Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Mkutano wa 18 wa Shirika la Francophonie nchini Tunisia

November 29, 2022
1836

Jibu la Swali

Swali:

Mkutano wa 18 wa Shirika la Francophonie ulifanyika nchini Tunisia mnamo tarehe 19 na 20/11/2022, na Rais wa Tunisia alitoa hotuba ya ufunguzi kwa lugha ya Kifaransa. Je, shirika hili linamaanisha nini na linamtumikia nani? Na nini umuhimu wa mkutano huu kwa Rais wa Tunisia, Kais Saied, na uhusiano wake na Ufaransa? Je, hii inamaanisha kuwa ushawishi wa Uingereza umetoweka kabisa nchini Tunisia? Kisha, kwa nini Algeria haikuhudhuria mkutano huo licha ya kuwa mwanachama wa Shirika la Francophonie? Mwenyezi Mungu akulipe kheri...

Jibu:

Ili kufafanua jibu, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Francophonie, inayomaanisha Jumuiya ya Kimataifa ya nchi zinazozungumza Kifaransa, inajumuisha wanachama wa kudumu na waangalizi 88 na makao makuu yake yako jijini Paris, Ufaransa. Ilianza kufanya mikutano yake kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 1986. Miongoni mwa wanachama wake ni makoloni ya zamani ya Ufaransa barani Afrika hasa, na kwingineko kwa ujumla, na miongoni mwa wanachama wake wapo wasiozungumza Kifaransa na hawakuwa makoloni ya Ufaransa. Nchi wanachama katika shirika hili si lazima ziwe kibaraka wa Ufaransa; baadhi ni vibaraka na nyingine sivyo. Idadi ya wazungumzaji wa Kifaransa duniani inakadiriwa kuwa karibu milioni 321. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1970 ili kukuza lugha ya Kifaransa na ushirikiano wa kisiasa, kielimu, kiuchumi, na kiutamaduni kati ya nchi wanachama kama ilivyoainishwa katika mkataba wake, ambapo inazingatia kueneza lugha ya Kifaransa, maadili ya Kifaransa, na fikra za Magharibi kama vile demokrasia, usekulari, uhuru wa umma, haki za binadamu, na haki za wanawake. Inafanya kazi kuhifadhi urithi wa kikoloni wa Ufaransa katika makoloni yake, na kuhakikisha mwendelezo wake kupitia kueneza lugha na utamaduni wa Kifaransa, jambo ambalo ni muhimu zaidi kwa Ufaransa kuendelea na ukoloni, kupanua ushawishi wake, na kuhakikisha ukuu wa Ufaransa. Baada ya Ufaransa kuondoka katika makoloni yake mwanzoni mwa miaka ya sitini ya karne iliyopita, ilianza kufikiria kuanzisha shirika mfano wa Commonwealth ya Uingereza iliyoanzishwa na Uingereza ili kudumisha ushawishi wake katika makoloni yake ya zamani ambayo ililazimika kuyapa uhuru wa kijuujuu ili kukabiliana na kampeni mpya dhidi yake na dhidi ya Ufaransa kutoka kwa mkoloni mpya, Marekani.

2- Rais wa Tunisia, Kais Saied, alikuwa na hamu kubwa ya kufanya mkutano wa kilele wa Francophonie nchini Tunisia na alitoa hotuba ya ufunguzi kwa lugha ya Kifaransa ili kuthibitisha uhusiano wake na Ufaransa na kufikia malengo yake ili iendelee kumuunga mkono. Alisema: "Ana imani kuwa mazingira ya Francophonie yataweza kubadilisha ahadi zetu kuwa vitendo vya mshikamano na mafanikio yanayoonekana kwa watu wetu, hasa wanawake na vijana wetu" (Monte Carlo ya Ufaransa, 21/11/2022). Nia ya Kais Saied katika mkutano huu ni kwa sababu anatafuta tegemeo la kuimarisha utawala wake, akalipata nchini Ufaransa. Anataka kuhalalisha hatua alizochukua za kuiondoa serikali iliyopita iliyochaguliwa na bunge, kisha kulivunja bunge, kufuta katiba ya 2014, na kuleta katiba mpya. Watu wengi walimpinga, na hatua hizo zilizingatiwa kuwa kinyume cha sheria na demokrasia kwa wanaotazama upande huo. Kwa hivyo, alikabiliwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi, na idadi ndogo ya washiriki katika upigaji kura wa katiba aliyoitoa mnamo 25/07/2022, ambayo ilikuwa karibu 27.54% kama ilivyotangazwa. Wakati nchi wanachama na nyinginezo zinapokuja Tunisia na kushiriki katika mkutano huu bila kuususia kama ishara ya kupinga alichokifanya, Ufaransa inakuwa imemhakikishia uungaji mkono. Kulikuwa na miito ya kufanya mkutano huo katika nchi nyingine, lakini Ufaransa ilisisitiza ufanyike Tunisia. Takriban wajumbe 89 walihudhuria, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali 31, na viongozi 7 wa mashirika ya kimataifa na kikanda, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni kukubali kile alichokifanya Kais Saied, kuhalalisha utawala wake, na kuimarisha mamlaka yake.

3- Rais wa Ufaransa, Macron, alitangaza tena uungaji mkono wake kwa Kais Saied akisema: "Sio jukumu la Rais wa Ufaransa kumpangia Rais wa Tunisia nini cha kufanya kuhusiana na nchi yake. Nilichompa Kais Saied, ambaye namuona kama rafiki yangu, ni kwamba Ufaransa itaiunga mkono Tunisia, ambayo imepitia mapinduzi, ikashinda ugaidi, na kukabiliana na janga la Corona kama ilivyotokea katika nchi zote duniani." Aliongeza: "Nadhani mtu wa sheria za katiba kama Kais Saied anajua mambo kama haya, na huu ndio ulikuwa msingi wa mkutano wangu naye punde tu. Tunisia leo inapitia mabadiliko katika mazingira ya kisiasa. Natumai mabadiliko haya yatakuwa na matokeo na kwamba uchaguzi ujao wa bunge utajumuisha vyama na nguvu zote za kisiasa nchini Tunisia kwa lengo la kukamilisha mchakato huo." Alitaja kuwa "alimualika Saied kuchunguza uwezekano wa ushirikiano kati ya Ufaransa na Tunisia ili kuiunga mkono Tunisia kukamilisha mchakato huu katika ngazi za kiuchumi na kisiasa. Msaada uliotolewa na Ufaransa kwa Tunisia wakati wa mkutano huu, kiasi cha euro milioni 200, si hundi tupu (sharti) kuhusu uhuru wa kimsingi na kanuni za kidemokrasia" (Ukrasa wa Al-Araby Al-Jadeed ukinukuu kituo cha TV5 Monde cha Ufaransa, 21/11/2022). Hapa Macron anatangaza kuwa Ufaransa inamuunga mkono Rais wa Tunisia kisiasa na kiuchumi na kumtaja kuwa rafiki yake, na aliunga mkono hatua alizochukua kwa sababu yeye ni mwanasheria anayejua anachofanya, yaani, hatua hizo ni halali na zinakubalika. Alimpa msaada wa kifedha ambao ni mkopo wa riba wa euro milioni 200, si kama hundi tupu, bali kwa ajili ya utiifu wake kwa Ufaransa, kwa jina la uhuru wa kimsingi na kanuni za kidemokrasia. Umoja wa Ulaya pia ulitangaza kutoa mkopo wa riba kwa Tunisia wa euro milioni 100 ili kusaidia bajeti yake. Wakati Kais Saied alipochagua kufanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi, alielekea Ufaransa mnamo Juni 2020, akionyesha unyonge na udhalili mbele ya Rais Macron. Alikataa ombi la bunge la kuitaka Ufaransa iombe radhi kwa kipindi chake cha ukoloni na alikataa kuuita ukoloni bali kuuita ni "ombi la ulinzi", na akapata mkopo wa riba wa euro milioni 350. Hivyo, alipata tegemeo lake nchini Ufaransa na katika Umoja wa Ulaya unaoongozwa na Ufaransa pamoja na Ujerumani.

4- Kais Saied alipata uungaji mkono wa Ufaransa alipofanya mapinduzi dhidi ya mfumo anaouongoza mnamo 25/07/2021. Yeye mwenyewe alitaja kuwa "alipokea ujumbe wa Kifaransa mnamo 23/07/2021 (yaani siku mbili kabla ya mapinduzi) uliokuja kutoa msaada wa matibabu kusaidia serikali kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa Corona, na kwamba alikuwa katika mchakato wa kuchukua baadhi ya hatua." Alionyesha kuwa "hatua hizo zingetekelezwa kwa idhini ya kimsingi kutoka kwa upande wenye ushawishi." Kufuatia hayo, yaani mnamo 25/07/2021, alilifunga bunge, akaiondoa serikali, na kusitisha katiba. Siku chache baadaye, tarehe 07/08/2021, Macron alimtangazia mwenzake wa Tunisia kuhusu "utayari wa Ufaransa kusimama upande wa Tunisia ili kuhifadhi na kutetea uhuru wake." Taarifa ya Elysee ilisema: "Tunisia inaweza kuitegemea Ufaransa kushinda changamoto za kiuchumi, kijamii na kiafya zinazoikabili" (Al Jazeera, 21/11/2021). Haya yote yanaonyesha kiwango cha uhusiano wa Kais Saied na Ufaransa, na kwamba alipata uungaji mkono kutoka kwayo kufanya mapinduzi dhidi ya mfumo wake ili kuimarisha mamlaka yake alipochukua maamuzi ya kulivunja bunge, kuiondoa serikali, na kuteua serikali inayoongozwa na mwanamke anayehusishwa na mkondo wa Francophonie, na kisha kufuta katiba na kutoa nyingine.

5- Katika kuhitimisha mkutano huo Jumapili tarehe 20 Novemba 2022 katika kisiwa cha Djerba nchini Tunisia, Katibu Mkuu wa shirika hilo, Mnyarwanda Louise Mushikiwabo, alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari: "Djerba haijatuangusha... Tunisia haijatuangusha... Tuko njiani kuelekea Francophonie ya baadaye, ya kisasa na yenye umuhimu"... Mushikiwabo alitoa wito wa kuwekeza katika elimu ya lugha ya Kifaransa katika bara la Afrika na kuiboresha, na kuimarisha uwepo wa lugha ya Kifaransa kwenye mtandao na katika mashirika ya kimataifa... (Monte Carlo ya Ufaransa, 21/11/2022).

Ni wazi kutokana na hayo yote kuwa kufanyika kwa mkutano wa shirika hilo nchini Tunisia, na kusisitiza kwa Ufaransa kuhusu mahali pa kufanyikia, na hotuba ya ufunguzi ya Kais Saied kwa Kifaransa! Kisha yale yaliyokuja katika hotuba ya Macron ya kumsifu Kais Saied, na hotuba ya Katibu Mkuu wa shirika hilo... yote hayo yanaonyesha kiwango cha uungaji mkono wa Ufaransa kwa Rais wa Tunisia na lugha ya Kifaransa!

6- Kuhusu kama hii inamaanisha kuwa ushawishi uliokita mizizi nchini Tunisia umekuwa wa Kifaransa pekee, na kwamba ushawishi wa Uingereza umetoweka nchini Tunisia? Jibu la swali hilo tayari tulilifafanua katika toleo letu la tarehe 01/08/2021, na nitarudia baadhi ya yaliyomo:

[... Kwa kuchunguza msimamo wa Uingereza, inabainika kuwa matukio ya Tunisia yameishtua. Gazeti la The Guardian la Uingereza, kwa mujibu wa tovuti ya Al Jazeera Net mnamo 27/07/2021, lilichapisha makala yenye kichwa "Mtazamo wa The Guardian kuhusu mapinduzi nchini Tunisia: Majira ya kuchipua yanageuka kuwa majira ya baridi." Lilitaja kuwa Tunisia inashuhudia mapinduzi ya kipingamizi, likizingatia kuwa ("kuvamia vituo vya televisheni kwa usalama si ishara nzuri hata kidogo"). Lilitaja kuwa "wananchi wanatenda kwa kutojali na kukubali dhana zisizo za kiliberali kwa sababu uhuru na demokrasia havikuleta utulivu wa kisiasa na uchumi wenye ustawi. Badala yake, ufisadi, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira uliendelea, na kwamba thuluthi moja ya familia nchini Tunisia zilikuwa na hofu ya kuishiwa na chakula mwaka jana baada ya mlipuko wa janga la Corona. Serikali, kulingana na nyaraka zilizovuja, ilikuwa tayari kufuta ruzuku ya mkate katika mazungumzo ya kupata mkopo wa dola bilioni 4 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambao ni wa nne katika miaka 10. Hasira dhidi ya jinsi serikali ilivyoshughulikia janga hili ilizidi tu kutokana na kiwango cha deni la taifa; malipo ya mikopo sasa ni mara sita ya ukubwa wa bajeti ya afya nchini humo"... Kwa haya yote, inabainika kuwa ushawishi wa Uingereza nchini Tunisia umedhoofika kweli, na kukiwa na hali zinazoendelea kuidhoofisha, Ufaransa imepata mlango wa kuingia kwa nguvu ndani ya Tunisia...], kisha tukaongeza katika hitimisho: [Viashiria vyote vya mgogoro mkali wa kimataifa nchini Tunisia vinaonyesha kuwa ni ushindani kati ya Uingereza, mwenye ushawishi wa zamani na mkubwa nchini Tunisia, na Ufaransa, mwenye ushawishi mpya na usio na utulivu... Kutokana na misimamo hii yote ya kimataifa, inabainika kuwa Ufaransa inapambana na Uingereza kugombea mamlaka nchini Tunisia, lakini ushindani huo ni wa ndani ya Ulaya... Kwa hivyo, hautachukua sura ya mzozo mrefu, bali mfumo wa mapatano utarejea na inaelekea kuwa ushawishi wa Uingereza hautaondoka Tunisia. Uingereza ni hodari wa ujanja wa kisiasa ambao Ufaransa haina... Mnamo 22 Dhul-Hijjah 1442 AH - 01/08/2021 AD] Mwisho wa nukuu kutoka kwenye jibu.

Ni wazi kutokana na hili kuwa ushawishi wa Kifaransa ndio wenye nguvu zaidi nchini Tunisia na Rais wa Tunisia Kais Saied anafuata nyayo zake sasa, na kwamba ushawishi wa Uingereza umedhoofika na kurudi nyuma. Lakini hii haimaanisha kuwa ushawishi wa Uingereza umetoweka na kuondoka Tunisia; bali watu wake wengi bado wanavuta kamba... na wanategemea ujanja wa kisiasa wa Uingereza ambao Ufaransa haina...

7- Kuhusu kwa nini Algeria haikuhudhuria mkutano wa Shirika la Francophonie nchini Tunisia, kwanza yenyewe ni mwanachama mwangalizi na si mwanachama kamili... Pili, mkutano huo ulifanyika wakati ambapo Algeria inashuhudia ghadhabu ya watu dhidi ya Ufaransa kutokana na kipindi cha ukoloni na kukataa kwake kuomba radhi kwa kipindi hicho, na kukataa kwake kulipa fidia kwa majanga iliyoyasababisha. Badala yake, imekataa kufungua mafaili yanayohusiana na hilo na milipuko yake ya nyuklia katika jangwa la Algeria katika miaka ya sitini ya karne iliyopita, mbali na kupiga vita lugha ya Kiarabu na Uislamu na majaribio yake ya kuwalazimishia Kifaransa. Idadi ya wazungumzaji wake imepungua sana hadi chini ya thuluthi ya nchi, hivyo Algeria inafanya kazi ya kuachana na matumizi ya Kifaransa. Rais wa Algeria alidokeza kuhusu Tunisia na uhusiano wake na Ufaransa aliposema: (Ufaransa inaipa Algeria uzito mkubwa, akielekeza maneno yake kwa mwandishi wa habari aliyemuuliza ikiwa Ufaransa bado inaichukulia Algeria kama mkoa wa Kifaransa, akisahihisha hilo kwa kusema "Hapana, hapana". Aliendelea: "Unamaanisha nchi nyingine wanayoipa amri kisha inanyamaza na kutekeleza". Baadhi waliona kuwa maneno ya Rais wa Algeria yalikuwa yanaiashiria Tunisia, hasa baada ya matamshi ya Rais Kais Saied wakati wa ziara yake nchini Ufaransa ambapo alisema Tunisia haikuwa chini ya ukoloni bali ilikuwa chini ya "ulinzi"... Tovuti ya Al-Hassary, 08/07/2021).

Kwa taarifa, Morocco pia, ambayo ni mwanachama wa shirika hilo, haikuhudhuria mkutano huo. Hii inaonyesha kuwa tawala za Algeria na Morocco, ambazo ni watiifu kwa Waingereza, zinakataa kutoa msaada kwa Kais Saied ambaye alipindua mfumo mtiifu kwa Waingereza nchini Tunisia na kuonyesha utiifu wake kwa Ufaransa. Mkutano huu unachukuliwa kama msaada kwa Kais Saied na kuhalalisha alichokifanya katika jaribio la kujiegemeza kwa Ufaransa na kujitenga na Uingereza, kinyume na nchi hizo mbili...

8- Katika kuhitimisha, tunasisitiza mambo mawili:

Kwanza: Kwamba yote yanayopigiwa upatu na Ufaransa na shirika lake la Francophonie, pamoja na nchi nyingine za Magharibi, kuhusu demokrasia, uhuru, haki za binadamu, haki za wanawake, na haki za waliowachache, hayamaanishi chochote ikiwa yenyewe ndiyo yenye ushawishi katika nchi hiyo, na ikiwa sivyo, inazitumia kama chombo cha shinikizo. Nchi hizi zilitawala makoloni yake kwa miongo mingi na baadhi kwa zaidi ya miaka mia moja, na hazikuhifadhi uhuru wala haki za binadamu wala demokrasia yao ya kufikirika. Zilikuwa zikivunja vyote hivyo, kuua watu, kuvunja heshima yao na mali zao, kukanyaga utu wao, na kupora utajiri wao kwa ajili ya hisia zao za ukuu na kufikia maslahi yao. Hivyo, si waaminifu na fikra zao; yaani, hawaheshimu kanuni yao wala hawana bidii ya kuitekeleza kama walivyo na bidii ya kupora utajiri na kunyonya damu za watu na kuwaacha wakiteseka kwa umaskini, kunyimwa haki, na magonjwa. Baada ya Ufaransa kuondoka katika makoloni yake, ilianzisha Francophonie, yaani kile kinachoitwa jumuiya ya watu wanaozungumza Kifaransa, ili kudumisha ushawishi wake na kuhakikisha maslahi yake, ikichukulia lugha ya Kifaransa kama njia ya kufikia hilo.

Pili: Kwamba wanasiasa hawa na vyama vyao katika makoloni ya nchi hizo ambao wanafuata demokrasia na fikra za kisekula, wanafanya uharibifu na hawafanyi marekebisho. Wana mtazamo mbovu wa kisiasa, kwani wameghafilika na Magharibi na fikra zake, na wamezoea utiifu kwa Magharibi, iwe kwa Uingereza, Ufaransa, au mkoloni mpya, Marekani, kwa ajili ya kupata msaada na kufika mamlakani.

Suala ni kuwaondoa wote katika ulingo wa kisiasa na utawala, na kufanya kazi ya kuwashawishi watu kuwafuata wanasiasa wanyoofu na wenye uelewa wanaotazama matukio ya kisiasa kutokana na mtazamo wa Uislamu. Wanasiasa wanaokataa utiifu wowote wa kisiasa, kifikra, kiutamaduni, kiuchumi, au kijeshi kwa nchi yoyote ya kikoloni, na wanaofuata ufumbuzi wa Kiislamu wakitegemea Kitabu na Sunnah, wakifanya kazi kwa nguvu na hekima kusimamisha Khilafah Rashidah kwa njia ya Utume ili kutekeleza hukumu za Uislamu... Hii ndiyo mwito wa haki, na hawa ndio watu wake:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلاً مِمَّنْ دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحاً وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

"Na ni nani mbora wa kusema kuliko yule amwitaye (watu) kwa Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, na kusema: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu (waliojisalimisha kwa Mwenyezi Mungu)?" (QS Fussilat [41]: 33)

04 Jamada al-Ula 1444 AH 28/11/2022 AD

Share Article

Share this article with your network