhuru na Mabadiliko na vyama vilivyoungana navyo miongoni mwa vibaraka wa Uingereza na wafuasi wake upande mwingine. Na kwa sababu hakuna upande wowote, Marekani au Uingereza, ulioweza kufikia sasa kueneza ushawishi wake katika jeshi na upande wa kiraia kwa pamoja, ndiyo maana Marekani na Uingereza zimeamua kufikia makubaliano kama ilivyotokea tangu mwanzo wa mabadiliko ya Bashir hadi hitilafu zao zilipopamba moto tarehe 25 Oktoba na kisha kurejea katika maridhiano sasa! Ni maridhiano ya muda hadi upande mmoja utakapoweza kuhodhi ushawishi kamili wa kijeshi na kiraia... Na tayari tushawahi kuashiria hilo tangu kuanza kwa utawala wa Burhan na hadi kutokea kwa (mapinduzi) ambapo tushawahi kuonya juu ya hilo katika matoleo mawili:
- Tulisema katika jibu la swali lililotangulia lililotolewa mnamo tarehe 23/09/2019, yaani tangu mwanzo wa ushirikiano wa pande mbili katika utawala, ambapo ilikuja ndani yake kuhusu makubaliano ya jeshi na upande wa kiraia kugawana mamlaka yafuatayo: (Ama kinachotarajiwa ni kwamba Marekani na Uingereza hazitaishi pamoja kwa utulivu, kwani maslahi yao ni tofauti na zana zao za ndani zinawafuata wao, na kwa hivyo kila mmoja wa pande mbili atafanya kazi ya kuhujumu harakati za mwingine! Na kutokana na kufuatilia matukio yanayoendelea na kutafakari mambo yanayohusiana nayo na kuchunguza matamshi ya nje na ndani, hasa ya maafisa wa Marekani na Ulaya... basi inawezekana kuainisha mbinu zitakazotumiwa na kila upande mmoja kumuudhi adui yake na kumdhibiti kisha kumuondoa madarakani...) Na tulizitaja huko. Na hivi ndivyo ilivyotokea kweli...
Kisha tulisema katika jibu la swali la baadaye mnamo tarehe 25/10/2021: (... Na kutokana na yale yaliyofikia hali nchini Sudan na njia chafu zilizochochewa na vibaraka wa Marekani na njia nyingine chafu ambazo vibaraka wa Waingereza na Wazungu walijaribu kuzifuata, na zote zina umwagaji wa damu, dhuluma, njaa na migogoro, basi watu nchini Sudan ni lazima wabainishe mambo yao na wawape migongo watawala hawa wote waliofeli, vibaraka wa Marekani, Waingereza na Wazungu ambao wanaweka damu ya watu wa Sudan na maliasili zao katika kutumikia nchi hizi kafiri, basi wahitimishe jambo lao na waunganishe safu zao dhidi ya vibaraka hawa wote...)
Kuhusu maswali je, makubaliano haya yatadumu na kutekelezwa? Hili ni jambo lenye mashaka. Na je, yataokoa nchi? Hilo ni jambo lisilowezekana, kwa sababu yamejengwa juu ya batili, na kwa sababu yametolewa na nguvu za kikoloni zinazovutana ambazo zimeafikiana kwa muda, na kwa sababu yametiwa saini kati ya pande vibaraka ambazo hazijali chochote isipokuwa vyeo na kuhifadhi mapato yao ya kifedha na kupata pesa zaidi. Hazijali mambo ya nchi na raia wala mwamko wake na ukombozi wake kutoka katika nira ya ukoloni na mikono ya wakoloni, wala hazijui kabisa njia ya mwamko, na kwa sababu zinafanya kazi kwa ajili ya madola ya kikoloni yanayofanya kazi ya kuimarisha ushawishi wao nchini humo kifikra na kisiasa, na kwa sababu madola haya ya kikoloni hasa Marekani na Uingereza yanavutana katika kueneza ushawishi nchini Sudan. Hivyo uingiliaji kati wa kigeni uko wazi kwa kila mtu kwani wageni walikuwepo wakati wa utiaji saini katika Ikulu ya Rais, bali aliyetunga makubaliano hayo ni mgeni, naye ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Marekani na Waingereza ambao ni pande za mzozo wa kimataifa nchini Sudan kwa jina la Quad na kwa jina la Troika. Quad ni Marekani ikiwa na kibaraka wake Saudi Arabia, na Uingereza ikiwa na kibaraka wake Imarati, kwani Marekani inamtumia kibaraka wake Saudi Arabia kuathiri pande za ndani na kutoa rushwa, na vivyo hivyo Uingereza inaitumia Imarati kwa mfano wa hayo kwa maslahi yake. Na Troika ni Marekani na Uingereza na pamoja nazo Norway kama upande wa Ulaya ambao hauna athari isipokuwa inapohitajika na kufanya mazungumzo ya siri ambayo mara nyingi hufanyika huko katika mji wake mkuu Oslo, maarufu kwa kuandaa makubaliano ya siri kabla ya kutolewa. Marekani inatishia yeyote atakayefelisha makubaliano kwa vikwazo, na Uingereza inaonya juu ya matokeo mabaya ikiwa makubaliano yakifeli...
Ama mjumbe wa Umoja wa Mataifa Mjerumani Volker Perthes ambaye anaziridhisha pande mbili zinazovutana, Marekani na Uingereza, yeye anaonya dhidi ya kufeli kwa makubaliano hayo, akisema katika maelezo yake mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa: "Wakati Sudan ikikaribia kufikia makubaliano ya mwisho ya kisiasa, wale ambao hawaoni uungaji mkono wa maslahi yao kupitia suluhu ya kisiasa wanaweza kuongeza majaribio ya kudhoofisha mchakato wa kisiasa unaoendelea" (Al-Rakoba ya Sudan 08/12/2022). Hivyo ni makubaliano ya muda kati ya pande mbili, labda yatakuwa kama mapumziko ya mpiganaji, na kisha mzozo utaanza tena hadi upande mmoja utakapoweza kumshinda mwingine. Na ikiwa upande mmoja utamshinda mwingine, upande huo hautakata tamaa bali utatengeneza matatizo nchini humo mashariki yake, magharibi yake, kaskazini yake, kusini yake na katikati yake katika mji mkuu, kwa sababu una vibaraka wake. Ikiwa nchi haitasafishwa kutokana nao, basi hali hazitatulia na watu hawaataona mwanga wa matumaini wala hawaataonja maisha yenye heshima na mazuri, na watapoteza furaha ya dunia na akhera. Bali ni wajibu kwa kila mkweli mwenye ikhlasi kufanya juhudi kubwa pamoja na wafanyakazi wa kusimamisha Khilafah ya Rashidah kwa njia ya Utume ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliibashiri:
ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ "Kisha kutakuwako Khilafah kwa njia ya Utume." (Imepokelewa na Ahmad na at-Tayalisi).
وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ "Na siku hiyo waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu. Yeye humnusuru amtakaye, Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS. Ar-Rum [30]: 4-5)
17 Jumada al-Ula 1444H 11/12/2022M