Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook "Feqhi"
Kwa Abu Muso
Swali:
Assalamu Alaikum ewe Amir wetu, hali yako? Wakati Dola ya Kiislamu itakaposimamishwa, ni katika marhala (hatua) gani Hizb ut-Tahrir itakuwa ikitembea?
Baadhi ya watu wanasema itaendelea kama ilivyo katika marhala ya tatu, na wengine wanasema wakati wa kuingia katika utawala, marhala ya tatu huisha na Chama huanza kazi mpya kabisa ambayo ni kuwahisabu watawala na kuwa wasimamizi wa jamii... Ni kauli gani sahihi na yenye nguvu zaidi?
Jibu:
Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Tulitaja katika Kitabu cha Utambulisho (At-Ta’reef) yafuatayo: [8- Njia ya Hizb ut-Tahrir
Njia ya kufuatwa katika kubeba da’wah ni hukumu za kisheria, zinazochukuliwa kutokana na njia ya Mtume ﷺ katika kubeba kwake da’wah kwa sababu ni wajibu kumfuata, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيراً
"Hakika mnao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kigezo chema kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamtaja Mwenyezi Mungu sana." (QS. Al-Ahzab [33]: 21)
Na kauli yake Mtukufu:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
"Sema: Ikiwa nanyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (QS. Al-Imran [3]: 31)
Na kauli yake Mtukufu:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا
"Na anachokupeni Mtume kichukue, na anachokukatazeni kiepukeni." (QS. Al-Hashr [59]: 7)
Na aya nyingine nyingi zinazofahamisha wajibu wa kumfuata Mtume ﷺ, kumfanya kigezo, na kuchukua kutoka kwake.
Kwa kuwa Waislamu leo wanaishi katika Dar al-Kufr (nyumba ya ukafiri), kwa sababu wanahukumiwa kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremsha, basi nchi yao inafanana na Makka wakati wa kutumwa kwa Mtume ﷺ. Kwa hiyo, marhala ya Makka katika kubeba da’wah ndiyo inayopaswa kuwa sehemu ya kuigwa.
Na yeyote anayefuatilia sira ya Mtume ﷺ kule Makka mpaka aliposimamisha Dola kule Madina, inabainika kuwa alipitia katika marhala zilizo wazi, akifanya humo kazi maalum za wazi. Hivyo basi, Chama kimechukua kutoka hapo njia yake ya mwendo, marhala zake, na kazi zinazopaswa kufanywa katika marhala hizi, ikiwa ni kuiga kazi alizozifanya Mtume ﷺ katika marhala za mwendo wake.
Kulingana na hayo, Chama kimebainisha njia yake ya mwendo kwa marhala tatu:
Ya Kwanza: Marhala ya thakafa (elimu) ili kupata watu wanaoamini fikra ya Chama na njia yake ili kuunda kitala cha kichama (kutla).
Ya Pili: Marhala ya kuingiliana (tafa’ul) na Ummah, ili kuubebesha Uislamu, mpaka uufanye kuwa ni kadhia yake, ili ufanye kazi ya kuleta Uislamu katika uhalisia wa maisha.
Ya Tatu: Marhala ya kuchukua utawala, na kutekeleza Uislamu utekelezaji wa kiujumla na mpana, na kuubeba kama ujumbe kwa ulimwengu.
- Ama Marhala ya Kwanza: Chama kiliianza mjini Al-Quds mwaka 1372 H - 1953 M mikononi mwa muasisi wake, mwanachuoni mtukufu, mfikiri mkubwa, mwanasiasa shupavu, na kadhi katika mahakama ya rufaa kule Al-Quds, Ustadh Taqiuddin al-Nabhani, Mwenyezi Mungu amrehemu. Chama kilikuwa kikifanya humo mawasiliano na watu wa Ummah mmoja mmoja, kikiwasilisha kwao fikra yake na njia yake kwa namna ya mtu mmoja mmoja. Na yule aliyekuwa akiitikia, alikuwa akiingizwa katika masomo ya kina katika halaka za Chama, mpaka ayeyushwe kwa fikra za Kiislamu na hukumu zake ambazo Chama kimezichukua (tabanni), na awe shakhsia ya Kiislamu inayotagusana na Uislamu, yenye akili ya Kiislamu (aqliyyah) na nafsi ya Kiislamu (nafsiyyah), na kuanza kubeba da’wah kwa watu. Pindi mtu anapofikia kiwango hiki, anajilazimisha kwa Chama, na Chama kinamuunganisha katika wanachama wake. Kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ katika marhala yake ya kwanza ya da’wah, ambayo ilidumu kwa miaka mitatu, akilingania watu mmoja mmoja, akiwaelezea yale aliyotumwa nayo na Mwenyezi Mungu. Na yule aliyekuwa akiamini, alikuwa akimuweka katika kitala pamoja naye kwa msingi wa dini hii kwa siri, na kuhakikisha anafundishwa Uislamu na kusomewa yale yaliyoteremka kwake na yanayoteremka katika Qur’ani mpaka akawayeyusha kwa Uislamu. Alikuwa akikutana nao kwa siri na kuwafundisha kwa siri katika sehemu zisizoonekana, na walikuwa wakitekeleza ibada zao kwa siri. Kisha habari za Uislamu zikaenea Makka na watu wakawa wanazizungumzia na kuingia makundi kwa makundi...
- Baada ya Chama kufanikiwa kuunda kitala hiki cha kichama, na jamii kuhisi kuwepo kwake, na kukijua pamoja na fikra zake na kile kinacholinganio, kilihamia katika:
Marhala ya Pili: Nayo ni marhala ya kuingiliana na Ummah ili kuubebesha Uislamu, na kuunda uelewa wa jumla (wa’yul ‘am) na maoni ya jumla (ra’yul ‘am) kwa Ummah juu ya fikra za Kiislamu na hukumu zake ambazo Chama kimezichukua, mpaka uufanye kuwa ni fikra zake, ufanye kazi ya kuzileta katika uhalisia wa maisha, na utembee pamoja na Chama katika kazi ya kusimamisha Dola ya Khilafah, na kumsimamisha Khalifa, ili kuanza tena maisha ya Kiislamu na kubeba da’wah ya Kiislamu kwa ulimwengu. Katika marhala hii, Chama kilihamia katika kusema na umma kwa usemaji wa pamoja. Kimekuwa kikifanya katika marhala hii kazi zifuatazo:
1- Thakafa ya kina katika halaka kwa wanachama ili kukuza mwili wa Chama, kuongeza idadi yake, na kutengeneza shakhsia za Kiislamu zenye uwezo wa kubeba da’wah, na kuingia katika dhoruba za mivutano ya kifikra na mapambano ya kisiasa.
2- Thakafa ya pamoja kwa umma wa Ummah kwa fikra za Kiislamu na hukumu zake ambazo Chama kimezichukua, kupitia darsa za misikitini, klabu, mihadhara, sehemu za mikusanyiko ya watu, magazeti, vitabu na vipeperushi, ili kuunda uelewa wa jumla kwa Ummah na kuingiliana nao.
3- Mvutano wa kifikra dhidi ya itikadi za kikafiri, mifumo yake na fikra zake, na dhidi ya itikadi potofu, fikra zenye makosa, na dhana zisizo sahihi, kwa kubainisha uharibifu wake, makosa yake na kugongana kwake na Uislamu, ili kuukomboa Ummah kutokana nazo na athari zake.
4- Mapambano ya kisiasa...
- Na wakati jamii ilipoganda mbele ya Chama kutokana na Ummah kupoteza imani yake kwa viongozi wake ambao walikuwa ni tegemeo lake, na kutokana na mazingira magumu yaliyowekwa katika eneo hili ili kupitisha mipango ya njama, na kutokana na utawala wa kidikteta na ukandamizaji unaofanywa na watawala dhidi ya mataifa yao, na kutokana na ukali wa maumivu wanayoyapata watawala kwa Chama na vijana wake; wakati ilipoganda kutokana na yote hayo, Chama kilifanya kazi ya kutafuta nusra kutoka kwa wenye uwezo nayo...
Pamoja na Chama kufanya kazi hizi za nusra, kiliendelea kufanya kazi zote kilizokuwa kikizifanya, kuanzia masomo ya kina katika halaka, thakafa ya pamoja, na kutilia mkazo kwa Ummah ili kuubebesha Uislamu na kuunda maoni ya jumla kwake, na kupambana na madola ya kikafiri ya kikoloni na kufichua mipango yao, na kufichua njama zao, na kupambana na watawala, na kuchukua maslahi ya Ummah na kusimamia mambo yake.
- Na kinaendelea katika yote hayo kikiwa na matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kukiletea yeye na Ummah wa Kiislamu ushindi na mafanikio, ili kuwe na:
Marhala ya Tatu: Ambapo ni kusimamisha Khilafah ya Uongofu, na hapo ndipo waumini watafurahia ushindi wa Mwenyezi Mungu.] Mwisho wa nukuu kutoka katika Kitabu cha Utambulisho.
Kwa hiyo, marhala tatu ni wakati wa kutokuwepo kwa Dola, na kisha kazi ya Chama inakuwa ni kutekeleza marhala hizo tatu... Ama wakati wa kusimama kwa Dola, basi kila kitu kinachohusiana na kusimamisha Dola kinakuwa hakipo tena katika kazi za Chama. Kwa mfano, kutafuta nusra katika mwisho wa marhala ya pili kwa ajili ya kusimamisha Dola kunakuwa hakuwezi kuwepo, vilevile marhala ya tatu yaani kusimamisha Dola, yote hayo yanakuwa hayapo, kwa sababu Dola tayari imeshasimama. Badala yake, nafasi ya yote hayo inachukuliwa na kuwahisabu watawala kulingana na dalili za kisheria... Ama marhala zilizobaki zinaendelea kwa nguvu zaidi na harakati kubwa zaidi, kwa sababu uadilifu baada ya kusimama Dola utachukua nafasi ya dhulma, na kutayarisha mazingira mazuri kwa kazi ya Chama kutachukua nafasi ya kusakamwa kwa mabavu, na hapo ndipo waumini watafurahia ushindi wa Mwenyezi Mungu.
Tumebainisha katika vitabu vyetu, hususan kijitabu (Al-Kurrasah), namna ya kuwahisabu watawala kulingana na hukumu za Sharia... Na katika hili kuna utoshelevu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye hikma zaidi.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
01 Dhul-Hijjah 1442 H Inayolingana na 11/07/2021 M
Kiungo cha jibu kutoka katika ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka katika ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) Mtandaoni