Jawabu la Swali
Kilicho Nyuma ya Kura ya Maoni kuhusu Kujitenga kwa Eneo la Kurdistan
Swali: Kwa nini Barzani anashikilia kufanya kura ya maoni ya kujitenga kwa eneo la Kurdistan licha ya kutokuwepo kwa ridhaa ya kimataifa na kikanda kuhusu kura hii? Je, kura hii ya maoni katika mazingira ya sasa si dhidi ya maslahi ya Wakurdi wenyewe? Na je, inatarajiwa kuwa kura hiyo itafanyika? Na ikiwa itafanyika na kupata idhini ya walio wengi, je, inawezekana kuanzishwa kwa dola ya Kikurdi katika eneo hilo? Jazakumullahu Khayran.
Jibu: Kuna kauli isemayo kwamba kiongozi akichukua uamuzi dhidi ya maslahi ya nchi yake, basi hii inamaanisha kuwa kiongozi huyo ni kibaraka, na kwamba uamuzi huu umeshinikizwa kwake na dola nyingine kwa ajili ya maslahi yake... Kauli hii inatumika kwa kiasi kikubwa kwa Wakurdi katika eneo la Kurdistan, na ufafanuzi wa hilo ni kama ifuatavyo:
1- Mwanasiasa yeyote mwenye ufahamu anatambua ugumu mkubwa wa Wakurdi kuwa na dola. Bali, jitihada katika mazingira ya sasa ya kimataifa ya kuanzisha dola ya Wakurdi zinaleta madhara kwa eneo la Kurdistan; si madhara ya kisiasa na kimaanawi tu, bali yanatufikisha kwenye madhara ya kimwili. Suala si tu kuanzisha dola kwa ajili ya Wakurdi nchini Iraq; kama ingekuwa hivyo, huenda ingeweza kuundwa... Kwani mfumo uliowekwa na Wamarekani baada ya kuikalia kwa mabavu Iraq, ambao ulikuja kujulikana kama katiba ya Bremer, mfumo huu umeifanya Iraq kuwa shirikisho la mikoa yenye mafungamano dhaifu na serikali kuu, kiasi kwamba mamlaka ya eneo la Kurdistan katika masuala ya utawala na maamuzi ndani ya eneo hilo imekuwa na nguvu zaidi kuliko serikali kuu mjini Baghdad! Mataifa ya kikafiri ya kikoloni yanabeba vichwani mwao mbegu za kuigawa nchi yoyote ya Kiislamu wanayoikalia na kuisambaratisha, na kilichopo ni kwamba yanasubiri tu fursa mwafaka, na hayo ni kutokana na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu... Tulitaja katika jawabu la swali lililopita la tarehe 12/08/2014 lililosema: (- Marekani tangu kuivamia Iraq mnamo 2003 inaendelea kuiandaa Iraq kwa ajili ya kusambaratika. Katiba iliyowekwa na Bremer ilijengwa juu ya misingi ya kimadhehebu na kikaumu kwa kugawa sehemu kwa makundi na madhehebu... aliigawa kwa Rais wa Jamhuri, Spika wa Bunge, na Waziri Mkuu. Na kwa sababu Waziri Mkuu ndiye mwenye mamlaka ya utendaji, na kwa sababu Bremer aliifanya nafasi hiyo kuwa ya kimadhehebu, imekuwa rahisi kuchochewa na kuibua hasira kwa makundi mengine... Katiba yenyewe iliyoandikwa inazungumzia utawala wa shirikisho wa mikoa, na mamlaka ya mikoa ni yenye nguvu. Hivyo basi, Marekani imefanikiwa kuandaa mazingira ya kuisambaratisha Iraq katika mikoa...) mwisho. Kwa hivyo, eneo hili kwa upande wa kivitendo ni dola inayokosa tu taratibu rasmi za balozi, uanachama wa Umoja wa Mataifa na mambo mengine kama hayo ya kishikili... Ama upande wa kivitendo, eneo la Kurdistan ni dola ndani ya dola na limetenganishwa kivitendo na dola kuu. Iraq kama dola moja imetoweshwa! Hivyo basi, eneo la Kurdistan halihitaji dola ndani ya Iraq kwani kivitendo ni dola... Na kama tulivyosema, suala si kuanzishwa kwa dola ya Kikurdi ndani ya mipaka ya eneo la Kurdistan nchini Iraq pekee bila kuwa na uhusiano na maeneo mengine ya Wakurdi nje ya Iraq; sivyo hivyo. Bali dola yoyote ya Wakurdi itakayoanzishwa, itavuta moja kwa moja harakati kali na za msukosuko za Wakurdi katika eneo zima. Dola ya Kikurdi haitaishia katika eneo la Kurdistan pekee... Kwa ajili hiyo, kutokea kwake ni pigo chungu, hasa kwa Marekani na vibaraka wake nchini Uturuki, Iran na Syria. Hivyo, mwanasiasa yeyote anatambua kuwa kuanzishwa kwa dola ya Wakurdi, iwe nchini Uturuki, Iraq au Syria, kuanzishwa huku hakuruhusiwi kwa sasa na mazingira ya kimataifa wala ya kikanda. Na ninadhani si rahisi kwa wanasiasa wa Kikurdi, na Barzani akiwa miongoni mwao, kutotambua hilo. Bali kama tulivyotaja hapo awali, wazo la kuanzisha dola ya Kikurdi katika mazingira ya sasa linaweza kusababisha kuvurugika kwa mambo na harakati zinazoweza kutoka nje ya udhibiti katika eneo hilo, hususan maeneo ya Wakurdi, jambo ambalo litawaletea madhara kama tulivyotaja; si kimaanawi na kisiasa tu bali kimwili. Hivyo basi, uamuzi wa Barzani ni dhidi ya maslahi ya nchi yake katika mazingira ya sasa... Hii ndiyo sehemu ya kwanza ya kauli hiyo.
2- Ama kuhusu ni dola gani iliyopo nyuma ya uamuzi wa Barzani, na kwamba uamuzi huo ni kwa ajili ya maslahi ya dola hiyo, basi ushahidi uko wazi, na si vigumu kuinyooshea kidole dola hiyo. Kutangaza kura ya maoni kwa ajili ya kuanzisha dola iliyojitenga na Iraq, tangazo hili Barzani hawezi kulitoa katikati ya upinzani wa Marekani na upinzani wa nchi za eneo zinazoizunguka Kurdistan ambazo ni watiifu kwa Marekani. Hawezi kuwa na nguvu ya kukabiliana na nguvu hizi pinzani kimataifa na kikanda, isipokuwa kuwe na dola nyingine kubwa inayomuunga mkono Barzani na kumshajiisha kuchukua uamuzi huu. Eneo la Kurdistan kwa hali yake yote ni dhaifu mno kuweza kuhimili mbele ya nchi hizo, hususan Marekani ambayo inaiongoza Iraq nzima. Si vigumu, kama tulivyosema hapo awali, kutambua kuwa dola hiyo kubwa inayosimama nyuma yake na kumuelekeza kuchukua maamuzi kama haya ni Uingereza. Familia ya Barzani imekuwa na uhusiano na Uingereza tangu mwishoni mwa Dola ya Osmania. Barzani ameurithi uhusiano huu kutoka kwa baba yake, Mustafa Mullah Barzani, na kabla yake ami yake Ahmad Barzani, na kabla yao Abdul Salam Barzani ambaye aliongoza uasi wa kijeshi wa Kikurdi dhidi ya Dola ya Osmania tangu mwaka 1909 hadi 1914 kwa msaada wa wazi kutoka kwa Uingereza. Hivyo familia hii ina historia ya kale katika uhusiano wake na Uingereza... Na kama tukifuatilia misimamo kuhusu kura ya maoni, tutakuta kuwa msimamo wa Uingereza ulikuwa unaunga mkono uamuzi wa kura hiyo hata kama ilikuwa kwa njia ambayo Uingereza inajulikana kwayo ya mbinu za hila na hadaa:
Kwa mfano, Barzani alikutana na Balozi wa Uingereza nchini Iraq mnamo tarehe 24/08/2017, Frank Baker, ili kuonyesha msaada wa Uingereza kwake. Ukurasa wa Kikurdi wa "Rudaw" mnamo tarehe 24/08/2017 uliripoti habari za mikutano hii ukisema: "Katika mkutano wa Barzani na Balozi wa Uingereza nchini Iraq, mgeni huyo alionyesha maelewano ya nchi yake kwa haki za watu wa Kurdistan, na alimfahamisha Rais wa eneo la Kurdistan kuhusu msimamo wa Uingereza juu ya kufanyika kwa kura ya maoni." Maana ya "maelewano" katika lugha ya kidiplomasia ni kuunga mkono, na maana ya kumfahamisha msimamo wa Uingereza bila kutaja kitu kingine ni kuunga mkono pia. Yaani msimamo wa Uingereza ni chanya kwa uamuzi wa Barzani, bali ni wenye kumuunga mkono na kumtaka aendelee licha ya upinzani wa Marekani na nchi watiifu kwa Marekani katika eneo hilo...
Na kwa mfano, (Afisa wa mahusiano ya nje katika eneo la Kurdistan, Falah Mustafa, aliiambia Kurdistan 24 kuwa "Uingereza haipingi kufanyika kwa kura ya maoni, wala haipingi matarajio ya Kikurdi." Kauli ya Mustafa imekuja baada ya mkutano wa Waziri wa Nchi wa Uingereza anayeshughulikia Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Alistair Burt, na maafisa wa Kikurdi mjini Erbil. Waziri huyo wa Uingereza aliwasili Erbil siku ya Jumapili ili kujadiliana na maafisa wa Kikurdi kuhusu masuala kadhaa, huku Wakurdi wakinuia kufanya kura ya maoni kuhusu uhuru wa eneo la Kurdistan kutoka Iraq mnamo Septemba 25 kama hatua ya awali ya kuanzisha dola huru...) (Kurdistan24 Erbil 05/09/2017).
Hivyo basi, Uingereza ndiyo dola inayosimama nyuma ya uamuzi wa kura ya maoni uliotolewa na Barzani...
3- Ama maslahi ya Uingereza nyuma ya uamuzi huu yamefungamana tangu kushinda kwa Trump katika uchaguzi na haraka ya Waziri Mkuu wa Uingereza, May, kwenda kumtembelea Trump mnamo tarehe 26/01/2017 na kumpongeza mjini Washington... Wakati huo, Trump alimwagia sifa May na May akafanya vivyo hivyo, lakini kila mmoja wao alikuwa na lengo tofauti na mwenzake! Ama Trump, alikuwa anataka Uingereza ifanye kila jitihada kuisambaratisha Umoja wa Ulaya kwa kujiondoa yenyewe Ulaya bila kuchelewa, na wakati huo huo ifanye kila jitihada kuweka mazingira ya kusambaratisha Umoja wa Ulaya, hasa nchini Ufaransa na Uholanzi ambazo zilikuwa karibu na uchaguzi... Ama May, alikuwa anataka kutoka kwa Trump mikataba ya kibiashara atakayoitumia kama shinikizo jipya kwa nchi za Umoja wa Ulaya ili kupata upendeleo wakati wa kujiondoa kwenye umoja huo. Trump na May wakati wa ziara hiyo kila mmoja alikuwa anaangazia lengo lake alilokusudia. May alijaribu, kama ilivyo ada ya Waingereza, kuficha lengo lake la kibiashara kwa mbinu za ujanja, lakini kukosekana kwa diplomasia kwa Trump na matamshi yake ya wazi hakukumruhusu May kuficha nia yake...
Hivyo basi, wakati wafuasi wa Umoja wa Ulaya waliposhinda nchini Ufaransa na Uholanzi, pamoja na ukweli kwamba Ujerumani inaunga mkono kwa nguvu Umoja wa Ulaya na kuupa umuhimu mkubwa, Trump alitambua kuwa Uingereza ilijali zaidi kufanya mikataba ya kibiashara na Marekani na haikutoa umuhimu mkubwa kwenye suala la kuisambaratisha Umoja wa Ulaya kama alivyotaka Trump. Haya yote yalimsababishia Trump hasira, na matokeo yake yakawa ni kuipiga Uingereza katika sehemu yake nyeti "Qatar" kwa kile kizuizi na makoiyo (boycott)! Tulishabainisha hayo katika jawabu la swali tulilotoa mnamo tarehe 23/07/2017 tuliposema: (- Ama Uingereza, ziara ya mapema ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, mjini Washington mnamo 26/01/2017 na shauku yake ya kutia saini mkataba wa kibiashara na Washington ilikuwa ni kielelezo kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya ili kuzishajiisha kujiondoa. Hivyo, Uingereza ilirejesha mafungamano yake na Marekani na ilifurahishwa sana na utawala wa Trump. Lakini baada ya kufifia kwa matumaini ya Marekani ya kuisambaratisha Umoja wa Ulaya, jambo lililodhihirika kwa ushindi wa wafuasi wa Ulaya katika uchaguzi wa Uholanzi na Ufaransa, mtazamo chanya wa Trump kwa Uingereza ulirudi nyuma, kwani alikuwa anaitaka iongoze harakati za kuisambaratisha Ulaya. Na wakati Brexit ya London haikujirudia Paris na Amsterdam, Marekani ilirejea nyuma na kuanza kumega maslahi ya kimataifa ya Uingereza, jambo lililosababisha mshtuko mjini London. Marekani inamsukuma kibaraka wake Sisi kumpa msaada zaidi Haftar bila kuzingatia maslahi ya Uingereza nchini Libya, na Marekani imewasukuma vibaraka wake kwa njia ya mshtuko kuishinikiza Qatar, ambayo inawakilisha kichwa cha mkuki cha Uingereza katika eneo la Kiarabu na Kiislamu...) mwisho. Hayo yote yalimfanya Trump kupoteza utulivu wake, hivyo aliharakisha kuitembelea Saudi Arabia na kufanya mkutano ule wa kilele, kisha akaipiga Uingereza katika sehemu nyeti kwa kizuizi na makoiyo yaliyotokea kwa Qatar.
4- Hapa ilikuwa ni lazima kwa Uingereza kufanya jambo fulani ili kuvuruga maslahi ya Marekani katika eneo hili. Hivyo ilikimbilia uamuzi ule wa kumtaka Barzani kuitisha kura ya maoni ili kuleta usumbufu kwa Marekani na vibaraka wake. Kwa kawaida, Uingereza haiwezi kufanya zaidi ya kuleta mvurugano kwa Marekani; haina uwezo wa kukabiliana na Marekani hadharani lakini inaweza kuvuruga na kusumbua, hasa ikichagua mazingira mwafaka na hatua yenye taathira kama ilivyopata katika kura ya maoni ya Kurdistan. Uingereza ilihakikisha kuwa Barzani anafikisha hatua hiyo hadi mwisho kwa sababu mazingira ya sasa ni ya joto kwa Marekani pamoja na vibaraka wake Uturuki, Iran na Syria kutokana na harakati za kijeshi zinazoendelea... Kwa ajili hiyo, Barzani amebaki akishikilia kura ya maoni, na Uingereza ilikuwa ikipigia debe kura hiyo kwamba itawaletea Wakurdi dola huru katika eneo la Kurdistan. Na kama ilivyo ada yake katika hadaa na upotezaji, haijali maslahi ya Wakurdi kiasi inavyojali kufikia maslahi yake, na historia ya Uingereza na Wakurdi imejaa mambo haya!
Tulitaja katika jawabu la swali mnamo tarehe 01/04/2009: (...Uingereza ilimwahidi Mahmoud al-Hafid mnamo mwaka 1919 kwamba ashambulie himaya ya Osmania mjini Sulaymaniyah mkabala na kupewa dola ya Kikurdi. Wakashambulia na kuwaua ndugu zao Waosmania katika himaya hiyo na kuwafukuza walionusurika. Kisha Uingereza ikavunja ahadi yake, bali ikamhamishia Mahmoud al-Hafid katika koloni lake la India. Vilevile, Uingereza ilishikilia katika mkataba wa Sèvres mnamo mwaka 1920 na Dola ya Osmania kuweka kipengele kinachohusiana na kuanzishwa kwa dola ya Kikurdi ili kumsumbua Khalifah Muhammad Wahiduddin, ambapo ujumbe wa Khalifah ndio uliokuwa ukifanya mazungumzo. Lakini Uingereza ilipofanikiwa baadaye kumsimika Mustafa Kemal kuwa Rais wa Jamhuri na Khilafah kukomeshwa, na mkataba ukawa na Jamhuri ya Mustafa Kemal mjini Lausanne mnamo 1924, Uingereza ilikataa kuweka kipengele cha dola ya Kikurdi kwa sababu ilikuwa imeshafikia lengo lake, nalo ni kuangusha Khilafah, hivyo haikuwa na haja tena ya kutumia suala kama hilo. Uingereza ilikuwa ikichochea hisia za kikaumu za Kikurdi na kuchochea hisia za kikaumu zote katika eneo hilo, na kuwatumia wale inayowachochea na kuwashawishi kufanya uasi na uasi dhidi ya Dola ya Kiislamu hadi ifikie malengo yake, na kisha huwatupa waliokuwa wakishirikiana nayo au kuwatumia kama watumwa wake pale inapowasimika kama watawala na viongozi...). Hivyo ndivyo ilivyo Uingereza katika hadaa na upotezaji...
5- Hivyo basi, Barzani amebaki akishikilia kufanyika kwa kura ya maoni mnamo 25/09/2017 ili awe na dola yake! Na hakujali misimamo ya kimataifa au ya kikanda inayopinga kura hiyo hata kutoka kwa baadhi ya Wakurdi wenyewe, bali alitamka akisema: (Eneo la Kurdistan limekariri siku ya Jumatano kukataa kwake kuahirisha au kufuta kura ya maoni ya kujitenga na Iraq iliyopangwa kufanyika Septemba 25 ijayo, licha ya juhudi za kimataifa na kikanda za kuizuia Erbil kuchukua hatua hiyo, na kukataa kwa serikali kuu mjini Baghdad kwa kura hii na matokeo yake.
Baraza Kuu la Kura ya Maoni katika eneo la Kurdistan lilijadili, wakati wa mkutano wa jana chini ya uenyekiti wa Rais wa eneo hilo Masoud Barzani, matokeo ya ziara ya hivi karibuni ya ujumbe wa Kikurdi mjini Baghdad kuhusu suala la kura ya maoni, na pia matokeo ya mazungumzo ya Barzani na Mattis mjini Erbil juzi. Mshauri wa Barzani alisema: "Kuna msisitizo kutoka kwa Rais Masoud Barzani kwamba kura ya maoni haitaahirishwa hata kwa dakika moja na itafanyika katika muda uliopangwa mnamo Septemba ishirini na tano" Alhamisi 2 Dhul-Hijjah 1438 H - 24 Agosti 2017 - Dubai - Al-Arabiya.net). Hii ni pamoja na kufahamu kuwa upinzani wa kimataifa na kikanda kwa kura hiyo ulikuwa wazi kabisa:
A- Marekani ilikataa kura hiyo tangu siku ya kwanza Barzani alipotangaza kuifanya mnamo 07/06/2017 ambapo alitangaza kuwa kura ya maoni itafanyika katika maeneo ya Wakurdi nchini Iraq mnamo Septemba 25 ijayo kuhusu kuanzisha dola huru ya Kikurdi. Marekani ilimjibu kupitia mjumbe wa Rais wa Marekani kwa muungano wa kimataifa, Brett McGurk: "Kufanya kura ya maoni kwa wakati huu kutasababisha kuvurugika kwa utulivu, na hatuoni kuwa kura ya maoni inapaswa kufanyika Septemba, kwa sababu kuifanya kwa mujibu wa ratiba hii ya haraka hususan katika maeneo yanayozozaniwa kutasababisha kuvurugika kwa utulivu kwa kiasi kikubwa" (AFP 08/06/2017).
Na hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, mnamo tarehe 11/08/2017 katika mazungumzo ya simu na Rais wa eneo la Kurdistan, Masoud Barzani, alielezea "hamu ya Washington ya kuahirisha kura ya maoni na msisitizo wake wa kuunga mkono mazungumzo na majadiliano na Baghdad... Marekani ilimtuma Waziri wake wa Ulinzi, James Mattis, mjini Baghdad mnamo 22/08/2017 ili kukutana na Waziri Mkuu wa Iraq, Abadi, kisha aende Erbil kukutana na Barzani, na kwenda Ankara mnamo 23/08/2017 ili kuichochea Uturuki ya Erdogan ambayo ni mkono wake tendaji katika eneo hilo...
B- Kadhalika nchi za eneo hilo watiifu kwa Marekani zilipinga... Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Saad al-Hadithi alisema "msimamo wowote au hatua inayochukuliwa na upande wowote nchini Iraq lazima iwe inategemea katiba, na uamuzi wowote unaohusu mustakabali wa Iraq inayofafanuliwa kikatiba kama nchi moja ya shirikisho ya kidemokrasia yenye mamlaka kamili ya kitaifa lazima uzingatie maandishi ya kikatiba yanayohusiana... hakuna upande mmoja unaoweza peke yake kuamua hatima ya Iraq bila kuhusisha pande nyingine." (Alhurra ya Marekani 09/06/2017).
Uturuki ilitangaza upinzani wake kwa kura ya maoni na tangazo la uhuru wa Kurdistan tangu siku ya kwanza, ambapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilitoa taarifa ikielezea uamuzi wa uongozi wa eneo hilo kuwa ni "kosa kubwa na kwamba unatishia umoja na usalama wa ardhi ya Iraq" (Alhurra ya Marekani 09/06/2017)... Erdogan alitangaza baada ya mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mattis, akisema: "Uamuzi wa kura ya maoni ni uamuzi wa kimakosa" (Al Jazeera 24/08/2017)...
Vilevile "Iran" ilitangaza mnamo Jumamosi 11 Juni 2017, muda mfupi baada ya tangazo la kura ya maoni, ilitangaza kuwa inapinga vikali kura ya maoni inayokusudiwa kufanyika Kurdistan ya Iraq mnamo Septemba ijayo. Ikisisitiza kuwa Tehran ina "msimamo wazi juu ya umoja wa ardhi ya Iraq. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi alisema: "Maamuzi ya upande mmoja na yaliyo mbali na vigezo na mifumo ya kitaifa na kisheria, yatasababisha matatizo zaidi na kuzorota kwa hali ya usalama nchini Iraq" (15/06/2017 http://afkarhura.com...). Tovuti ya Afkar Hura http://afkarhura.com/?p=6839 ilichapisha mnamo 7 Septemba 2017 tamko la Msaidizi Maalum wa Spika wa Majlisi ya Shura ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa, Hossein Amir-Abdollahian, ambapo alisema: (Alisisitiza kuwa kufanyika kwa kura ya maoni Kurdistan ya Iraq kutazua mgogoro mpya...).
Kisha Marekani ina wafuasi ndani ya Kurdistan, miongoni mwao ni harakati ya Gorran (Mabadiliko) ya Kikurdi na chama cha Patriotic Union of Kurdistan (PUK) cha Talabani. Harakati ya Gorran ilipinga tangazo la Barzani la kufanya kura ya maoni ambapo Hoshyar Abdullah, mwanachama wa harakati hiyo katika bunge la Kurdistan alisema "harakati ya Mabadiliko bado ina maoni yaleyale kwamba muda huu wa kura ya maoni ni wa kimakosa na ajenda hii nzima ni ajenda ya kibinafsi na ya kichama ya Masoud Barzani" akisisitiza kuwa "Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan (KDP) ni kikaragosi na si mchezaji." (Elaph 05/08/2017). Vilevile Rais wa Jamhuri ya Iraq, Fuad Masum ambaye anatoka chama cha PUK cha Talabani alipinga kura hiyo... Na chama cha KDP katika taarifa yake kilielezea tamko la Masum kuwa ni "la hatari na ujumbe mbaya kwa nchi za dunia unaokwamisha matokeo ya kura ya maoni na kupunguza umuhimu wake." (Chanzo kilichotajwa hapo awali).
Licha ya upinzani huu wa kimataifa na kikanda, Barzani anashikilia kufanya kura ya maoni na anatangaza kuwa hataichelewesha hata kwa dakika moja kama tulivyotaja hapo awali, na yote haya ni kwa sababu ya msukumo wa Uingereza katika suala la kura ya maoni kwa njia tuliyoibainisha katika uchambuzi wetu wa mwenendo wa mambo.
6- Na sasa baada ya kuchambua matukio ya kura ya maoni kwa mazingira tofauti yenye taathira... basi tunaweza kujibu yale yanayotarajiwa kuhusiana na suala la kura ya maoni... Kinachopewa uzito kuhusiana na jambo hili, kwa mujibu wa tulivyobainisha, ni yafuatayo:
A- Katika hali zote, haitarajiwi kuanzishwa kwa dola ya Wakurdi kwa maana ya kisheria ya dola, kwa sababu mradi wa Marekani kwa ajili ya Iraq ni kuwa Iraq iwe nchi ya shirikisho ya mikoa yenye mafungamano dhaifu kati ya mikoa na serikali kuu. Yaani kuwe na mgawanyo wa kivitendo katika usimamizi wa utawala nchini Iraq, na ama kwa upande wa kishikili basi ibaki dola ya shirikisho ya mikoa inayoitwa Iraq... Huu ndio mradi wa Marekani kwa ajili ya Iraq tangu kuivamia mnamo 2003 ambapo ilikuwa ikibeba mbegu za kuigawa Iraq na kuisambaratisha wakati wa uvamizi wake, lakini bila kuitangaza kuwa ni dola rasmi bali kwa wakati mwafaka. Wakati huo, Bremer, mtawala wa Marekani nchini Iraq, aliweka katiba ya shirikisho ya mikoa nchini Iraq kiasi kwamba hali ya Iraq kuwa dola moja yenye nguvu na mamlaka ya serikali kuu ifikie mwisho, na badala yake iwe dola dhaifu ya shirikisho ambapo mamlaka ya mikoa ndani yake ina nguvu kuliko mamlaka ya serikali kuu! Ili Iraq iwe tayari wakati ambapo Marekani itaweza na kuona ni maslahi kwake, iwe tayari kuifanya Iraq kuwa dola kadhaa rasmi... Ama sasa, mradi wa Marekani ni dola ya shirikisho ya mikoa nchini Iraq yenye mafungamano dhaifu na serikali kuu... Tulitoa jawabu la swali lililopita mnamo 12/08/2014 lililosema: (- Marekani tangu kuivamia Iraq mnamo 2003 inaendelea kuiandaa Iraq kwa ajili ya kusambaratika. Katiba iliyowekwa na Bremer ilijengwa juu ya misingi ya kimadhehebu na kikaumu kwa kugawa sehemu kwa makundi na madhehebu... aliigawa kwa Rais wa Jamhuri, Spika wa Bunge, na Waziri Mkuu. Na kwa sababu Waziri Mkuu ndiye mwenye mamlaka ya utendaji, na kwa sababu Bremer aliifanya nafasi hiyo kuwa ya kimadhehebu, imekuwa rahisi kuchochewa na kuibua hasira kwa makundi mengine... Katiba yenyewe iliyoandikwa inazungumzia utawala wa shirikisho wa mikoa, na mamlaka ya mikoa ni yenye nguvu. Hivyo basi, Marekani imefanikiwa kuandaa mazingira ya kuisambaratisha Iraq katika mikoa...) mwisho... Hivyo basi, siasa ya sasa ya Marekani haitaki dola kadhaa nchini Iraq bali inataka dola legelege ya shirikisho iliyogawanyika kivitendo na kubaki kama dola kishikili. Kwa sababu hiyo, ni vigumu katika mazingira ya sasa kuigawa Iraq kama dola kadhaa kisheria, bali Iraq itabaki kwa mujibu wa mradi wa Bremer ikiwa imegawanyika kivitendo na mikoa yake ina nguvu kuliko serikali kuu! Angalau katika muda unaoonekana hivi karibuni.
B- Kwa kuwa kutangazwa kwa kura ya maoni ni kwa amri ya Uingereza kwa ajili ya kupumua kutokana na mkwamo wa Uingereza kufuatia yaliyotokea kwa Qatar, basi kura ya maoni itafutwa ikiwa Marekani itasaidia kuondoa makoiyo dhidi ya Qatar au hata kuipunguza kwa namna inayofaa itakayoilinda heshima yake...
C- Marekani inaweza kuifuta kura ya maoni ikitaka kwa sababu ndiyo dola pekee inayoidhibiti Iraq, iwe kwa kuifuta kura hiyo moja kwa moja kutoka Marekani au kwa kuzichochea harakati za Kikurdi watiifu kwake nchini Kurdistan, au kwa kuzichochea Uturuki na Iran dhidi ya eneo hilo na hasa dhidi ya Barzani hata kama itabidi kutumia mashinikizo ya kimwili. Mkuu wa Majeshi wa Iran, Mohammad Baqeri, alifanya ziara nchini Uturuki kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Iran mwaka 1979. Ziara hiyo iliyofanyika mnamo 15/08/2017 ilichukua siku 3, na alipokelewa na Rais wa Uturuki Erdogan katika jengo la Rais mjini Ankara na mkutano kati yao ulichukua dakika 50 kama ilivyoelezwa na shirika la habari la Uturuki la Anadolu, jambo linaloashiria umuhimu wa suala hilo. Mkuu wa Majeshi wa Iran aliambatana na mkuu wa majeshi ya ardhini na mkuu wa ulinzi wa mipakani pamoja na idadi ya makamanda wa juu wa kijeshi wa Iran kama ilivyoelezwa na shirika la habari la Iran la IRNA. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi aliielezea ziara hiyo na mkutano wake na mwenzake wa Uturuki kuwa ni "hatua kubwa" na kwamba ni "hatua ya kukamilishana katika uhusiano kati ya nchi mbili..." (Shirika la habari la Mehr la Iran 21/08/2017). Hivyo si vigumu kuwa ziara hii ilikuwa kwa ajili ya uratibu kuhusu hatua zozote za kimwili katika eneo hilo ikiwa zitahitajika ili kufuta kura ya maoni au kuondoa matokeo yoyote yenye tija... Na inapewa uzito zaidi na ukweli kwamba Waziri wa Ulinzi wa Marekani alizuru Ankara mnamo 23/08/2017 yaani baada ya ziara ya Mkuu wa Majeshi wa Iran...
D- Na ikiwa Marekani itahofia kutokea kwa mvurugano mkali kufuatia kipengele cha (c), basi inawezekana Marekani isizuie kufanyika kwa kura ya maoni lakini bila ya kuwa na matokeo yoyote yenye taathira, au yenye tija... na kusiwe na hatua zozote zenye mwelekeo wa uhuru zitakazofuatia kura hiyo...
7- Na mwishowe, ni jambo la kusikitisha sana kwamba mafungamano ya Kiislamu ambayo Waislamu, Waarabu kwa wasio Waarabu, walikuwa wakipata utukufu kwayo, mafungamano haya makafiri wakoloni wamefanikiwa kuyaweka mbali na maisha ya Waislamu na nafasi yake kuchukuliwa na mafungamano yenye harufu mbaya; zana za uharibifu zilizowafanya Waislamu kuwa vipande vipande: vita kati yao vimeshamiri, na udugu umetoweshwa!
Hakika utaifa ni zana ya kubomoa jengo la Ummah. Kama ulivyokuwa jana zana ya uharibifu katika Dola ya Kiislamu, basi huyu kafiri mkoloni anaendelea kuitumia zana hii ili kubomoa kile kilichobaki katika chombo cha Ummah ikiwa ataweza... na kisha kuyafanya miji ya Waislamu kuwa uwanja wa mapambano kati ya madola yake makubwa na njia ya kumwaga damu za Waislamu, na ndugu kupigana wao kwa wao! Uislamu umeharamisha hayo yote, na umesisitiza juu ya umoja wa Waislamu na udugu wao. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ
"Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msifarakane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa maadui nanyi akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akawaokoeni nalo. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka." (QS. Ali Imran [3]: 103)
Na amesema Mtukufu:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ
"Hakika Waumini ni ndugu." (QS. Al-Hujurat [49]: 10)
Kadhalika, Uislamu umeharamisha aina zote za ubaguzi (asabiyyah): utaifa, uzalendo na ukabila n.k. Kutoka kwa Amr bin Dinar amesema: Nimemsikia Jabir bin Abdullah akisema: Tulikuwa katika vita, mtu mmoja katika Muhajirina akampiga (teke) mtu mmoja katika Ansari. Ansari akasema: "Enyi Maansari (njooni nisaidieni)!" Na yule Muhajiri akasema: "Enyi Wamuhajirina (njooni nisaidieni)!" Mtume wa Allah ﷺ akasikia akasema: "Ni nini hiki?" Wakasema: Mtu katika Muhajirina akampiga mtu katika Ansari, yule Ansari akaita: "Enyi Maansari!" Na yule Muhajiri akaita: "Enyi Wamuhajirina!" Mtume ﷺ akasema:
دَعُوهَا فَإِنَّهَا مُنْتِنَةٌ
"Iacheni (tabia hiyo), kwani hiyo inanuka vibaya." (Imetolewa na Bukhari). Na kutoka kwa Abi Mijlaz, kutoka kwa Jundub bin Abdullah al-Bajali amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
مَنْ قُتِلَ تَحْتَ رَايَةٍ عُمِّيَّةٍ، يَدْعُو عَصَبِيَّةً، أَوْ يَنْصُرُ عَصَبِيَّةً، فَقِتْلَةٌ جَاهِلِيَّةٌ
"Atakayeuawa chini ya bendera ya upofu, akiita kwenye asabiyyah (utaifa/ukabila) au akinusuru asabiyyah, basi kifo chake ni cha kijahilia." (Imetolewa na Muslim).
Waislamu waliishi kwa mamia ya miaka wakiwa watukufu kwa dini yao na wenye nguvu kwa Mola wao, udugu wa Kiislamu ukiwaunganisha. Katika Maswahaba wa Mtume ﷺ walikuwepo Abu Bakr, Umar, Uthman, Ali, Salman al-Farisi na Bilal al-Habashi... walikuwa waja wa Allah ndugu, wakipigana jihadi katika njia ya Allah... Umar Mwarabu aliingia Al-Quds kama mshindi, na Salahuddin Mkurdi akaikomboa Al-Quds kutoka kwa Mashambulizi ya msalaba (Crusaders), na Abdul Hamid Mturki akailinda Al-Quds kutokana na uchafu wa Mayahudi... Hivi ndivyo Waislamu wanavyokuwa na utukufu, na hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa yule anayetega sikio naye ni mshuhuda.
إِنَّ فِي هَٰذَا لَبَلَاغًا لِّقَوْمٍ عَابِدِينَ
"Hakika katika haya yapo mawaidha ya kutosha kwa watu wafanyao ibada." (QS. Al-Anbiya [21]: 106)
18 Dhul-Hijjah 1438 H Sawia na 09/09/2017 M