Swali:
(Imenukuliwa katika kitabu cha Mafahim Siyasiyyah cha Hizb ut Tahrir) ukurasa wa 54 chini ya anuani "Sababu za Mapambano kati ya Mataifa" kile kinachosema: "Mapambano ya kimataifa tangu kuanza kwa historia hayajawahi kutoka nje ya moja ya sababu mbili: Ama kupenda utawala na fahari, au kukimbilia manufaa ya kimaada. Na kupenda utawala: Ama ni kupenda utawala wa umma na watu kama ilivyokuwa kwa Ujerumani ya Kinazi na Italia ya Kifashisti, au ni kupenda utawala wa Itikadi (Mabda') na uenezaji wake kama ilivyokuwa kwa Dola ya Kiislamu kwa kipindi cha takriban miaka elfu moja na mia tatu, na kama ilivyokuwa kwa dola ya Kikomunisti kwa kipindi cha miaka thelathini ya umri wake, kabla ya kusambaratika mwanzoni mwa miaka ya tisini ya karne iliyopita, baada ya miaka sabini tangu kuasisiwa kwake."
Tunajua kwamba mapambano ya Dola ya Kiislamu na mataifa mengine hayaji kutokana na kupenda utawala wa Itikadi kwa sababu kupenda utawala ni mojawapo ya dhihirisho la silika ya kujihami (gharizat al-baqa'), na kueneza mfumo wa Uislamu na kuupenda kwetu hakuji kutokana na silika ya kujihami, bali kunakuja kupitia amri na makatazo ya Allah yaani kunafungamana na silika ya kidini (gharizat al-tadayyun). Hivyo basi, kwa nini tulisema ni kwa sababu ya silika ya kujihami badala ya kuwa kwa sababu ya silika ya kidini kwani mapambano ya kimataifa kwa upande wa Dola ya Kiislamu ni kwa ajili ya kueneza Uislamu? Ninaomba ufafanuzi wa jambo hili lililoelezwa katika Mafahim, na Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
Inaonekana kuwa mwenye kuuliza swali ametatizika kuhusu dhihirisho la silika akidhani kuwa linaasibishwa kwa dola, na kwa sababu hiyo amedhani kuwa sentensi "kupenda utawala wa Itikadi..." ni sentensi inayoashiria dhihirisho la silika ya kujihami.
Kuchanganyikiwa huku kutaondoka kwake ikiwa atatambua kuwa dhihirisho la silika limefungamana na watu binafsi na si kwa mataifa. Tukisema mtu huyu anapenda utawala, basi hapa utawala ni dhihirisho la silika ya kujihami, na kauli yetu kuwa mtu anapambana na wengine kwa ajili ya kupenda utawala ina maana kuwa ni kwa ajili ya kutosheleza dhihirisho la silika ya kujihami... Na kwa ajili hiyo, haijuzu kusema kuwa mtu huyu anapigana jihadi kwa ajili ya kupenda utawala au kwamba kupenda utawala ndio msukumo wake wa jihadi, bali msukumo wake lazima uwe ni kumtii Mwenyezi Mungu (swt) na kutekeleza amri Yake... Lakini jambo hili haliihusu dola, hivyo haisemwi kuwa dola ina silika ya kidini, silika ya kujihami, au silika ya aina (gharizat al-naw') ambayo dola inataka kuitosheleza!
Huenda tatizo hili likaisha ikiwa muulizaji atajiuliza kuhusu silika ya aina na dhihirisho lake, kwani bila shaka itambainikia kuwa hawezi kusema kwamba dola ina silika ya aina ya kutosheleza! Na hivyo ndivyo ilivyo katika kila silika kwani imefungamana na watu binafsi.
Ikiwa hili limekuwa wazi kwa muulizaji, basi swali lake tayari limebeba jibu lake, kwa sababu iliyoelezwa katika kitabu ni:
"Mapambano ya kimataifa tangu kuanza kwa historia mpaka kusimama kwa Saa (Qiyama) hayatoki nje ya moja ya sababu mbili: Ama kupenda utawala na fahari, au kukimbilia manufaa ya kimaada. Na kupenda utawala: Ama ni kupenda utawala wa umma na watu... au ni kupenda utawala wa Itikadi na uenezaji wake kama ilivyokuwa kwa Dola ya Kiislamu..." Mwisho.
Na hii ina maana kwamba mapambano ya kimataifa kwa upande wa Dola ya Kiislamu ni kupenda utawala wa Itikadi ya Kiislamu, yaani utekelezaji wa hukmu ya kisheria juu ya utawala wa Itikadi kwa kuwa na dola inayotekeleza Uislamu na kuueneza. Na hapa haisemwi kuwa hili ni dhihirisho la silika ya kidini ya dola, wala dhihirisho la silika ya kujihami ya dola, bali ni hukmu ya kisheria ambayo ni lazima kwa dola kuitekeleza, kwa sababu dola haina silika bali silika ni za watu binafsi.