Home About Articles Ask the Sheikh
Siasa

Jibu la Swali: Mabadiliko Mapya ya Kisiasa nchini Lebanon

January 24, 2025
86

Jibu la Swali

Mabadiliko Mapya ya Kisiasa nchini Lebanon

Swali: Gazeti la Al-Araby Al-Jadeed lilichapisha katika tovuti yake mnamo tarehe 21/01/2025: (...na Nawaf Salam alitoka baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri Joseph Aoun jioni ya leo Jumanne, katika ikulu ya Baabda akiwa amebeba faili nyeusi mkononi mwake bila kufichua ikiwa amewasilisha rasimu yoyote ya majina au muundo wa baraza la mawaziri...), ikifahamika kuwa: [Baada ya ombwe la urais lililozidi miaka miwili kutokana na hitilafu za kisiasa, Bunge la Lebanon lilimchagua Aoun kuwa rais wa nchi hiyo mnamo 09/01/2025. Siku 4 baada ya kuchaguliwa kwake, Aoun alimteua Nawaf Salam kuunda serikali mpya ya Lebanon... Al Jazeera 20/01/2025]. Ni nini kinachoendelea nchini Lebanon kutokana na kasi ya makubaliano ya kumsimika mkuu wa jeshi Joseph Aoun kuwa rais mnamo 09/01/2025 baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miaka miwili, kisha siku chache baadaye kukubaliana juu ya Nawaf Salam kuwa Waziri Mkuu mnamo 13/01/2025? Je, yote haya yamewezekanaje kwa kasi hii? Kisha, je, kasi hii inamaanisha kuwa kulikuwa na kazi iliyokuwa ikiandaliwa na bado inaandaliwa kubadilisha sura ya Lebanon ndani na nje, au ni mabadiliko ya kawaida kama yanavyotokea katika eneo hili?

Jibu: Ili kuweka wazi majibu ya maswali yaliyo hapo juu, tunapitia yafuatayo:

Kwanza: Maendeleo makubwa ya kisiasa katika eneo hili na ulimwenguni ndiyo yaliyopelekea mabadiliko haya ya haraka nchini Lebanon, na kisha Aoun akachaguliwa kuwa rais wa Lebanon, na Nawaf Salam akateuliwa kuongoza wizara. Ili kufafanua hilo, tunasema:

1- Mara tu baada ya kumuua viongozi wa Chama cha Iran (Hezbollah) na kabla ya kusitisha mapigano, kulijitokeza miito nchini Lebanon ya kumchagua rais na kukomesha ombwe la nafasi hiyo. Miito hii iliongozwa na wapinzani wa Chama cha Iran, kama vile kundi la Samir Geagea ambalo lilitangaza waziwazi kukataa kwake kuiunga mkono Gaza katika vita. Huku kulikuwa ni kutumia fursa ya hali iliyotokana na vita na kulikuwa kwa kushauriwa na wajumbe wa Ulaya waliokuwa wakizunguka nchini Lebanon sambamba na ziara za mjumbe wa Marekani Hochstein, ambazo zilikuwa zikizingatia usitishaji vita. Chama cha Iran kilikuwa kikipinga miito hiyo kutoka kwa upinzani wa Lebanon.

2- Baada ya vikao 12 vilivyofeli vya kumchagua rais nchini Lebanon katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, nguvu mbalimbali za kisiasa nchini Lebanon zilikubaliana ghafla juu ya shakhsia ya mkuu wa jeshi Joseph Aoun kuwa rais mpya atakayekomesha hali ya ombwe katika nafasi hiyo. Chama cha Iran kilikuwa kikitangaza kuwa mgombea wake ni Sleiman Frangieh (Chaneli ya Al-Alam, 07/01/2025), na huyu Frangieh anahesabiwa kuwa katika mhimili wa Iran na utawala ulioanguka wa Bashar. Kisha Sleiman Frangieh akatangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro ili kuwe na makubaliano.

3- Wafuasi wa mhimili wa Iran (Chama chake pamoja na Harakati ya Amal) hawakumchagua Joseph Aoun katika kikao cha kwanza, yaani upigaji kura ulishindwa kwa sababu ya kutopata asilimia ya theluthi mbili (kura 86). Kisha katika kikao cha pili na baada ya mkutano na makundi haya ya bunge, walimpigia kura na akapata kura 99. Kwa hivyo, upigaji kura kwa Joseph Aoun katika kikao cha pili ulilenga kuonyesha kwamba lau si kura za Chama cha Iran na Harakati ya Amal, Joseph asingeshinda urais. Ingawa hilo lina maana fulani kwamba ushawishi wa wafuasi wa Iran bado upo na kwamba wanaathiri upigaji kura, lakini kuacha kwao kuzuia mchakato huo, huku wakiwa na uwezo wa kufanya hivyo, kunamaanisha kurudi nyuma.

4- Mnamo tarehe 13/01/2025, Waziri Mkuu mpya wa Lebanon, Nawaf Salam, aliteuliwa. Alipigiwa debe kama mgombea wa makubaliano ya kisiasa; yeye si Najib Mikati, mgombea wa Chama cha Iran na washirika wake, wala si Fouad Makhzoumi, mgombea wa kundi la Samir Geagea, yaani wapinzani wa Chama cha Iran. Hivyo ndivyo Nawaf Salam alivyoteuliwa kuwa Waziri Mkuu nchini Lebanon.

5- Nawaf Salam alikuwa mgombea aliyekataliwa na Chama cha Iran na nguvu shirika nchini Lebanon. Chama cha Iran kilimkataa mnamo mwaka 2019 baada ya kujiuzulu kwa Saad Hariri na kumwita wakati huo "mgombea wa Marekani" na Hassan Diab akateuliwa wakati huo. Chama kilikataa uteuzi wake tena katika mwaka huo huo baada ya mlipuko wa bandari ya Beirut mnamo 04/08/2019.

6- Inaonekana kuwa chaguo hili limekihasirisha Chama cha Iran na Harakati ya Amal: (Mwandishi wa chaneli ya Al Jazeera aliripoti mnamo 13/01/2025, kwamba kundi la wabunge wa Hezbollah halikumtaja mgombea yeyote kwa ajili ya urais wa serikali ya Lebanon. Na kufuatia mkutano wa wabunge wa kundi la "Hezbollah" na Rais wa Lebanon kwa ajili ya kumtaja waziri mkuu, mbunge wa chama hicho Muhammad Hassan Raad alielezea masikitiko yake, akisema kuwa baadhi wanafanya kazi ya kuitenga na kuifuta harakati hiyo. Aliongeza, katika taarifa kwa waandishi wa habari, "Tulipiga hatua chanya katika mkutano wetu na Rais wa Jamhuri, lakini hatukupata mkono wa ushirikiano," akisisitiza kuwa harakati hiyo itatenda kwa utulivu na hekima kwa ajili ya maslahi ya taifa. Chanzo kilicho karibu na Hezbollah kilikuwa kimeripoti kuwa chama hicho na mshirika wake Harakati ya Amal, inayoongozwa na Spika wa Bunge Nabih Berri, wanaunga mkono kuteuliwa tena kwa Mikati kuongoza serikali. Alifafanua kuwa kumtaja tena Mikati ni "sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na mjumbe wa Saudia nchini Lebanon Yazid bin Mohammed bin Fahd Al Farhan, ambayo yalipelekea Hezbollah na Amal kuendelea na uchaguzi wa Aoun kama rais siku ya Alhamisi iliyopita"), na kwa maana hiyo hiyo, BBC iliripoti mnamo 13/01/2025 kutoka kwa mkuu wa kundi la Chama cha Iran bungeni kuwa kumtaja tena Aoun ni "sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na mjumbe wa Saudia nchini Lebanon, ambayo yalipelekea Hezbollah na Amal kuendelea na uchaguzi wa Aoun kama rais".

Pili: Hivyo ndivyo mambo yalivyokwenda nchini Lebanon ambapo Bunge lilimchagua rais mpya na kumteua waziri mkuu mpya pia. Kwa kuangalia kwa umakini tunapata yafuatayo:

1- Tunapata kuwa Marekani imeridhika kikamilifu na maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon, bali usahihi zaidi ni kwamba yeye ndiye anayeyasimamia. Rais Biden alisema katika taarifa: ("Nampongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Lebanon", na akaendelea: "Rais Aoun atatoa uongozi madhubuti wakati Lebanon na (Israel) zinatekeleza usitishaji kamili wa uhasama na kurejea kwa mamia ya maelfu ya watu katika nyumba zao na wakati Lebanon inapopata nafuu na kujijenga upya. Rais Aoun ana imani yangu. Naamini kwa dhati kuwa yeye ndiye kiongozi sahihi kwa wakati huu". CNN Arabic, 09/01/2025), na vilevile wakala wa Marekani Mohammed bin Salman nchini Saudi Arabia alimpongeza (Al-Hurra, 09/01/2025).

2- Hivyo basi, maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon hayana uhusiano na mzozo wa kimataifa juu yake, kwani Lebanon ilikuwa mikononi mwa Marekani wakati wa urais wa Michel Aoun ambaye alionekana kama sehemu ya mhimili wa Iran, na rais wa sasa Joseph Aoun aliteuliwa mnamo mwaka 2017 kuwa mkuu wa jeshi na wakala wa Marekani Michel Aoun, ikimaanisha kuwa rais wa sasa Joseph Aoun asili yake ni kutoka kwenye mduara wa mawakala wa Marekani. Bali Marekani kabla ya ombwe la nafasi ya urais mwaka 2022 na baada yake ilikuwa ikitoa misaada ya kijeshi kwa jeshi la Lebanon, yaani ina uhusiano wa karibu na mkuu wa jeshi Joseph Aoun. Na haiwezekani kwa Nawaf Salam pia kutoka nje ya mkondo huu, ambaye ametumia maisha yake katika elimu na ufundishaji katika vyuo vikuu vya Ufaransa na Marekani na taasisi za kimataifa, na mwisho wake akiwa Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

3- Kwa hiyo, Marekani inafanya mabadiliko ya sheria za mchezo wake nchini Lebanon leo. Baada ya kuwa ikitegemea Iran na mhimili wake na nguvu zinazofuata mhimili huo nchini Lebanon ili kuimarisha ushawishi wake, leo inafanya kazi ya kuzitenga nguvu hizi kwa ajili ya kuibua shakhsia mpya ili kuendeleza ushawishi wake nchini Lebanon. Lebanon ilikuwa mikononi mwa Marekani na bado iko, lakini Marekani inabadilisha sura na muundo.

4- Ama nguvu zinazofuata nchi za Ulaya, zinajua kuwa ushawishi wao ni mdogo kuliko ule wa Marekani. Ufaransa kupitia ushiriki wake katika Kamati ya Mataifa Matano ilikuwa ikikataa jina la Joseph Aoun kama mgombea wa urais tangu mwaka 2023 wakati Marekani na Saudi Arabia zilipopendekeza jina lake mapema (Al-Araby Al-Jadeed, 22/09/2023), lakini ililazimika mwishowe kumkubali. Kwa upande mwingine, nchi za Ulaya hazina ushawishi wa kumfanya rais kuwa mfuasi wao; kwani Samir Geagea, ambaye ni mmiliki wa kundi kubwa la Kikristo bungeni, hakuonyesha hata nia yake ya kugombea urais kutokana na upinzani mkali wa uteuzi wake kutoka kwa Chama cha Iran. Chama cha Iran kilisema (Hakuna kizuizi kwa jina lolote isipokuwa kwa Samir Geagea; kwa sababu mradi wake ni wa uharibifu kwa Lebanon. Asharq Al-Awsat, 06/01/2025). Vilevile, jina la mgombea Fouad Makhzoumi kwa ajili ya uwaziri mkuu lilikataliwa, ambalo lilipendekezwa na vyama vya upinzani (RT, 13/01/2025). Kwa hivyo, nguvu zinazofuata nchi za Ulaya haziwezi kuhodhi nafasi yoyote kati ya urais wa aina tatu nchini Lebanon na kwamba nafasi hizi zinabaki mikononi mwa wafuasi wa Marekani.

5- Lakini nchi za Ulaya zinakubali maendeleo mapya ya kisiasa nchini Lebanon, (Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alimpongeza Aoun kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Lebanon, katika ujumbe aliouchapisha kupitia akaunti yake kwenye jukwaa la "X". Macron aliona kuwa uchaguzi huu "unafungua njia kwa ajili ya mageuzi na kurejesha mamlaka ya Lebanon na ustawi wake". Al-Hurra, 10/01/2025). Alichosema rais wa Ufaransa kinaakisi hali ya nguvu za Ulaya na furaha yao kwa kupungua kwa kivuli cha Iran nchini Lebanon, yaani wanaridhika na kufikia sehemu ya matakwa yao ambayo ni kuiweka Lebanon kwenye njia iliyo mbali na Iran. Wanaridhika na kuwepo katika Kamati ya Mataifa Matano ya kushughulikia masuala ya Lebanon iliyoundwa baada ya ombwe la nafasi ya rais; kwani Ufaransa inakaa ndani yake bega kwa bega na Marekani, Misri, na Saudi Arabia, huku Qatar ikiwakilisha maslahi ya Waingereza ndani yake.

Yaani Marekani ndiye mchezaji mkuu wa kimataifa anayetawala nchini Lebanon leo, na ndiye anayebadilisha nyuso na sura. Ama nchi za Ulaya zinatosheka na yote hayo kwa kuondolewa kwa kivuli cha Iran nchini Lebanon.

Tatu: Ama kuhusu kubadilisha sura ya Lebanon ndani na nje, hilo linabainika kupitia mambo yafuatayo:

1- Ama ndani ya Lebanon, uwezekano mkubwa ni kwamba vikwazo dhidi ya silaha za Chama cha Iran vitaongezeka. Istilahi ya "Muqawama" (mapambano) ambayo hapo awali ilikuwa ikiambatana na matamshi na taarifa za urais nchini Lebanon imetoweka katika matamshi ya rais mpya na imetoweka katika taarifa zake:

a- (Tofauti na hotuba za kimapokeo zilizopamba tawala zilizopita baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon, hotuba ya Aoun ilikuja ikiwa na jumbe zilizo wazi, muhimu zaidi ikiwa ni msisitizo wake juu ya umuhimu wa "kuimarisha haki ya dola kuhodhi silaha" kama nguzo ya msingi ya kuimarisha mamlaka ya Lebanon. Al-Hurra, 10/01/2025). (Aoun alisema katika hotuba yake: Dola ya Lebanon - na narudia dola ya Lebanon - itajikomboa kutoka kwa uvamizi wa Kiisraeli, CNN Arabic, 10/01/2025).

b- (Nawaf Salam alizungumzia uvujishaji wa habari za vyombo vya habari kuhusu ugawaji wa wizara kwa vyama vya kimapokeo na kufuata pia masharti ya Hezbollah na Harakati ya Amal, hasa kwa kuzipa wizara ya fedha... Salam aliongeza kuwa "hajafungika na kutoa wizara yoyote kwa upande wowote, ama wizara ya fedha ni kama wizara nyinginezo si milki ya dhehebu fulani".. akisisitiza kuwa anapendelea serikali ya mawaziri 24... Al-Araby Al-Jadeed, 21 Januari 2025).

2- Ama kwa nje, kwa kutafakari kile kinachoendelea inazingatiwa yafuatayo:

a- Kinyume na ilivyozoeleka, hakuna jukumu lolote la Iran lililojitokeza katika kumchagua rais na waziri mkuu, ingawa kiini cha jukumu hili kipo nyuma ya misimamo ya chama chake nchini Lebanon. Kwa sababu Chama cha Iran na washirika wake wanaweza kuzuia maendeleo hayo na hawakufanya hivyo, basi mabadiliko haya ya Marekani ambayo yameelezewa kama mapinduzi yanafanyika kwa ridhaa ya kimya ya Iran. Ushawishi wa Iran unapungua kweli katika eneo la Kiarabu, na Marekani imeipa Uturuki jukumu la ufumbuzi wa kisiasa nchini Syria, na kuiondoa Iran kutoka humo kama ilivyoiondoa Urusi kwenye mlinganyo wa Syria kabisa. Hii ndiyo sera mpya ya Marekani katika eneo hili, na hiki ndicho ilichokifanya nchini Lebanon. Hii si sera ya utawala wa Biden pekee, bali utawala ujao una maono hayo hayo, na utafanya kazi ya kuimarisha zaidi nchini Syria na Lebanon na kuipanua hadi Iraq. Sera hii ya Marekani inaendana kabisa na kile anachokitaka Kiyani Yahudi, na huenda ikawa ni kati ya ahadi ambazo utawala wa Biden uliahidi Kiyani Yahudi ulipoushawishi kukubali kusitisha mapigano nchini Lebanon.

b- Inaonekana kuwa Rais mpya wa Lebanon anatambua kuwa Marekani inamleta katika hatua hii kwa ajili ya mabadiliko makubwa katika sura ya Lebanon, (Rais Aoun alisema mwanzoni mwa hotuba ya kiapo: "Waheshimiwa wabunge wamenipa heshima kwa kunichagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Lebanon, nayo ni nishani kubwa zaidi ninayoibeba na majukumu makubwa zaidi. Nimekuwa Rais wa kwanza baada ya karne ya kwanza ya kuasisiwa kwa dola ya Lebanon Kubwa, katikati ya mtetemeko wa Mashariki ya Kati ambapo ushirikiano umepata nyufa na tawala zimeanguka na huenda mipaka ikabadilika". Independent Arabic, 11/01/2025). Kwa mujibu wa chanzo hicho hicho, ataelekea Saudi Arabia katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi, (Rais wa Lebanon Joseph Aoun alisema leo Jumamosi kuwa Saudi Arabia itakuwa nchi yake ya kwanza ya ziara ya nje, kufuatia kupata mwaliko wa kuizuru wakati wa mazungumzo ya simu aliyoyafanya na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Mwanamfalme Mohammed bin Salman).

c- Inabainika kutokana na yote haya pia kuwa Marekani inaipa Saudi Arabia jukumu la masuala ya Lebanon safari hii, baada ya kuwa Iran safari iliyopita. Kwa hivyo, jukumu la Saudia litakuwa maarufu katika masuala ya Lebanon, na itakuwa na nafasi katika ujenzi mpya hasa kwa kuwa inatarajiwa kuwa Iran itakumbwa na shinikizo jipya la kibiashara na kifedha litakalowekwa na utawala wa Trump. Hivyo Saudia itakuwa mbadala wa Iran nchini Lebanon, upande wa kisiasa na vilevile kifedha kwa ajili ya ujenzi mpya na kuunga mkono dola ili kuimarisha jeshi lake na kurahisisha upokonyaji silaha wa Chama cha Iran. Hilo linaweza kuivuta Lebanon kwenye tathbi' (kuhalalisha mahusiano) na Kiyani Yahudi hasa kwa kuwa rais ajaye wa Marekani Trump anahimiza tathbi' ya Saudia na Kiyani Yahudi.

Nne: Hali hii ya kutisha inatarajiwa kuendelea nchini Lebanon na maeneo jirani ya Lebanon mpaka Allah atakapoleta jambo lililoahidiwa, ikasimamishwa Dola ya Kiislamu, Dola ya Khilafah, na kutoweka nguvu hizi zote za kisiasa kutoka Lebanon na maeneo jirani ya Lebanon, na kutoweka pamoja nazo Kiyani Yahudi, kama ulivyotoweka utawala wa Assad nchini Syria. Hivyo ardhi ya Sham itarejea kama ilivyokuwa siku zote, kuwa moyo unaodunda kwa ajili ya Umma wa Kiislamu mzima. Sisi tuna utulivu na kurejea kwa Khilafah upya baada ya utawala huu wa kijabari tunamoishi ndani yake.. Ahmad amepokea kutoka kwa Hudhayfah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

«ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ. ثُمَّ سَكَتَ»

"Kisha utakuwepo utawala wa kidikteta (kijabari) na utakuwepo kwa muda anaotaka Allah uwepo, kisha Atauondoa Atapotaka Auondoe, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume. Kisha (Mtume) akanyamaza."

Na kwamba mahali popote itaposimama itafika Sham na kutulia humo. Al-Tabarani amepokea kutoka kwa Salama bin Nufayl amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

«عُقْرُ دَارِ الإِسْلامِ بِالشَّامِ»

"Makao makuu ya nchi ya Uislamu yako Sham."

Na itapigana na Mayahudi na kuondoa kiyani chao kinachokalia kwa mabavu ardhi iliyobarikiwa na kuirejesha Palestina yote katika nchi ya Uislamu.. na hakika kesho iko karibu kwa mwenye kuingojea.

Lakini sunna ya Allah imehitaji kuwa hawatashuka kwetu malaika kutoka mbinguni watakaotusimamishia Khilafah itakayopigana na adui yetu huku tukiwa tumekaa, bali anawateremsha malaika wake kama msaada na bishara ya ushindi wake kwa wanaume walioamini Mola wao na akawazidishia uongofu, wanajeshi Waislamu, wenye subira katika vita, wanaolindwa kwa Imamu wao na kupigana nyuma yake dhidi ya maadui zao.. na kisha tutakuwa miongoni mwa waliohakikishiwa bishara:

نَصْرٌ مِنَ اللهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

"Msaada unatokana na Allah, na ushindi uko karibu. Na wabashirie Waumini." (QS. As-Saff [61]: 13)

Katika tarehe 23 Rajab 1446 H 23/01/2025 M

Share Article

Share this article with your network