Swali: Ni nini kinachokusudiwa na sentensi iliyoko mwishoni mwa Ibara (10): (... na ni wajibu wa Dola kuzuia kila kitu kinachoashiria kuwepo kwao miongoni mwa Waislamu). Je, hii inamaanisha kuwa itatolewa amri ya kuwazuia Mashuikh na Maimamu wa misikiti kuvaa mavazi rasmi (Kofia ya Tarboosh, Kilemba na Juba)?
Jawabu: Sivyo hivyo. Kile ambacho Dola itakiondosha ni dhana ya viongozi wa kidini (clergy) iliyopo kwa Wakristo. Kwani wao wana mavazi maalum (ya viongozi wa kidini) yanayowafanya wawe na mamlaka ya pekee ya kuhalalisha na kuharamisha kuliko wengine. Kisha ikatokea dhana inayofungamana na hilo baada ya kuchomoza kwa Ubepari, kwamba mamlaka ya kiroho yawe yameganda kwa "viongozi wa kidini" kupitia mavazi yao maalum yaliyohodhiwa na wao pekee, na mamlaka ya kiserikali yawe kwa watu wa kidunia (viongozi wa dola). Kwa hivyo, hairuhusiwi kwa kiongozi wa serikali kwao kuvaa mavazi ya "viongozi wa kidini" kwa mujibu wa msingi wa Kibepari. Yaani, kuna utenganishaji wa dini na dola unaofungamana na Ubepari kwao.
Sisi katika Uislamu hatuna watu maalum waliohodhi peke yao tafsiri ya dini, kuhalalisha na kuharamisha. Vilevile, kwetu hakuna utenganishaji wa dini na dola; hivyo hakuna mamlaka ya kiroho wala mamlaka ya kidunia. Dhana hii na kila kinachoashiria hiyo ndicho kinachopaswa kuondoshwa.
Ama kuhusu kuhodhi kuhalalisha na kuharamisha kwa watu maalum wenye mavazi fulani, dhana hii haipo kwa idadi kubwa ya Waislamu. Na harakati ambazo Chama (Hizb) kimezifanya katika suala hili zimezaa matunda; kwani watu wengi sasa hawaelekei kuchukua hukumu kutoka kwa hawa Mashuikh wenye mavazi rasmi kwa sababu ya kutokuwa na imani nao.
Ama kuhusu kuhodhi mambo ya "kiroho" kwa watu wenye mavazi ya "kidini" rasmi, jambo hilo pia karibu halipo tena kwa Waislamu. Kwani Waislamu leo hii wanawakubali Mashuikh wanaozungumzia utawala na siasa, wanawathamini na kuwaheshimu. Ama Mashuikh wanaozingatia ibada pekee na wasioingilia kuwahisabu watawala, watu wanawatazama bila uthamini wala heshima.
Hata hivyo, kuhodhiwa kwa mavazi haya na Mashuikh na Maimamu wa misikiti kunaweza kuleta mkanganyiko kwa watu wa kawaida, wakadhani kuwa kuna watu maalum wa dini kwa maana ya ibada na mfano wake, na kwamba hawa hawana uhusiano na siasa wala mambo yake, bali kuna viongozi wa dola kwa ajili ya kazi hizo.
Kwa sababu hiyo, Dola itafanya kazi ya kuondosha muonekano wa vazi maalum kwa ajili ya Mashuikh na Maimamu wa misikiti. Lakini si kwa kuwazuia kuvaa, bali kwa kuondosha uhodhi wa vazi hilo. Kwa mfano, watu wamuone mtoza bili za maji na umeme amekuja akiwa amevaa juba na kilemba, au wamuone Khalifa na Gavana (Wali) ana kilemba kama ilivyokuwa katika zama za awali za Kiislamu, na wamuone Imamu wa msikiti amevaa vazi la kawaida. Yaani, kuondosha uhodhi wa vazi fulani. Jambo hili halihitaji amri ya serikali, bali baadhi ya mbinu mwafaka. Kwa mfano, ukienda kuchukua leseni ya ujenzi, unamkuta mhandisi anayekuja na wewe kukagua akiwa amevaa kilemba, na unamkuta mfungishaji ndoa (Ma’dhun) amevaa kilemba cha kijadi (Iqal na Hutwah), na kadhalika; kiasi kwamba usione vazi maalum lililotengwa kwa ajili ya kiongozi au Sheikh pekee. Hili ni jambo linalokubalika na lenye mantiki katika Uislamu, bali ndivyo Waislamu walivyokuwa. Kwani Khalifa alikuwa akiwaongoza watu na kuswali nao, na hakuna Muislamu yeyote aliyeweza kumtofautisha kiongozi na kadhi au mtu wa kawaida kupitia mavazi yao. Na yule mtu aliyekuja kwa Waislamu waliokuwa wameketi na Mtume (saw), alisimama na kuwauliza: "Ni nani miongoni mwenu aliye Mjumbe wa Allah?"
Kwa hiyo, Dola haitotoa amri ya kupiga marufuku mavazi ya Mashuikh, bali itaondosha dhana yake na kuyafanya mavazi hayo yasiwe maalum kwa taaluma fulani kwa dhana inayopingana na Uislamu. Kadhalika itafanya hivyo kwa vazi lolote linaloashiria kuwa kuna watu maalum wa "dini" na watu wengine maalum wa Dola. Kila mmoja katika raia atavaa vazi lolote la halali analotaka bila vazi fulani kuhodhiwa na mtu maalum "wa dini" ili watu waweze kuelekea kwake kumuuliza masuala ya "kiroho", na waelekee kwa mwengine kumuuliza masuala ya kisiasa. Badala yake, Waislamu wote watakuwa wakibeba dhamana ya Uislamu katika nyanja zake mbalimbali, na kila anayejua suala fulani atakuwa ni mwanachuoni katika suala hilo, iwe amevaa kilemba au yuko wazi kichwa.
3 Jumada al-Ula 1425 H 21/06/2004 M