Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Masuluhisho Yanayopendekezwa kwa ajili ya Baada ya Vita Dhidi ya Gaza

March 23, 2024
3452

Jibu la Swali

Swali: Pamoja na kuendelea kwa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na kiyan cha kiyahudi kwa uungaji mkono wa Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya watu wa Gaza kwa zaidi ya miezi mitano, ambapo wahanga wamefikia zaidi ya laki moja kati ya mashahidi na majeruhi, pamoja na uharibifu wa majengo yake mengi; kuna mazungumzo mengi kuhusu miradi ya masuluhisho ya baada ya vita vya Gaza na jinsi mambo yatakavyokuwa kisiasa kulingana na mipango ya nchi za kikoloni, ikiongozwa na Marekani. Je, nini kinachotarajiwa kutokana na mipango na masuluhisho haya? Je, inatarajiwa kuwa Ukingo wa Magharibi utabaki kama ulivyo na kuwe na uvamizi wa kijeshi wa Gaza? Au kuwe na dola katika Ukingo wa Magharibi na Gaza isiyo na silaha? Au Ukingo wa Magharibi ubaki kama ulivyo na Gaza iwe chini ya utawala wa kimataifa na Kiarabu, au utawala wa kibinafsi kama Ukingo wa Magharibi? Na lipi ndilo suluhisho sahihi? Shukrani.

Jibu: Mwanzoni na kabla ya kujibu maswali hapo juu, tunapitia yafuatayo:

Kwanza: Baadhi ya mambo muhimu kuhusu Palestina, Ardhi Iliyobarikiwa:

1- Inafahamika kuwa Ahadi ya Balfour, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, iliyojumuishwa katika barua yake ya tarehe 02/11/1917 kwa Lord Rothschild, ilijumuisha uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa kuanzishwa kwa makazi ya kitaifa ya Mayahudi huko Palestina. Ahadi hii ilikuwa katika siku za mwisho za kuanguka kwa Khilafah ya Kiothmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na khiyana ya baadhi ya wanaume miongoni mwa Waarabu na Waturuki. Miaka kadhaa kabla ya hapo, Herzl, mjumbe wa jumuiya za Kizayuni zilizoungwa mkono na Uingereza, alikuwa amewasilisha ombi tarehe 18/05/1901 kwa Khalifa wa Kiothmania, akijaribu wakati huo kutumia vibaya mgogoro wa kifedha uliokuwa ukiikabili Khilafah kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kuziba nakisi ya Khilafah mkabala wa kupewa ardhi huko Palestina. Hata hivyo, jibu la Khalifa Abdul Hamid kwa Herzl lilikuwa jibu lenye nguvu na la hekima: (Siwezi kuachia hata shubiri moja ya ardhi ya Palestina, kwani si mali yangu, bali ni mali ya Umma wa Kiislamu. Watu wangu wamepigana kwa ajili ya ardhi hii na kuinywesha damu yao... Mayahudi na wabaki na mamilioni yao. Ikiwa dola ya Khilafah itasambaratishwa siku moja, hapo ndipo wataweza kuichukua Palestina bila malipo. Lakini nikiwa hai, hilo halitakuwa...). Khalifa alikuwa na busara na maono ya mbali na alikuwa mkweli katika mtazamo wake; kwani Palestina ilitolewa kwa Mayahudi baada ya kuondoka kwa Khilafah bila malipo! Hivyo ndivyo ilivyoanza kisa cha kunyang'anywa Palestina, kufukuzwa kwa watu wake na mauaji yao, na yakatimia yale aliyotabiri Khalifa Abdul Hamid, Mwenyezi Mungu amrehemu. Kuvunjwa kwa Khilafah (1342 H - 1924 M) kulikoongozwa na Magharibi chini ya uongozi wa Uingereza wakati huo kwa kushirikiana na wasaliti miongoni mwa Waarabu na Waturuki, ilikuwa ndiyo utangulizi halisi wa kuundwa kwa kiyan cha kiyahudi haramu nchini Palestina.

2- Kisha Marekani iliingia rasmi baada ya Vita vya Pili vya Dunia na ikachangia kwa ufanisi katika kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la kugawanya Palestina nambari 181 mnamo Novemba 1947... Marekani ikawa mshindani wa Uingereza na Ulaya nzima katika kuasili Uzayuni wa kiyahudi. Biden alisema katika hotuba aliyoitoa katika Ikulu ya White House wakati wa kusherehekea sikukuu ya Mayahudi (Hanukkah): ("Si lazima uwe Yahudi ili uwe Mzayuni, na mimi ni Mzayuni." Asharq Al-Awsat, 12/12/2023). Na Rais wa Marekani Biden, alipotembelea Tel Aviv mnamo 18/10/2023 kufuatia operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa, alikutana na maafisa huko na kusema: ("Israel lazima irudi kuwa mahali salama kwa Mayahudi. Na kwamba kama kusingekuwa na Israel, tungefanya kazi kuanzisha moja" na akasema "ataliomba Bunge la Marekani kutoa kifurushi cha msaada ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa Israel wiki hii.. Hatutasimama bila kufanya lolote, si leo, wala kesho, wala kamwe"... Al Jazeera 19/10/2023). Hii inaashiria kuwa Marekani ndiyo inayopigana vita hivi, na kwamba kiyan cha kiyahudi hakiwezi kuendelea na vita bila uungaji mkono wa nje, hasa uungaji mkono wa Marekani usio na kikomo. Ni kiyan ambacho kiasili hakiwezi kusimama chenyewe. Kiyan cha kiyahudi kinachora kushindwa kwake kwa mikono yake chenyewe; kwani wao si watu wa vita isipokuwa kwa kamba kutoka kwa watu kama alivyosema Mwenye Nguvu, Mwenye Enzi:

ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ

"Wamepigwa na udhalili popote walipokutwa, isipokuwa (wakishika) kamba ya Allah na kamba ya watu." (QS. Ali 'Imran [3]: 112)

Wameikata kamba ya Allah na kubakiwa na kamba ya watu kutoka Marekani, Ulaya, na vibaraka wao miongoni mwa watawala wasaliti katika nchi za Waislamu ambao hawachukui hatua yoyote mbele ya uvamizi wa kikatili wa kiyahudi; bali bora wao ni yule anayesimama kuhesabu mashahidi na majeruhi! Hii pia inaashiria kuwa Marekani inakiona kiyan hiki kama kituo chake kikuu ambacho kupitia hicho inapigana na Umma wa Kiislamu ili kuzuia umoja wake na kuanzishwa kwa dola yake, dola ya Khilafah.

3- Kiyan cha kiyahudi kimefanya uvamizi wa kikatili mara kadhaa dhidi ya Gaza baada ya kujiondoa huko mnamo 15/08/2005, hadi ilipokuja operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa mnamo tarehe saba Oktoba 2023, ambayo ilivunja kiburi cha adui pale mujahidina walipopenya ngome zake na kuua mamia ya wanajeshi wake hadi kufikia takriban 1200 na kuwateka idadi ya wanajeshi wake. Adui alifanya mashambulizi ya kikatili ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Gaza na bado yanaendelea kwa zaidi ya miezi 5, na ameharibu majengo yake mengi, akilenga hospitali, kuua wagonjwa na kuwafukia wakiwa hai, pamoja na shule walizokimbilia watu wa Gaza. Idadi ya mashahidi imefikia zaidi ya elfu 31, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, na idadi ya majeruhi imezidi elfu 70. Adui amefuata sera ya njaa kwa kuzuia kuingia kwa misaada, chakula, maji, na mahitaji ya kimsingi kwa watu ili kuwashinikiza mujahidina kuwaachilia mateka wanaowashikilia. Vita vyake vilikuwa vita vya mauaji ya kimbari kwa maana halisi ya neno hilo... Alitiwa moyo na uungaji mkono wa Magharibi, pande zote mbili za Marekani na Ulaya na wafuasi wao, na viongozi wa Magharibi walimiminika kutembelea kiyan hicho kuonyesha uungaji mkono kamili kwa kiyan cha kiyahudi katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendesha huko Gaza.

4- Pia alitiwa moyo na ukimya wa serikali katika nchi za Kiarabu na Kiislamu. Badala ya kuyaamrisha majeshi kusaidia watu wa Gaza, baadhi yao walilaani shambulio la mujahidina na kuendeleza mahusiano yao na kiyan cha kiyahudi kana kwamba hakuna kilichotokea. Nchi zilizohalalisha uhusiano (mapatano) ziliendelea na mapatano yao na adui, zile za zamani na za hivi karibuni. Hawakukata uhusiano na kuacha khiyana ya mapatano, wala hawakufuta mikataba na makubaliano na kiyan cha kiyahudi kama vile Camp David na utawala wa Misri na Wadi Araba na utawala wa Jordan na mingineyo. Yaani, hata kiwango cha chini kabisa cha hali ya vita hawakukifanya. Zaidi ya hayo, mahusiano ya kibiashara na idadi ya nchi hizi hayakuathiriwa na uvamizi wa kikatili wa kiyahudi; Waziri wa Uchukuzi wa Uturuki Abdulkadir Uraloğlu alikiri mnamo 11/01/2024 (kwamba takriban meli 701 ziliondoka bandari za Uturuki kuelekea Israel tangu tarehe 7 Oktoba hadi 31 Desemba 2023, yaani wastani wa meli 8 kwa siku... Al Jazeera 11/01/2024). Hata baadhi ya nchi hizi si tu kwamba hazikutangaza nusra kwa Gaza kwa kurudisha uvamizi dhidi yake, bali hazikutangaza vita dhidi ya kiyan cha kiyahudi kwa ajili ya kuwanusuru wanajeshi wao; kwani kiyan cha kiyahudi kililenga maeneo ya Iran nchini Syria na kuua wanajeshi wake wengi, lakini Iran haikutangaza vita dhidi yake!

5- Kisha Marekani inasisitiza katika taarifa zake suluhisho la mataifa mawili, huku ikihakikisha ulinzi kwa kiyan cha kiyahudi na kutetea vitendo vyake vyote vya kinyama na kuupa msaada. Lakini inaogopa kupoteza kile kilichobaki katika nafasi yake ya kimaadili, kana kwamba ina maadili yoyote! Rais wake Biden alisema ("Hakuna kurudi katika hali ilivyokuwa mnamo tarehe sita Oktoba, na hii inamaanisha kuhakikisha kuwa Hamas haiwezi tena kuifanyia ugaidi Israel.. na hii pia inamaanisha kwamba mgogoro huu utakapomalizika lazima kuwe na maono ya kile kitakachofuata.. kwa maoni yetu lazima iwe suluhisho la mataifa mawili na inamaanisha kufanya juhudi za pamoja kwa pande zote..." Tovuti ya CNN ya Marekani, 25/10/2023). Na alisema mnamo 12/12/2023: ("Kuna wasiwasi wa kweli kote duniani kwamba Marekani inapoteza nafasi yake ya kimaadili kwa sababu ya uungaji mkono wetu kwa Israel"... Al Jazeera, 12/12/2023).

Lakini alisisitiza sera ya Marekani akisema ("Hataachana na Israel kamwe, na ulinzi wa Israel ni muhimu sana. Hakuna mstari mwekundu wa kusitisha silaha zote kwake, na hivyo kuwa na 'Iron Dome' ili kuwalinda"... Kituo cha MSNBC cha Marekani, 09/03/2024).

Hivyo, Marekani ni muungaji mkono wa kiyan cha kiyahudi licha ya mvutano wa uhusiano wa Biden na Netanyahu kutokana na ukaribu wake na Trump, mpinzani wa Biden katika uchaguzi.

6- Marekani pia inafanya kazi ya kukishawishi kiyan cha kiyahudi kukubali suluhisho la mataifa mawili kwa kuufanya utawala wa Saudia kuitambua Israel na kuhalalisha uhusiano nayo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al Saud alisema katika mkutano wa Davos ("Saudia inaweza kuanzisha uhusiano wa amani na Israel ikiwa mgogoro wa Palestina utatatuliwa... Independent, 20/01/2024). Kabla ya hapo, mrithi wa kiti cha enzi wa utawala wa Saudia, Ibn Salman, alisema mnamo 21/09/2023 katika mahojiano na mtandao wa Fox News wa Marekani: "Kila siku tunakaribia zaidi na zaidi kuhalalisha mahusiano na Israel". Na mnamo 26/09/2023, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas alimkaribisha katika makao yake makuu mjini Ramallah balozi wa Saudia Naif al-Sudairi ambaye aliwasili mapema katika Ukingo wa Magharibi kupitia kituo cha ukaguzi cha kiyahudi, ikiwa ni utangulizi wa kuhalalisha mahusiano na kiyan cha kiyahudi kwa kisingizio cha kuwa balozi wa ajabu na mwenye mamlaka kamili asiye mkazi nchini Palestina na konsuli mkuu mjini Jerusalem!

Pili: Sasa tunajibu yale yaliyokuja katika swali kuhusu matarajio ya mipango ya Marekani na kiyan cha kiyahudi baada ya kumalizika kwa vita vya Gaza:

1- Kukabidhi Ukanda wa Gaza kwa Mamlaka ya Palestina katika mfumo wa suluhisho la mataifa mawili... Suluhisho hili linadaiwa na Marekani kwa maneno si kwa vitendo, yaani ni mchezo wa maneno. Biden anataka iwe isiyo na silaha, yaani si dola yenye mamlaka kamili. (Rais wa Marekani Joe Biden alisema - jana Ijumaa - kwamba alijadili suala la suluhisho la mataifa mawili na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, na kwamba huyu wa mwisho hakupinga suluhisho hili. Biden aliongeza katika taarifa kwa waandishi wa habari, kwamba kuna mifumo kadhaa ya suluhisho la mataifa mawili, akiashiria kuwa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao vya kijeshi.. Al Jazeera, 04/01/2024). Yaani Biden anaashiria dola ya aina hiyo isiyo na vikosi vya kijeshi! Pamoja na hayo, kiyan cha kiyahudi hakikubaliani hata na mpango huu wa Marekani. (Katika mkutano na waandishi wa habari uliofuatiliwa na Anadolu, Netanyahu alisisitiza kuwa Tel Aviv "inakataa kabisa kuanzishwa kwa dola ya Palestina upande mmoja"... Anadolu, 18/02/2024). Vyovyote iwavyo, suluhisho la mataifa mawili linalopendekezwa na serikali ya Marekani haliwezi kutekelezwa bila amri nzito kutoka kwa Marekani... Na serikali ya Biden haitoi shinikizo kwa Netanyahu na serikali yake kutokana na uchaguzi ujao wa Rais wa Marekani, kwa sababu anahitaji kura za Mayahudi katika uchaguzi na fedha za kundi la shinikizo la kiyahudi (Lobby) kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi, hasa kwa kuwa mpinzani wake ni Trump anayeiunga mkono sana kiyan cha kiyahudi. Ama Ulaya na Uingereza, wao wanafuata hatua za Marekani... Na ama madai ya watawala katika nchi za Waislamu kwa suluhisho la mataifa mawili ni khiyana isiyovuka yale inayoyasema Marekani kwa mfumo wa kutokuwa na silaha wala mamlaka kamili, yaani inafanana na utawala wa kibinafsi!

2- Kuvamiwa tena kwa Ukanda wa Gaza na kiyan cha kiyahudi. Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Ben-Gvir, na Waziri wa Fedha, Smotrich, ni miongoni mwa watu wanaounga mkono sana mpango huu. Mawaziri hawa wawili wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia wanadai kuwa raia wa kiyahudi pamoja na wanajeshi wa uvamizi, lazima wawe ndani ya Gaza na kwamba hii ndiyo njia pekee ya kudumisha udhibiti wa ukanda huo. (Ben-Gvir, ambaye anaongoza moja ya vyama vidogo vya kitaifa katika muungano wa mrengo wa kulia wa Netanyahu, alisema katika mkutano kwamba kurudi kwa walowezi wa kiyahudi na jeshi ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kutorejelewa kwa shambulio la uharibifu lililofanywa na wapiganaji wa Hamas dhidi ya Israel mnamo 7 Oktoba... Reuters, 29/01/2024). Hata hivyo, Marekani na Mayahudi wengi hawaungi mkono maoni haya. (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alisisitiza Jumatano kwamba Israel "haiwezi kuikalia" Gaza baada ya kumalizika kwa vita inavyopigana sasa dhidi ya harakati ya Hamas. Aliongeza: "Sasa, ukweli ni kwamba kunaweza kuwa na haja ya kipindi fulani cha mpito mwishoni mwa mzozo.. Hatutarajii uvamizi tena na kile nilichosikia kutoka kwa viongozi wa Israel ni kwamba hawana nia ya kuikalia tena Gaza..." Al-Hurra, 08/11/2023). Hii ni kwa sababu uvamizi wa kijeshi tena wa Gaza utasababisha gharama kwa kiyan cha kiyahudi na hasara za kijeshi na kiuchumi.

3- Kuendelea kwa udhibiti wa Hamas huko Gaza. Marekani, Ulaya, na kiyan cha kiyahudi hawataki Hamas ibaki madarakani Gaza, kwa sababu wanaamini kuwa hilo litasababisha kurejelewa kwa mashambulizi ya 7 Oktoba. Blinken aliwaambia waandishi wa habari mjini Tokyo: "Hamas haiwezi kuendelea kuiongoza Gaza, kwani hilo linaweka mazingira ya kurejelewa kwa yale yaliyotokea tarehe saba Oktoba... 08/11/2023). Na Gallant alisema (kwamba Hamas haitadhibiti Ukanda wa Gaza baada ya vita, na kwamba Tel Aviv inajiandaa kwa ajili ya kudhibitiwa kwake na "kiyan cha kimataifa"... Anadolu, 18/12/2023).

4- Kuhamisha usalama katika ukanda huo kutoka kwa jeshi la kiyan cha kiyahudi kwenda kwa kikosi cha kimataifa. Hili lilikuwa miongoni mwa mambo yaliyofanyiwa utafiti, hasa na baadhi ya wanasiasa wa Marekani, kwamba kuwe na vikosi vya kimataifa huko Gaza kutoka nchi za Kiarabu na nchi nyinginezo.. Na jambo hilo lilionekana katika vyombo vya habari..

(Kulingana na gazeti la Wall Street Journal... Kushawishi nchi za Kiarabu zilizotia saini makubaliano ya amani au makubaliano ya mapatano na Israel kutoa kikosi cha usalama kwa ajili ya Gaza au kuisimamia, lakini hilo litahitaji baadhi ya nchi au mashirika kubeba jukumu la kiutawala na usimamizi wa usalama, na gazeti linasema kuwa baadhi ya majirani wa Kiarabu wanasitasita... Al-Hurra, 03/11/2023). Kisha utafiti huo ulijirudia tena, ambapo Russia Today ilichapisha mada hii tena mnamo 04/12/2023 kama ifuatavyo: "Washington pia inaunga mkono kuhamisha usalama katika ukanda huo kutoka kwa jeshi la Israel kwenda kwa kikosi cha kimataifa, labda kitakachoundwa na baadhi ya nchi za Kiarabu. Lakini Israel haikubaliani na mazingira ya kutumwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika eneo la mzozo, na pia haiamini uwezo wa shirika hilo la kimataifa kulinda maslahi ya Israel".

5- Kukabidhi utawala wa kiraia huko Gaza kwa Wapalestina bila kuungana na Ukingo wa Magharibi lakini kiyan cha kiyahudi kitakuwa na jukumu la usalama kama ilivyo katika Ukingo wa Magharibi. Al Jazeera ilichapisha mnamo 27/02/2024 kwamba mnamo 23 Februari 2024, Waziri Mkuu wa kiyan cha kiyahudi Benjamin Netanyahu aliwasilisha mpango wa "Siku Inayofuata" kwa ajili ya Gaza kwa Baraza la Mawaziri la Usalama na Siasa. (Mpango uliowasilishwa na Benjamin Netanyahu kwa wajumbe wa serikali yake ulikuja na maelezo mengi kuhusu mustakabali wa Ukanda wa Gaza, na miongoni mwa sifa zake kuu katika nyanja ya usalama; Israel itahifadhi uhuru wa hatua za kijeshi na usalama katika maeneo yote ya ukanda huo bila ukomo wa muda, pamoja na kuanzisha ukanda wa usalama ndani ya Ukanda wa Gaza, kando ya mipaka yake na Palestina inayokaliwa tangu mwaka 1948.. Zaidi ya hayo, Israel itafanya upokaji wa silaha katika Ukanda wa Gaza, na kuiondolea uwezo wowote wa kijeshi, isipokuwa kile kinachohitajika kwa ajili ya kudumisha usalama wa umma..)

6- Kwa kuzingatia uwezekano uliotangulia wa mipango ya Marekani na Mayahudi, jambo linalotarajiwa miongoni mwa wanayopanga kutekeleza ni lile lililotajwa katika kipengele cha (5) hapo juu bila Gaza kuwa kitu kimoja na Ukingo wa Magharibi, bali hatua za usalama na kijeshi katika maeneo yote mawili ziwe zinashabihiana (Israel inahifadhi uhuru wa hatua za kijeshi na usalama katika maeneo yote ya ukanda huo bila ukomo wa muda..) hasa kwa kuwa Mayahudi wanatekeleza mpango huu huu katika Ukingo wa Magharibi. Na ilitajwa katika habari kwamba Netanyahu aliwasilisha mpango huu kwa maafisa wa Marekani na inaonekana unapata idhini yao (Na ilidaiwa kuwa Netanyahu alihakikisha kuwa mpango aliouandaa unaenda sambamba na mpango wa Marekani kwa ajili ya suluhisho la kudumu katika Mashariki ya Kati, na kwamba Marekani ilishauriwa kuhusu mpango huo kupitia Waziri wa Masuala ya Kimkakati Ron Dermer, mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Vita la Israel ambaye ana uhusiano wa karibu na Washington... NTV, 31/01/2024). Yaani Marekani inaufahamu mpango wa Netanyahu mapema.

Ama yale anayoyakariri Biden kuhusu suluhisho la mataifa mawili, hayana tofauti sana, bali kama ilivyokuja katika taarifa yake ya awali kipengele cha (1) ambayo ni (Biden aliongeza katika taarifa kwa waandishi wa habari, kwamba kuna mifumo kadhaa ya suluhisho la mataifa mawili, akiashiria kuwa nchi kadhaa katika Umoja wa Mataifa hazina vikosi vyao vya kijeshi.. Al Jazeera, 04/01/2024), yeye anaashiria upokaji wake wa silaha, na hana kizuizi kwa suluhisho la mataifa mawili kutanguliwa na hatua ya mpito kama ilivyokuja katika taarifa yake kipengele cha (2) (Sasa ukweli ni kwamba kunaweza kuwa na haja ya kipindi fulani cha mpito mwishoni mwa mzozo... Al-Hurra, 08/11/2023).

Tatu: Suluhisho Sahihi la Kisheria linalopaswa kufanywa:

1- Kwa kuzingatia yaliyotangulia, inadhihirika kutokana na mipango ya Marekani na dola ya kiyahudi kwamba wanapanga kufanya Ukingo wa Magharibi na Gaza kuwa maeneo yaliyopokwa silaha na kwamba mamlaka ya usalama katika maeneo hayo yawe ya Mayahudi, iwe ni chini ya jina la dola moja katika maeneo yote mawili, yaani kwa kuyaunganisha hata kama itakuwa kwa hatua kama inavyotaka Marekani, yaani Ukingo wa Magharibi ubaki umetengwa na Gaza katika hatua ya mpito kisha baada ya hapo Gaza iunganishwe na Ukingo wa Magharibi bila nguvu ya kijeshi, au kama inavyotaka dola ya kiyahudi Gaza ibaki tangu mwanzo hadi mwisho ikiwa imetengwa na Ukingo wa Magharibi na yote mawili bila nguvu ya kijeshi, na mamlaka halisi katika maeneo hayo yawe ya kiyan cha kiyahudi. Ni wazi kutokana na hayo kwamba kile kinachopangwa na Marekani na Mayahudi ni sumu mbaya na ni khiyana kwa Allah, Mtume Wake na Waumini... Pamoja na kwamba si ajabu kwa kiyan cha kiyahudi na Marekani kupanga hayo, kwani wao ni maadui, lakini cha ajabu ni kutochukua hatua kwa yeyote miongoni mwa watawala katika nchi za Waislamu na hasa wale walio jirani na Palestina, ili kuliamrisha jeshi lake kunusuru Gaza, watu wake, Aqsa na mazingira yake, na kuling’oa kiyan cha kiyahudi kutoka mizizi yake, na kisha kuirudisha Palestina yote kwa watu wake. Je, si yule aliyekalia ardhi ya Waislamu na kuwafukuza watu wake humo anastahili kupigwa vita na majeshi ya Waislamu na wamtoe humo kama alivyowatoa watu wake?

وَاقْتُلُوهُمْ حَيْثُ ثَقِفْتُمُوهُمْ وَأَخْرِجُوهُمْ مِنْ حَيْثُ أَخْرَجُوكُمْ

"Na waueni popote mnapowakuta, na wafurubisheni kutoa mahali walipowafurubisha." (QS. Al-Baqarah [2]: 191)

Mbona watawala hawadiriki hilo?! Lakini shari zao zimewatawala, kwani wao ni watifu kwa makafiri wakoloni na hasa Marekani, hawarudishi ombi lake lolote ili kulinda viti vyao vilivyopinda.

قَاتَلَهُمُ اللهُ أَنَّى يُؤْفَكُون

"Allah awaangamize! Wanageuzwa wapi hawa?" (QS. At-Tawbah [9]: 30)

2- Vita hivi vimefichua mambo mawili muhimu: Kwanza ni udhaifu wa Mayahudi na udhalili wao kama Allah alivyowataja katika Kitabu Chake:

ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ

"Wamepigwa na udhalili popote walipokutwa, isipokuwa (wakishika) kamba ya Allah na kamba ya watu." (QS. Ali 'Imran [3]: 112)

Wameikata kamba ya Allah baada ya Mitume wao na hawajabakiwa isipokuwa na kamba ya watu; Marekani na wafuasi wake, na watu wenye hali hii si watu wa vita wala ushindi... Pili ni khiyana ya watawala katika nchi za Waislamu, kwani wanatazama yanayotokea na bora wao ni yule anayehesabu mashahidi na majeruhi.

صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَرْجِعُونَ

"Viziwi, mabubu, vipofu, kwa hiyo hawatarejea." (QS. Al-Baqarah [2]: 18)

Inastahili kwa mambo haya mawili kuwasukuma wenye ikhlasi miongoni mwa watu wa nguvu katika majeshi ya Waislamu kutangaza mwelekeo wa jumla (Jihadi) ili kutekeleza faradhi ya Allah kwa kupigana na Mayahudi waliokalia Palestina.

وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ إِنْ تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللهِ مَا لَا يَرْجُونَ

"Wala msilegee katika kuwafuatilia watu hao (maadui); ikiwa nanyi munaumia, basi na wao pia wanaumia kama mnavyomia, nanyi mnamtarajia Allah (malipo) wasiyoyatarajia wao." (QS. An-Nisa [4]: 104)

Na hivyo mtaondoa kiyan chao kwani wao ni duni mbele ya Allah kuliko hata washinde katika vita, na kisha itatimia ahadi ya Allah:

فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ لِيَسُوءُوا وُجُوهَكُمْ وَلِيَدْخُلُوا الْمَسْجِدَ كَمَا دَخَلُوهُ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَلِيُتَبِّرُوا مَا عَلَوْا تَتْبِيراً

"Basi itakapofika ahadi ya mwisho, (tutatuma waja wetu) ili wazisikitishe nyuso zenu, na waingie Msikitini (Aqsa) kama walivyoingia mara ya kwanza, na ili waharibu kile walichokiteka kwa uharibifu mkubwa." (QS. Al-Isra [17]: 7)

Basi simameni kuwanusuru ndugu zenu huko Gaza na ikiwa serikali za kidikteta zilizopo katika nchi za Waislamu zitasimama mbele yenu, basi wadhibiti kabisa... na simamisheni hukumu ya Allah mahali pao, Khilafah kwa njia ya Utume, ikiwa ni utimizaji wa bishara ya Mtume wa Allah ﷺ:

ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ، ثُمَّ سَكَتَ

"...kisha kutakuwepo na utawala wa kidikteta (wa kulazimisha), na utakuwepo kwa muda anaotaka Allah uwepo, kisha Allah atauondoa anapotaka kuuondoa, kisha kutakuwepo na Khilafah kwa njia ya Utume, kisha akanyamaza." (Musnad ya Imam Ahmad)

Na hapo ndipo Khalifa, wasaidizi wake, na askari wa Kiislamu kuanzia wa cheo cha juu kabisa hadi cha chini watakuwa wakitoka kwenye ushindi mmoja kwenda ushindi mwingine, wakipiga Takbira na Umma ukipiga Takbira pamoja nao, wakiwa wenye nguvu kupitia kwa Mola wao, wenye izza kupitia dini yao, hapo hakuna adui atakayethubutu kuwa na kiyan katika ardhi ya Kiislamu.

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

"Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa nusura ya Allah; Humnusuru amtakaye, Naye ni Mwenye Nguvu, Mwenye kurehemu." (QS. Ar-Rum [30]: 4-5)

12 Ramadhani 1445 H 22/03/2024 M

Share Article

Share this article with your network