Jibu la Swali
Maendeleo ya Kisiasa katika Uwanja wa Libya
Swali: Mnamo tarehe 4/11/2017, gazeti la Asharq Al-Awsat lilichapisha: (Kuhitimishwa kwa mikutano ya Cairo kwa makubaliano ya kuunganisha taasisi ya kijeshi ya Libya), na maafisa wa kijeshi wa Libya walikuwa wamekutana mjini Cairo mnamo tarehe 30/10/2017 chini ya tangazo la kupanga muundo wa jeshi la Libya. Ikumbukwe kwamba Ghassan Salamé, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, alianza kuongoza mazungumzo ya Libya na serikali ya Sarraj na baraza la wawakilishi huko Tobruk kuhusu ramani ya njia aliyoiandaa kwa ajili ya suluhu kuanzia tarehe 21/9/2017, lakini mazungumzo hayo yalisitishwa kabla ya kukamilisha mwezi mmoja kutokana na tatizo la Kifungu cha Nane katika makubaliano ya Skhirat yaliyotiwa saini tarehe 17 Disemba 2015. Swali ni: Je, kuanza kwa mikutano ya kijeshi kunamaanisha kuwa mikutano ya kisiasa imefeli? Kwa maneno mengine, je, mazungumzo ya kijeshi ni kwa ajili ya kupata suluhu ya kijeshi kwa Kifungu cha Nane baada ya kufeli kwa mazungumzo ya kisiasa? Kisha, ni nini kipya kilichojitokeza katika miaka hii miwili baada ya makubaliano ya Skhirat ambapo pande zote mbili zilitia saini wakati huo, na sasa wanatofautiana?! Ahsante.
Jibu: Hakuna jipya lililojitokeza, kwani pande zote mbili zilitia saini makubaliano ya Skhirat huku mbegu za hitilafu zikiwepo, lakini utiaji saini huo ulifanywa na kila upande kwa malengo tofauti na misukumo tofauti. Ili picha iwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:
1/ Katika enzi ya Qaddafi, tabaka la kisiasa lenye ushawishi lilikuwa likiungana na Uingereza, huku ushawishi wa Marekani ukiwa hauna nguvu katika enzi hiyo. Wakati enzi ya Qaddafi ilipoisha, tabaka la zamani la kisiasa lilipanda tena kwa sababu mizizi yake ilikuwepo na haikung'olewa. Kwa sababu hiyo, wanasiasa wengi walitawaliwa na ushawishi wa Uingereza, wakati wanasiasa wanaoiunga mkono Marekani walikuwa hawana uwepo wenye nguvu... Kwa sababu hiyo, Ulaya ilikuwa na shauku ya kufanya uchaguzi ili kupata serikali na baraza la wawakilishi haraka iwezekanavyo kwa sababu ilitarajia kuwa matokeo yangekuwa kwa faida yake kutokana na ushawishi wa tabaka la zamani la kisiasa... Marekani yenyewe ilikuwa na nia ya kukwamisha uchaguzi wowote hadi itengeneze tabaka jipya la kisiasa litakalosimama dhidi ya tabaka la kisiasa linaloiunga mkono Uingereza. Kwa maneno mengine, kile kilichoihusu Ulaya kilikuwa ni kuharakisha suluhu ya kisiasa, wakati kwa upande wa Marekani, ilichoijali ni kuchelewesha suluhu hadi itengeneze tabaka jipya la kisiasa, na hakuwa na chaguo la kutengeneza tabaka hili isipokuwa kupitia kiburi cha kijeshi kama ilivyo ada ya Marekani.
2/ Marekani ilimtuma ofisa wa Libya (Haftar) kufanya kazi nchini Libya kwa ajili ya kuhudumia maslahi yake, na historia ya maisha yake inazungumza wazi kuhusu utiifu wake kwa Marekani... Alitekwa nchini Chad yeye na takriban wanajeshi 300 wa Libya mnamo Machi 1987. Baada ya hapo, Marekani ilifanya upatanishi na Chad, na shirika la ujasusi la Marekani (CIA) lilifanya mazungumzo mnamo mwaka 1990 ili aachiwe huru. Ndege za Marekani zilimbeba Haftar na kundi lake hadi Zaire kisha hadi Marekani, ambapo walimpa hifadhi ya kisiasa nchini Marekani na akajiunga na harakati ya upinzani wa Libya nje ya nchi. Hivyo, Haftar alitumia miaka 20 iliyofuata katika jimbo la Virginia, Marekani, ambapo alipewa mafunzo ya vita vya msituni na shirika la ujasusi la CIA, na hakurejea Libya isipokuwa baada ya mapinduzi ya tarehe 17 Februari. Marekani ilimtuma Libya ili ajaribu kuanzisha nguvu ya kijeshi ili apate maeneo nchini Libya na kutengeneza tabaka jipya la kisiasa kupitia "ushindi" wa kijeshi, kwa kumfadhili kwa silaha na pesa moja kwa moja kupitia kwayo, au kupitia kibaraka wake Sisi nchini Misri... Marekani ilikuwa ikizuia suluhu yoyote ya kisiasa nchini Libya ikisubiri Haftar aweze kupata ushawishi wenye nguvu, na alikuwa akizingatia Mashariki kwa sababu Tripoli ilikuwa imejaa tabaka la kisiasa linaloiunga mkono Ulaya na hususan Uingereza. Alifanikiwa kwa kiasi fulani kuimarisha nguvu Mashariki mwa Libya na kutawala baraza la wawakilishi huko Tobruk.
3/ Mnamo mwaka 2015, Ulaya ilikuwa na shauku ya kutongojea zaidi ya mwaka huo ili kupata suluhu ya kisiasa kabla ya uhalisia wa tabaka la kisiasa kubadilika. Ulaya ilifanya jitihada kubwa katika kuelekeza nguvu zake kumpata mjumbe anayeiunga mkono Ulaya kwenda Libya ili kuharakisha hatua, na ilifanikiwa kumtuma Leon... Ikaanza kupigia debe suluhu ya kisiasa na ikaweza kutengeneza mazingira yenye shinikizo katika Baraza la Usalama, na wakati huo huo mazingira ya kuiaibisha Marekani ikiwa itakataa suluhu ya kisiasa... Kwa upande wa Marekani, ilitazama jambo hilo kwa mtazamo mwingine; iliona kuwa kupinga suluhu ya kisiasa baada ya kupigiwa debe huko hakukuwa kwa faida yake. Wakati huo huo, ikafanya mpango wake kuwa ni kukubali makubaliano ya Skhirat ili kuyadhibiti kwa kuyafanyia marekebisho au kuyaangamiza... Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwani Kifungu cha Nane katika makubaliano hayo kilihusiana na udhibiti wa nguvu za kijeshi... Kundi la Ulaya lilikuwa likitambua kuwa Haftar ni kibaraka wa Marekani, na kwamba Marekani inamtaka awe mkuu wa jeshi, kwa hivyo waliweka kifungu hiki kinachoeleza kuwa jeshi liko chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, kwani Sarraj anawaunga mkono wao... Kifungu hiki kikawa ni kizingiti kikubwa ambacho Marekani iliona kuwa ni fursa nzuri ya kukwamisha makubaliano hadi Haftar atakapofanikiwa kuwa na nguvu yenye ushawishi jeshini na ardhini, na kisha kupata tabaka la kisiasa lenye ushawishi linaloshindana na tabaka la kisiasa la Ulaya huko Tripoli na maeneo mengine...
4/ Huu ndio uhalisia wa sasa, na haujabadilika sana tangu makubaliano ya Skhirat mwishoni mwa mwaka 2015. Hakuna jipya lililojitokeza kwenye malengo ya pande mbili na misukumo yao ya kisiasa na kijeshi... Tulishatoa majibu ya maswali kuhusu mada ya Libya tangu makubaliano ya Skhirat, na tumeelezea jambo hili ndani yake kwa kila mwenye moyo au anayetega sikio naye amehudhurisha akili:
Ilikuja katika jibu la swali la tarehe 3/6/2014: (Marekani inatambua kuwa mazingira ya kisiasa nchini Libya ni zao la Uingereza likiwa na baadhi ya ushawishi wa Ufaransa unaoimarisha mazingira ya kisiasa yanayoiunga mkono Uingereza nchini Libya, jambo ambalo linamaanisha kuwa uchaguzi wowote ujao, washindi wake watakuwa ni watu wa Ulaya pamoja na idadi ndogo ya "watu wasiofungamana na upande wowote", na kisha hali itatulia na tamaa za Marekani zitatoweka, yenyewe ambayo ilikuwa inataka kutumia ushawishi wake wa kijeshi wa kihalisia katika kumaliza utawala wa Qaddafi ili sehemu yake ya ushawishi iwe kubwa na pana zaidi. Hilo haliwezi kuipatia Marekani kupitia kufanya uchaguzi katika mazingira haya ambayo bado ni ya Ulaya, kwa hivyo ilifikiria kuchanganya karata kijeshi na kupanga upya mazingira nchini Libya ili kuanzisha tabaka jipya la kisiasa linaloiunga mkono, kisha baada ya hapo kufanya uchaguzi. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kumteua mtu wa kijeshi ili achukue hatua inayofanana na mapinduzi dhidi ya hali iliyopo inayotawaliwa na Bunge la Kitaifa (General National Congress) ambapo wengi ndani yake ni watu wa Ulaya... Hiyo ni ili kuchanganya karata na kuahirisha uchaguzi hadi mazingira yatakapokuwa bora kwa Marekani. Ikiwa mazingira hayatakuwa mikononi mwake pekee, basi yawe ni kwa kushirikiana na Ulaya, ili uwanja usibaki kwa Ulaya pekee. Hivyo, Haftar alichukua hatua na historia ya maisha yake inazungumza wazi kuhusu utiifu wake kwa Marekani...).
Ilikuja katika jibu la swali la tarehe 11/4/2015: (Ulaya inatambua jambo hili kuwa Marekani inafanya kazi ya kufelisha mazungumzo, na kwa sababu hiyo imemteua mjumbe anayeaminika kwake naye ni Bernardino Leon, ambaye asili yake ni mjumbe wa Ulaya... Bernardino Leon alianza kuhimiza hatua ili afikie suluhu ya kisiasa na jambo lililomshughulisha ni kukamilisha kazi yake katika kipindi chake cha kwanza cha utume kilichopangwa kuisha mwishoni mwa Machi 2015, kabla ya kuongezewa muda kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama namba 2213, hadi tarehe 15 Septemba 2015. Alikuwa na haraka ya kuikamilisha katika kipindi cha kwanza, na "mazungumzo" yalianza Geneva kisha yakahamia Libya na kisha Morocco na Algeria na kisha yakarejea kufanyika Morocco. Katika duru ya mazungumzo ya Morocco siku ya Alhamisi tarehe 12/3/2015, wanachama wa bunge la Tobruk waliomba kuahirishwa kwa kurejelewa kwa mazungumzo ya kisiasa kati ya pande za Libya kwa wiki nyingine, yaani hadi Alhamisi tarehe 19/3/2015 kwa ajili ya mashauriano zaidi... Leon alisisitiza umuhimu wa kutoka na suluhu ya kisiasa haraka iwezekanavyo... Vilevile, mnamo tarehe 16/3/2015, taarifa ya pamoja ilitolewa na Umoja wa Ulaya ikionya dhidi ya kufeli kwa mazungumzo ikisema: "Kufeli kufikia makubaliano ya kisiasa kutahatarisha umoja wa Libya.. Pindi tu makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na mipango husika ya kiusalama yatakapofikiwa, Umoja wa Ulaya utakuwa tayari kuimarisha msaada wake kwa Libya" (Shirika la Habari la Ujerumani 16/3/2015)...).
Na ilikuja katika jibu la swali la tarehe 19/1/2016: (Uingereza ilikuwa ikitambua kuwa mazingira ya kisiasa au mengi yake yako upande wake, kwa hivyo ilikuwa na utulivu kuwa serikali yoyote ya mpito kulingana na mapendekezo ya Leon itakuwa upande wake. Kwa hivyo, ilikuwa na nia ya kuharakisha makubaliano ya Skhirat na kuidhinishwa kwake katika enzi ya Leon. Wakati haikuweza na Kobler akaja, na kukawa na marekebisho, Uingereza ilitambua kuwa marekebisho haya yalikuwa ni shinikizo la Marekani kwa Kobler kama hatua miongoni mwa hatua nyingine za Marekani za kufelisha makubaliano kikamilifu hadi Marekani iyatengeneze upya kama inavyotaka, na hilo ni baada ya kutengeneza tabaka jipya la kisiasa kutokana na harakati za kijeshi zinazofanywa na Haftar sambamba na njama za kisiasa zinazoendeshwa na Marekani. Kwa hiyo, Uingereza iliona umuhimu wa kuharakisha kufunga makubaliano kabla ya kutokea mambo mengine yasiyotarajiwa, kwani makubaliano hata yakiwa na marekebisho ya "Kobler" bado yanakubalika kwake. Hivyo, iliharakisha mambo, ikajihimiza kufanya makubaliano ya mwisho huko Skhirat, Morocco mnamo tarehe 17/12/2015. Na ili kuyafanya hayo kuwa halali na yenye kukubalika kimataifa, ilikimbilia Baraza la Usalama na kuwasilisha mswada wa azimio namba 2259 kwa ajili ya kuunga mkono maamuzi ya makubaliano ya mwisho... Kile kilichopelekea Uingereza kuharakisha ni harakati za Marekani za kukwamisha makubaliano... Na hilo liliashiriwa na mshauri wa zamani wa rais wa baraza la wawakilishi la Libya, Issa Abdel Qayyum mnamo tarehe 13/12/2015 kupitia televisheni ya Al-Ghad Al-Araby aliposema: (... kauli za Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, zilifafanua kuwa Wamarekani hawana hamasa ya kutosha ya kutatua mgogoro kinyume na Waingereza na Wafaransa ambao walionyesha hamasa ya hilo...).
Na ilikuja katika jibu la swali la tarehe 12/3/2016: (Ama sababu ya ukwamishaji huu "wa Marekani" ni kwamba wanasiasa wengi nchini Libya ni masalia ya Qaddafi, yaani watiifu kwa Ulaya... Na muundo wowote wa wizara utakuwa wa aina hiyo kama ilivyo katika wizara mpya. Marekani inamtegemea Haftar na kundi la wanajeshi wanaomzunguka... Na kwa ajili hiyo, Marekani inakwamisha suluhu ya kisiasa kwa kiasi kikubwa iwezavyo kwa kuingilia kijeshi yenyewe, na kupitia Haftar, na wafuasi wake, hadi itakapoweza kuhakikisha utawala ambao itakuwa na sehemu kubwa ndani yake... Hii ni kinyume na Ulaya, yenyewe inafanya kazi ya kufanikisha makubaliano na kuunda serikali na kuidhinisha kwa sababu bado inadhibiti mazingira ya kisiasa na ushahidi wa hilo ni mwingi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Philip Hammond alifanya ziara nchini Algeria na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Ramtane Lamamra mnamo tarehe 19/2/2016 na kusisitiza huko kuwa "kuingilia kijeshi nchini Libya hakuwakilishi suluhu mwafaka ya kutatua mgogoro unaoshuhudiwa nchini humo na alitoa wito wa suluhu ya kisiasa", Al-Khabar ya Algeria 19/2/2016).
5/ Kwa hivyo, mambo yalikuwa wazi kwa kila mwenye macho tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya Skhirat mnamo mwezi wa 12/2015, bali hata kabla ya hapo, kwamba Ulaya ilikuwa ikiharakisha suluhu kwa sababu tabaka la kisiasa lililopo ni mtiifu kwake, na Marekani ilikuwa ikikwamisha suluhu hadi itakapoweza kupata mamlaka ya kijeshi kupitia chombo chake, Haftar, na kisha kutengeneza mamlaka mpya ya kisiasa... Kwa ajili hiyo, mazungumzo yalikuwa yakisuasua mahali pale pale, mara yakikaribia kisha yakatofautiana, na hivi ndivyo ilivyoendelea. Baada ya chini ya mwezi mmoja tangu kuanza kwake, kukatokea kujiondoa kwa ujumbe wa Tobruk, kisha yakasitishwa... Salamé alikuwa akikutana na huyu na yule, akitoa mapendekezo hapa na pale, na kuhalalisha kujiondoa kwao na kurejea kwao kutoka Tunisia kwenda Libya kwa ajili ya kushauriana na viongozi wao... Na labda anajua kuwa makubaliano ya pande mbili juu ya suluhu ya mwisho yanahitaji ridhaa ya nguvu za kimataifa zilizoko nyuma yao, na hili Ghassan Salamé hamiliki, na hata pande mbili hawamiliki isipokuwa wale walioko nyuma yao wakubaliane. Hivyo ndivyo kujiondoa, kusitisha na kurejea kutoka Tunisia kwenda Libya kulivyofanyika kwa kisingizio cha kushauriana na viongozi wao:
- (Mwandishi wa Al-Jazeera amesema kuwa ujumbe wa baraza la wawakilishi la Libya ulijiondoa kwenye mazungumzo na Baraza Kuu la Dola bila kufichua sababu za hilo, baada ya duru mbili za mazungumzo mjini Tunisia kwa ajili ya kurekebisha makubaliano ya Skhirat... Lakini mwandishi aliripoti kuwa sababu zinaweza kuhusiana na uandishi wa Kifungu cha Nane ambacho kilijadiliwa katika kikao cha kelele asubuhi ya leo ambapo mada ya Baraza la Urais na serikali ilijadiliwa. Al-Jazeera... 16/10/2017)... Na (Chanzo kimeiambia Al-Jazeera kuwa mkutano unafanyika katika makao makuu ya utume wa Umoja wa Mataifa mjini Tunisia kati ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé na wakuu wa ujumbe wa mazungumzo Moussa Faraj na Abdulsalam Nassia ili kutathmini kile kilichotokea jana Jumatatu cha kusitishwa kwa vikao kati ya wajumbe wawili... Al-Jazeera 17/10/2017)... Na (Mwandishi wa Al-Jazeera mjini Tunisia aliripoti kuwa utume wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulikabidhi pande mbili za mazungumzo za Libya karatasi iliyojumuisha uandishi wa vipengele vya makubaliano na hitilafu kati yao ili kuzisoma katika mikutano yao wakati wa mchana wa leo na kutoa maoni yao juu yake, kila mmoja peke yake. Al-Jazeera 18/10/2018)... (Na wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Salamé mjini Tunisia Jumamosi 21/10/2017, aliashiria kuwa kuna maeneo ya maelewano na makubaliano kati ya wajumbe wa baraza la dola na wawakilishi wa Libya wanaozungumza mjini Tunisia, jambo ambalo linapelekea kurejea kwao Libya Jumapili ili kushauriana na viongozi wa kisiasa huko, akibainisha uwepo wa vipengele vya hitilafu miongoni mwavyo ni Kifungu cha Nane ambacho utume wa Umoja wa Mataifa utajaribu kuviondoa. Al-Jazeera 24/10/2017).
6/ Kwa sababu hiyo, Haftar alikuwa akizingatia harakati za kijeshi, na hilo halikuwa siri, bali harakati za kijeshi za Haftar na kauli zake wakati wa mazungumzo ya Baraza la Urais na bunge la Tobruk chini ya usimamizi wa Ghassan Salamé yaliyoanza tarehe 21/9/2017, alikuwa akizingatia harakati za kijeshi, na kauli zake wakati huu zilikuwa zikitilia shaka ufanisi wa mazungumzo. Al-Jazeera ilichapisha tarehe 14/10/2017: (Meja Jenerali mstaafu Khalifa Haftar ametilia shaka uwezekano wa kutatua mgogoro wa Libya kulingana na mkondo wa mazungumzo unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa... Haftar amesema katika hotuba kwenye mkutano wa kwanza wa usalama katika mji wa Benghazi kuwa hakuna viashiria vinavyoihakikishia umma kuwa mazungumzo yanayoendelea ndiyo suluhu pekee ya mgogoro wa kisiasa wa sasa. Haftar alitishia mbadala mwingine wa mazungumzo ya kisiasa, miongoni mwayo ni jeshi na vyombo vyote vya usalama, "ambavyo vitatii matakwa ya umma"), na Haftar alikuwa ametoa kauli katikati ya Agosti 2017: "Tumedhamiria kuendeleza mapambano hadi jeshi lieneze udhibiti wake katika ardhi yote ya Libya..." (Asharq Al-Awsat 15/8/2017).
Kwa ajili hiyo, msisitizo wa Marekani kwenye suluhu ya kijeshi ili iongoze suluhu ya kisiasa ni jambo lililoko katika kiini cha kazi zake nchini Libya. Inakwamisha suluhu ya kisiasa hadi Haftar atakapoweza kuongeza eneo lake la udhibiti wa kijeshi na kisha suluhu ifanyike kwa ushawishi wa Marekani ulio na nguvu zaidi kuliko ushawishi wa Ulaya. Yaani Marekani inazingatia suluhu ya kijeshi ili iongoze suluhu ya kisiasa, na inatumia kila fursa inayofaa kwa jambo hili... Kwa hiyo, ilipopata fursa inayofaa ya kufanya mkutano wa kijeshi mjini Cairo ili kuhakikisha ushawishi wa kihalisia wa Haftar jeshini, ilimwamuru Haftar kufanya hivyo tarehe 30/10/2017 kukawa na mkutano wa makundi ya kijeshi ya Libya mjini Cairo, na yote hayo yanamuunga mkono Haftar au hayampingi... Kisha mkutano ukahitimishwa jioni ya tarehe 2/11/2017: (Asharq Al-Awsat imebaini kuwa duru ya tatu ya mazungumzo ya kuunganisha taasisi ya kijeshi ya Libya yaliyofanyika mjini Cairo kati ya maafisa wa Libya na ambayo yalimaliza kazi zake jioni ya juzi, yamefikia vipengele vya makubaliano ya karibu ya mwisho kuhusu kuunganisha jeshi la Libya na uhusiano wake na mamlaka ya kiraia nchini Libya ambayo inakumbwa na machafuko ya kijeshi na usalama tangu mwaka 2011... Asharq Al-Awsat 4 Novemba 2017). Katika hili kuna dalili kuwa Marekani na vyombo vyake, Misri na Haftar, wamepiga hatua kwa kiasi fulani ambapo Haftar amekuwa ni mhusika mwenye uzito mwenye udhibiti katika sehemu kubwa ya ardhi, hususan Mashariki na kwenye eneo la mafuta (Oil Crescent), mkabala na kusuasua kwa faida za Ulaya (Uingereza na kiasi fulani Ufaransa na Italia). Pamoja na hayo, hii haina maana kuwa mzozo umeisha, kwani Ulaya pia ina nguvu zake nchini Libya mbali na kuwa ni wajanja zaidi katika harakati za kisiasa kuliko Marekani... Hivyo, kinachotarajiwa ni kuendelea kwa mzozo wa kimataifa kuhusu Libya kati ya Marekani na vyombo vyake, na kati ya Ulaya na vyombo vyake... Na wanapata maumivu ya mzozo huu ni Walibyaenyewe...!
7/ Na ni vyema kutaja kuwa masuala ya Waislamu yanatatuliwa na mikono ya Waislamu na si kwa mikono ya maadui zao, na suluhu ni rahisi na nyepesi kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfanyia wepesi. Silaha yake ni ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu kwa siri na dhahiri, na ukweli kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika kauli na kitendo. Hapo ndipo wazungumzaji wataona kuwa wako mbele ya nchi kongwe ya Kiislamu tangu ufunguzi wa Kiislamu katika enzi ya Khalifah Rashid Umar bin Al-Khattab (ra), na watu wake wote ni Waislamu, na suluhu ya masuala yake iko katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) na Sunnah za Mtume wake (saw), bila ya uhusiano wowote na makafiri wakoloni.
وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تَنْصَرُونَ
"Wala msiwategemee wale walio dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, kisha hamtanusuriwa." (Hud [11]: 113)
Na kwa kuhitimisha, tunakariri kile tulichokisema huko nyuma: Ni jambo la kuumiza kwamba nchi za Kiislamu ambazo zilikuwa chimbuko la ufunguzi na uenezaji wa Uislamu unaobeba uadilifu na kheri kwa pembe za dunia... nchi hizi zimekuwa uwanja wa vita ambapo wakoloni makafiri wanashindana kutuua na kupora utajiri wetu... wanacheka kwa vinywa vyao vyote kwa kila tone la damu linalotiririka kutoka kwetu, si kwa mikono yao tu, bali pia kwa mikono ya vibaraka wao miongoni mwa watu wetu!
Hakika wakoloni makafiri ni maadui zetu kwa hivyo si ajabu wakijitahidi kutuua, lakini kujiunga nao kwa makundi ya Libya, baadhi yao wakiiunga mkono Marekani, na wengine wakiiunga mkono Ulaya, kisha wanauana wao kwa wao, vita ambavyo si kwa ajili ya Uislamu na kuitukuza neno la Mwenyezi Mungu, bali kwa ajili ya maslahi ya wakoloni makafiri... hakika hilo ni miongoni mwa makosa makubwa. Kwani kuuawa kwa Waislamu wao kwa wao ni jinai kubwa katika Uislamu. Mtume (saw) amesema:
كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حَرَامٌ، دَمُهُ، وَمَالُهُ، وَعِرْضُهُ
"Kila Mwislamu juu ya Mwislamu mwenzake ni haramu: damu yake, mali yake, na heshima yake." (Imepokewa na Muslim kutoka kwa Abu Hurairah)
Na Mtume (saw) amesema:
لَزَوَالُ الدُّنْيَا أَهْوَنُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ قَتْلِ رَجُلٍ مُسْلِمٍ
"Kuondoka (kuangamia) kwa dunia ni jambo jepesi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kuuawa kwa mtu Mwislamu." (Imepokewa na An-Nasa'i kutoka kwa Abdullah bin Amr)
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ ألقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ
"Hakika katika hayo kuna ukumbusho kwa mwenye moyo (wa kuzingatia) au anayetega sikio naye amehudhurisha akili." (Qaf [50]: 37)