Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI KUHUSU SABABU YA UHABA

November 01, 2010
3108

Jibu la Swali

Kuhusu Sababu ya Uhaba

Swali:

Imetajwa katika kitabu cha An-Nizam al-Iqtisadi ukurasa wa (33) kwamba thamani ya bidhaa ni: (kiwango cha manufaa yaliyomo ndani yake huku ikizingatiwa sababu ya uhaba), na imetajwa katika ukurasa wa (34) kwa ufafanuzi zaidi ikisema: (Ama thamani, kinachotawala katika ukadiriaji wake ni kiwango cha manufaa yaliyomo ndani ya bidhaa wakati wa ukadiriaji huku ikizingatiwa sababu ya uhaba bila kuifanya kuwa sehemu katika ukadiriaji). Ikiwa sababu ya uhaba haiingii katika ukadiriaji, basi kwa nini tunaiingiza katika ufafanuzi? Na nini faida ya kuizingatia? Tunaomba ufafanuzi wa jambo hilo, na Mwenyezi Mungu awalipe heri.

Jibu:

Hakika ufafanuzi wa thamani kuwa ni kiwango cha manufaa yaliyomo ndani ya bidhaa huku ikizingatiwa sababu ya uhaba, ni sahihi. Na kutokuichukulia sababu ya uhaba kama sehemu katika ukadiriaji pia ni sahihi. Ama kuhusu kwa nini imetajwa, basi huu hapa ni ufafanuzi wake:

Hakika mzingatio wa sababu ya uhaba si sehemu ya ukadiriaji, bali ni kwa ajili ya umakini, utunzaji na uhifadhi wa thamani hiyo. Kwa mfano, ikiwa ungekuwa na mkate mmoja na ukakadiria thamani yake kutokana na manufaa yaliyomo ndani yake: viambato vyake, sifa zake, matumizi yake... na kisha kupatikana kwake kukawa ni haba (nadra), basi utakuwa makini nao na unaweza kula robo yake asubuhi na robo nyingine jioni, na hivyo hivyo katika siku ya pili. Na ikiwa kipande kidogo kitakuanguka, utafanya haraka kukiokota... lakini ikiwa ungekuwa na mikate mingine mingi kama huo, licha ya kwamba manufaa ya asili yaliyomo ndani yake ni yale yale – yaani thamani yake ni ile ile – lakini hutokuwa na umakini wala kuutunza kama utunzaji wako kwa ule wa kwanza, bali unaweza usiokote hata kipande kikianguka, na unaweza kuula wote na mingine kama huo katika siku yako hiyo.

Kwa sababu hiyo, kitabu kimeongeza katika (mzingatio wa sababu ya uhaba) wakati wa kuelezea, maneno (katika wakati huo), ambapo kilisema mwishoni mwa uk. 33: (Kwa sababu thamani ya bidhaa hukadiriwa kwa kiwango cha manufaa yaliyomo ndani yake wakati wa ukadiriaji huku ikizingatiwa sababu ya uhaba katika wakati huo). Yaani wakati unaoambatana na thamani wakati wa kuikadiria na kadhalika. Maana yake ni kwamba thamani ni manufaa yaliyomo ndani ya kitu huku ikizingatiwa sababu ya uhaba kwa ajili ya sababu nyingine isiyo ya ukadiriaji wa thamani, bali ni kwa ajili ya kuhifadhi thamani hiyo na kuitunza kwa sababu ya ugumu wa kupata mfano wake ikiwa itapotea kwa sababu ya uhaba wake. Mzingatio huu ni muhimu ili kutofuja thamani bali kuzitumia kwa kiasi, hii ni mbali na ukweli kwamba mzingatio wa sababu ya uhaba unasaidia katika kulinganisha kati ya uthabiti wa thamani na mabadiliko ya bei kupanda na kushuka kulingana na sababu ya uhaba.

Share Article

Share this article with your network