Home About Articles Ask the Sheikh
Masuala

Jibu la Swali: Sababu za Azerbaijan Kuukomboa Mkoa wa Karabakh

October 05, 2023
2684

Swali:

Zaidi ya Waarmenia 100,000 kati ya 120,000 waliondoka katika mkoa wa Karabakh kufikia tarehe 30/09/2023. Waliondoka mkoani humo na kukimbilia Armenia baada ya operesheni ya kijeshi iliyofanywa na Azerbaijan mnamo tarehe 19/09/2023 katika mkoa huo ili kuukomboa na kuusafisha kutoka kwa vikosi vya waasi wa Kiarmenia ambao waliweka chini silaha zao na kutangaza kusalimu amri. Vikosi vya kulinda amani vya Urusi, ambavyo ni wadhamini wa usalama wao, haviingilia kati, na Armenia ilijitenga na mapigano hayo pamoja na mazungumzo ya amani yaliyofanyika kati ya Azerbaijan na vikosi vya waasi. Ni nini kilitokea? Na kwa nini Armenia ilijitenga? Na kwa nini vikosi vya Urusi havikuingilia kati? Na ni upi msimamo wa Marekani na Ulaya, hususan Ufaransa ambayo pamoja na Marekani ni wanachama wa Minsk Group?

Jibu:

Ili kuweka wazi jibu, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Tulisema katika jibu la swali la tarehe 05/10/2020 kwamba "uasi wa Waarmenia dhidi ya Azerbaijan ulianza mnamo mwezi Februari 1988 kwa uungaji mkono wa Urusi, na walitangaza udhibiti wao wa eneo la milimani la Karabakh mwaka 1991. Pia walitangaza jamhuri huru humo na vita viliendelea hadi mwaka 1994. Azerbaijan ilipoteza zaidi ya 20% hadi 24% ya ardhi yake ambayo inajumuisha mkoa wa Karabakh wenye mikoa 5, pamoja na mikoa mingine 5 upande wa magharibi wa nchi hiyo, mbali na sehemu kubwa za mikoa ya Agdam na Fizuli. Waliwafukuza takriban Waislamu milioni moja wa maeneo hayo." Waarmenia walifanya operesheni ya usafishaji wa kikabila dhidi ya Waislamu katika miaka hiyo, wakaua makumi ya maelfu na kuwafukuza karibu Waislamu wote kutoka mkoani humo na maeneo jirani, na kupora ardhi na mali zao kwa msaada wa Warusi. Kwa sababu hiyo, baada ya Azerbaijan kufanya operesheni yake ya hivi karibuni, Waarmenia waliokamata mkoa huo tangu miaka 30 iliyopita walianza kuogopa adhabu au kulipizwa kisasi, hivyo walianza kuhama mkoani humo kuelekea Armenia. Azerbaijan iliwafungulia Ukanda wa Lachin kwa ajili ya kuhama. Waziri Mkuu wa Armenia alisema ("kwamba hakuna Mwarmenia atakayebaki Karabakh ndani ya siku chache" na akadai kuwa "kuna usafishaji wa kikabila na kufukuzwa kwa lazima"... Al-Jazeera 28/09/2023). Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan ilimjibu katika taarifa ikisema ("kwamba Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan, anatambua vyema kuwa wakazi wa Kiarmenia wanaondoka Karabakh kwa hiari yao wenyewe... Azerbaijan haikuwalenga kabisa raia katika operesheni yake ya hivi karibuni huko Karabakh", ikinukuu tamko la Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan mwenyewe, kwamba "hakuna tishio la moja kwa moja kwa raia huko Karabakh". Taarifa hiyo iliongeza, "Tuko tayari kuwapatia hali bora ya maisha kuliko walivyokuwa wakati walipokuwa mateka wa baraza la kijeshi lililoundwa na Armenia"... "Na Kremlin ilisema 'haioni sababu ya Waarmenia kukimbia eneo hilo'"... Anadolu, Asharq Al-Awsat 28/09/2023). Shirika la habari la AFP liliripoti mnamo 29/09/2023 kwamba "wale waliokutana nao katika mji wa mpakani wa Armenia, Goris, ambapo wanaume wote wana uzoefu wa kijeshi na mapigano, walichoma sare zao na nyaraka zao za kijeshi na hata zaidi ya hapo." Hivyo, inaonekana kwamba vikosi vya Azerbaijan havikuwalenga Waarmenia kwa kuwaua au kuwafukuza kama walivyofanya wao miaka 30 iliyopita dhidi ya Waislamu.

2- Marekani ilikuwa ikifanya kazi ya kuiondoa Armenia kutoka kwenye ushawishi wa Urusi na kuweka ushawishi wake kupitia Uturuki kwa kufanya mikataba kati ya pande hizo mbili ili kuzikurubisha, kama ilivyotokea mwaka 2009. Lakini bunge la Armenia halikuidhinisha mkataba huo hivyo haukutekelezwa; badala yake, Armenia iliufuta mkataba huo kabisa. Tuliashiria hilo katika jibu la swali la tarehe 05/10/2020 tukisema, "Lakini baada ya miaka tisa; mnamo Machi 2018, kwa shinikizo kutoka kwa Urusi, Armenia iliufuta rasmi mkataba huo kwa sababu ya kufuata ushawishi wa Urusi. Kwa hivyo, Marekani ilipoteza fursa ya kuichukua Armenia kutoka kwa Urusi kupitia mkataba huu na Uturuki. Badala yake, Urusi iliimarisha ushawishi wake nchini Armenia kwa kuimarisha ghala lake la makombora katika kituo chake cha kijeshi cha Gyumri nchini Armenia, na kisha ikasaini mkataba wa ulinzi wa anga wa pamoja mnamo Desemba 2015 na Armenia, ikapeleka kikosi cha ndege za MiG-29, maelfu ya wanajeshi, magari ya kivita, na mifumo ya ulinzi wa anga na makombora ya masafa marefu ya S-300 pamoja na ulinzi wa anga wa masafa ya kati wa SA-6. Urusi pia iliingiza Armenia katika soko lake la Eurasian Economic Union ambalo lilianza kutumika tarehe 01/01/2015 pamoja na Belarus, Kazakhstan, na Kyrgyzstan. Nchi hizi, ikiwemo Armenia, zikawa soko la bidhaa za Kirusi chini ya kisingizio cha uhuru wa harakati za bidhaa na huduma katika nyanja zote, na Pato la Taifa la soko hili linakadiriwa kuwa zaidi ya dola trilioni 5 za Marekani, ambapo sehemu kubwa ni kwa faida ya Urusi." Na tulisema katika jibu la swali lililotajwa, "Urusi iko nyuma ya Armenia, nchi ndogo kwa eneo, idadi ya watu, na uwezo ikilinganishwa na Azerbaijan. Urusi ndiyo inayofadhili na kuiunga mkono Armenia kwa silaha, zana, na kila kitu kinachohitajika ili kubaki, na ni mwanachama wa Jumuia ya Mkataba wa Usalama wa Pamoja (CSTO) inayoongozwa na Urusi na ina uwepo mkubwa wa kijeshi huko." Ikiwa uungaji mkono huu utasimama, Armenia itaanguka na haitaweza kusimama mbele ya Azerbaijan ambayo imeanza kuungwa mkono na Uturuki na Marekani iko nyuma yake. Kisha yakaja mazingira ya mwaka 2020 ambapo Azerbaijan iliweza kurejesha eneo moja katika operesheni ya kijeshi iliyofanywa kwa uungaji mkono wa Uturuki, iliyoanza tarehe 27/09/2020 na kuendelea kwa siku 44. Kisha makubaliano yakafikiwa kati ya Azerbaijan na Armenia mnamo 09/11/2020 ambapo Armenia ingejiondoa kutoka maeneo ya Azerbaijan yaliyokaliwa, isipokuwa mkoa wa Karabakh ambao ulikuwa na idadi kubwa ya Waarmenia waliotangaza jamhuri humo. Urusi ilikubaliana na pande zote mbili na Uturuki kuingiza vikosi vyake vya takriban wanajeshi elfu mbili mkoani humo hadi mazungumzo yatakapoamua hatima ya mkoa huo, na Urusi ilitosheka na hilo.

3- Lakini baada ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine na ugumu iliyopata katika kumaliza vita hivyo, ambavyo vinaendelea tangu vilipoanza tarehe 24/02/2022 hadi leo, Marekani iliona fursa ya kuiondoa Armenia kutoka kwenye ushawishi wa Urusi au kushiriki nayo, na kufidia kushindwa kwake katika jaribio la awali lililoanza mwaka 2009 kama tulivyotaja hapo juu. Hasa kwa kuwa Marekani ilikuwa imepata njia ya kumfikia Pashinyan, Waziri Mkuu wa Armenia. Marekani ilianza kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Armenia mnamo 11/09/2023 kwa muda wa siku 10 karibu na mji mkuu wa Armenia, Yerevan. Jambo hilo lilizua hasira ya Urusi ambapo iliyalaani yalipotangazwa wiki moja kabla ya kufanyika, jambo linaloonyesha kuwa Armenia ilichukua uamuzi huo bila kuifahamisha Urusi, hatua inayoonyesha nia yake ya kuachana na utiifu kwa Urusi na kuifuata Marekani. Msemaji wa Kremlin, Peskov, alisema mnamo 07/09/2023 ("Ni wazi kwamba kufanya mazoezi kama haya hakuleti utulivu katika eneo au kuimarisha mazingira ya kuaminiana... Na Urusi itaendelea na majukumu yake kama msimamizi wa usalama"... Asharq Al-Awsat, 07/09/2023). Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan, alikuwa amekanusha moja kwa moja tangazo la Urusi kwamba Armenia ingeandaa mazoezi ya CSTO mwaka huu, jambo lililoilazimu Urusi kuyafanyia nchini Belarus mnamo tarehe 1 na 06/09/2023, na Pashinyan alikataa kutuma vikosi vya Armenia kushiriki!

4- Katika mazingira haya, Marekani ilimwashiria Aliyev kupitia Uturuki kufanya mashambulizi ili kuukomboa mkoa wa Karabakh. Azerbaijan ilitangaza mnamo 19/09/2023 kufanya operesheni ya kijeshi kuukomboa mkoa wa Karabakh uliokuwa umekaliwa na Waarmenia, na ikatakeleza kusalimu amri kikamilifu na bila masharti kwa Waarmenia, na ikatangaza kudhibiti takriban maeneo 90 ya Waarmenia katika eneo hilo. Wakati huo huo, mamlaka za Kiarmenia huko Karabakh zilitangaza kwamba ("idadi ya wahanga wa operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan iliyodumu kwa siku moja mkoani humo ilifikia vifo 213 na majeruhi 400, na zaidi ya watu 7,000 walihamishwa kutoka vijiji 16". Ikumbukwe kwamba mkoa huo unakaliwa na takriban watu 120,000, wengi wao wakiwa Waarmenia baada ya kuwafukuza wakazi wake Waislamu kwa msaada wa Urusi miaka 30 iliyopita. Wakati huo huo, Azerbaijan ilitangaza kwamba ilipoteza wanajeshi wapatao 192 na zaidi ya 500 walijeruhiwa katika operesheni ya kijeshi iliyofanyika kurejesha Karabakh. Rais wa Azerbaijan, Aliyev, alitangaza mnamo 20/09/2023 kwamba nchi yake imerejesha mamlaka yake juu ya Karabakh, na Baku ilizungumzia kuanza kwa wanamgambo wa Kiarmenia kusalimisha silaha zao... Al-Jazeera, Al-Arabiya 21/09/2021). Urusi haikupinga kwani haitaki kujishughulisha sasa na vita vingine mradi imetingwa na vita vya Ukraine.

5- Armenia yenyewe haikushiriki katika mapigano ya hivi karibuni dhidi ya Azerbaijan na ilijitenga nayo, kiasi kwamba haikulaani operesheni hiyo. Inaonekana lengo lilikuwa ni kuifichua Urusi na kuiweka katika hali ngumu kwa sababu ya kushughulika kwake na Ukraine, na kisha kuonyesha usaliti wake kwa Waarmenia kwa kutowatetea kama utangulizi wa Waarmenia kujitenga na Urusi kikamilifu au kwa kiasi fulani. Armenia haiwezi kupigana vita dhidi ya Azerbaijan bila uungaji mkono wa Urusi. Kwa sababu hiyo, Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan, alitoa mwito wa amani ya kudumu kati ya Armenia na Azerbaijan, na kuhakikisha haki na usalama kwa wakazi wa Karabakh. Armenia haiwezi kukabiliana na Azerbaijan bila msaada wa Urusi, na maadamu Urusi na "vikosi vya amani vya Urusi" havikucheza upande wa Waarmenia mkoani humo, bali vilijitenga, basi vikosi vya waasi wa Kiarmenia vilisalimu amri na kuanza kusalimisha silaha zao. Kisha mamlaka za Kiarmenia katika eneo la Nagorno-Karabakh zilisema Alhamisi 28/09/2023: (kwamba Rais wa jamhuri iliyotangazwa upande mmoja, Samvel Shahramanyan, alisaini amri ya kuvunja taasisi zote za serikali kuanzia Januari 1, 2024. Kwa mujibu wa amri hiyo, jamhuri iliyotangazwa upande mmoja haitakuwepo kuanzia siku hiyo, kwa mujibu wa kile kilichoripotiwa na shirika la habari la Reuters... Asharq Al-Awsat, 28 Septemba 2023). Kremlin ilitangaza (kwamba imepokea taarifa ya tangazo la mamlaka za Karabakh kuwa itajivunja mnamo Januari 1, 2024. Kutokuingilia kati kwa Urusi katika operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan kuliifanya Armenia kuishutumu Moscow, mshirika wake wa jadi, kwa kuitupa... Asharq Al-Awsat, 28/09/2023). Hivyo, Urusi ilionekana mbele ya Waarmenia kama imeacha kuwatetea kwa sababu imetingwa na Ukraine!

6- Marekani inaonekana ikiendeleza mawasiliano yake na pande zote mbili, Azerbaijan na Armenia, kana kwamba ndiyo inayosimamia mzozo huo. Waziri wake wa mambo ya nje, Blinken, alifanya mazungumzo ya simu na marais wa pande zote mbili, Aliyev na Pashinyan, na kuwahimiza kufanya mazungumzo, akimhakikishia Pashinyan "uungaji mkono wa Washington kwa enzi ya Armenia". Alieleza kuwa "amani ya haki italeta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili na itakuwa mabadiliko makubwa kuelekea uzuri katika mkondo wa historia baada ya miaka mitatu ya mapigano." Marekani haikutetea kwa jina la waziri wake wa mambo ya nje enzi ya Waarmenia huko Karabakh, bali ilitetea enzi ya Armenia pekee, na ikataka kupatikana kwa amani kati ya Azerbaijan na Armenia. Hii inaonyesha kuwa Marekani inakubaliana na operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan na kwamba hilo lina maslahi kwake katika kuweka utawala wa Marekani katika eneo hilo. Marekani inatafuta kuipata Armenia kama ilivyoipata Azerbaijan kupitia Erdogan, na kuifanya iachane na utiifu wake kwa Urusi inapoona ya mwisho ikaisaliti. Marekani imefanikiwa kwa kiasi fulani katika hilo kwani imeonekana kwa Waarmenia kwamba Urusi imewasaliti na haiwezi kudhamini usalama wao, nao ni watu maskini, waliofungiwa kati ya milima, wachache kwa idadi na zana, na dhaifu kwa nguvu ikilinganishwa na Azerbaijan ambayo inawazidi mara nyingi kwa idadi, zana, nguvu, utajiri, bahari na hali ya hewa. Marekani ilianza kuwasiliana nao na kufanya mikutano kati ya maafisa wao na Waazerbaijan baada ya operesheni ya Azerbaijan ya mwaka 2020 ili kuwapokonya Warusi udhibiti. Waziri wake wa mambo ya nje, Blinken, aliwakutanisha wenzake wa Azerbaijan na Armenia huko Washington mnamo tarehe 20/09/2022 na 08/11/2022.

7- Ulaya ilijaribu kuingilia kati lakini ikashindwa. Ufaransa ilikuwa miongoni mwa nchi zilizochukizwa zaidi na operesheni hiyo, ambapo Rais wake Macron alitangaza kuwa ("analaani vikali operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa na Azerbaijan katika mkoa wa Karabakh" na akatoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa shambulio hilo"... France24, 20/09/2023). Pamoja na hayo, haikuweza kuwasiliana na nchi hizo mbili, na ilijaribu kwa msaada wa Ujerumani kucheza nafasi madhubuti katika suala hilo. Iliwakaribisha pamoja na Ujerumani maafisa wa kidiplomasia kutoka Azerbaijan na Armenia huko Brussels mnamo 26/09/2023 ili kujadili mkondo wa matukio ya hivi karibuni. Ufaransa pia ilitoa wito wa ("hatua za kidiplomasia za kimataifa kukabiliana na kuitupa Armenia kwa Urusi. Iliona kuwa kuhama kwa watu huko Karabakh kunatokea mbele ya macho ya Urusi inayoshirikiana na inayopeleka vikosi vya kulinda amani katika eneo hilo". Ujerumani kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, Annalena Baerbock, ilitoa wito wa "kuruhusu kutumwa kwa waangalizi wa kimataifa huko Karabakh" na ikaona kuwa hilo "litakuwa ushahidi wa kuaminika kwamba Azerbaijan iko siri katika ahadi yake ya usalama wa wakazi wa Karabakh" na kwamba itaongeza msaada wake kwa Waarmenia kutoka euro milioni mbili hadi euro milioni 5 kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu... Al-Arabiya, na Al-Jazeera 27/09/2023). Ufaransa inataka kubaki na nafasi yoyote ile, na inaichochea Ujerumani kushirikiana nayo ili wawe na nafasi. Pamoja na hayo, nafasi hii bado haina nguvu mbele ya nafasi ya Marekani ambayo inakaribia kushikilia karata zote za suala hilo!

8- Na muhtasari ni kwamba matukio ya Karabakh yanaashiria mambo yafuatayo:

a- Urusi inaelekea imetambua kuwa vita hivi vimelekezwa dhidi yake na vimepangwa na Marekani kupitia Uturuki ya Erdogan na Azerbaijan ambayo imekuwa chini ya usimamizi wake, na vita hivyo vitaishughulisha bila faida na kutawanya nguvu zake, wakati yenyewe sasa inajikita kwenye vita vyake nchini Ukraine. Hivyo ni vita vya hatima na haitaki kuvipoteza, na inajua kuwa ikivipoteza itapoteza kila kitu, na ikivishinda itaweza kurejesha ushawishi wake katika maeneo iliyoyapoteza. Wakati huo huo, haitaki kugongana na Uturuki huku ikiihitaji katika mazingira haya na vikwazo vilivyowekwa dhidi yake, kwani Uturuki ndiyo lango lake kuelekea ulimwengu wa Magharibi. Vilevile inataka kudumisha uhusiano wake na Azerbaijan ambapo ina uwekezaji huko, hasa katika rasilimali za nishati zenye thamani ya dola bilioni 6, na ujazo wa biashara kati yao ni zaidi ya dola bilioni 4. Ama kuhusu Armenia, nchi hiyo ni mzigo kwake katika kila kitu. Wala haiondoi uwezekano wa kuirejesha katika ushawishi wake kamili kama ilivyokuwa ikiwa itashinda vita nchini Ukraine.

b- Inafahamika kutokana na hatua za Marekani kuwa iko nyuma ya vita hivi, na inataka kuishughulisha Urusi navyo ikiwa itasimama na kuzingatia mkataba wa usalama wa pamoja ambao Armenia ni mwanachama wake. Mkataba wake unasisitiza kuwa "shambulio dhidi ya mwanachama yeyote ndani yake linachukuliwa kama shambulio dhidi ya wanachama wengine wote." Hivyo ingeilazimu kuingilia kati ili kuwalinda Waarmenia kama ilivyoingilia kati mwanzoni mwa mwaka 2022 nchini Kazakhstan, mwanachama mwingine wa jumuia hii. Hasa kwa kuwa ina kituo cha kijeshi nchini Armenia, na ilikiimarisha kwa kuanzisha vituo viwili vipya kusini mwa Armenia karibu na mpaka wa Azerbaijan ikichukulia vituo hivyo kama dhamana ya ziada ya usalama. Ikiwa itaiingilia kati kwa mujibu wa mkataba, basi nguvu zake zitadhoofika nchini Ukraine. Ni wazi kutokana na haya yote kwamba Marekani ilitumia mazingira ya sasa ya Urusi nchini Ukraine na kuisukuma Azerbaijan kushambulia.

c- Jaribio la Ulaya, hasa Ufaransa na Ujerumani, la kuwa na nafasi katika matukio hayo, ni jaribio lisilofanikiwa kama tulivyobainisha hapo juu.

d- Makafiri wakoloni uadui wao baina yao ni mkali; maslahi yao ndiyo yanayowaongoza hata kama ni ya kishetani na kinyama, na thamani zao hazina ukweli wala haki. Kwa hivyo, kuisukuma kwao Azerbaijan kuukomboa mkoa wa Karabakh kutoka kwa Waarmenia wakati ambapo Urusi imetingwa na vita vya Ukraine, si kwa kuipenda Azerbaijan nchi ya Kiislamu, bali ni utangulizi wa kuingiza ushawishi wa Marekani nchini Armenia na kuiondoa Armenia kutoka kwa Urusi baada ya Urusi kuisaliti Armenia kwa kutoinusuru mkoani humo. Ikiwa mazingira yangebadilika na kukaliwa kwa mkoa huo na Armenia kukatimiza lengo la Marekani, basi Marekani ingeunga mkono kukaliwa kwa Karabakh na Armenia upya! Ukaliaji wa Waarmenia mkoani humo uliendelea kwa takriban miaka 30 na Marekani haikuingilia kati kama ilivyoingilia kati leo. Hivyo ndivyo walivyo makafiri wakoloni; hawana thamani thabiti za kheri na shari kwao.

هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ قَاتَلَهُمُ اللهُ أَنَّى يُؤْفَكُونَ

"Wao ndio adui, basi jihadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Ni vipi wanavyopotolewa (na haki)?" (QS. Al-Munafiqun [63]: 4)

Mnamo tarehe kumi na tisa Rabi' al-Awwal 1445 AH Sawa na tarehe 04/10/2023 BK

Share Article

Share this article with your network