Jibu la Swali
Mashambulizi ya Ndege zisizo na Rubani (Droni) na Maendeleo ya Vita nchini Sudan
Swali:
Siku za hivi karibuni zimeshuhudia maendeleo ya kustaajabisha katika vita nchini Sudan, ambapo droni zilishambulia mji wa Port Sudan, mji mkuu wa kiidara, kwa siku sita mfululizo. Mashambulizi hayo yalilenga uwanja wa ndege wa kiraia, kituo cha anga, na bohari za mafuta, jambo lililosababisha mgogoro wa mafuta nchi nzima. Pia droni zilishambulia mji wa Kassala ulioko mpaka wa mashariki na Eritrea, pamoja na miji mingine. Haya yote yameyalazimu majeshi yaliyokuwa yakielekea Al-Fashir kurudi na kujikita katika kuulinda upande wa Mashariki wa Sudan, kama ilivyoripotiwa na BBC mnamo 2025/5/10. Je, hii inamaanisha kuwa mashambulizi dhidi ya Mashariki mwa Sudan yanalenga kuliondoa jeshi huko Darfur ili eneo hilo libaki mikononi mwa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF)? Je, matukio haya ni utangulizi wa mkutano wa mazungumzo wa Jeddah? Au kuna malengo mengine? Shukrani.
Jibu:
Ili kufichua malengo ya mashambulizi ya droni dhidi ya maeneo nyeti mashariki mwa Sudan, tunabainisha yafuatayo:
Kwanza: Maendeleo yaliyotangulia mashambulizi makali dhidi ya Mashariki mwa Sudan, hususan Port Sudan:
1- Jeshi la Sudan limepata mafanikio makubwa kwa kuvifukuza vikosi vya RSF kutoka miji muhimu ya katikati, kama vile Khartoum, Bahri na Omdurman. Ushindi huu mkubwa umeongeza ari ya jeshi la Sudan ambalo limeanza kujiandaa kuvifukuza vikosi vya RSF huko Darfur. Hali hii ya kupanda kwa ari ya jeshi ni jambo la kawaida baada ya mafanikio hayo, na mwelekeo huu unawalazimu viongozi kuendana na hali hiyo mpya kutokana na shinikizo la umma na shinikizo kutoka kwa maafisa wa jeshi wenye vyeo vya chini, yaani wale wasiojua mambo yanayoendeshwa na mataifa ya nje: (Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, alithibitisha siku ya Alhamisi dhamira ya jeshi ya kuikomboa nchi kutoka kwa "mamluki na vibaraka na kutokomeza RSF." Shirika la Anadolu, 2025/3/13). Kauli hii ilikuwa ya kuendana na hali halisi, na kwa kuwa hali hii ilikuwa na athari kubwa kwa watu na ndani ya jeshi, vikosi vya jeshi vilianza kupambana na RSF katika baadhi ya maeneo ya Darfur. Jeshi lilijitolea kishujaa kuulinda mji wa Al-Fashir, ambao ni mji pekee kati ya miji mikuu mitano ya Darfur ambao bado upo mikononi mwa jeshi, na jeshi likaanza kuelekea Darfur kwa wingi:
(Maendeleo ya hivi karibuni nyanjani yanaashiria kusonga mbele kwa vikosi vikubwa vya jeshi na vikosi vya pamoja kuanzia mji wa Ad-Dabbah kaskazini mwa nchi ili kuvunja mzingiro wa mji wa Al-Fashir, huku vikosi vingine vya pande hizo vikisambaa katika majimbo ya Kordofan na kupata ushindi mkubwa njiani kuelekea mjini humo kutoka upande mwingine. Al-Quds Al-Arabi, 2025/4/19). Mwelekeo huu unaosukumwa na watu baada ya ushindi wa Khartoum na kupata mwangwi mkubwa ndani ya jeshi, si mwelekeo wa Marekani. Hivyo, Burhan alijaribu kuzuia mwelekeo huu: (Al-Burhan alionya dhidi ya kampeni za upotoshaji zinazoeneza fikra kwamba vita vinalenga makabila fulani, akisisitiza kuwa "vita vyetu ni dhidi ya yeyote anayebeba silaha dhidi ya dola, na si dhidi ya kabila lolote," akiona kuwa uvumi huu unalenga "kuwahamasisha watu na kuwavuta kwenye mauaji." Alibainisha kuwa "uasi wa kiongozi wa kabila haumaanishi uasi wa kabila zima," RT, 2025/4/29). Ni kana kwamba alitaka kuzuia kasi ya jeshi kuelekea Darfur kwa kisingizio kuwa baadhi ya makabila huko yanadhani jeshi liko dhidi yao, na kana kwamba anataka jeshi lisubiri kidogo.
2- Baada ya kushindwa vibaya kwa vikosi vya RSF katika eneo la katikati na kupoteza maeneo yao makubwa huko Khartoum, Bahri na Omdurman, na kupoteza wapiganaji na viongozi wengi nyanjani, vimeingia katika hali ya unyonge na udhaifu. Baada ya hapo, vilielekea ngome yao huko Darfur ambako vinadhibiti sehemu kubwa na kuuzingira mji wa Al-Fashir. Kukusanyika huku kwa vikosi vya RSF kulikuwa kulingana na malengo ya Marekani nchini Sudan. Ni kawaida katika hali kama hii kwamba baadhi ya wafuasi wa RSF wajitenge na vikosi hivyo na kuwe na ugumu katika kuajiri wapiganaji kutoka makabila yanayowaunga mkono, kwa kuwa wanapigana vita ambavyo tayari vimeshindwa mbele ya mpinzani mwenye nguvu, ambaye ni jeshi la Sudan. Hii inamaanisha kuwa ari ya RSF iko chini. Kwa hivyo, vikosi vya jeshi ndani ya Al-Fashir vilikuwa na uwezo wa kuzuia mashambulizi yake ya mara kwa mara, ikimaanisha kuwa shambulio lake dhidi ya Al-Fashir lilikosa nguvu. Hivyo, kulihitajika hatua kubwa ili kurudisha ari ya vikosi vya Hemedti na kuonyesha kuwa bado vina nguvu na vina uwezo wa kushambulia na kutishia maeneo ya mbali na salama ya jeshi la Sudan kama vile Mashariki mwa Sudan.
3- Licha ya utiifu wa watawala wake kwa Waingereza, nchi ya Imarati (UAE) haijaacha kutoa msaada kwa kibaraka wa Marekani na kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), kwa matumaini ya kuwa na ushawishi kwake na kwa wafuasi wake. Hiki ni kitendo kinachofanana na kile inachofanya huko Libya kwa kumuunga mkono kibaraka wa Marekani, Haftar. Sudan imetangaza mara kwa mara kutoridhishwa kwake na UAE na kuishutumu kwa kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa RSF. Kutokana na shutuma hizi, UAE ilifunga ubalozi wake nchini Sudan na haikuuhamishia mji wa Port Sudan kama nchi nyingine zilivyofanya baada ya kuanza kwa vita huko Khartoum mnamo Aprili 2023. Lakini Sudan iliendelea kubaki na ubalozi na ubalozi wake mdogo nchini UAE. Katika hali hii ya hasira iliyoongezeka, Sudan iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya UAE kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari yanayofanywa na RSF nchini Sudan, lakini mahakama hiyo ilikataa ombi hilo la Sudan: (Mahakama ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa haiwezi kusikiliza kesi iliyofunguliwa dhidi ya UAE, na ilikataa ombi la Sudan la kutoa amri ya hatua za dharura na kuamuru kuondolewa kwa kesi hiyo kwenye ajenda yake. Reuters, 2025/5/6). Kisha Sudan ilichukua hatua nyingine kali dhidi ya UAE, ambayo ni kukata uhusiano wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu, na kuuondoa ubalozi na ubalozi mdogo wa Sudan huko. Kisha matukio yanayohusiana na UAE yakafuatana: (Jeshi la Sudan lilitangaza, Jumapili, kuhusu kuharibiwa kwa ndege ya mizigo ya Imarati na msaada wa kijeshi kwa vikosi vya RSF... na kueleza kuwa ndege hiyo ilikuwa imebeba mahitaji ya kijeshi... pamoja na droni za kujilipua na za kimkakati. Sudan Tribune, 2025/5/4).
Pili: Malengo ya maendeleo haya na matokeo yake:
1- Kutokana na kuongezeka kwa mapigano huko Khartoum tangu 2023, Baraza la Uongozi lililazimika kuuhamisha mji mkuu kwa muda hadi mji wa Port Sudan ikiwa ndilo eneo salama zaidi. Pamoja na wanachama wa Baraza la Uongozi, ujumbe wa kidiplomasia wa kigeni, mashirika ya misaada ya kimataifa, na wakazi wengi waliokimbia eneo la katikati walihamia huko kutafuta usalama na kuwa wakimbizi. Eneo hili linawakilisha mapafu ambayo Sudan inavuta kwayo pumzi wakati wa vita; hapo kuna bandari inayoisambazia Sudan bidhaa zinazotoka nje, na hapo kuna uwanja wa ndege wa kimataifa pekee unaofanya kazi, kwani uwanja wa ndege wa Khartoum bado haufanyi kazi hadi sasa licha ya jeshi kuudhibiti. Kwa kuwa ni mapafu ya Sudan na makao makuu ya muda ya serikali, mashambulizi ya droni ya mfululizo kwa siku kadhaa yamesababisha mshtuko mkubwa miongoni mwa Wasudan na ndani ya jeshi. Mashambulizi haya yanaonyesha vikosi vya RSF kama nguvu ambayo haijavunjika kama wengine walivyodhani, bali inamiliki uwezo mkubwa ambao haujauonyesha hapo awali. Pia inaonyesha kuwa jeshi halipaswi kujitawanya katika jangwa la Darfur, bali lazima lijikite katika kuimarisha vituo hivi muhimu na kuvilinda, kama vile bandari, uwanja wa ndege, na bohari za mafuta. Aidha, moto mkubwa uliozuka katika bohari za mafuta unatoa ishara kwa jeshi kuhusu kuharibiwa kwa huduma zake za kilojistiki zinazohitajika kwa vita vya Darfur, hivyo lazima lisubiri na kuzifanyia marekebisho kabla ya kuelekea Darfur.
2- Mashambulizi yaliyopata vituo vya mji wa Port Sudan, uwanja wa ndege wa Kassala na bandari ya "Flamingo" yalifanywa kwa droni nzito za China kulingana na uchambuzi wa vyanzo mbalimbali ikiwemo BBC mnamo 2025/5/10. Moja ya droni hizo inaweza kubeba kilo 40 na nyingine kilo 200 za mabomu na makombora yanayoongozwa. Vikosi vya RSF havikuwahi kutumia droni kama hizo hapo awali, na droni zinazofanana na hizo zimeonekana katika uwanja wa ndege wa mji wa Nyala unaodhibitiwa na vikosi vya RSF, ambao ni uwanja ule ule ambao jeshi lilisema limeharibu ndege ya mizigo ya UAE ndani yake.
3- Nchi ya UAE ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza katika eneo hili kupata droni za China miaka kadhaa iliyopita. Tovuti ya Defence News mnamo 2019/5/2 ilizungumzia matumizi ya UAE ya droni hizi kumuunga mkono Khalifa Haftar katika kuushambulia mji wa Tripoli nchini Libya. Tovuti ya Times Aerospace pia ilizungumzia matumizi ya UAE ya droni hizi za Kichina kushambulia maeneo ya harakati za kijihadi nchini Iraq na Afghanistan mwaka 2014. Hii inaashiria kuwa UAE imejihami kwa miaka mingi na aina mbalimbali na nzito za droni za Kichina. Inawezekana kabisa kuwa ndiyo inayohusika na mashambulizi haya Mashariki mwa Sudan, iwe moja kwa moja kutoka baharini au kwa kuvipatia vikosi vya RSF droni hizo, ikiwa na hasira kutokana na serikali ya Al-Burhan kuumbua uovu wake katika mahakama ya kimataifa, kukata uhusiano nayo, na kuharibu ndege yake ya mizigo.
4- Lengo la mashambulizi lilikuwa ni viwanja vya ndege, bandari, na kituo cha jeshi la majini cha "Flamingo", na mara nyingi moto ulizuka ambao ulihitaji siku kadhaa kuudhibiti, jambo linaloashiria kulengwa kwa hifadhi za mafuta. Waziri wa Nishati na Mafuta wa Sudan, Mohieddin Mohamed Naeem, alifichua kuungua kwa bohari kuu tano za kuhifadhia mafuta kutokana na mashambulizi ya droni katika siku ya kwanza ya kampeni hiyo (Sauti ya Sudan, 2025/5/6). Kutokana na kuendelea kulengwa kwa vituo vya nishati, waziri huyo alitoa maelekezo ya kufunga bomba la kusafirisha mafuta ya Sudan Kusini kutokana na droni kushambulia kituo cha kusukuma mafuta hayo mashariki mwa Atbara (Al Jazeera Net, 2025/5/11).
5- Shambulio hilo lilijikita katika mafuta, yaani kulinyima jeshi la Sudan nishati hiyo ili kuzuia lisiweze kufanya operesheni kubwa huko Darfur na hasa mji wa Al-Fashir. Hii ni pamoja na kuifanya serikali ionekane dhaifu na isiyoweza kulinda makao makuu yake pamoja na kutoa mafuta na umeme kwa mahitaji yote ya Sudan, (Shirika la Umeme la Sudan lilitangaza "kuharibiwa kwa kituo cha umeme cha Sudan kutokana na kulengwa kwa droni na kukatika kwa umeme." Anadolu, 2025/5/8).
6- Ni wazi kutokana na haya yote kuwa mashambulizi makubwa Mashariki mwa Sudan, hususan dhidi ya vituo vya kimkakati vya mji wa Port Sudan, yanahusiana na vita vya Darfur. Yanatokea ili kulilazimisha jeshi kuacha kuishambulia Al-Fashir na kuelekea Mashariki kuulinda mji wa Port Sudan... BBC iliripoti mnamo 2025/5/10 kuwa vikosi vya jeshi vilivyokuwa vikielekea Al-Fashir vimezalimika na shambulio la Mashariki mwa Sudan kurudi na kujikita katika kuulinda upande huo.
Tatu: Hitimisho linalotokana na matukio haya:
1- Inawezekana kuwa jeshi la Sudan baada ya mashambulizi haya mazito limeanza kuhofia uwezo mpya wa vikosi vya RSF, na linapoteza uwezo wa kupata mafuta yanayohitajika kuendesha zana zake katika vita lilivyopanga huko Al-Fashir na Darfur nzima. Hii ni mbali na umuhimu wa kuimarisha ulinzi Mashariki mwa Sudan kwa hofu ya mawimbi mengine ya mashambulizi, na hivyo shinikizo la jeshi huko Darfur kupungua na jeshi kushughulishwa na upande wa Mashariki.
2- Kwa upande wa vikosi vya RSF, vikosi vyake vitapata nguvu na kuwa katika hali bora ya kisaikolojia kupata matokeo huko Al-Fashir, haya yote yakiwa na msaada kutoka UAE na kutoa droni nzito za Kichina.
3- Inatarajiwa kuwa mashambulizi yataongezeka dhidi ya mji wa Al-Fashir na kwamba vikosi vya jeshi vilivyokuwa njiani kusaidia mji huo vitarudi nyuma, na Baraza la Uongozi litachukua muda kurekebisha uharibifu huo Mashariki mwa Sudan. Haielekei kuwa mazungumzo ya Jeddah yataanza tena kabla ya vikosi vya RSF kuudhibiti mji wa Al-Fashir, au kuwa na nguvu kubwa hapo, kwani mji huo ni muhimu huko Darfur. Wakati huo, Marekani itatengeneza mizani ya nguvu na udhibiti kati ya pande mbili za Sudan (Jeshi na RSF), ili mazungumzo ya Jeddah yakianza tena, RSF iwe imejivua vazi la kushindwa na kusimama kwa kujiamini kwa nguvu na udhibiti wake imara, ikiwa tayari imeunda serikali ya de-facto huko Darfur. Hii ina maana ya kuandaa mazingira ya kukomaza mgawanyiko, na kuufanya kuwa ukweli unaopaswa kukubalika.
Nne: Inasikitisha sana kuona Marekani kafiri mkoloni ikiweza kuendesha vita vinavyoangamiza roho nchini Sudan na kuwatumia vibaraka wake kutekeleza hilo hadharani na si kwa siri, waziwazi na si kwa kujificha. Al-Burhan na Hemedti wanapigana kwa damu za watu wa Sudan bila sababu yoyote isipokuwa kutumikia maslahi ya Marekani, ambayo inataka kurudia mgawanyiko wa Sudan kama ilivyofanya katika kuitenganisha Kusini mwa Sudan. Sasa inajitahidi kuitenganisha Darfur kutoka sehemu iliyobaki ya Sudan. Kwa hivyo, jeshi linaelekeza nguvu zake katika maeneo mengine ya Sudan na RSF inaelekeza nguvu zake huko Darfur. Ikiwa waaminifu ndani ya jeshi watachukua hatua kurudisha udhibiti wa Darfur, RSF huhamishia vita katika maeneo mengine ya Sudan ili kulishughulisha jeshi, hivyo vikosi vyake hujiondoa Darfur kuelekea Mashariki mwa Sudan ambako RSF inazidisha mashambulizi ya droni... hayo yote ni kwa ajili ya kuiwezesha RSF kuidhibiti Darfur kikamilifu!
Katika kuhitimisha, tunawalingania kwa namna ile ile tuliyowalingania katika jibu letu lililopita la tarehe 2023/12/19:
Enyi watu wetu katika Sudan ya Uislamu mtukufu... Sudan ya msikiti wa Dunqula, msikiti wa kwanza uliojengwa na Waislamu wa mwanzo nchini Sudan... Sudan ya ushindi mkubwa wa Kiislamu katika zama za Khalifa Uthman (ra), ambapo aliamuru gavana wa Misri kuingiza nuru ya Uislamu nchini Sudan, akatuma jeshi la Uislamu likiongozwa na Abdullah bin Abi As-Sarh, na ushindi ukapatikana mwaka wa 31 Hijiria... Na hivyo Uislamu ukaenea kwa kasi kwa fadhila za Allah (swt) hadi ukaijaza Sudan yote, kuanzia Kaskazini hadi Kusini na Mashariki hadi Magharibi... Kisha ukaendelea katika zama za Makhalifa wa Kiislamu...
Enyi watu wetu nchini Sudan wapiganaji jihadi dhidi ya Waingereza tangu mwaka 1896 hadi katikati ya Vita vya Kwanza vya Dunia 1916, pale alipouawa shahidi shujaa mcha Mungu na mwenye nguvu "Ali bin Dinar", gavana wa Darfur, mwanachuoni huyo mujahid ambaye alikuwa na fadhila ya kurekebisha Mikat ya Madina na watu wa Sham "Dhul-Hulayfah" na kuchimba visima vya kuwanywesha mahujaji ambavyo vinaitwa kwa jina lake hadi leo "Abyar Ali"...
Enyi watu nchini Sudan... Tunawalingania, basi darasini jambo hili kabla ya majuto na wakati huo majuto hayatofaa... Washikeni mikono pande zote mbili zinazopigana na walazimisheni kufuata haki... Na kinusuruni Hizb ut Tahrir ili kusimamisha Khilafah ya Rashidun, kwani ndani yake mna utukufu wa Uislamu na Waislamu na udhalili wa ukafiri na makafiri... Na radhi kutoka kwa Allah ni kubwa zaidi...
إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ
"Hakika katika hayo kuna mawaidha kwa mwenye moyo au akatega sikio, naye akawa shahidi (mwenye kuhudhurisha akili)." (QS Qaf [50]: 37)
Mnamo tarehe 23 Dhul-Qi'dah 1446 Hijiria 2025/5/21 Miladi