Jibu la Swali
Dola ya Ndani (Deep State)
Swali:
Matumizi ya neno "Dola ya Ndani" yameenea miongoni mwa wanasiasa na katika vyombo vya habari, lakini kwa kufuatilia kauli hizo, inabainika kuwa zina maana tofauti. Je, inawezekana kufafanua maana yenye nguvu zaidi (rajih) ya suala hili ili tuweze kuelewa matukio ya kisiasa yanayohusiana na neno hili, pamoja na kutoa mifano kadhaa kwa ajili ya ufafanuzi zaidi... Na radhi kwenu ikiwa ombi langu la mifano hii litawashughulisha na kazi zenu muhimu zaidi, na shukrani ni kwenu.
Jibu:
Naam, kuna tofauti katika kile kinachochapishwa kuhusu neno Dola ya Ndani (Deep State). Wapo wanaoifanya imaanishe matabaka yenye ushawishi ambayo hayapo madarakani, yanayofanya kazi kwa siri dhidi ya mfumo uliopo, kama ilivyokuwa ikitokea Uturuki. Wengine wanaifanya kuwa ndiyo nguvu inayodhibiti mfumo, inayoiongoza nchi inapotaka, na likitokea tatizo ambalo inataka kulibebesha wengine, huachia madaraka na kuleta upande mwingine wa kubeba lawama za tatizo hilo, kisha hurejea tena madarakani, kama inavyotokea Uingereza. Wapo pia wanaoifanya kuwa ni mapambano kati ya vyama vyenye ushawishi kama inavyotokea sasa katika zama za Trump nchini Marekani. Wengine huifanya kama kisingizio cha kutundika mapungufu ya utawala wao na kufeli kwao, hivyo huambatanisha hili na kile wanachokiita Dola ya Ndani. Wapo wanaochezea neno hili kila wanapotaka kuwashughulisha watu na jambo fulani, wakilitaja kwa neno hilo au maneno mengine. Na wapo wanaoona kuwa nchi za kikoloni ndizo Dola ya Ndani katika makoloni yao. Ili kubainisha maana yenye nguvu zaidi katika suala hili, tunapitia mambo yafuatayo:
Jambo la Kwanza: Baadhi ya tafsiri zilizotolewa kuhusu Dola ya Ndani:
Kamusi ya Webster, moja ya kamusi kongwe zaidi duniani, inaifafanua Dola ya Ndani kama: (Mtandao wa siri unaodaiwa wa maafisa wa serikali ambao hawajachaguliwa, na wakati mwingine taasisi binafsi zinazofanya kazi nje ya sheria ili kuathiri sera ya serikali na utekelezaji wake. Hii inamaanisha kuwa chini ya mifumo na katiba, kuna nguvu ya ndani zaidi inayodhibiti taifa. Nguvu hii ina ajenda yake na inaweza kudhoofisha maamuzi ya serikali iliyochaguliwa).
Imekuja katika Wikipedia: (Dola ya Ndani nchini Uturuki inajulikana kwa Kituruki kama "derin devlet" ikiwa ni kundi la miungano yenye ushawishi inayopinga demokrasia ndani ya muundo wa kisiasa wa Uturuki. Inajumuisha maafisa wa ngazi za juu ndani ya vyombo vya usalama vya ndani na nje, jeshi la Uturuki, idara za usalama, mahakama, na Mafia... Kihistoria, vurugu na njia nyingine za shinikizo zilitumika kwa siri kubwa kudhibiti wasomi wa kisiasa na kiuchumi na kuhakikisha maslahi fulani yanafikiwa ndani ya mfumo wa "kidemokrasia wa dhahiri" wa mazingira ya kisiasa).
Kwa kuchunguza kile wanachokusudia watu hawa kwa neno Dola ya Ndani, tunapata maana ya kuwepo kwa nguvu ya siri ndani ya chombo cha dola au nje yake inayodhibiti mfumo wa kisiasa. Yaani, inalazimisha sera zake, maoni yake, na mwelekeo wake kwa wanasiasa waliochaguliwa kisheria. Nguvu hii ya siri ni mtandao uliopangwa wa watu wanaopenya katika vituo nyeti kama vile nguvu za kijeshi, usalama, na kisiasa, na hufanya kazi kwa kujitegemea kutoka kwa serikali iliyochaguliwa. Wakati mwingine maneno tofauti hutumiwa kurejelea mtandao huu, kama vile "Deep State", au "Dola Sambamba", au "Dola Kivuli", au "Dola ndani ya Dola"...
Kuna tafsiri nyingine tofauti inayotolewa na mwanasiasa aliyeshindwa katika utawala au uchaguzi, akiitumia kama kisingizio cha kutundika kufeli kwake. Kwa maneno mengine, ni dhana ya kupotosha, inayotumiwa kuwaondolea hatia watawala katika hali ya kuenea kwa ufisadi na dhuluma nchini au kufanya usaliti. Ni hila ya mtawala ambapo anatupa lawama kwa watu waliojificha anaowaita Dola ya Ndani, na hivyo kuwapotosha watu wasijue kuwa yeye ndiye anayewajibika na anapaswa kubadilishwa.
Kuna kauli inayosema kuwa nchi za kikoloni ndizo Dola ya Ndani katika makoloni yao; kwani zinadhibiti mifumo ya makoloni yao, zikimwacha mtawala huyu na kumwondoa yule.
Jambo la Pili: Tafsiri yenye Nguvu (Ar-Rajih)
Kwa kuchunguza tafsiri hizi na kutafakari yaliyomo, tafsiri yenye nguvu zaidi ni kwamba Dola ya Ndani katika nchi fulani inamaanisha kuwa kuna nguvu yenye ushawishi, iwe ni nguvu za kisiasa, kiuchumi, au familia za kiaristokrasia zenye ushawishi kutoka kwa watu wa nchi hiyo ndani au nje. Rasmi hawamo katika vyombo vya utawala, bali huathiri dola kwa siri. Wanakuwa na shinikizo lenye ufanisi na lenye nguvu juu ya vyombo rasmi vya utawala ili kutekeleza wanachotaka, au kuvibadilisha.
Ama kuwapotosha watu kunakofanywa na mtawala ili kuepuka tuhuma za ufisadi na kuzinasibisha na upande mwingine anaouita Dola ya Ndani, yaani kisingizio cha kutundika matendo yake mabaya na ufisadi wake, basi kuita upotoshaji huu kuwa ni Dola ya Ndani si sahihi. Hii ni kwa sababu ni hila iliyotengenezwa na mtawala na si kutoka kwa pande nyingine dhidi yake.
Ama kuichukulia nchi ya kikoloni kuwa ndiyo Dola ya Ndani, hilo pia liko mbali na ukweli. Kwani nchi za kikoloni ndizo zinazodhibiti makoloni yao na ni wageni kwake, si nguvu nyingine ya watu wa nchi hiyo inayofanya kazi kwa siri iliyofichika mbali na nguvu zilizochaguliwa zinazotawala ambazo pia ni za watu wa nchi hiyo.
Jambo la Tatu: Mifano ya kuelezea Dola ya Ndani katika baadhi ya nchi kwa ufafanuzi zaidi:
1- Uturuki
a- Asili ya neno Dola ya Ndani ilitokea Uturuki. Mwishoni mwa Dola ya Ottoman, maofisa wa kijeshi wa kundi la Ittihad ve Terakki (Umoja na Maendeleo) walioathiriwa na fikra za Magharibi walifanya mapinduzi mwaka 1909 na kumwondoa Khalifa Abdul Hamid II, kisha wakamteua kaka yake Muhammad Rashad kama Khalifa mwenye mamlaka yaliyo chini ya mamlaka yao.
- Huu ulikuwa mwanzo wa kutokea kwa tabaka lenye nguvu kuliko Khalifa na lenye kuathiri kubaki kwake au kuanguka kwake kwa njia ya wazi na si ya siri. Lakini hawakuangusha Khilafah na utawala wa Kiislamu. Kwa hakika, wao hawakuwa dola ndani ya dola kwa maana ya dola ya ndani ya siri, walikuwa wazi ndani ya dola, lakini walikuwa ni wenye mabavu juu ya utawala.
b- Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Mustafa Kemal, aliyekuwa mtiifu kwa Waingereza, aliweza kudhibiti utawala na kisha akaweza kuibomoa Khilafah, kuondoa Sharia na kufanya kazi na sheria za kutungwa na wanadamu. Alitangaza Jamhuri na kuijenga juu ya misingi ya kisekula, akifanya mapinduzi yake dhidi ya utawala wa Kiislamu, na hata dhidi ya alama za Kiislamu kama vile mapinduzi ya "Herufi" (kubadilisha herufi za lugha ya Kituruki kutoka Kiarabu kwenda Kilatini), au mapinduzi ya "Mavazi" ya kisheria ili nafasi yake ichukuliwe na mavazi ya Magharibi na mengineyo. Hivyo, alianzisha jeshi na vyombo vya usalama kwa vigezo maalum vya kulinda Jamhuri na usekula, na kuzuia kurejea kwa Uislamu katika utawala na kusimamisha Khilafah upya. Jeshi likawa nguvu yenye mabavu juu ya utawala likiingilia kati kila linapoona kuna mkengeuko kutoka kwenye mfumo wa Kemal, huku likilinda utiifu kwa Uingereza. Ubeberu wa utawala wa Kemal na uungaji mkono wa Uingereza vilikuwa vizuizi vya kutojitokeza kwa dola ya ndani dhidi ya utawala huu.
c- Wakati Erdogan alipokuja kutawala Uturuki kwa nguvu ya matokeo ya masanduku ya kura, na kwa uungaji mkono wa kisiasa, kifedha, na kiuchumi wa Marekani, alikuwa akitambua nguvu ya majenerali wa jeshi walinzi wa usekula wafuasi wa Waingereza na kwamba wao wanawakilisha uti wa mgongo wa dola na wanaweza wakitaka kufanya mapinduzi dhidi yake. Kwa hiyo, alikuwa akitukuza thamani za demokrasia na uhuru na kuwazingira kwa nguvu ya uhalali wa umma ili kuwazuia wasimpindue. Marekani ilikuwa ikiwahamasisha Waturuki kupitia mifereji yake ya kifedha na kiuchumi. Erdogan alikuwa akiwaogopa wanajeshi hao na hakuwa na uwezo wa kuwafuta kazi kwa sababu ya wingi wao na udhibiti wao wa jeshi kwa miaka mingi. Lakini punde si punde alitengeneza hali mpya katika maisha ya Uturuki yenye anuani ya "Demokrasia" na mafanikio ya kiuchumi, jambo lililokuwa kizuizi cha mapinduzi.
- Katika kipindi hiki, sifa ya kuwepo kwa "Dola ya Ndani" nchini Uturuki ikifanya kazi kwa siri ndani ya vyombo vya dola na hasa jeshi, ikipinga na kujaribu kufelisha mwelekeo wa Waziri Mkuu aliyechaguliwa Erdogan, ilikuwa ni sifa sahihi. Watu hawa walikuwa kama mtandao ambao haukuonekana kwa wale wenye mtazamo wa juu juu tu ambao walidhani mambo yanakwenda kwa njia kamilifu na kwamba kila mtu amejitolea kwa katiba na sheria. Mtandao huu wa Uturuki, mbali na kujikita ndani ya vyombo vya jeshi, mahakama na wizara, ulikuwa umeunganishwa na vyama vya kisekula vilivyokuwa nje ya dola na vikiwakilisha upinzani, na ulikuwa umeunganishwa na kituo kikuu huko London. Watu wake walikuwa wakikutana kwa siri, wakishauriana na kujadili masuala ya mfumo wa utawala wa Erdogan hadi walipoamua kufanya mapinduzi mwaka 2016, lakini hayakufanikiwa. Kisha Erdogan akachukua hilo kama kisingizio na kuwang'oa jeshini, pamoja na wafuasi wao katika mahakama na wizara hadi zoezi la kusafisha liliwafikia maprofesa wa vyuo vikuu. Kwa hilo, Erdogan alifanikiwa kuing'oa Dola ya Ndani ya Waingereza ndani ya jeshi la Uturuki na akakaribia kumaliza kuwepo kwake, lakini walibakiwa na wafuasi, ingawa ni dhaifu kuliko awali, wakijaribu kurejesha sifa ya "Dola ya Ndani" dhidi ya mfumo.
2- Marekani
a- Utawala nchini Marekani umegawanyika katika ngazi mbili halisi. Ngazi ya kwanza inaonekana ikiwakilisha uhalali wa umma, ikifanya kazi kufikia matakwa ya watu waliomchagua rais huyu na wabunge hawa, hivyo muonekano wa dola unakuwa wa "kidemokrasia". Lakini ngazi hii ya kisheria haiwezi kuongoza sera za nchi isipokuwa kulingana na kile ambacho ngazi ya pili inataka. Nayo ni ngazi ya ndani isiyoonekana na isiyochaguliwa, yaani isiyo halali kwa mujibu wa mfumo wa "kidemokrasia", na ndiyo wanayoiita "Dola ya Ndani". Wanachama wa ngazi hii, yaani wawakilishi wa Dola ya Ndani, ni watu wanaoshikilia nafasi nyeti katika vyombo vya dola. Vyombo wanavyovidhibiti haviwezi kwenda kulingana na mwelekeo wa ngazi ya kwanza isipokuwa kupitia kwao, kwa sababu nafasi zao ni nyeti. Watu hawa nchini Marekani ni aidha mabeberu wakubwa au wawakilishi wao; kwani mabeberu wakubwa nchini Marekani wanahakikisha kuwa watumishi waandamizi katika vyombo vya dola wanalinda maslahi yao, na wanabaki katika mawasiliano ya mara kwa mara na watumishi hao ili kuendesha maslahi yao. Kwa mfano, makampuni ya fedha yanahakikisha kuwa yana wafuasi miongoni mwa watumishi wa idara za kodi, huku makampuni ya silaha yakihakikisha yana wafuasi katika Pentagon na idara za mikataba ya kijeshi katika wizara ya mambo ya nje. Makampuni ya dawa yanahakikisha kuwa yana wafuasi katika idara za wizara ya afya na idara za bima ya serikali, na kadhalika. Kwa kupita kwa muda mrefu, makampuni makubwa yamefanikiwa kudhibiti dola nchini Marekani kupitia watumishi hawa katika vituo nyeti na kupitia makundi ya shinikizo (lobbies).
b- Huku ndiko ukweli wa mfumo wa kisiasa nchini Marekani. Kwa hiyo, mabeberu wakubwa na makampuni makubwa ndiyo chimbuko la Dola ya Ndani nchini Marekani na mzizi wake hai. Nayo ndiyo nguvu iliyofichika inayosimama nyuma ya mwelekeo wa kisiasa wa dola, na ndiyo inayowashughulisha watumishi katika nafasi nyeti kupinga mwelekeo wa dola ikiwa unapingana na maslahi ya makampuni hayo. Kwa sifa hii, iko nje ya chombo cha dola na ndani yake, na inafanya kazi katika sekta ya fedha, biashara na viwanda, lakini harakati zake zinaonekana ndani ya vyombo vya dola nchini Marekani.
c- Donald Trump alipokuja mwaka 2016 kama rais, alikuta mbele yake manung'uniko kutoka kwa watumishi waandamizi wa dola na mashirika mbalimbali, hasa mashirika ya usalama. Alihisi upinzani wao kwa sera zake, kisha ukaendelea na kuwa upinzani mkali kutoka ndani ya dola nchini Marekani mfano wa uasi. Yakazidi matukio ya kuvujisha habari zenye kumdhalilisha kutoka vyombo vya usalama na ujasusi... Kisha yakafunguliwa dhidi yake kesi nyingi, maarufu zaidi ikiwa ni uungaji mkono wa Urusi kwake katika uchaguzi, na kukawa na uchunguzi na majaribio ya kumwondoa madarakani katika Congress hadi Wizara ya Sheria ya Marekani ikawa miongoni mwa maadui zake wakubwa kwa njia ya wazi. Mashambulizi dhidi yake hayakuwa kutoka ndani ya dola pekee, makampuni ya dawa yaliyofanikiwa kugundua chanjo ya Corona yalijizuia kutangaza uvumbuzi huo hadi baada ya kutangazwa kwa ushindi wa Biden katika uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2020. Yaani, kuzuia Trump asifaidike na uvumbuzi huo katika uchaguzi. Kisha rais, kutokana na kutaabika kwake na nguvu hii ya siri iliyopangwa inayofanya kazi dhidi yake, alitilia shaka matokeo ya uchaguzi na hakuyatambua, na kuyaona kuwa yamechakachuliwa na kwamba ushindi umeibiwa kutoka kwake, na akaiongeza kamati ya uchaguzi ya serikali kwenye orodha ya maadui zake. Trump alisema baada ya kuondoka madarakani mbele ya umati wa wafuasi wake huko Texas mwaka 2023: "Aidha Dola ya Ndani iiharibu Marekani au sisi tuiharibu Dola ya Ndani". Kwa kuchunguza hali hii ya Marekani wakati wa utawala wa kwanza wa Trump na sifa hiyo ya kuwepo kwa nguvu ya siri nchini Marekani inayomzuia rais aliyechaguliwa kufanya mabadiliko, tunakuta sifa hii ni sifa ya hali halisi katika mfumo wa utawala nchini Marekani.
d- Mnamo Machi 21, 2023, Trump alitangaza katika kipande cha video mpango wa vipengele 10 na akasema katika video hiyo: ("Kwa njia hii nitahujumu Dola ya Ndani na kuirejesha serikali kuwa chini ya udhibiti wa watu na kwa ajili ya watu"... Daily Mail ya Uingereza, 21/3/2023).
Huku ndiko ukweli wa mfumo wa kisiasa nchini Marekani. Kwa hiyo, mabeberu wakubwa na makampuni makubwa ndiyo chimbuko la Dola ya Ndani nchini Marekani na mzizi wake hai. Nayo ndiyo nguvu iliyofichika inayosimama nyuma ya mwelekeo wa kisiasa wa dola, na ndiyo inayowashughulisha watumishi katika nafasi nyeti kupinga mwelekeo wa dola ikiwa unapingana na maslahi ya makampuni hayo. Kwa sifa hii, iko nje ya chombo cha dola na ndani yake, na inafanya kazi katika sekta ya fedha, biashara na viwanda, lakini harakati zake zinaonekana ndani ya vyombo vya dola nchini Marekani.
3- Uingereza
Ama Uingereza, ndani yake kuna Dola ya Ndani. Hiyo ni kwa sababu mfumo wa utawala ndani yake unawakilishwa na Wahafidhina (Conservatives), ambao ni familia za kiaristokrasia za Uingereza na matajiri wake wakubwa, na hao ndio watawala halisi wa Uingereza. Lakini mwelekeo wao uliotangazwa wakati mwingine unaifikisha dola kwenye migogoro, yaani wakati mwingine unadhuru maslahi ya dola, kwa hiyo chama cha Wahafidhina hupumzika na nchi kutawaliwa na chama cha Wafanyakazi (Labour Party). Kazi ya chama cha Wafanyakazi inakuwa ni kutatua migogoro na kusitisha udhuruji wa maslahi ya dola, kisha huondoka. Na tulichokiona hivi karibuni cha kushindwa vibaya kwa chama cha Wahafidhina na ushindi mkubwa wa chama cha Wafanyakazi si chochote bali ni matokeo ya kazi ya Wahafidhina. Uingereza baada ya "Brexit" inapitia mgogoro mkubwa wa kiuchumi; bali hata kujiondoa kwake katika Umoja wa Ulaya kulikuwa ni matokeo ya mahesabu yake mabaya katika kura ya maoni ya Uingereza kuhusu Ulaya. Kwa kuwa Wahafidhina ndio waliohusika na mgogoro huo na kuusababisha, basi chama cha Wafanyakazi leo kinatakiwa kuutatua.
Dola ya Ndani nchini Uingereza ni familia kongwe na matajiri, na hao ndio watawala wa Uingereza siku zote. Ikiwa watajitenga pembeni na kukileta chama cha Wafanyakazi, ni kwa ajili ya kutatua mgogoro uliosababishwa na Wahafidhina. "Dola ya Ndani" nchini Uingereza inadhibiti utawala kwa urahisi na wepesi. Hii ina maana kwamba familia kongwe za Uingereza na matajiri wake ndio chimbuko la utawala na walinzi wake, iwe wanautumia wao wenyewe au "wamewakodisha" chama kingine kuutumia. Ili kuendeleza udhibiti huo kwa urahisi na wepesi huo, "chimbuko la utawala amilifu" nchini Uingereza na "mzizi wake hai" hueneza thamani zinazokataa mabadiliko, hivyo kutukuza ukongwe na fahari ya mambo ya kale... Na hili ndilo linaloonekana nchini Uingereza kutokana na umuhimu mkubwa wa umma kwa familia ya kifalme na habari zake, hadithi zake, siku za kuzaliwa za wakuu wake, na mfumo wao wa maisha...!
Muhtasari:
Dola ya Ndani ni nguvu yenye ushawishi katika utawala uliopo na kwamba ni mtandao wa watu wa nchi husika ndani au nje, unaofanya kazi kwa siri au kifichoni dhidi ya tabaka linalotawala katika nchi hiyo ili kulibadilisha au kulidhoofisha.
Ama ikiwa mtandao huu si wa watu wa nchi hiyo bali ni nguvu ya kigeni, kwa mfano dola ya kikoloni inayofanya kazi dhidi yake, au dola adui dhidi yake, basi nguvu hizi hazichukuliwi kama Dola ya Ndani, bali utafiti wake unaingia katika mlango wa ukoloni au vita na uchokozi.
Vile vile ikiwa mtandao huu umeandaliwa na tabaka linalotawala kwa kunasibishiwa kazi dhidi ya dola na mipango yake ili kuondoa tuhuma kwa mtawala na kuzihamishia kwenye mtandao wa kufikirika alioutengeneza kama hila kwa watu dhidi ya ufisadi wa mtawala na kushindwa kwake, basi hili pia halichukuliwi kama Dola ya Ndani.
Muhtasari wa muhtasari ni kwamba ni mtandao wa watu wa nchi hiyo ndani au nje unaofanya kazi dhidi ya mfumo uliopo katika nchi hiyo ili kuubadilisha au kuudhoofisha. Kwa maana hii, haitokei isipokuwa katika nchi zinazofuata sheria za kutungwa na wanadamu, ambapo inawezekana kukawa na mitandao ndani au nje inayotofautiana katika aina ya utawala inaoutaka, hivyo hutokea mzozo kati yao katika aina ya utawala wa kibinadamu unaohitajika.
Ama ikiwa utawala umesimama juu ya sheria kutoka kwa Mola wa walimwengu wote, basi Waislamu wawe ndani au nje, hakuna miongoni mwao Dola ya Ndani inayofanya kazi kubadilisha utawala wa Kiislamu kwa sheria nyingine tofauti, isipokuwa Waislamu wanaofanya kazi ndani au nje wawe wanasukumwa na nguvu ya nje ya kikoloni au ya uchokozi. Katika hali hizi mbili haitakuwa Dola ya Ndani kama tulivyotaja hapo awali.
Kwa hiyo, kile kinachoonekana kama mabadiliko au mapinduzi katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama ilivyotokea au inavyotokea Pakistan au Bangladesh au Misri... n.k., basi pande zilizo nyuma ya mapinduzi hayo hazisifiwi kuwa ni Dola ya Ndani kwa sababu ukoloni ndio unaoendesha matukio katika nchi vibaraka wake.
- Ama ikiwa kuna harakati katika nchi za Kiislamu zinazofuata sheria za kibinadamu, na harakati hii inafanya kazi kubadilisha utawala huo katika nchi za Kiislamu kwenda kwenye utawala wa Kiislamu, Khilafah Rashidah, basi harakati hii haitwi Dola ya Ndani, bali ni watu wa nusra kwa ajili ya Allah (swt) na Mtume wake ﷺ.
Na hakika tunamuomba Allah (swt) msaada na taufiki ya kusimamisha Khilafah Rashidah upya, ili Uislamu na Waislamu wapate utukufu, na ukafiri na makafiri wapate udhalili:
وَعَدَ اللهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ
"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale miongoni mwenu walioamini na wakatenda mema, kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao." (QS. An-Nur [24]: 55)
6 Dhul-Qi'dah 1446 AH 4/5/2025 AD