Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Matukio ya Hivi Karibuni katika Suala la Kupro

January 22, 2017
4590

Jibu la Swali

Swali: Mazungumzo ya Kupro yalimalizika Ijumaa tarehe 20/01/2017, baada ya kuanza tena tarehe 18/01/2017... Mazungumzo haya yalikuwa yamekwama tangu mwanzoni mwa mwaka 2013 na kisha kusimama tangu Novemba 2014... Yakarejea na kuanza tena mnamo Mei 2015 na kuendelea kwa kusimama na kuanza hadi mwishoni mwa 2016... Kisha yakashika kasi ya ajabu tarehe 09/01/2017 huko Geneva kwa ajili ya kuunganisha tena Kupro kwa ushiriki wa kiongozi wa Waturuki wa Kupro, Mustafa Akinci, na mwenzake wa Wagiriki wa Kupro, Nicos Anastasiades, kisha yakajiunga mataifa matatu wadhamini wa usalama wa Kupro ambayo ni Uturuki, Ugiriki, na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya... Ni nini kilichojitokeza katika suala la Kupro hadi kuanza tena kwa kasi hivi? Na ni suluhu gani inayotarajiwa kwa suala la Kupro? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu: Ili kujibu maswali haya, tutapitia suala hili kutoka nyanja zake mbalimbali: (za ndani, za kikanda, na za kimataifa), kisha nyanja zinazoingiliana (ndani, kikanda, na kimataifa)... Na kisha yatabainika matukio yaliyosababisha harakati hizi za kasi, na baada ya hapo tutaona suluhu inayotarajiwa kwa suala hili, In Shaa Allah:

Kwanza: Nyanja za Ndani:

Chimbuko la mgogoro wa Kupro ndani ya nchi ni mapambano ya madaraka kati ya Waturuki wa Kupro ambao ni Waislamu na Wagiriki wa Kupro. Ili kuhodhi madaraka na kuwafukuza Waislamu wa Kituruki kutoka katika vyombo vya dola, wazalendo wa Kigiriki wa Kupro waliweka mpango uliotambulika wakati huo kama "Mpango wa Akritas" wa mwaka 1963, uliokusudia kuwaondoa Waturuki katika nyadhifa zao ili kuandaa muungano na Ugiriki. Operesheni za kulipiza kisasi za kumwaga damu dhidi ya Waislamu zilianza; mauaji, kufukuzwa makazi, na kunyang'anywa mali ndiyo ilikuwa siasa iliyotumiwa na Wagiriki wa Kupro kwa ajili ya kuungana na Ugiriki, na jambo hilo halikuwa mbali na ushawishi wa Uingereza. Ni vyema kutaja kuwa Uingereza, mtawala halisi wa kisiwa hicho wakati huo na mmiliki wa kambi mbili kubwa za kijeshi hapo, iliipa kisiwa hicho uhuru mwaka 1960 kwa sharti kwamba Wagiriki wa Kupro waachane na wazo la kuungana na Ugiriki linaloitwa Enosis, mkabala na Waturuki kuachana na wazo la kuungana na Uturuki linaloitwa Taksim. Kufikia mwaka 1967, mgawanyiko wa kweli ulikuwa ndio hali halisi kisiwani humo, na uadui kati ya Wagiriki wa Kupro na Waislamu wa Kituruki ulijitokeza wazi.

Pili: Nyanja za Kikanda:

Ugiriki ilikuwa ikiwaunga mkono Wagiriki wa Kupro na kuwapa msaada huku ikipanga kukimeza kisiwa hicho, na mkabala wake Uturuki ilikuwa ikitoa msaada kwa Waislamu wa Kituruki. Mataifa haya mawili ndiyo yalikuwa nguvu za kikanda zilizochochea hali ya mgawanyiko wa ndani huko Kupro. Mnamo tarehe 15/07/1974, baraza la kijeshi la Ugiriki, kwa maelekezo ya Amerika, liliunga mkono mapinduzi ya kijeshi huko Kupro ili wapinduzi hao waamue suala la kujiunga na Ugiriki. Ilitarajiwa kuwa mchakato halisi wa Ugiriki kuimeza Kupro ungeanza kama si kuingilia kati kwa jeshi la Uturuki siku tano baada ya mapinduzi hayo, na kuivamia kaskazini mwa kisiwa hicho kwa maelekezo ya Waingereza. Kisha jeshi la Uturuki likageuza makazi madogo na yaliyotengwa ya Waislamu wa Kituruki kuwa eneo moja lililoungana kijiografia linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 3,335, yaani thuluthi moja ya ardhi ya kisiwa hicho, lakini ikiwa na wakazi 210,000 tu, yaani sehemu ya tano ya wakazi wote. Nguvu hizi mbili, yaani Uturuki na Ugiriki, ndizo nguvu za kikanda zenye ushawishi huko Kupro, lakini dola ya Kiyahudi pia ina ushawishi, ingawa ni wa kificho, katika nyanja za usalama na uchumi hususan mikataba ya gesi.

Tatu: Nyanja za Kimataifa:

Tangu Uingereza ilipokimeza kisiwa hicho rasmi mwaka 1914 mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia, na hadi hivi karibuni, Uingereza imekuwa ndio mdau wa kimataifa mwenye nguvu zaidi nchini Kupro. Ilipokipa uhuru mwaka 1960, Uingereza ilibaki rasmi kulingana na mikataba kuwa ndiyo nguvu pekee ya kimataifa inayodhamini hali ya Kupro baada ya kuzijumuisha nguvu mbili za kikanda, Uturuki na Ugiriki, mwaka 1955 kama mataifa wadhamini wa Kupro. Uingereza ilitaka kupitia ujumuishaji wa nguvu hizi za kikanda kuzuia Amerika, kupitia ushawishi wake nchini Ugiriki, kuimeza Kupro, hivyo ikaweka kikwazo cha Uturuki (iliyokuwa tiifu kwake wakati huo) katika mipango ya Ugiriki. Uingereza iliendelea kubaki na kambi mbili za kijeshi huko Kupro ambazo ni miongoni mwa kambi kuu za kijeshi za Uingereza duniani, zikiwa na wanajeshi 24,000 na nguvu kubwa za majini na angani. Leo hii kambi hizo ni alama kubwa ya ukoloni wa Uingereza; kutoka huko ndiko ilikozindua mashambulizi katika vita vya Suez mwaka 1956, na kutoka huko ilishiriki kwa ndege zake pamoja na dola ya Kiyahudi katika vita vya 1967, na vita vya Uingereza bega kwa bega na Amerika katika kuivamia Iraq miaka ya 1991 na 2003, na kutoka huko hufanya ujasusi na kufuatilia eneo hilo. Kwa hiyo, usalama wa Kupro ni sehemu ya usalama wa Uingereza hadi leo, na kiuchumi Uingereza inaitumia pia kama maficho ya kodi (tax haven) miongoni mwa mfululizo wa visiwa vya mbali ili kuvutia fedha zilizoibiwa na watawala, fedha za makampuni yanayokwepa sheria za kodi, na fedha za magenge ya uhalifu "Mafia" hususan ya Kirusi. Kwa sababu hizi zote, kisiwa cha Kupro kina nafasi ya pekee kwa Waingereza. Hivyo, Uingereza imeweza kwa werevu wake kuvuka majaribio yote ya Amerika ya kurithi koloni hili muhimu, na Ugiriki ilikuwa karata ya Amerika ya kuingilia Kupro, lakini Uingereza iliweza kuizuia kupitia Uturuki na kupitia mawakala wake huko Kupro. Inaweza kusemwa kuwa suala la Kupro kimataifa katika miongo michache iliyopita limekuwa ni suala la ushindani mkali kati ya wafuasi wa Amerika na wafuasi wa Uingereza. Amerika ilikuwa haioni lingine huko Kupro isipokuwa kuondoa kambi za kijeshi za Uingereza na kuchukua nafasi yake, na ilikuwa ikitumia juhudi za Umoja wa Mataifa kama nyenzo ya kufikia malengo yake. Ama Uingereza, imeendelea kuwa na uwezo wa kuvuka vikwazo vya Amerika kwa werevu wake, na ilifanikiwa kuifanya Kupro ibaki imegawanyika ili kuhalalisha kuwepo kwa kambi zake za kijeshi, na ilizuia mipango ya Amerika isitekelezwe kikamilifu nchini Kupro... Kisha Uingereza ilikaribia kufikia malengo yake kikamilifu katika kulinda kambi zake kupitia jaribio la mapinduzi (nchini Uturuki) ili kuleta utawala tiifu kwake badala ya utawala wa sasa ulio tiifu kwa Amerika... Ingawa jaribio hilo lilifeli, lakini lilipiga kengele ya hatari kwa pande zote mbili, Amerika na Uingereza, kuhusiana na utawala wa Uturuki na hivyo athari yake kwa suala la Kupro...

Nne: Nyanja Zinazoingiliana:

1- Harakati za Kiislamu zenye athari katika eneo:

Mapinduzi ya Syria yalikuwa kama fundo la mafundo kwa siasa za Amerika katika eneo hili, kwani haikuweza kuondoa hatari yake licha ya kupita miaka mingi, na licha ya wingi wa nyenzo za Amerika kuanzia Iran na wafuasi wake, Urusi na nguvu zake za kijeshi, Uturuki na nchi za Ghuba na mawasiliano yao na msaada wao wa kifedha, Geneva na wajumbe wa kimataifa. Amerika ilikuwa inatambua kwa yakini kuwa inapambana na Uislamu nchini Syria, na ni uzoefu mpya kwa siasa za Amerika kwa ukubwa huu ambao umemfanya Obama awe na mvi kichwani kama ilivyokuja katika tamko lake kwenye mkutano na waandishi wa habari tarehe 04/08/2016 aliofanya baada ya mkutano wake na Baraza la Usalama la Taifa na viongozi wa kijeshi katika Wizara ya Ulinzi ya Amerika: "Nina uhakika kabisa kwamba sehemu kubwa ya mvi kichwani mwangu imetokana na mikutano niliyofanya kuhusu Syria..." (Russia Today, 05/08/2016).

Amerika na Magharibi zimechukulia harakati za Kiislamu katika eneo hili kwa uzito mkubwa, na kwamba kufanikiwa kwa Waislamu kusimamisha dola yao imekuwa ni wasiwasi mkubwa kwa Amerika na Magharibi. Kubaki kwa jeshi la Uturuki (takriban wanajeshi 30,000) huko Kupro kutakuwa hatari kwao, kwani wanachukulia kwa uzito harakati za Kiislamu za kusimamisha Khilafah, na kuwepo kwa jeshi la Kiislamu la Uturuki katika kisiwa hicho wakati huo kutakuwa ni kichwa cha mkuki wa kukirejesha kisiwa hicho katika asili yake kama nchi ya Kiislamu tangu kilipofunguliwa katika zama za Khalifa Othman (ra)... Kwa hiyo, wanaona umuhimu wa kuliondoa jeshi hili na hivyo kuharakisha mazungumzo ili kufikia lengo hilo.

2- Sababu mpya ya nishati: Tangu kugunduliwa kwa gesi asilia katika pwani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu mwaka 2009 na kuanza kwa dola ya Kiyahudi kuitumia kibiashara mwaka 2013... kisha matarajio ya Ugiriki, Uturuki na Kupro pande zote mbili hivi karibuni katika utafutaji... yote haya yamefanya nishati kuwa miongoni mwa vichocheo vipya vya mgogoro wa Kupro na kuupa nguvu kubwa kama ifuatavyo:

a- Takwimu za kiufundi za mashamba ya gesi yaliyogunduliwa katika pwani ya Mashariki mwa Mediterania zinaashiria kuwepo kwa kiasi kikubwa cha gesi, kinachotosha kuwa mbadala wa uingizaji wa gesi barani Ulaya na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa gesi ya Urusi. Rais wa Kupro Nicos Anastasiades, na mawaziri wa mawasiliano, biashara, kilimo, na mazingira, wametamka hadharani katika matukio mbalimbali "kwamba akiba ya gesi ya Kupro inaweza kuiwezesha Ulaya kuwa na vyanzo mbalimbali mbali na Urusi". (Noon Post, 11/11/2014). (Mamlaka za Ugiriki zinafanya utafiti wa mafuta na gesi katika shamba la Leviathan kusini mashariki mwa Nicosia, shamba ambalo lina mapipa bilioni 1.7 ya mafuta yanayoweza kuchimbwa, na futi za ujazo bilioni 122 za gesi asilia. Kama hatua ya kupinga hatua ya Ugiriki, Ankara ilisaini makubaliano na mamlaka za Waturuki wa Kupro kwa ajili ya utafiti wa mafuta katika pwani ya kaskazini...) (Dot Egypt, 27/04/2015).

b- Ugiriki na Wagiriki wa Kupro, ambao wote wanakabiliwa na migogoro mikubwa ya kiuchumi, wanatamani kuimarisha hazina zao kwa mapato ya gesi kutoka pwani ya Kupro na kupitia bomba la usafirishaji la Ugiriki kuelekea Ulaya, na Ugiriki kuwa nchi ya mpito kwa gesi ya Kupro na ya dola ya Kiyahudi kuelekea Ulaya.

c- Lakini ndoto hizi za Ugiriki, Kupro, na Ulaya zinakaribia kuvurugwa na Uturuki kwani inazuia moja kwa moja operesheni za utafutaji wa mafuta na gesi katika pwani ya Kupro. Mara tu ushirikiano wa Wagiriki wa Kupro na Ugiriki ulipoanza na dola ya Kiyahudi katika utafutaji na utumiaji wa nishati mashariki mwa Mediterania, Uturuki ilijitokeza na kusimama dhidi ya Ugiriki na Kupro katika operesheni hizo na kuimarisha udhibiti wake wa majini. Katika majibu ya moja kwa moja, Uturuki ilisaini makubaliano ya utafiti wa nishati na Kupro ya Kituruki si tu katika eneo la bahari kati yao, bali pia katika eneo la kusini karibu na shamba la Aphrodite la Wagiriki wa Kupro, na Uturuki ilitishia kuchimba, jambo ambalo linaamsha mzozo kati yao. Haioni njia ya utafutaji isipokuwa kwa kutatua suala la Kupro kulingana na mradi wa Amerika kupitia mazungumzo na kutoendelea na utafutaji wa Kupro hadi mazungumzo yaishe... Msimamo huu wa Uturuki unathibitishwa pia na kile alichotangaza Rais wa Uturuki Erdogan kwamba "kung'ang'ania kwa mamlaka za Wagiriki wa Kupro kufanya utafutaji wa mafuta, hakuna lengo lingine isipokuwa kuharibu mchakato wa mazungumzo unaoendelea kati ya watu wa Kupro..." (Dot Egypt, 27/04/2015). Yaani, Uturuki inataka kufanya utafutaji wa gesi na uwekezaji wake kuwa suala lililofungamana na suluhu ya mwisho, yaani kuzisukuma pande husika kuelekea suluhu, hususan katika kipindi cha hivi karibuni ambapo maslahi ya pande hizo katika utafutaji yameongezeka... Yote haya yanaharakisha suala la mazungumzo ili kufikia suluhu itakayofanya utafutaji uwezekane bila migogoro.

Tano: Kutokana na yaliyotangulia, yanabainika matukio yaliyosukuma kwenda katika mazungumzo ya Kupro kwa kasi kubwa zaidi na nguvu zaidi, nayo ni kama ifuatavyo:

1- Jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini Uturuki: Kutokana na ukubwa wa tishio la jaribio hili kwa ushawishi wa Amerika nchini Uturuki na eneo hilo, Rais wa Amerika Obama mnamo 16/07/2016 alifanya mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Taifa la Amerika kufuatia jaribio hilo. Mkutano huu ulikuwa ni ishara ya umuhimu mkubwa ambao Amerika inaupa ushawishi wake nchini Uturuki kutokana na nchi hii kuwa na athari pana katika mazingira yake. Jaribio la mapinduzi lilipofeli, Rais Erdogan alitangaza hali ya hatari nchini, na kuanza kulisafisha jeshi na dola kutokana na wafuasi wa Waingereza na bado anaendelea. Operesheni hizi za usafishaji zitadhoofisha msimamo wa Uingereza nchini Uturuki, na kuwapokonya karata ya viongozi wa jeshi nchini Uturuki, ambayo kwa muda mrefu walikuwa wakiitumia kuzuia hatua za Amerika dhidi yao huko Kupro... Hivyo, njia ya Amerika kuelekea suluhu ya suala la Kupro kulingana na mipango yake, hususan mpango unaojulikana kama "Mpango wa Annan" wa Muungano wa Kupro, njia hii imekuwa wazi zaidi baada ya operesheni ya kuwasaka watu wa Waingereza jeshini ambao walikuwa wakikwamisha suluhu ya Amerika huko Kupro na kuiunga mkono Uingereza katika kulinda kuendelea kwa kambi mbili huko Kupro... Kila usakaji unavyoongezeka, mazungumzo yanakuwa na tija zaidi kwa Amerika.

2- Harakati za Kiislamu katika eneo: Kama tulivyotaja hapo awali, Amerika na Magharibi wanachukulia kwa uzito harakati za Kiislamu za kusimamisha Khilafah, na kuwepo kwa jeshi la Kiislamu la Uturuki katika kisiwa hicho wakati huo kutakuwa ni kichwa cha mkuki wa kukirejesha kisiwa hicho katika asili yake kama nchi ya Kiislamu tangu kilipofunguliwa katika zama za Khalifa Othman (ra)... Kwa hiyo, wanaona umuhimu wa kuliondoa jeshi hili na hivyo kuharakisha mazungumzo ili kufikia lengo hilo...

3- Sababu mpya ya nishati: Kutazama sababu hii mpya inayoongezeka kunabainisha kuwa inaunda, kwa upande wa kiuchumi, kichocheo chenye athari katika kuharakisha suluhu ya mgogoro wa Kupro, na kuondoa kinachozuia mradi huu wa kiuchumi wenye matarajio makubwa. Hivyo, maslahi ya pande zote za mgogoro wa Kupro sasa yanahitaji kupata suluhu ya mgogoro huo na kukubaliana juu ya hisa za kiuchumi za baharini na mabomba ya gesi, na hivyo kuharakisha mazungumzo kwa umakini zaidi...

Sita: Kwa athari ya sababu hizi, pande husika zimesukumwa kwa bidii mwishoni mwa mwaka uliopita na mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 kama ifuatavyo:

a- Duru ya kwanza ya mazungumzo ya Kupro ilifanyika katika mji wa Mont Pèlerin nchini Uswisi tarehe 7-11 Novemba 2016, huku duru ya pili ikifanyika katika mji huo huo tarehe 20-21 mwezi huo huo wa Novemba 2016. Duru hizo mbili hazikufanikiwa kufikia lolote.

b- Duru ya tatu ya mazungumzo ya Kupro yenye lengo la kupata suluhu ya kisiasa kisiwani humo ilifanyika katika mji wa Geneva nchini Uswisi tarehe 09 Januari mwaka huu chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yalijikita katika mada 6 nazo ni "Tatizo la kiuchumi la Kupro, Umoja wa Ulaya, umiliki, uhamiaji na ushiriki wa madaraka, ardhi na usalama, na dhamana".

c- Mnamo tarehe 10/01/2017, ulifanyika mkutano mwingine wa pande zinazohusika na suala la Kupro huko Geneva katika ngazi ya juu ya kidiplomasia kwa mahudhurio ya Rais wa Jamhuri ya Waturuki wa Kupro, Mustafa Akinci, na Rais wa Jamhuri ya Wagiriki wa Kupro, Nicos Anastasiades...

d- Tarehe 12/01/2017 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, mazungumzo ya Kupro kati ya kiongozi wa Waturuki wa Kupro Mustafa Akinci na mwenzake wa Wagiriki wa Kupro Nicos Anastasiades yalimalizika. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kupro, Espen Barth Eide, alisema: "Tumefanya mazungumzo yenye tija katika siku tatu zilizopita," na kuongeza kuwa matatizo mengi yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu yametatuliwa, na kwamba maendeleo yamekuwa ya haraka, kulingana na maelezo yake.

e- Rais wa Kupro alitangaza: (Kwa upande wake Rais wa Kupro alisema katika mkutano na waandishi wa habari, Ijumaa, kwamba mazungumzo ya kisiasa yamepata maendeleo makubwa kwa mara ya kwanza, kwani mjadala umeanza kuhusu masuala ya msingi hasa...) (Russia Today, 13/01/2017).

f- Kisha zilifanyika duru za tarehe 18-20/01/2017 na baada ya hapo taarifa ya mwisho ilitolewa ikisema:

(...Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kupro, Espen Barth Eide, alieleza kuwa vikundi kazi vimemaliza kazi zao vilipojadili suala la dhamana kwa mafanikio. Ilarifiwa kuwa vikundi kazi vilijadili masuala ya usalama na dhamana katika nyanja zote... Tunaweza kusema kuwa suala la usalama na dhamana limeandaliwa kama kazi za kitaalamu kwa hatua inayofuata baada ya mikutano 4 iliyodumu kwa siku mbili... Inafaa kutajwa kuwa pande hizo zimekubaliana kufanya mkutano wa kilele ambapo pande hizo zitawakilishwa na ngazi za juu katika hatua ijayo, jambo ambalo lina maana kuwa hatua ya tatu ya mazungumzo ya Geneva itaendelea kwa mkutano wa kilele utakaoshirikisha mawaziri wakuu wa nchi tano. Inatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini Mustafa Akinci na kiongozi wa Wagiriki Nicos Anastasiades watajadili mada zinazohusiana na kikao cha kisiasa cha mkutano wa pande tano, kupitia mkutano watakaofanya tarehe 26 mwezi huu wa Januari mjini Nicosia... Ujumbe ulioongozwa na Naibu Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Ahmed Mukhtar Gun, uliiwakilisha Uturuki katika mkutano huo, huku ujumbe ulioongozwa na mpatanishi Ozdil Nami ukiwakilisha upande wa Kituruki wa kisiwa hicho. Naibu Waziri Mkuu Tugrul Turkes aliondoka kuelekea Geneva kupata taarifa kuhusu kazi za kikundi kazi kilichopo Geneva katika mchakato wa mazungumzo ya Kupro. Mazungumzo ya Kupro yanajumuisha mada kuu 6 nazo ni: Uchumi, Umoja wa Ulaya, umiliki, utawala na ugavi wa madaraka, ardhi na usalama na dhamana...) (TRT Arabic, 20/01/2017).

Saba: Ama kuhusu suluhu inayotarajiwa ambayo Amerika na utawala wa Uturuki ulio tiifu kwake wanaitafuta: Inayoelekea zaidi ni kuwa katika sura ya dola ya shirikisho nchini Kupro kama hatua ya kwanza, ili dola hii kupitia Umoja wa Mataifa na kwa msaada wa Amerika iondoe kambi mbili za Uingereza huko Kupro. Hili ndilo lengo kuu la wimbi la mazungumzo ya Kupro yaliyoanza rasmi mwanzoni mwa mwaka huu. Suluhu hii inahitaji kufutwa kwa mataifa wadhamini: (Uingereza, Uturuki, na Ugiriki), jambo linalopelekea kuondoka kwa jeshi la Uturuki na wanajeshi wa Ugiriki, na bila shaka, na katika daraja la umuhimu zaidi, kambi mbili za Uingereza.

Lakini kuna baadhi ya vikwazo kwa suluhu hii, baadhi ni vikwazo halisi vyenye athari ambavyo si rahisi kuvishinda kwa muda mfupi... na vingine ni vikwazo vya pembeni vyenye athari ndogo vilivyokusudiwa kuhalalisha malengo fulani na hivyo vinaweza kushindwa...

  • Ama vikwazo vya msingi vyenye athari ni kujiondoa kwa Uingereza katika kambi zake mbili zilizopo kisiwani humo nazo ni (Akrotiri na Dhekelia). Kambi ya Akrotiri iko kusini magharibi mwa Kupro, wakati kambi ya Dhekelia iko mashariki mwa kisiwa hicho. Kambi hizi kwa Uingereza ni muhimu sana kwani ndizo kitovu cha shughuli zake, na haitaacha juhudi yoyote katika kukwamisha suluhu inayoweza kuizuia kubaki humo... Inaweza kujaribu kuahirisha au kuikwamisha kwa mbinu za ujanja kama vile kuweka sharti la kubaki katika kambi hizo ili kukubali suluhu ya Amerika. Bila shaka inatambua ugumu mkubwa wa Amerika kukubali hilo, hususan kwa kuwa Uingereza imepoteza nyenzo nyingi za ushawishi ndani ya Uturuki, na hivyo huko Kupro kufuatia operesheni za hivi karibuni za usafishaji alizofanya Erdogan jeshini na katika vyombo vingine vya dola.

  • Ama vikwazo vingine ni upande wa kisaikolojia wa kuondoa jeshi la Uturuki kutoka Kupro, kwa sababu suluhu ya Amerika inataka kuondoka huku kama hatua ya awali ya kuiaibisha Uingereza katika kuondoa kambi zake, kwa kigezo kwamba dola mpya ya Kupro haifai kuwa na vikosi vilivyotengwa na mwili wa dola. Hiyo ni kwa sababu kambi mbili za Uingereza huko Kupro, kwa upande wa kivitendo, ziko nje ya mamlaka ya dola ya Kupro, kiasi kwamba ripoti zilikuwa zikisema kuwa Kupro inaundwa na mikoa minne: (Kupro ya Kaskazini, eneo lisilo na upande katikati, Kupro ya Kusini, na kambi mbili za Uingereza). Uingereza kwa sasa inataka hali hii ya mvutano na mgawanyiko iendelee ili iwe kigezo cha kuendelea kwa kambi hizo. Kwa hiyo, kuunda dola moja nchini Kupro au shirikisho kama mradi wa suluhu wa Amerika ni hatua ya awali ya kuondoa kambi za kijeshi. Kutokana na hapa, matamshi kuhusu kufuta mataifa wadhamini na hivyo ushawishi wao ni matamshi yanayovutia katika mazungumzo ya mwanzoni mwa mwaka huu. Rais wa Kupro Nicos Anastasiades alitamka: "Ni lazima vikosi vya Uturuki viondoke Kupro ili kufikia suluhu itakayomaliza miongo ya mgawanyiko kisiwani humo. Anastasiades aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva kuwa 'lazima tukubaliane juu ya kuondoka kwa jeshi la Uturuki' lenye idadi ya wanajeshi wapatao 30,000 nchini Kupro." (BBC, 13/01/2017). Ama yaliyosemwa na Erdogan akimjibu baada ya swala ya Ijumaa, Januari 13: "Haifai kwa Ugiriki kutarajia suluhu ya suala la kisiwa hicho bila nafasi ya Uturuki kama nchi mthamini. Uturuki itabaki Kupro. Na uwezekano wa wanajeshi wa Uturuki kuondoka Kupro haupo kabisa..." (Russia Today, 13/01/2017). Msimamo huu wa Uturuki si msimamo wa kweli, bali ni katika mlango wa "kukataa ili kukubali"! Tamko lake la baadaye katika siku hiyo hiyo linabatilisha tamko lake la awali, kwani Reuters ilimnukuu siku hiyo hiyo akisema: "Erdogan alisema 'haiwezekani kuondoka kabisa kwa wanajeshi wa Uturuki na tayari tulishajadili hilo. Ikiwa jambo kama hilo linafanyiwa utafiti basi inapaswa pande zote mbili ziondoe wanajeshi wao kutoka huko'. Ugiriki ina kikosi chenye takriban wanajeshi 1,100 nchini Kupro. Erdogan anasema kuna mpango wa kubakisha wanajeshi 650 wa Kituruki na wanajeshi 950 wa Kigiriki kisiwani humo baada ya suluhu..." (13/01/2017). Kwa hiyo yeye anakubali kuondoka kwa mabadilishano haya yasiyo na usawa! Hilo linathibitishwa na maneno ya kiongozi wa Waturuki wa Kupro aliyenukuliwa na Reuters siku hiyo hiyo, yaani 13/01/2017: "Kiongozi wa Waturuki wa Kupro Mustafa Akinci alisema siku ya Ijumaa 'kwamba haipaswi kuwa na mada mwiko katika mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa ya kuunganisha Kupro'. Aliongeza, 'Ikiwa tutasema kwamba masuala haya ni mwiko na kwamba hatuwezi hata kuyajadili na kwamba kila kitu lazima kibaki kama kilivyo, basi hii pia haitapelekea mafanikio.'" Kwa hiyo, matamshi haya si ya kweli bali ni kwa ajili ya kutengeneza mazingira katika mazungumzo yanayoruhusu kujadili suala la kuondoka kwa nguvu za kijeshi kutoka kisiwani kama mlango wa kujadili suala la kambi mbili za kijeshi.

  • Muhtasari ni kwamba mazungumzo wakati huu ni ya umakini zaidi kuliko yaliyopita, na Amerika inataka kupitia mazungumzo hayo kupata hali ya shirikisho kisiwani humo itakayopelekea kuondoa kambi hizo kutoka mamlaka ya Uingereza... Ama Uingereza, inataka kuendelea kwa hali iliyopo ili ibaki inatawala kambi hizo na haidhuriwi na suluhu nyingine yoyote ikiwa itabaki inamiliki kambi hizo.

Nane: Ama suluhu sahihi ambayo Uislamu unaamrisha kwa tatizo la Kupro: Ni kwamba iunganishwe yote na Uturuki, kwani Kupro ni nchi ya Kiislamu, na ni lazima iunganishwe na asili yake ambayo ni Uturuki. Kisiwa cha Kupro ni kisiwa cha Kiislamu kilichofunguliwa na Waislamu katika zama za bwana wetu Othman, Khalifa Mwongofu wa tatu. Washambuliaji wa Msalaba wa Ulaya walikikalia kwa mabavu katika vita vyao vya msalaba vya kwanza walivyovianzisha dhidi ya nchi za Kiislamu, lakini Waislamu walikikomboa baadaye na kukirejesha katika asili yake kama nchi ya Waislamu. Kilikuwa chini ya utawala wa Dola ya Kiothmani kama nchi nyinginezo za Waislamu kwa sababu Khilafah ilihamia kwao. Waingereza walitangaza udhibiti wao rasmi juu yake katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutangaza kukimeza kuwa sehemu ya Uingereza; huo ni mchakato batili na uchokozi wa dhuluma usio na thamani wala uzito. Waislamu nchini Uturuki na kwingineko wanaichukulia Kupro kama sehemu ya ardhi yao inayopaswa kurejea kikamilifu katika ardhi ya Kiislamu... Hii ndiyo suluhu sahihi kwa Kupro, kwamba irejee katika asili yake kama nchi ya Kiislamu. Alifungua kisiwa hicho Gavana wa Sham, Muawiya bin Abi Sufyan, baada ya kupewa ruhusa na Khalifa Othman (ra) mwaka 28 Hijria, na ilikuwa miongoni mwa vita vya kwanza vya majini vya Waislamu. Walishiriki katika kuifungua kundi la Maswahaba wa Mtume (saw), miongoni mwao ni Abu Dharr, Ubada bin as-Samit akiwa na mke wake Umm Haram, Abu al-Darda na Shaddad bin Aws (ra). Hadi leo kaburi la Sahaba mtukufu Umm Haram ni miongoni mwa sehemu zinazozuriwa nchini Kupro. Kufunguliwa kwake kulikuwa ni pigo kubwa kwa Dola ya Byzantium na mfalme wake kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kulikuwa ni kuzinduliwa kwa enzi ya jeshi la majini la Kiislamu lililoimarika baada ya vita hivyo vya ushindi...

Hii ndiyo suluhu na hii ndiyo haki:

فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ فَأَنَّى تُصْرَفُونَ

"Basi kuna nini baada ya haki isipokuwa upotevu? Basi mnageuzwa wapi?" (QS. Yunus [10]: 32)

Na suluhu si ile inayopangwa na Amerika au Uingereza. Kwa maneno mengine, suluhu si Kupro kuwa na nchi mbili, iwe moja imeunganishwa na Uturuki na nyingine na Ugiriki au la, wala Kupro kuwa nchi ya shirikisho inayotawaliwa na Wagiriki, wala kuwa nchi moja inayotawaliwa na Wagiriki pia. Kwani nchi yoyote ya Kiislamu haifai kuachiwa makafiri wawe na mamlaka juu yake:

وَلَنْ يَجْعَلَ اللَّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا

"Wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini." (QS. An-Nisa [4]: 141)

Hakika Kupro itarejea, In Shaa Allah, kama ilivyokuwa nchi ya Kiislamu. Siku zinabadilika, na mikono mingi imepita juu ya Kupro, lakini mwisho mwema daima ni kwa wacha Mungu.

وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَى أَمْرِهِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

"Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika jambo Lake, lakini watu wengi hawajui." (QS. Yusuf [12]: 21)

24 Rabi' al-Thani 1438 H 22/01/2017 M

Share Article

Share this article with your network