Jibu la Swali
Swali:
Mvutano umeongezeka tena kati ya Afghanistan na Iran kutokana na mzozo wa muda mrefu kuhusu ugawaji wa maji ya Bwawa la Helmand, ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa nchi zote mbili. Gazeti la Deutsche Welle (DW) lilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 2023/6/3: (Mapigano makali yalitokea kati ya Iran na Taliban wiki iliyopita karibu na mpaka wa pamoja, na kusababisha vifo na majeraha ya wanajeshi kadhaa katika wimbi jipya la mvutano kati ya pande hizo mbili huku wakitupiana lawama kuhusu nani aliyeanza kufyatua risasi. Mapigano hayo yalikuja huku kukiwa na kuongezeka kwa tofauti kati ya Kabul na Tehran kuhusu Mto Helmand au "Hirmand" kama unavyoitwa nchini Afghanistan, ambao ni chanzo kikuu cha maji katika nchi zote mbili...) Al Jazeera pia ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo 2023/6/1 ikinukuu gazeti la Kirusi la Izvestia (Mahusiano kati ya Iran na serikali ya Taliban yameshuhudia mivutano mbalimbali kutokana na msaada wa Tehran kwa Muungano wa Kaskazini uliokuwa unapinga harakati ya Taliban wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan, pamoja na tofauti za kidini na kisiasa kati ya nchi hizo mbili, bila kusahau mgogoro wa rasilimali za maji za Mto Helmand unaomiminika katika Ziwa Hamun katika ardhi ya Iran. Kwa mujibu wa mikataba iliyotiwa saini mwaka 1973, Afghanistan inapaswa kuipatia Iran mita za ujazo milioni 850 za maji kila mwaka kutoka mto huu, suala ambalo limekuwa tata baada ya Taliban kuingia madarakani...) Je, ni zipi sababu za matatizo haya na kutokea kwa mapigano kati ya pande hizo mbili? Na mambo haya yataishia wapi? Na je, kuna nguvu kuu zinazochochea mzozo huu au kufaidika nao na kuutumia kufikia miradi yao ya kikoloni?
Jibu:
Ili kuelewa sababu hizi na kule mambo yanapoelekea, tunayapitia yafuatayo:
1- Shirika la habari la Fars liliripoti mnamo 2023/5/27 kwamba ("Mapigano ya silaha yamezuka kati ya walinda mpaka wa Iran na kikosi cha serikali ya Taliban kwenye ukanda wa mpaka kati ya nchi hizo mbili karibu na kituo cha Sasoli" na likanukuu chanzo chenye habari kwamba "mvutano ulitokea kati ya kikosi cha walinda mpaka wa Iran na wapiganaji wa Taliban na kuongezeka hadi kufikia ufyatuaji risasi". Katika taarifa ya kwanza ya rasmi, Naibu Kamanda Mkuu wa vikosi vya usalama nchini Iran, Qasim Rezai, alisema "Tehran haitaruhusu tukio lolote la kusikitisha kutokea kwenye mpaka na Afghanistan. Makosa kadhaa yametokea upande wa harakati ya Taliban kwenye mpaka wa pamoja kati ya Iran na Afghanistan... Tunaziambia nchi jirani kuwa mipaka yetu ni mipaka ya urafiki na hatupaswi kuruhusu tukio la kusikitisha kutokea. Kikosi cha Taliban kilifyatua risasi asubuhi ya leo kuelekea upande wa Iran na walinda mpaka walijibu, na mapigano yalisimama kwa muda lakini yalizuka tena baadaye na bado yanaendelea". Alibainisha kuwa Kamanda Mkuu wa vikosi vya usalama, Ahmad Reza Radan, "aliwaamuru walinda mpaka kujibu kwa ukali ukiukaji wowote au uchokozi wa mipakani"). Shirika la habari la serikali ya Iran IRNA liliripoti (kwamba mapigano yaliyotokea leo 2023/5/27 kati ya walinda mpaka na wanachama wa Taliban yalisababisha vifo vya askari wawili wa harakati ya Taliban na vifo vya askari wawili wa Iran na kujeruhi raia wengine").
2- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan, Abdul Nafi Takor, alisema kupitia akaunti yake ya Twitter "kwamba watu wawili waliuawa katika mapigano ya leo katika jimbo la mpaka la Nimruz, mmoja kutoka Iran na mwingine kutoka Afghanistan, na wengine walijeruhiwa, na kwamba Imara ya Kiislamu haiungi mkono mapigano na majirani zake" (Chaneli ya ndani ya Tolo News 2023/5/27). Polisi wa Afghanistan walithibitisha mnamo 2023/5/29 kwamba kivuko cha mpaka cha "Daraja la Hariri" kati ya Afghanistan na Iran kimefunguliwa tena baada ya kufungwa mnamo 2023/5/28 kutokana na mapigano ya silaha yaliyochukua saa kadhaa kati ya pande hizo mbili... Haya yote yanaonyesha kuwa hali ya usalama mipakani mwa nchi hizo mbili ni tete, na wakati wowote inaweza kulipuka tena. Tukijua kuwa ndani ya miaka miwili tangu Taliban kuingia madarakani hadi leo, mapigano zaidi ya 10 yamezuka kati ya pande hizo mbili, jambo hilo linathibitisha kuwa kuna hali ya mvutano ya karibu ya kudumu kati yao.
3- Mivutano iliongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya Afghanistan na Iran kuhusu ugavi wa maji kutoka Mto Helmand au Hirmand kama unavyoitwa nchini Iran. Tofauti hizi ni za zamani kati ya nchi hizi mbili kuhusu suala hili; mkataba ulitiwa saini kati ya nchi hizo mbili mwaka 1973 ambapo Afghanistan ilitakiwa kuipa Iran mita za ujazo milioni 820 kila mwaka kutoka mtoni humo, lakini Iran inasema kuwa haijapata isipokuwa mita za ujazo milioni mbili tu. Inaonekana kuwa moja ya matatizo makubwa kati ya nchi hizo mbili ni tatizo la maji. Tatizo hili lilianza karne moja na nusu iliyopita wakati Waingereza walipoigawa nchi hiyo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Mousavi, alisema kupitia akaunti yake ya Twitter mnamo 2023/5/28: "Ni lazima tuwe macho, kile kilichotokea leo kwenye mpaka wa (Zabol - Nimruz) ni mwendelezo wa njama za wakoloni.. Ikiwa Goldsmith alifikisha Sistan Abad katika hali yake ya sasa mwaka 1872 kwa njama yake, warithi wake leo wanataka kuiharibu Iran na Afghanistan.. Wananchi na wasomi wa nchi zote mbili lazima waelewe kuwa aina yoyote ya mzozo ni hasara ya kimkakati kwa wote wawili".
4- Kisa kilianza wakati nchi hizo mbili zilipokubaliana kurejea kwenye kamati ya usuluhishi ya Kiingereza iliyoongozwa na Jenerali Goldsmith ambayo ilianza kuweka mipaka kati ya nchi hizo mbili mwaka 1871 na kukamilisha hilo ndani ya mwaka mmoja. Mpaka wa pamoja kati ya nchi hizo mbili ni mrefu na unaanza kutoka Mlango wa Zulfiqar ambapo kuna pembetatu ya mpaka kati ya Iran, Afghanistan na Turkmenistan upande wa kaskazini, na kuenea hadi Mlima Malik Siah ambapo kuna pembetatu ya mpaka kati ya Iran, Afghanistan na Pakistan upande wa kusini kwa umbali wa kilomita 945. Wakati huo, mzozo wa ugavi wa maji ya Helmand uliibuka baada ya Waingereza kuigawa eneo la Sistan na Baluchistan wakati wa uwekaji mipaka ili kutengeneza kitovu cha mzozo wa kudumu kati ya nchi za Kiislamu za Afghanistan, Iran na Pakistan kama walivyofanya katika nchi zote za Kiislamu na zisizo za Kiislamu walizozivamia na kuzitawala kisha wakazigawa, ili kuchochea uasi katika eneo lililogawanywa ambapo kuna harakati ya uhuru wa eneo hilo kutoka kwa nchi hizo tatu, ili kuwe na mwanya kwao, yaani kwa Waingereza, kuingilia nchi hizi huku zikigombania mipaka kati yao na watu wake kuuana wao kwa wao. Hivyo, Waingereza hudumisha ushawishi wao katika nchi hizo na kufanya kazi ya kuzidhoofisha ili zisichomoke mikononi mwao au kurejesha ushawishi wao ndani yake ikiwa wataupoteza.
5- Mzozo kati ya nchi hizo mbili uliendelea mipakani, hasa baada ya kugeuza mkondo wa Mto Helmand mwaka 1896, ambao urefu wake unakadiriwa kuwa kilomita 1150 na unapita katika majimbo kadhaa ya Afghanistan, pamoja na jimbo la Sistan na Baluchistan ambalo Waingereza waliligawa kati ya Afghanistan, Iran na Pakistan! Na unamiminika katika Ziwa Hamun linaloshirikiwa na Iran. Mipaka ilichorwa upya kati ya nchi hizo mbili kupitia Kanali wa Kiingereza Henry McMahon na akagawa maji ya mto kati ya pande hizo mbili mwaka 1905, na akaweka sharti kwa Afghanistan kutojenga mabwawa ambayo yangedhuru usambazaji wa maji kwa Iran na akahukumu kuwa Iran ichukue thuluthi moja ya maji ya mto. Lakini upande wa Afghanistan wakati wa Amir wa Afghanistan, Habibullah Khan, haukukubali hilo na uliliona kuwa ni upendeleo kwa Iran. Tofauti ziliendelea na kamati kadhaa za usuluhishi ziliundwa na mikataba kusainiwa kisha kuvunjwa kwa kipindi cha miongo kadhaa. Mzozo ulizidi kati ya pande hizo mbili mwaka 1934. Pande hizo mbili ziliamua kutorejea kwenye Ibara ya Kumi ya mkataba wa 1921 uliotiwa saini kati yao ambao unataja "usuluhishi wa Uingereza katika migogoro ya mipakani". Pande hizo mbili zilirejea kwenye kamati ya usuluhishi ya Uturuki lakini kamati hiyo ilifeli... Kisha mazungumzo yalianza kati ya pande hizo mbili miaka ya 1936 na 1939 na wakati Wairani walipodai nusu ya maji yanayomiminika kwenye bwawa la "Kamal Khan", Waafghan walikataa na mazungumzo yakafeli. Hali kadhalika mazungumzo ya 1951 yalifeli, pamoja na mwaka 1958 hadi ulipofika mwaka 1973 ambapo mkataba ulitiwa saini kati yao ukiwapa Wairani chini ya 10% ya maji. Lakini bunge la Afghanistan halikuuidhinisha. Kisha wakomunisti walifanya mapinduzi nchini Afghanistan mwaka 1978 na kuukataa mkataba huo mzima, na kufuatiwa na uvamizi wa Kisovieti ukiongozwa na Urusi nchini Afghanistan mwaka 1979 na kuikalia nchi hiyo, hivyo hali ikabaki kama ilivyokuwa kati ya nchi hizo mbili.
6- Hali hiyo iliendelea baada ya kushindwa kwa Warusi na washirika wao na kujiondoa kwao kwa madhila nchini Afghanistan na kuundwa kwa serikali ya Mujahidina hadi kuingia kwa Taliban kwa mara ya kwanza madarakani kati ya miaka 1996 na 2001. Kisha ukaja uvamizi wa Marekani na kuikalia Afghanistan, na katika kipindi hiki hasa wakati Ashraf Ghani alipoingia madarakani mwaka 2014 alidhamiria kujenga mabwawa upande wa magharibi na mashariki mwa nchi kwenye mito yote kumi inayochimbuka Afghanistan na kumiminika nchi jirani bila Afghanistan kufaidika nayo, hivyo akajenga mabwawa takriban 49. Ujenzi wa bwawa la Kamal Khan katika jimbo la Nimruz karibu na mpaka wa Iran ulikamilika, ujenzi wake ulichukua miaka 4 na lilifunguliwa mnamo Machi 2021 na limeathiri pakubwa fungu la Iran la maji. Ashraf Ghani aliashiria kuwa hana nia ya kupitisha maji isipokuwa kwa kubadilishana na mafuta. Na kwa kuingia kwa harakati ya Taliban madarakani kwa mara ya pili mnamo 2021/8/15, Iran iliomba serikali mpya kurejea kwenye mkataba wa mwaka 1973. Ikumbukwe kuwa Iran yenyewe inashirikiana na nchi jirani katika suala la maji, jambo linalopelekea kutokea kwa matatizo ikiwa migawanyiko ya kikoloni itabaki kuwepo.
7- Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, aliwaonya watawala wa Afghanistan wakati wa ziara yake katika mji wa Chabahar katika jimbo la Sistan na Baluchistan mnamo 2023/5/18 akisema ("Kwamba haki ya maji kutoka Mto Hirmand 'Helmand' ni haki ya watu wa eneo la Sistan na Baluchistan na ndivyo ilivyoelezwa katika mikataba na makubaliano" na akasema akiwatishia watawala wa Afghanistan "Watawala wa Afghanistan wasichukulie jambo hili kuwa la kawaida na lazima walishughulikie suala hili kwa uzito, na tunawaonya juu ya umuhimu wa kutoa haki za watu wa Sistan ya Pakistan na Sistan na Baluchistan ya Iran kutokana na maji ya Mto Hirmand haraka iwezekanavyo" na akasema "Serikali inafanya kila juhudi kuleta maji kutoka Bahari ya Oman kwenda maeneo ya mashariki mwa Iran, lakini mradi huu unachukua muda"... Ukurasa wa Al-Alam wa Iran 2023/5/18). Shirika la habari la IRNA la Iran lilimnukuu Balozi wa Iran nchini Afghanistan, Hassan Kazemi, akisema ("Ikiwa itathibitika kuwepo kwa maji katika bwawa la Kajaki na Taliban wanazuia kuipa Iran fungu lake la maji ya Hirmand basi lazima wawajibike na wakati huo hoja itakuwa imetimia na serikali ya Iran inajua jinsi ya kuchukua hatua"... Al-Arabiya 2023/5/25). Inaonekana kutokana na matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa Iran anayefanya kazi nchini Afghanistan kuna vitisho vya kulipuka kwa hali kati ya nchi hizo mbili. Na hili Iran haukulifanya hapo awali wakati wa kuwepo kwa Wamarekani na serikali za Afghanistan zilizokuwa kibaraka wao, kwani uhusiano wake na serikali hizo ulikuwa mzuri licha ya kuwepo kwa tatizo hili kwa miongo kadhaa. Matamshi ya Rais wa Iran na maafisa wengine wa Iran yenye onyo na vitisho yanathibitisha kuwa hali kati ya nchi hizo mbili haiendi vizuri, na mvutano utabaki kuwa hali ya juu hadi Iran itatue tatizo la maji kwa upande wake kwa eneo lake la Sistan na Baluchistan kama alivyoashiria Rais wa Iran kwa kuleta maji kutoka Bahari ya Oman kisha kuyasafisha na kisha kuyasambaza kwenye ardhi ya kilimo. Inaonekana maafisa wa Iran wanataka kulitumia suala hilo kwa maslahi yao na kufanya sababu ya tatizo kuwa ni serikali ya Afghanistan inayozuia mtiririko wa maji kutoka Afghanistan, ikumbukwe kuwa tatizo hili lina umri wa zaidi ya karne moja na nusu, kwani kuna kutoridhika kati ya watu wa eneo hili dhidi ya utawala wa Iran na wanateseka kwa kutelekezwa na kutengwa, na eneo hilo linashuhudia harakati za maandamano dhidi ya utawala na kuna harakati inayolingania kujitenga.
8- Msemaji wa Imara ya Kiislamu ya Afghanistan, Zabihullah Mujahid, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter mnamo 2023/5/27 akisema ("Kwamba Kabul inashikilia kutekeleza ahadi zake lakini kiwango cha maji kimepungua kutokana na ukame mkali" na akasema: "Matamshi yasiyofaa yanayotolewa na upande wa Iran kuhusiana na hili yanaweza kudhuru uhusiano kati ya nchi hizo mbili na hivyo hayapaswi kurudiwa"). Hili ni jibu la kistaarabu lisilo na tishio lakini linakataa vitisho na kuonya dhidi yake, iwe ni kwa matamshi ya Raisi au maafisa wengine waliotoa matamshi ya vitisho kwa Afghanistan wakiidharau, na inaonekana kuwa Afghanistan haitaki kuharibu uhusiano na Iran.
9- Kuna mito ya mipakani nchini Afghanistan inayopakana na Iran kama Mto Helmand, Mto Farah na Mto Harirud, na kuna mito midogo zaidi kama Harut, Khasbush, Mto Khash na Mto Budai na yote yanachimbuka Afghanistan na kumiminika katika Ziwa Bozak na Ziwa Sabri yaliyoko kwenye mpaka wa pamoja kati ya nchi hizo mbili. Mto Helmand unachukuliwa kuwa chanzo kikuu cha kusambaza maji katika uwanda wa Sistan, na unachukuliwa kama mshipa wa uhai kwa jimbo la Sistan na Baluchistan ambalo linakabiliwa na ukame wa kudumu. Inaonekana kuwa mito ya Afghanistan na hasa Mto Helmand inacheza nafasi kubwa ya kijiopolitika katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili na Afghanistan inaweza kutumia suala la maji kama chombo chenye nguvu cha shinikizo kwa Iran na wengine ili kufikia malengo yake ya kiuchumi na kisiasa, hasa kwa kuwa takriban 95% ya maji haya yanatiririka ndani ya Afghanistan yenyewe.
10- Haya yote yaliyotangulia yanaonyesha kuwa asili ya tatizo ni kile walichokifanya Waingereza kwa "kupasua" nchi za Waislamu, wakafanya Sistan na Baluchistan kuwa sehemu tatu! Sehemu moja kwa Iran, sehemu kwa Pakistan na ya tatu kwa Afghanistan, na kwa sababu hiyo mkondo wa mto na mahali unapoishia umekuwa ukigombaniwa na vyombo vitatu vinavyotofautiana na kupigana juu yake, na lau nchi hizi tatu zingekuwa chombo kimoja, dola moja kama alivyoamuru Allah, mambo yangekuwa sawa na kunyooka. Na kwa sababu hiyo, suluhisho la tatizo hili lililofikia hatua ya mapigano kati ya Iran na Afghanistan haliwezi kuwa isipokuwa kwa kufuta vyombo hivi vya Iran na Afghanistan na vyombo vinginevyo vilivyopo katika ulimwengu wa Kiislamu na kuviunganisha katika dola moja inayosimama juu ya Uislamu, na kufuta tofauti za kirangi, kimadhehebu na mipaka iliyochorwa na Waingereza. Asili ya tatizo inajulikana kuwa ni mgawanyiko wa kikoloni wa nchi za Kiislamu, na kila mmoja ameunguzwa na moto wa ukoloni na mabaki yake, na baadhi ya maafisa wa Iran wamelieleza hilo kama tulivyoonyesha hapo juu. Na suluhisho la tatizo linajulikana kuwa ni umoja wa nchi hizi kama zilivyokuwa kabla ya ukoloni na kuzifanya kuwa dola moja inayosimama juu ya Uislamu kikweli, kwa misingi yake yote, matawi yake na nyanja zake, na hapo ndipo maji yatatiririka katika mikondo yake, na watu watakunywa na wanyama watapata maji na ardhi itatoa mazao yake kwa heri zake apendavyo Allah, na utajiri wa mafuta pia utagawanywa kwa wote, hivyo kila mmoja atafurahia neema alizowapa Allah, na watakuwa na furaha chini ya kivuli cha hukumu za Uislamu...
Na masuluhisho mengine yote ni ya sehemu tu na ya muda na ni mabomu yanayosubiri muda yaliyo tayari kulipuka wakati wowote. Hivyo tunatoa wito kwa wote kufanya kazi kwa bidii na juhudi kubwa kusimamisha Khilafah Rashidah kwa njia ya Utume itakayounganisha nchi za Waislamu, na kisha Waislamu watukuzwe kwa utukufu wa Uislamu na wawe waja wa Allah ndugu.
Hili ndilo suluhisho ambalo Uislamu unatuita kuelekea kwalo; ambapo kuna utukufu na maisha mema ya heshima:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا للهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ
"Enyi mliowaamini! Muitikieni Allah na Mtume Wake anapowaitia jambo litakalo kupeni uzima (wa kiroho na kimaisha). Na fahamuni kwamba Allah huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba kwake Yeye tu mtakusanywa." (QS. Al-Anfal [8]: 24)
17 Dhul-Qi'dah 1444 H 2023/6/6 M