Jibu la Swali
Maendeleo ya Kisiasa nchini Indonesia
Swali: Mnamo tarehe 20/10/2024, Jenerali wa zamani Prabowo Subianto (mwenye umri wa miaka 73) aliapishwa kuwa rais mpya wa Indonesia mbele ya Bunge, kufuatia uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Februari uliopita na kutangazwa kwa ushindi wake mnamo 20/03/2024. Marekani haikuchelewa kumpongeza; Waziri wake wa Mambo ya Nje, Blinken, alituma pongezi zake na kusema, ("Washington inatarajia ushirikiano wa karibu na Prabowo"... Al Jazeera, 20/03/2024). Vilevile, aliharakisha kuizuru China mnamo 01/04/2024 hata kabla ya kuapishwa kwake! Yaani, akiwa rais mteule ambaye alikuwa bado hajapokea mamlaka yake rasmi, alifanya mkutano na Rais Xi na kusema: ("Anaunga mkono kikamilifu maendeleo ya uhusiano wa karibu kati ya Indonesia na China, na anatamani kuendeleza sera ya urafiki ambayo Rais Joko alikuwa nayo na China"... Reuters, 01/04/2024).
Swali sasa ni: Je, pongezi hizi za haraka kutoka Marekani na ziara ya haraka nchini China zinaashiria nini kuhusu uhusiano wa Indonesia na Marekani pamoja na China? Kwa maneno mengine, je, kutakuwa na mabadiliko katika sera ya Indonesia kuelekea Marekani? Na sera yake itaendaje kuelekea China? Kisha, sera yake ni ipi kuelekea uchokozi wa Mayahudi dhidi ya Gaza?
Jibu: Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:
Kwanza: Sera ya Marekani na Indonesia:
Marekani ilianza kufanya kazi ili kuchukua nafasi ya ukoloni wa Uholanzi baada ya Indonesia kujikomboa mnamo 1949, kupitia utoaji wa misaada na mikopo. Lakini Indonesia ilikataa hilo kwa sababu ilitambua kuwa ni njia ya utawala na upanuzi wa ushawishi; haikutaka kujiondoa katika ukoloni wa Uholanzi ili kuingia chini ya ukoloni wa Marekani kwa namna nyingine. Marekani iliishinikiza na kuibua vurugu na machafuko, na kufuatia hayo, rais wake Ahmed Sukarno alisalimu amri na kukubali misaada na mikopo ya Marekani mnamo 1958. Marekani ilianza kupenya nchini humo na kutafuta vibaraka zaidi, ikafanikiwa kupata vibaraka wapya jeshini wakiongozwa na Muhammad Suharto, ambaye alipindua serikali kijeshi mnamo 1966 dhidi ya Ahmed Sukarno. Marekani ilifanya kazi kuimarisha ushawishi wake kwa kumsaidia kuwaangamiza Wakomunisti, kisha ikamsaidia kuikomboa Timor Mashariki kutoka kwa wakoloni wa Kireno mnamo 1975. Lakini ilipotaka kuitenganisha Timor Mashariki na Indonesia, Suharto alisitasita kutekeleza hitaji lake. Marekani ilimletea matatizo ya kiuchumi, na vyombo vyake vya kifedha kama Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia vilichukua jukumu muhimu katika kufanya hali kuwa mbaya, jambo lililosababisha kuanza kwa maandamano ya wanafunzi na ghasia hadi Suharto alipolazimika kutangaza kujiuzulu mnamo 1998. Marekani ilimtupa katika shimo refu kama inavyomtupa kibaraka yeyote anayechelewa kutekeleza miradi yake au muda wake wa matumizi unapokwisha!
Baada ya Suharto, makamu wake Jusuf Habibie alichukua urais wa nchi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kati ya 1998 na 1999. Alitekeleza matakwa ya Marekani kwa kukubali kufanya kura ya maoni ya kujiamulia hatima ya Timor Mashariki kama maandalizi ya kujitenga kwake, na akaahidi kutoidai tena, huku akiweka mfumo wa uchaguzi chini ya jina la mageuzi ya kidemokrasia. Kisha Abdurrahman Wahid alitawala kwa takriban miaka miwili kati ya 1999 na 2001, ambapo Bunge lilimwondoa madarakani kwa tuhuma za ufisadi. Megawati Sukarnoputri, binti wa rais wa kwanza wa Indonesia Ahmed Sukarno, aliteuliwa kuchukua nafasi yake na alishikilia urais kati ya 2001 na 2004. Katika kipindi chake, kujitenga kwa Timor Mashariki na Indonesia kuliidhinishwa rasmi mnamo 2002, akifanya usaliti kama waliomtangulia!
Uchaguzi wa moja kwa moja wa rais ulifanyika nchini humo kulingana na marekebisho mapya, ambapo rais anaruhusiwa vipindi viwili pekee ikiwa atachaguliwa tena, kila kimoja kikidumu miaka 5. Yudhoyono alichaguliwa kuanzia 2004 hadi 2014. Katika mwaka huo, uchaguzi wa rais ulifanyika ambapo Joko Widodo (Jokowi) alishinda, kisha akachaguliwa kwa mara ya pili mnamo 2019 na muhula wake uliisha mwezi Oktoba 2024. Widodo alikuwa na hamu ya kuendeleza utiifu wa mfumo wa Indonesia kwa Marekani. Katika ziara yake ya mwisho nchini Marekani na mkutano wake na Rais Joe Biden mnamo 13/11/2023, alikubaliana naye kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kuimarisha nafasi ya Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN). Marekani inajaribu kudhibiti maamuzi katika jumuiya hii ambayo ina nchi nyingi ambazo si zote zipo chini ya ushawishi wake, hivyo inafanya kazi kuitumia Indonesia kufikia lengo hili ili iweze kuitumia kusimama dhidi ya China au kuishinikiza, kuzuia China kusiika ushawishi wake katika eneo la Bahari ya Kusini ya China. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken aliashiria hili alipotuma pongezi katika hafla ya uhuru wa Indonesia mnamo 17/08/2024 akisema, "Katika hatua mpya ya kihistoria katika uhusiano wetu, Rais Joko Widodo na Rais wa Marekani Joe Biden walifanya kazi kupandisha kiwango cha uhusiano kati ya Marekani na Indonesia hadi kuwa ushirikiano wa kimkakati wa kina mwezi Novemba uliopita" (Youm7, 17/08/2024).
Ushindi wa Prabowo Subianto "ambaye ni mkwe wa rais wa zamani Muhammad Suharto" na makamu wake Gibran, mwana wa rais anayemaliza muda wake Joko Widodo, ulitangazwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika mnamo 14/02/2024 kwa asilimia 58.58%. Ikumbukwe kwamba Gibran hakuwa na sifa za kugombea nafasi ya makamu wa rais kwa kuwa ana umri wa miaka 36, kwani sheria zinakataza watu kugombea nyadhifa za juu kama rais na makamu wake chini ya umri wa miaka 40. Lakini Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Indonesia, ambaye ni shemeji wa Rais Widodo, alifanya marekebisho kabla ya uchaguzi kuruhusu wale walio chini ya miaka arobaini kugombea nyadhifa hizo. Rais Widodo mwenyewe alikuwa anafikiria jinsi ya kurefusha muhula wake lakini hakuweza, hivyo akafanya mpango na Prabowo kumuunga mkono kwa sharti la kumfanya mwanawe, Gibran, kuwa makamu wa rais. Dola ilimuunga mkono Prabowo kwa uwazi kupitia vyombo vyake vyote, kuanzia kwa Rais Widodo hadi jeshi, usalama, na polisi, na Marekani haikupinga jambo hilo kama ilivyo ada yake katika matukio kama haya. Inatajwa kuwa wenzake jeshini walikuwa wakimwita "mvulana wa Marekani" (US boy), kwani alipata mafunzo huko, katika kambi ya Fort Benning katika jimbo la Georgia, na Fort Bragg katika jimbo la North Carolina. Marekani haikuchelewa kumbariki kwa ushindi wake ulipotangazwa rasmi mnamo 20/03/2024. Waziri wake wa Mambo ya Nje Blinken alituma pongezi zake akisema, "Washington inatarajia ushirikiano wa karibu na Prabowo" (Al Jazeera, 20/03/2024), jambo linalothibitisha utiifu wake kwake na kuimarishwa kwa utiifu huo!
Prabowo alitangazwa rasmi na kuapishwa, kisha akaunda serikali mpya mnamo 20/10/2024. Katika kipindi cha mpito tangu ushindi wake hadi kuapishwa kwake, takriban miezi saba, aliendelea kushika nafasi yake ya awali kama Waziri wa Ulinzi. Katika kipindi hiki, Marekani ilifanya mazoezi makubwa ya kijeshi na Indonesia katika eneo la Sidoarjo, kisiwani Java, kilichopo katika Bahari ya Kusini ya China, mnamo 26/08/2024 yaliyodumu kwa wiki mbili. Mazoezi hayo yalishirikisha nchi za Japan, Thailand, Uingereza, Singapore, Ufaransa, Canada na New Zealand. Pia alifanya ziara nyingi nje ya nchi ikiwemo Marekani ambapo alikutana na Waziri wake wa Ulinzi, Austin, katika jengo la Pentagon. Balozi wa Marekani nchini Indonesia, Kamala Shirin Lakhdhir, alisema ("Uhusiano wa nchi yake na Rais mpya wa Indonesia umeanza miaka mingi hata kabla hajashika wadhifa wake kama Waziri wa Ulinzi mwaka 2019"... Al Jazeera, 20/10/2024), yaani wakati alipokuwa afisa jeshini ambapo alifunziwa katika kambi zao na mikononi mwa maafisa wao, na wakati alipokuwa akiongoza jeshi katika zama za Suharto. Aidha, tovuti ya VOI - Voice of Indonesia ilichapisha mnamo 29/10/2024, yaani siku chache baada ya kuapishwa kwa Prabowo:
(Waziri wa Ulinzi wa Indonesia, Sjafrie Sjamsoeddin, na Balozi wa Marekani nchini Indonesia, Kamala Shirin Lakhdhir, walijadili fursa za ushirikiano wa kiulinzi kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo usalama wa baharini. Mkuu wa Ofisi ya Uhusiano wa Umma katika Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Indonesia, Brigedia Jenerali Edwin Adrian Sumantha, alisema siku ya Jumatatu kuwa Balozi wa Marekani alimweleza Waziri wa Ulinzi wa Indonesia hamu ya Marekani kuongeza ushirikiano katika nyanja ya usalama wa baharini. Katika mkutano kwenye ofisi ya Wizara ya Ulinzi ya Indonesia, Balozi wa Marekani pia alielezea hamu ya nchi yake kuendeleza mazoezi ya Super Garuda Shield ambayo kwa sasa yanafanyika mara moja kwa mwaka nchini Indonesia. Katika mkutano huo, Sjafrie alimshukuru Balozi Kamala kwa ziara yake na kuelezea ahadi ya Indonesia ya kuimarisha ushirikiano ulioanzishwa kati ya nchi hizo mbili).
Kwa kuzingatia yaliyotangulia, inabainika kuwa Rais mpya wa Indonesia, Prabowo, tangu kutangazwa kwa ushindi wake mnamo 20/03/2024 hadi kuapishwa kwake mnamo 20/10/2024, na pia baada ya hapo... anafuata nyayo za waliomtangulia, bali amezidi kushikamana na Marekani, na kwamba ushawishi wake bado ndio unaotawala nchini Indonesia!!
Pili: Sera ya China na Indonesia:
Prabowo alifanya ziara nchini China mnamo 01/04/2024 akiwa rais mteule, ingawa hakuwa amepokea mamlaka yake wakati huo, na akafanya mkutano na Rais Xi akisema: "Anasupport kikamilifu kuendeleza uhusiano wa karibu kati ya Indonesia na China, na anapenda kuendeleza sera ya urafiki aliyoifuata Rais Joko na China" wakati Xi alisema: "Beijing inaangalia uhusiano wake na Indonesia kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, na inajiandaa kukuza ushirikiano wa kimkakati wa kina"... (Reuters, 01/04/2024). Ikumbukwe kwamba China ina shughuli kubwa za kiuchumi nchini Indonesia katika ngazi ya uhusiano wa kibiashara na uwekezaji, na nchi zote mbili ni wanachama wa ASEAN. Hili linahitaji muamala kati yao kiasi kwamba Indonesia isichukue msimamo wa uadui na China huku ikiendelea kubaki mfuasi wa sera za Marekani kama tulivyoeleza hapo juu.
Gazeti la Kuwait lilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 09/11/2024: (Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Indonesia Prabowo Subianto wakisalimiana wakati wa hafla ya utiaji saini katika Ukumbi Mkuu wa Watu mjini Beijing katika kituo chake cha kwanza cha nje ya nchi, tangu alipochukua madaraka wiki tatu zilizopita, Rais wa Indonesia Prabowo Subianto alikutana na mwenzake wa China Xi Jinping mjini Beijing, na akaahidi kudumisha uhusiano wa karibu na China, mshirika wa kwanza wa kibiashara wa Indonesia, na mmoja wa wawekezaji muhimu wa kigeni nchini humo. Subianto, Jenerali wa zamani mwenye umri wa miaka 73, alisema wakati wa mkutano na Xi, "Indonesia inaichukua China si kama tu nguvu kuu, bali kama ustaarabu mkubwa," akiongeza kuwa nchi hizo mbili zina uhusiano wa karibu wa karne nyingi, "kwa hivyo naamini ni jambo la kawaida tu sasa katika hali ya sasa, ya kijiopolitika na kijiuchumi, kwamba Indonesia na China ziwe washirika wa karibu sana katika nyanja nyingi sana." Xi aliahidi kuunga mkono utawala wa Subianto na akamshukuru kwa kuizuru China kwanza, akisema anaamini kuwa "Indonesia itazingatia mkondo wa maendeleo huru, na itaendelea kupata mafanikio mapya katika safari ya kufikia ustawi wa kitaifa na uimarishaji wa kitaifa, na itachukua jukumu muhimu katika nyanja za kikanda na kimataifa." China na Indonesia ni washirika wakuu wa kiuchumi, lakini nchi hizo mbili zimeingia katika mabishano ya maneno kuhusu haki ya mamlaka katika Bahari ya Kusini ya China, na inatarajiwa Subianto baada ya Beijing kuelekea Washington, kuitikia mwaliko wa Rais wa Marekani Joe Biden, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kimataifa inayojumuisha pia Peru, Brazil, na Uingereza...).
Kwa kuzingatia hayo, inabainika kuwa uhusiano kati ya Indonesia na China hauvuki nyanja za kibiashara ambazo haziathiri ushawishi wa kisiasa wa Marekani nchini Indonesia. Nyanja za kibiashara ndizo msingi, lakini zikihamia kwenye upande wa ushawishi, mamlaka na Bahari ya Kusini ya China, hapo huingia katika mabishano!
Tatu: Sera ya Indonesia kuelekea masuala ya Waislamu
Inajulikana kuwa Indonesia ni nchi ya Kiislamu ya kale, ambapo watu wake walianza kuingia katika Uislamu tangu karne ya kwanza Hijiria. Idadi ya watu wake inakaribia milioni 300, wengi wao wakiwa Waislamu kwa asilimia 90, na eneo lake ni kubwa linalofika zaidi ya kilomita za mraba milioni 1.9. Ni nchi tajiri kwa maliasili na ghafi, na ina uwezo wa kuwa dola kubwa ikiwa mradi wa Katiba ya Kiislamu utatekelezwa na uongozi wa kisiasa wa Kiislamu wenye ufahamu utatawala.
Kuhusu sera ya nje ya Rais mpya kuelekea masuala ya Waislamu, inafuata mfumo wa mtangulizi wake kwa kuchukua mtazamo wa Marekani. Prabowo alitamka mnamo 01/06/2024 katika hotuba wakati wa mkutano wa Shangri-La Dialogue, jukwaa kubwa la usalama barani Asia linalofanyika Singapore, akisema: ("Pendekezo la Rais wa Marekani Joe Biden lenye hatua tatu kuhusu kusitisha mapigano Gaza ni hatua katika mwelekeo sahihi," na akaongeza: "Mahitaji yatakapojitokeza na Umoja wa Mataifa utakapoomba hilo, tuko tayari kushiriki kwa vikosi vikubwa vya kulinda amani ili kudumisha na kusimamia usitishaji vita, pamoja na kutoa ulinzi na usalama kwa pande zote na nyanja zote." Alitoa wito wa "suluhu ya haki kwa hali ya Palestina" na akasema, "Hii ina maana kwamba haki ya kuwepo si ya Israel pekee, bali pia ina maana ya haki ya watu wa Palestina kuwa na nchi yao na dola yao na kuishi kwa amani"... Reuters, 01/06/2024). Ikumbukwe kuwa wajibu wake ni kusimama na kuwanusuru watu wa Gaza kwa kutuma majeshi na silaha za kutosha kuzuia adui mkatili anayewaua kwa wingi, hasa kwa vile adui huyu anawalenga watoto, wanawake, na wanaume wasio na ulinzi, na shabaha za kiraia kama nyumba, shule, na hospitali. Msaada pekee wa Indonesia kwa watu wa Gaza ni kujenga Hospitali ya Indonesia, ambayo tayari imeharibiwa na umbo la Kiyahudi, adui wa Uislamu na Waislamu, ambaye anaungwa mkono na Marekani inayomtumia silaha kali, vifaa, na misaada bila kusimama. Pamoja na haya yote, Rais mpya Prabowo anaimarisha uhusiano wake na Marekani zaidi na kushikamana nayo zaidi na kutekeleza matakwa yake kwa sababu ya uhusiano wake wa kale nayo na msaada wake kwake.
Nne: Na kwa akili hizi za kisiasa zinazoshika utawala nchini Indonesia na kuitii Marekani, fursa inapotea kwa nchi hiyo kuwa dola kubwa endapo utawala ungechukuliwa na viongozi wa kisiasa wa Kiislamu wenye uelewa na uaminifu wanaotekeleza Katiba ya Kiislamu inayotokana na itikadi ya watu wa nchi hiyo na dini yao ya Uislamu, na kisha kufanya kazi kuunganisha nchi za Kiislamu, hususan zinazoipakana kama Malaysia, ili iwe kituo cha kuanzia cha Dola ya Khilafah Rashidah kwa njia ya Utume.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ
"Enyi mlioamini! Muitikieni Allah na Mtume Wake anapowaitia yale yatakayowapa uzima (wa kiroho na kimaisha)." (QS. Al-Anfal [8]: 24)
9 Jamada al-Ula 1446 H 11/11/2024 M