Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa Maswali ya Watembeleaji wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali Tofauti Kati ya Kulingania Uislamu na Kufanya Kazi kwa ajili ya Uislamu Kwa: Fahmi Burhan
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Ta'ala Wabarakatuh,
Tafadhali, ningependa kuulizia kuhusu maana ya kulingania (da’wah) na kufanya kazi (amal).
Mwandishi amesema katika kitabu cha At-Takattul al-Hizbi: “Tunaamini kuwa falsafa ya kweli ya mwamko ni itikadi inayokusanya fikra na njia pamoja, na kwamba itikadi hii ni Uislamu, kwa sababu ni akida ambayo inachipua mfumo wa masuala yote ya dola na umma, na kushughulikia matatizo yote ya maisha. Licha ya kuwa ni mfumo wa kimataifa, si katika mbinu yake kufanya kazi kwa ajili yake tangu mwanzo kwa namna ya kimataifa, bali ni lazima ulinganiwe ulimwenguni kote, na uwekewe nyanja ya kufanya kazi katika nchi au nchi kadhaa mpaka uimarike humo, na kisha dola ya Kiislamu isimame... nk.”
Nilielewa kutokana na nukuu hii kwamba kuna tofauti kati ya kulingania na kufanya kazi, kana kwamba maneno haya yana istilahi maalum ndani ya Hizb. Hii ni pale aliposema kuwa katika mbinu ya Uislamu si kufanya kazi kimataifa bali ni lazima ulinganiwe kimataifa tangu mwanzo. Mwandishi pia amesema katika sehemu nyingine ya kitabu cha At-Takattul al-Hizbi: “Hali ya hewa inabadilika juu yake ikiwa ya joto na baridi, upepo unavuma kwa ukali na kwa upole, na anga hubadilika kati ya usafi na mawingu; ikiwa itathibiti mbele ya mambo haya, basi fikra yake itakuwa imekomaa, njia yake itakuwa wazi, watu wake watakuwa wameandaliwa, fungamano lake litakuwa na nguvu, na itaweza kupiga hatua ya kivitendo katika kulingania na kufanya kazi kutoka katika mshikamano wa kihizbu kuelekea katika chama cha kiitikadi kilichokamilika... nk.”
Hizb ut Tahrir pia imeeleza katika kitabu cha Nuqtat al-Intilaq: “Kwa hivyo, ni lazima kulingania kuwe kupitia chama, na kwa jina la chama, yaani kulingania ni kwa ajili ya Uislamu, na kufanya kazi ni kwa ajili ya kuanza tena maisha ya Kiislamu, lakini anayelingania Uislamu na kufanya kazi ya kuanza tena maisha ya Kiislamu ni Hizb ut Tahrir.”
Swali langu ni:
Je, Hizb ut Tahrir ina dhana maalum kuhusu kulingania (da’wah) na kufanya kazi (amal)?
Na je, kuna tofauti kati ya kulingania na kufanya kazi?
Mwenyezi Mungu akulipeni heri nyingi kwa kusimamishwa kwa Khilafah ya Kiislamu, na ninaomba radhi kwenu ikiwa nimeelewa vibaya nukuu hizo, na ninaomba mnisahihishe ikiwa nimekosea kuzielewa, huenda Mwenyezi Mungu akaleta nusra Yake hivi karibuni, na siku hiyo waumini watafurahi.
Jibu:
Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Ndiyo, kuna tofauti katika muktadha unaoulizia katika kitabu cha At-Takattul kati ya kulingania Uislamu na kufanya kazi kwa ajili ya Uislamu. Kulingania Uislamu ni kubeba fikra zake, kuzifikisha na kuzifafanua, ama kufanya kazi kwa ajili ya Uislamu inamaanisha kufanya kazi ya kuusimamisha katika uhalisia wa maisha, dola, na jamii. Njia ya kufikia hilo ni kupitia kuwepo kwa mshikamano wa kisiasa (at-takattul as-siyasi) unaobeba Uislamu kwa kufanya kazi katika nchi au nchi kadhaa ili kubadilisha jamii humo, kusimamisha dola, na kuchukua utawala... Kisha kueneza da’wah kupitia dola ili kuunganisha nchi za Waislamu na kueneza Uislamu pamoja na kuutekeleza ulimwenguni kote... Tofauti hii imebainishwa katika kitabu cha At-Takattul kwenye mistari uliyoinukuu katika swali lako na mistari inayofuata, ambapo imeelezwa katika kitabu cha At-Takattul yafuatayo:
"[Tunaamini kuwa falsafa ya kweli ya mwamko ni itikadi inayokusanya fikra na njia pamoja, na kwamba itikadi hii ni Uislamu, kwa sababu ni akida ambayo inachipua mfumo wa masuala yote ya dola na umma, na kushughulikia matatizo yote ya maisha. Licha ya kuwa ni mfumo wa kimataifa, si katika mbinu yake kufanya kazi kwa ajili yake tangu mwanzo kwa namna ya kimataifa, bali ni lazima ulinganiwe ulimwenguni kote, na uwekewe nyanja ya kufanya kazi katika nchi au nchi kadhaa mpaka uimarike humo, na kisha dola ya Kiislamu isimame ambayo itakua ukuaji wa asili mpaka ijumuishe nchi zote za Kiislamu kwanza, kisha dola ya Kiislamu iubebe (Uislamu) kuelekea sehemu zilizobaki za ulimwengu, ikizingatiwa kuwa ni ujumbe wake, na ikizingatiwa kuwa ni ujumbe wa kibinadamu wa kimataifa wa kudumu] Mwisho."
Kadhalika, imekuja katika kitabu cha Mafahim Hizb ut Tahrir kile kinachozidi kufafanua jambo hili:
"[Na ili kutoa matokeo ya kazi, ni lazima kuainisha mahali ambapo kazi itaanza, na kikundi ambacho kazi itaanza nacho. Ndiyo, Uislamu ni wa kimataifa na unatazama ubinadamu wote, na unawachukulia wanadamu wote kuwa sawa, na hautilii maanani tofauti za mazingira, hali ya hewa, udongo na mfano wa hayo katika kulingania, bali unawachukulia wanadamu wote kuwa wanafaa kuikubali da’wah, na unawachukulia Waislamu kuwa na jukumu la kufikisha da’wah hii kwa wanadamu wote. Lakini pamoja na hayo, hauanzi na ulimwengu kwa sababu kuanza na ulimwengu kunachukuliwa kuwa ni kazi itakayofeli na haileti matokeo kabisa. Bali ni lazima kuanza na mtu binafsi, na kumalizia na ulimwengu. Kwa hivyo, ilikuwa ni wajibu kubeba da’wah katika mahali ambapo itaimarika mpaka pawe ni hatua ya kuanzia, kisha hapo au sehemu nyingine ambapo da’wah imeimarika pachukuliwe kuwa ni sehemu ya kurukia ambapo da’wah itatokea kuelekea katika njia yake, kisha hapo au penginepo pachukuliwe kuwa ni kituo cha kuegemea ambapo dola itasimama ambapo da’wah imeimarika na kufuata njia yake ya asili: njia ya Jihad] Mwisho wa nukuu kutoka katika kitabu cha Mafahim Hizb ut Tahrir."
Kwa hili, tofauti inakuwa wazi kati ya kulingania Uislamu kwa kuwa ni mfumo wa kimataifa unaofaa kubebwa na kulinganiwa na kufikishwa kwa watu katika kila sehemu ya ulimwengu, na kati ya kufanya kazi kwa ajili ya Uislamu kwa kubana uwanja wa utendaji katika nchi au zaidi kwa lengo la kubadilisha jamii humo na kusimamisha dola inayotawala kwa Uislamu na kuubeba ulimwenguni kwa kulingania na Jihad.
Natumai kuwa jambo hili limekuwa wazi.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
21 Rajab Al-Khayr 1442 H Muwafaka na 05/03/2021 M
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Mtandao