Jibu la Swali
Hujuma ya Ndege Zisizo na Rubani juu ya Kremlin
Swali:
Wataalamu wa ndege zisizo na rubani nchini Marekani waliona kuwa (ndege mbili zisizo na rubani zilizopata ajali juu ya Kremlin Jumatano iliyopita, ziliepuka mifumo mingi ya ulinzi ndani na karibu na Moscow, jambo linaloashiria uwezekano wa kurushwa kwake kutoka ndani ya Urusi. Al-Jazeera, Reuters 06/05/2023). Hujuma hiyo ya ndege zisizo na rubani dhidi ya kasri ya Kremlin katikati mwa Moscow ilitokea usiku wa tarehe 03/05/2023. Katibu wa kamati ya mambo ya nje katika bunge la Ukraine alisema kuwa (hujuma dhidi ya Kremlin imepangwa na Moscow... Al-Jazeera 03/05/2023). Swali ni: Je, hujuma hii imepangwa kutoka nje "Ukraine" kama Urusi inavyoishutumu? Au imepangwa kutoka ndani "Moscow" kama walivyosema wataalamu wa Marekani na Ukraine? Kwa maneno mengine: Ni nani aliye nyuma ya hujuma hii baada ya matamshi haya tofauti?
Jibu:
Ndiyo, urais wa Urusi ulitangaza kuzuia hujuma ya ndege mbili zisizo na rubani dhidi ya Kremlin, na kuifafanua kama ya "kigaidi". Mara moja, Ukraine ilikanusha kuhusika kwayo katika hujuma hiyo, ikiishutumu Moscow kuwa iliangazia makusudi tukio hilo katika vyombo vya habari ili kuhalalisha uwezekano wa kuongeza kasi ya mgogoro. Kremlin ilisema kuwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hakudhurika... Na ili kuelewa malengo ya hujuma hii, ni lazima kuzingatia yafuatayo:
Kwanza: Baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita nchini Ukraine vilivyoanzishwa na Urusi mnamo Februari 2022, baadhi ya maeneo ya mapigano yamepatwa na hali ya kudumaa. Isipokuwa kwa mapigano yanayoendelea katika mji wa Bakhmut tangu miezi minane iliyopita na baadhi ya mashambulizi ya makombora ya Urusi ndani ya Ukraine, maeneo mengine ya vita yanashuhudia utulivu. Kudumaa huku kuna sababu mbili; ya kwanza ni ya kimaumbile kutokana na majira ya baridi, na ya pili ni kutokana na uhaba wa risasi kwa pande zote mbili. Kutokana na mazungumzo yanayoendelea kuhusu shambulizi tarajiwa la Ukraine, hujuma dhidi ya Kremlin itakuwa imemaliza hali ya kudumaa kwa maeneo ya vita, na kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa mapigano.
Pili: Magharibi ikiongozwa na Marekani, kupitia uungaji mkono endelevu na wa hatua kwa hatua kwa Ukraine, imeweza kuidhoofisha Urusi. Kiongozi wa kundi la Wagner la Urusi linalopigana hasa katika mji wa Bakhmut, analalamika mara kwa mara kuhusu uhaba wa risasi, na hata kuvishutumu vyombo ndani ya taasisi ya kijeshi ya Urusi kwa kufanya hivyo makusudi, hasa kwa kuwa maeneo mengine ya vita yalikuwa yamesimama wakati wa majira ya baridi. Kadhalika, mashambulizi ya Urusi ndani ya Ukraine mara nyingi huchukua mfumo wa mawimbi, ikimaanisha kuwa huenda Urusi haina makombora na ndege za kutosha kufanya mashambulizi mfululizo; kana kwamba inakusanya kiasi inachotengeneza kwa mwezi mmoja, kisha inakirusha ndani ya Ukraine. Hili ni kielelezo kingine cha hali ya kudhoofika nchini Urusi, mbali na uhaba wa vipuri muhimu katika sekta ya kijeshi ya Urusi kutokana na vikwazo vya Magharibi. Ingawa habari zinazungumzia pia kudhoofika kwa akiba ya risasi kwa upande wa Magharibi, hili ingawa ni kweli, sekta ya kijeshi ya Magharibi ina uwezo mkubwa kuliko sekta ya Urusi kuziba pengo hili.
Tatu: Matokeo yake, jeshi la Urusi, licha ya kampeni za kuandikisha wanajeshi, linaonekana kupoteza uwezo wa mashambulizi ya ardhini hasa. Linajenga mahandaki kando ya maeneo ya vita kama ushahidi wa hofu yake dhidi ya shambulizi tarajiwa la Ukraine kwa silaha za kisasa za Magharibi. Hata kiongozi wa kundi la "Wagner" amelielezea shambulizi tarajiwa la Ukraine kama "maafa kwa Urusi". Hili likiunganishwa na kile kinachoonekana kama kutokuwepo kwa nguvu ya anga ya Urusi – silaha ambayo imeshindwa kabisa kudhibiti anga ya Ukraine na kutosheka tu na kuelekeza baadhi ya mashambulizi kutokea mbali – udhaifu huu wa Urusi uko wazi kwa Magharibi na Marekani ambayo inaendesha vita hivi kutoka nyuma ya pazia nchini Ukraine. Kwa sababu hiyo yote, mipango ya vita imeanza kuchukua vipimo dhidi ya Urusi ambavyo havikutazamiwa wakati vita vilipoanza. Hasa kwa kuwa Marekani na Magharibi bado zinafanikiwa kuweka mbali tishio la vita vya nyuklia, kwani ishara zote za Urusi zinazofikia kiwango cha tishio la kutumia silaha za nyuklia zimekabaliwa na ukosoaji mkubwa, na hata kuitia hofu Urusi kutokana na kukurupuka kwake na radiamali ya Marekani.
Nne: Katika mazingira haya yote, msimu huu wa joto huenda ukawa na joto kali na usio na vizuizi vingi. Miongoni mwa vizuizi hivyo ni kwamba vita vilikuwa vikiendelea ndani ya Ukraine pekee. Mashambulizi kadhaa yametokea ndani ya Urusi bila Ukraine kutangaza kuhusika kwayo, na hata kumebuniwa "upinzani wa Kirusi" unaopinga utawala wa Putin kana kwamba ndio unaohusika na mashambulizi ndani ya Urusi. Na hujuma hii dhidi ya kasri ya Kremlin katikati ya mji mkuu Moscow inajeruhi sana kiburi cha Urusi. Urusi imeainisha tukio hilo kama jaribio la kumuua Rais wa Urusi Putin. Hata iwe ni wapi zilipotokea ndege hizo mbili, kufika kwake juu ya mapaa ya majengo ya Kremlin na kulipuka kwake juu ya Kremlin moja kwa moja kunaonesha udhaifu wa Urusi.
Tano: Kutokana na mshtuko uliopo mjini Moscow na Urusi kwa ujumla kufuatia ujasiri wa hujuma hiyo ambayo Urusi imeishutumu Ukraine kuitekeleza, matamshi makali yametolewa yanayoashiria ukubwa wa mshtuko kwa viongozi wa Urusi:
1- Makamu wa Rais wa Baraza la Usalama la Urusi, Dmitry Medvedev, alitangaza: (kwamba chaguo pekee baada ya hujuma ya utawala wa Kyiv dhidi ya Kremlin ni kumuangamiza Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na wasaidizi wake. Medvedev aliandika kupitia chaneli yake ya Telegram, Jumatano: "Baada ya shambulizi la kigaidi lililotokea leo 'dhidi ya Kremlin', hakuna chaguo jingine isipokuwa kumuangamiza kimwili Zelensky na genge lake... Sputnik ya Urusi, 03/05/2023)
2- Spika wa Bunge la Urusi (Duma), Vyacheslav Volodin, alitaka (kutumiwa kwa "silaha zenye uwezo wa kuzuia utawala wa kigaidi mjini Kyiv na kuuangamiza" kujibu hujuma ya ndege mbili dhidi ya Kremlin. Volodin aliongeza – katika taarifa kwenye programu ya Telegram – kwamba Urusi haifai kufanya mazungumzo na Rais wa Ukraine baada ya hujuma hiyo "inayodaiwa" ambayo Kyiv ilikanusha kuhusika kwayo, akibainisha kuwa mazungumzo na utawala wa Zelensky "hayawezekani, kwani yanatishia usalama wa Urusi, Ulaya na ulimwengu mzima". Al-Jazeera Net, 03/05/2023).
Kwa hili, inabainika ukubwa wa mshtuko uliotanda nchini Urusi kutokana na hujuma ya ndege mbili zisizo na rubani dhidi ya Kremlin.
Sita: Ama kuhusu kuwa Urusi ndiyo iliyopanga hujuma hiyo ili kuongeza kasi ya vita nchini Ukraine, hili halielekei kwa upande mmoja kwa kuwa ni jeraha kwa kiburi chake na kofi kwa ukubwa wake na onyo kwamba hakuna anayeiogopa tena wala kumuogopa Rais wake. Na kwa upande mwingine, Urusi haina uwezo wa kuongeza kasi ya vita nchini Ukraine kwa ufanisi isipokuwa kwa silaha za nyuklia, na haina uthubutu wa kuzitumia ndani ya Ukraine kwa hofu ya radiamali ya Marekani. Jambo jingine linalokanusha uwezekano wa Urusi kujishambulia yenyewe ni kwamba Urusi imeelekeza shutuma kwa Marekani moja kwa moja kuhusika katika hujuma hiyo. Hili pia halina mfano wa awali na linaashiria ukubwa wa mshtuko mjini Moscow kutokana na ujasiri wa hujuma hiyo, na matamshi yanayohusiana na hilo yanabainisha hili:
1- Msemaji rasmi wa Kremlin, Dmitry Peskov, alitangaza (kwamba Marekani ndiyo inayohusika na hujuma ya Ukraine dhidi ya Kremlin kwa msaada wa ndege zisizo na rubani na ndiyo iliyochagua malengo ya Kyiv. Hili lilikuja katika mkutano na waandishi wa habari wa Peskov leo Alhamisi "04/05/2023", ambapo aliendelea: "Majaribio kama haya ya kujitenga na hili kule Kyiv na Washington bila shaka ni ya kipuuzi kabisa. Tunajua vyema kwamba maamuzi kuhusu vitendo kama hivi na hujuma za kigaidi kama hizi hayachukuliwi Kyiv, bali Washington. Na Kyiv inafanya kile inachoamriwa, na amri za hilo zimeshatolewa. Marekani ilikanusha hili kupitia mratibu wa mawasiliano ya kimkakati katika Baraza la Usalama la Taifa katika Ikulu ya Marekani, John Kirby, kupitia chaneli ya MSNBC, ambapo alisema: "Bado hatujui nini kilitokea, na hatufanyi tathmini yoyote. Nimeona tu maoni ya Dmitry Peskov asubuhi ya leo, na madai kuhusu kuhusika kwetu kwa namna fulani katika jambo hili. Naweza kuwathibitishia kwamba hapakuwa na ushiriki wowote kutoka upande wa Marekani, na vyovyote itakavyokuwa, Marekani haikuhusika". RT, 04/05/2023).
2- Kwa sababu hiyo yote, inaweza kusemwa kuwa Marekani imeanza kuchukua vita vya Ukraine na kuvipeleka mbali zaidi na bila vizuizi vingi dhidi ya Urusi kutokana na kile inachokiona cha udhaifu na kudhoofika nchini Urusi. Bali hujuma dhidi ya Kremlin inawakilisha tishio la kibinafsi kwa Rais wa Urusi. Na inavyoonekana kutokana na matamshi ya Peskov, msemaji wa Kremlin, ni kwamba Urusi imeelewa ujumbe huo, ndiyo maana ilitaka kuiambia Marekani kwamba inajua kuwa Marekani iko nyuma ya hujuma hiyo, lakini "Urusi" inajizuia kuitishia Marekani moja kwa moja kutokana na hofu yake kubwa kwake, na kutosheka na kuitishia Ukraine na kutishia kumuua Rais wake Zelensky.
3- Kinachoashiria pia kuwa hujuma hiyo ni changamoto kwa Urusi iliyopangwa na Marekani, ni kumtoa Rais wa Ukraine nje ya Ukraine. Alionekana ghafla asubuhi ya siku ya hujuma hiyo kuwa yuko ziarani Helsinki, Finland, kisha baadaye ndege yake ikaonekana ikitua Amsterdam, Uholanzi, kisha baadaye ikabainika katika ratiba ya Kansela wa Ujerumani kuwa inajumuisha kumpokea Rais wa Ukraine Zelensky. Haya yote ni kwa ajili ya kumepusha Rais wa Ukraine Zelensky na radiamali ya Urusi, yaani kuizuia kumuua kama alivyotaka Medvedev.
4- Ama Marekani yenyewe, ilionekana kana kwamba haitaki kutoa maoni kuhusu tukio hili, bali ilionyesha kutilia shaka simulizi ya Urusi, (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alisema kuwa ameona ripoti kutoka Moscow kuhusu hujuma inayodaiwa ya ndege isiyo na rubani kutoka Ukraine dhidi ya Kremlin, lakini "hawezi kuthibitisha ukweli wake kwa namna yoyote ile". Alisema: "Sisi kwa ufupi hatujui". Blinken aliongeza: "Tutaona ukweli ni nini. Na ni vigumu sana kutoa maoni au kukisia jambo hili bila kujua ukweli". CNN Arabic, 03/05/2023).
5- Kinachoashiria jukumu la Marekani katika jaribio la kumuua Rais wa Urusi Putin ni kwamba nyaraka za Marekani zilizovuja katika miezi iliyopita na kufichuka mnamo Aprili 2023, zilizungumzia kuuawa kwa Rais wa Urusi Putin kama mojawapo ya hali (scenarios) za vita, (Inaonekana kuwa mchakato wa kuvuja kwa nyaraka za siri kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani "Pentagon" umebeba mshangao na siri nyingi, ikiwemo kile kilichofichuliwa na gazeti la "New York Times" kuhusu hati ya siri ya kijasusi iliyoipata inayojumuisha maelezo ya mipango iliyowekwa kushughulikia dharura baada ya mwaka mmoja wa vita nchini Ukraine. Hati hiyo inajumuisha uchambuzi uliofanywa na Shirika la Kijasusi la Ulinzi la Marekani unaoainisha hali 4 zinazoweza kutokea, na jinsi zinavyoweza kuathiri mkondo wa mgogoro nchini Ukraine iwapo zitatokea. Hali hizo zinazoweza kutokea ni pamoja na: "Kuuawa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin... na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky... na mabadiliko ya uongozi wa majeshi ya Urusi... na mashambulizi ya Ukraine dhidi ya Kremlin". Gazeti la Al-Sharq, 12/04/2023).
Saba: Kwa ufupi, hujuma ya ndege mbili zisizo na rubani dhidi ya kasri ya Kremlin mjini Moscow ni ongezeko la hatari la vita nchini Ukraine, na inaashiria kuwa Marekani pamoja na Ukraine wanamiliki vibaraka wa kutosha ndani ya Urusi kufanya mashambulizi makali yanayoweza kubadilisha mkondo wa vita. Milipuko imeanza na kuchukua mwelekeo wa kuongezeka ndani ya Urusi inayolenga reli, vituo vya mafuta, umeme na vinginevyo, ikimaanisha kuwa mchakato wa kuhamisha vita kutoka Ukraine hadi ndani ya Urusi unaendelea kivitendo, na kwa ujasiri mkubwa hasa kwa kuwa jeshi la Urusi limedhoofishwa kwa kiasi kikubwa nchini Ukraine na ni vigumu kwake kufanya mashambulizi yenye tija yanayobadilisha mkondo wa vita. Kadhalika, Magharibi ikiongozwa na Marekani inaendelea kuiunga mkono Ukraine kwa silaha za kisasa zaidi ili kubadilisha mkondo wa vita kwa faida ya Ukraine, ikizingatiwa kuwa mkondo wa sasa wa vita si kwa faida ya Urusi baada ya Ukraine kukomboa mji wa Kherson na maeneo ya Kharkiv, pamoja na ukubwa wa hasara ya Urusi katika shambulizi lake linaloendelea tangu miezi minane katika mji wa Bakhmut bila kuuteka.
Haya ndiyo vipimo vya hujuma hii dhidi ya Kremlin nchini Urusi, na hayo yalikuwa mazingira yake. Haya yote yanaashiria kuyumba kwa uwezo wa kijeshi na kiusalama wa Urusi hadi kufikia kutoeweza kulinda kitovu chake cha kisiasa katikati ya Moscow! Ni kweli kwamba mapigano si kati ya Urusi na Ukraine pekee, bali Marekani na Magharibi zinaunga mkono Ukraine kimali na kimaadili. Pamoja na hayo, kuendelea kwa shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine kwa zaidi ya mwaka mmoja na bado utulivu wa Urusi unayumba sana katika maeneo iliyoyakalia nchini Ukraine pamoja na hasara kubwa za mali na watu, yote hayo yanaashiria kuondoka kwa Urusi katika hadhi ya dola kubwa, kuondoka kuliko wazi mbele ya macho. Inaonekana Urusi inatambua hilo na ndiyo maana imejitahidi kurejesha heshima ya hadhi hii kwa kuuteka Bakhmut kikamilifu kabla ya sherehe za Urusi tarehe 09/05/2023 lakini imeshindwa hadi leo licha ya kuongeza mashambulizi na kukusanya kundi la Wagner.
Ama Marekani na Magharibi, zinapigana hadi mwanajeshi wa mwisho wa Ukraine! Hazitaki kuingilia kati mapigano hayo, bali mataifa hayo yanatimiza maslahi yao kwa damu za wengine.
Mwishoni, ninarudia kile nilichowahi kukitaja katika Jibu la Swali la tarehe 01/03/2023: [...hakika nchi hizi makafiri za kikoloni zinazoitwa kubwa katika ulimwengu wa leo zinazozana zenyewe kwa zenyewe si kwa ajili ya heri ya ulimwengu bali kwa ajili ya shari na madhara. Urusi inaivamia Ukraine ili kumuua kila Myukraine anayesogea, na Marekani na Magharibi wanapambana na uvamizi huo kwa kila Myukraine na si kwa wanajeshi wao! Pande zote mbili zinazozana nchini Ukraine ili kumuua kila Myukraine... Hivyo ndivyo zilivyo nchi hizi zinazofanya ufisadi duniani, hazithamini wingi wa damu inayomwagika maadamu inazitimizia maslahi yao, bali hata sehemu ndogo ya maslahi yao... Ni kana kwamba historia inajirudia wakati dola za Uajemi na Roma zilipokuwa zikizozana, huyu anashinda na huyu anashindwa na hivyo hivyo mfululizo... Kila mmoja wao anafanya kazi kama mashine inayofyonza damu ya watu ili kutimiza maslahi yake... Na hilo liliendelea mpaka Mwenyezi Mungu alipowakirimu watu wa haki na uadilifu, Umma wa Kiislamu, kwa nusura na ushindi ulio wazi, Uislamu na Waislamu wakawa na utukufu, na ukafiri na makafiri wakadhalilika. Na hakika hili litatokea tena kwa idhini ya Mwenyezi Mungu,]
وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ
"Na siku hiyo waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu. Yeye humnusuru amtakaye, Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (Ar-Rum [30]: 4-5)
Na hilo ni kwa kusimamisha Khilafah ya uongofu.
وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيباً
"Na watasema: Lini hayo? Sema: Huenda yakawa karibu." (Al-Isra [17]: 51)
19 Shawwal 1444 H
09/05/2023 M