(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook)
Kwa Dede Tahboub
Swali:
Assalamu Alaikum,
Nina maoni kuhusu moja ya kurasa za kitabu cha Hizb ut-Tahrir ambacho kinatambulisha Chama, kilichoandikwa tarehe 9/5/1985. Katika ukurasa wa 20, nakuta kuwa njia ya Chama ya kujielezea inakifanya kijikurubishe na hadhi ya Uungu, na labda hili ndilo lililokuwa sababu ya kuchelewa kwa nusura yetu mpaka sasa. Kinsema katika kitabu hicho: "Na kimeepuka (kimevirekebisha) mapungufu yote na sababu zilizopelekea kufeli kwa makundi (takatul) yaliyoanzishwa ili kuwainua Waislamu kwa Uislamu." Hapa kinajiondolea sifa ya kukosea, na hii ni miongoni mwa sifa za Mola wa walimwengu, kwani kila kiumbe hukosea. Lakini lau kingesema haya na kisha kikaongeza "kwa idhini ya Mwenyezi Mungu," labda hili lingekuwa sababu ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwetu. Pia kinasema: "Bali ni wajibu kwa Ummah kukikumbatia na kutembea nacho kwa sababu ndicho Chama cha pekee kilichomeza (kuelewa kwa kina) fikra yake..." Sifa ya upekee (al-wahdaniyyah), ingawa ilihusishwa na sifa fulani, naona kuwa ni maalum kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu; kwani hakuna kiumbe aliye pekee kuliko wengine kwa sifa yoyote ile isipokuwa ile ambayo Mwenyezi Mungu (swt) ameihusisha kwa muujiza. Kwa hiyo, naona kuwa neno "cha pekee" lina kosa fulani, na labda ni kosa kubwa lililochelewesha nusura ya Mwenyezi Mungu kwetu.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Inaonekana kuna mkanganyiko uliokupata katika maana ya ibara iliyotajwa. Kilichotajwa ni: "Na kimeepuka mapungufu yote na sababu zilizopelekea kufeli kwa makundi (takatul) yaliyoanzishwa ili kuwainua Waislamu kwa Uislamu." (At-Ta'rif)
Chama kilitaja hayo katika utambulisho (At-Ta'rif) baada ya kuwa kimeainisha sababu za kufeli kwa harakati katika kitabu cha At-Takatul (Mshikamano), ambapo kilisema:
"Mwenye kufuatilia majaribio haya, na mtafiti wa harakati hizi, anaona kuwa sababu kuu ya kufeli kwazo zote, inarudi upande wa kimshikamano (takatul) katika mambo manne:
La kwanza: Zilikuwa zikisimama juu ya fikra ya jumla isiyobainishwa vizuri, hata ikawa ni yenye utata au nusu utata, mbali na kuwa ilikosa uwazi na usafi.
La pili: Zilikuwa hazijui njia (tariqah) ya kutekeleza fikra yake, bali fikra hiyo ilikuwa ikifuata njia za kubahatisha na zenye kupinda, mbali na kuwa iligubikwa na utata na kutoeleweka.
La tatu: Zilikuwa zikitegemea watu ambao ufahamu (wai) sahihi haujakamilika kwao, na matakwa sahihi hayajajikita kwao, bali walikuwa ni watu wenye hamu na msisimko pekee.
La nne: Kwamba watu hawa ambao walikuwa wamebeba mzigo wa harakati hawakuwa na mafungamano sahihi baina yao isipokuwa mshikamano tu unaochukua sura za vitendo na maneno mbalimbali ya majina." (At-Takatul).
Kisha Chama kilifanya juhudi (ijtihad) na kuepuka (kurekebisha) sababu hizo. Sasa, kuna kosa gani katika kauli yake: "Na kimeepuka mapungufu yote na sababu"? Na kuna uhusiano gani wa hayo na ukweli kwamba kila kiumbe hukosea? Na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye aliyetakasika na kila upungufu? Sasa nakuuliza: Ikiwa wewe ni mwalimu wa shule, ukamwambia mwanafunzi wako baada ya kuangalia jibu lake: "Kuna mapungufu katika jibu lako kadha wa kadha," na ukamainishia mapungufu hayo 1, 2, 3... n.k., kisha ukamwambia: "Nenda kayakamilshe." Mwanafunzi akaenda na kuyarekebisha mapungufu hayo, kisha akakurudia akisema: "Nimeepuka (nimeyarekebisha) mapungufu yote uliyoyataja kwangu, ewe mwalimu mtukufu, na hili ndilo jibu langu upya." Je, mwanafunzi huyo atakuwa amejisifu kwa sifa za Mola wa walimwengu? Je...?
Ama kuhusu maoni yako mengine, unasema: "Bali ni wajibu kwa Ummah kukikumbatia na kutembea nacho kwa sababu ndicho Chama cha pekee kilichomeza fikra yake...", nami nitakunukulia kipengele kabla ya maneno haya kisha kipengele ulichonukulia swali lako. Kilichotajwa ni hiki:
"Kikafahamu fikra na njia kwa ufahamu wa kifikra makini kutokana na yale yaliyoteremshwa kwa wahyi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume wake, na yale yaliyoashiriwa na ijma' as-Sahaba na qiyas. Hakikufanya uhalisia kuwa chanzo cha fikra yake, bali ni sehemu ya kuifanyia fikra ili kuubadilisha kulingana na hukumu za Uislamu. Na kikalazimiana na njia ya Mtume (saw) katika mwenendo wake wa kubeba Da'wah na kwenda nayo kule Makka mpaka akasimamisha Dola kule Madina, na kikafanya fungamano linalounganisha kati ya watu wake kuwa ni itikadi (aqidah) na yale kilichoyatabani katika fikra za Kiislamu na hukumu zake.
Na kwa ajili hiyo, kilistahiki kukumbatiwa na Ummah, na kutembea nacho, bali ni wajibu kwake (Ummah) kukikumbatia na kutembea nacho kwa sababu ndicho Chama cha pekee kilichomeza fikra yake, chenye kuiona njia yake, chenye kuelewa kadhia yake, chenye kulazimiana na kufuata nyayo za mwenendo wa Mtume (saw) bila kupinda, na bila kurudishwa nyuma na yeyote katika kufikia lengo lake." (At-Ta'rif).
Wewe unatoa maoni yako juu ya kauli "kwa sababu ndicho Chama cha pekee kilichomeza fikra yake, chenye kuiona njia yake...", unatoa maoni kwa kusema: "Upekee" (al-wahdaniyyah) ni miongoni mwa sifa za Muumba (swt).
Mada hapa ni tofauti, ewe dada yangu mpendwa. Chama hakisemi kuwa chenyewe ni cha pekee katika kila kitu, bali chenyewe kimeistimbati fikra na njia istimbati sahihi kwa dalili za kisheria kulingana na misingi (usul). Hivyo basi, kimaumbile itakuwa chenyewe ndicho kilichomeza (kuelewa kikamilifu) fikra hii kilichoiistimbati. Na maneno haya si kuhusu mtu, bali ni kuhusu Chama kinachotabani fikra hii na njia hii. Hivyo basi, kila aliyemeza fikra hii na njia hii, basi yeye ni miongoni mwa Chama na sifa hiyo inamsadiki. Kwa hiyo, inasadiki kwa Chama kilichoistimbati njia yake na fikra yake kwa kusema kuwa ndicho cha pekee kilichomeza fikra hiyo; kwani chenyewe ndicho kilichoistimbati, kikaisoma, kikafanya kazi kwayo na kikapambana kwa ajili yake. Sasa kuna ubaya gani kusema kuwa ndicho cha pekee kilichomeza fikra hii? Na kuna uhusiano gani wa kauli hii na Upekee wa Mwenyezi Mungu (swt) ambaye ni Mmoja (al-Ahad), Mtegemewa (as-Samad), ambaye hakuna chochote kinachofanana naye?
Namuomba Mwenyezi Mungu (swt) akuongoze katika amri iliyoongoka zaidi, na akufungue kifua chako kwa yale yaliyo kheri, na Mwenyezi Mungu (swt) ndiye Mwongozi wa njia iliyonyooka.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus