Home About Articles Ask the Sheikh
Maamuzi

Jibu la Swali: Hukumu ya Yanayotokana na Miamala ya Kifedha ya Makafiri Kabla ya Kusilimu Kwao

October 20, 2016
6365

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Kwa Michael Christensen

Swali:

(Michael Christensen

Barakallahu feek. Swali langu linahusiana na Uchumi ambapo natafuta ufafanuzi kuhusu kushughulika na hisa (stocks): Huu ndio mchakato; Tangu nikiwa mdogo (chini ya miaka 10 - karibu miaka 20 iliyopita) mama yangu alinipa baadhi ya Hisa katika benki kwa jina langu. Hisa hizi zimeongezeka thamani na mnamo mwaka 2015 mama yangu aliniuzia hisa hizo kwa niaba yangu na kunipa pesa hizo.

Sijatumia pesa hizo kwa sababu sijui kama ni halali kwangu. Nilisilimu miaka 6 iliyopita na sijui mengi kuhusu mfumo wa Uchumi wa Kiislamu, lakini sijui (sasa najua) kuwa Hisa ni haramu. Lakini ni ipi hukumu katika hali hii yangu kwani nimeambiwa kuwa maelezo niliyotoa ni muhimu katika jambo hili. Je, inawezekana kwako kunipa hitimisho fupi lakini la kina la Kiislamu kuhusu mimi kubakiwa na pesa hizo au kuzitupa?

Natumai unaelewa swali langu, vinginevyo niulize kwa maelezo zaidi, asante.

*not know = do know Stocks are forbidden) Mwisho.

Jibu:

(Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Tumechelewesha jibu mpaka tulipopata jibu lako la ufafanuzi wa swali lako kama ifuatavyo:

1- Tarehe ya kusilimu kwako, hata kwa kukadiria: Septemba 2010.

2- Tarehe ya kujua kwako kuwa hisa ni haramu: 2015.

3- Ulipomwakilisha mama yako kuuza hisa zilizo kwa jina lako, je, mama yako alikuwa kafiri, au alikuwa Muislamu wakati wa uwakilishi? she was and still is kafirah (alikuwa na bado ni kafiri).

4- Alimuuzia nani hisa hizo? Je, aliyenunua ni Muislamu au kafiri?

the shares were sold back to the Bank (money bank), not muslims (Hisa ziliuzwa tena kwa benki (benki ya fedha), wamiliki wake si Waislamu).

  • Kutokana na hayo, tumeelewa kutoka kwa swali lako la asili na jibu lako kwa ufafanuzi wetu yafuatayo:

Mama yako asiye Muislamu alikupa zawadi ya hisa takriban miaka ishirini iliyopita ulipokuwa chini ya umri wa miaka kumi na hukuwa Muislamu wakati huo... Na mama yako akaweka hisa hizo kwa jina lako benki... Thamani yake ikaongezeka katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita kuliko thamani yake ya asili... Kisha ukasilimu takriban miaka sita iliyopita, yaani karibu mwaka 2010...

Na kwamba ulijua kuwa hisa hizi ni haramu kwa Muislamu, na ilikuwa mwaka 2015... Na ukamwakilisha mama yako katika mwaka huo huo wa 2015 kukuuzia, na mama yako alikuwa kafiri wakati ulipomwakilisha... Naye akauza hisa hizo kwa benki kwenu ambayo wamiliki wake ni makafiri...

  • Na sasa unauliza ni kipi halali kwako katika mali hii?

Ndugu mpendwa, mwanzoni namhimidi Mwenyezi Mungu aliyekuongoza kwenye Uislamu ukasilimu, na akakuongoza katika kushikamana na halali na haramu, kwani unauliza ni nini halali kwako... Basi Mwenyezi Mungu akubariki, na akuneemeshe kwa riziki ya halali na nzuri, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe.

  • Ama jibu kuhusu nini ni halali kwako katika hisa hizo ni kama ifuatavyo:

1- Hakika kile kinachotokana na miamala ya kifedha ya makafiri kabla ya kusilimu kwao, ni halali kwao baada ya kusilimu, isipokuwa ikiwa mali hiyo ilikuwa ni ya kunyang'anywa au kuibiwa, kwani hiyo si halali kabla ya Uislamu wala baada ya Uislamu. Miongoni mwa dalili za hayo ni:

A- Miamala ya kifedha kabla ya Uislamu:

Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Amr bin al-Aas kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: إِنَّ الْإِسْلَامَ يَجُبُّ مَا كَانَ قَبْلَهُ "Hakika Uislamu unafuta yaliyokuwa kabla yake."

Na Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Amr bin al-Aas kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwamba amesema: أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ الْإِسْلَامَ يَهْدِمُ مَا كَانَ قَبْلَهُ؟ "Je, hufahamu kwamba Uislamu unabomoa (unafuta) yaliyokuwa kabla yake?"

Hadithi hizi zinaonyesha kuwa anayesilimu hawajibiki kwa yaliyokuwa kwake kabla ya kusilimu kwake... An-Nawawi amezungumzia katika sharhi yake ya Sahih Muslim wakati wa kufafanua hadithi hii yafuatayo: (Na kauli yake (saw) "Uislamu unabomoa yaliyokuwa kabla yake" ina maana unayaangusha na kufuta athari yake)... Kwa hivyo, kile anachochuma kafiri katika mali kabla ya kusilimu kwake hatowajibishwa nacho baada ya kusilimu kwake, bali itakuwa ni mali yake hata kama aliichuma kwa njia ya haramu, yaani itakuwa ni mali halali kwake kwa mujibu wa Sharia...

Mtume (saw) aliwakubalia Waislamu mali zao walizozichuma wakiwa makafiri, hakuwa akiwataka (saw) wanaposilimu watoe mali zao walizozichuma kupitia riba, kuuza pombe, kamari, au njia yoyote nyingine ya kumiliki mali au kuikuza ambayo Uislamu umeiharamisha, yaani miamala iliyoharamishwa katika Uislamu... Bali aliwaachia mali zao walizokuwa nazo wakati wa kusilimu kwao, lakini (saw) alikuwa akiwahisabu kwa miamala yao ya kifedha baada ya kusilimu, yaani kuanzia wakati wa kusilimu kwao, na hiyo ni kwa mujibu wa hukumu za kisharia; riba ni haramu, pombe ni haramu, kamari ni haramu... Na hivyo ndivyo ilivyo lazima kushikamana na miamala ya kifedha kwa mujibu wa hukumu za kisharia baada ya kusilimu.

B- Ama ikiwa ni mali ya kunyang'anywa au kuibiwa kabla ya kusilimu kwake na ipo naye baada ya kusilimu kwake, basi inarudishwa kwa mwenyewe. Hii ni kwa sababu unyang'anyi unapaswa kufidiwa kwa aliyenyang'anywa, hivyo ni lazima kwa mnyang'anyi kurudisha kitu alichonyang'anya kwa mwenyewe kutokana na yaliyopokewa kutoka kwa Samurah, kutoka kwa Mtume (saw) amesema: عَلَى اليَدِ مَا أَخَذَتْ حَتَّى تُؤَدِّيَ "Ni juu ya mkono kile ilichokichukua mpaka ikirejeshe." Ameitoa At-Tirmidhi na akasema hii ni hadithi Hasan.

Na Muslim amepokea kutoka kwa Wail bin Hujr amesema: "Nilikuwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) wakaja watu wawili wakigombania ardhi, mmoja wao akasema: 'Hakika huyu amevamia (intaza) ardhi yangu, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika zama za Jahiliyyah' - naye ni Imru’u al-Qais bin Abis al-Kindi na mpinzani wake ni Rabia bin Abdan - akasema: 'Ushahidi wako', akasema: 'Sina ushahidi', akasema: 'Kiapo chake', akasema: 'Basi ataichukua', akasema: 'Huna lingine ila hilo', akasema: Aliposimama ili aapie, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: مَنِ اقْتَطَعَ أَرْضًا ظَالِمًا لَقِيَ اللَّهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْـبَانُ "Mwenye kuchukua kipande cha ardhi kwa dhuluma, atakutana na Mwenyezi Mungu huku Yeye akiwa amemkasirikia."

Na maana ya intaza ‘ala ardhi ni kuishinda na kuimiliki, yaani kuichukua kwa nguvu (unyang'anyi). Mtume (saw) aliangalia madai ya mtu huyo dhidi ya aliyemnyang'anya ardhi yake akijua kuwa ilikuwa katika zama za Jahiliyyah, na hii inaonyesha kuwa mali ya kunyang'anywa ina hukumu nyingine tofauti na hukumu ya mali anazochuma mtu kwa miamala ya haramu kabla ya kusilimu kwake. Mali ya kunyang'anywa haiwi halali kwa kafiri anaposilimu, bali inabaki kuwa mali ya mwenyewe wa asili, na ni juu ya kafiri aliyesilimu kurudisha mali hiyo kwa mwenyewe wa asili kwa mujibu wa hukumu za kisharia...

Na mali ya kuibiwa vivyo hivyo, Ahmad ametoa kutoka kwa Samurah, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: إِذَا سُرِقَ مِنَ الرَّجُلِ مَتَاعٌ، أَوْ ضَاعَ لَهُ مَتَاعٌ، فَوَجَدَهُ بِيَدِ رَجُلٍ بِعَيْنِهِ، فَهُوَ أَحَقُّ بِهِ، وَيَرْجِعُ الْمُشْتَرِي عَلَى الْبَائِعِ بِالثَّمَنِ "Mtu anapoibiwa bidhaa, au akapoteza bidhaa, kisha akaikuta mkononi mwa mtu fulani, basi yeye ana haki zaidi nayo, na mnunuzi atadai thamani (pesa zake) kutoka kwa muuzaji." Huu ni andiko la wazi kuwa mali ya kuibiwa inarudishwa kwa mwenyewe.

  • Na kwa kuwa mali ambayo mama yako alikuwekea kabla ya kusilimu kwako ni muamala wa kifedha usio wa kunyang'anya wala kuiba, basi hiyo ni halali kwako baada ya kusilimu kwako.

2- Ama baada ya kusilimu kwako, ikiwa muamala wa kifedha ni miongoni mwa mambo ambayo mfano wako anaweza kuyaidunika (kutoyajua), basi ni halali kwako mradi tu hukuwa unajua kuwa ni haramu. Ukijua kuwa ni haramu, ni lazima uache kuishughulikia mara moja. Na kwa sababu hukuwa unajua kuwa hisa ni haramu isipokuwa mwaka 2015, yaani takriban miaka mitano baada ya kusilimu kwako, na hisa ni miongoni mwa mambo ambayo mfano wako anaweza kuwa hajui hukumu yake, basi ni halali kwako tangu ulisilimu mwaka 2010 mpaka ulipojua kuwa ni haramu mwaka 2015. Unapaswa kuainisha mwezi uliojua kuwa hisa ni haramu, basi itakuwa halali kwako mpaka tarehe hiyo ya mwaka 2015.

Dalili ya kwamba asiyejua anasamehewa mpaka anapojua ni kwamba ikiwa hukumu ya kisharia ni miongoni mwa mambo ambayo mfano wa mtendaji anaweza kuwa hajui, basi hawajibishwi kwa kitendo hicho, na kitendo chake kinakuwa sahihi, hata kama hukumu ya Sharia ndani yake ni kuwa ni batili. Hii ni kwa sababu Mtume (saw) alimsikia Muawiyah bin al-Hakam akimwombea rehema aliyepiga chafya (tashmit) naye yuko katika swala. Baada ya kumaliza swala, Mtume alimfundisha kuwa maneno yanabatilisha swala, na kumwombea rehema aliyepiga chafya kunabatilisha swala, na hakumuamuru kurudia swala. Muslim ametoa katika Sahih yake kutoka kwa Muawiyah bin al-Hakam as-Sulami, amesema: "Wakati nikiswali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), mtu mmoja alipiga chafya, nikasema: 'Yarhamukallah' (Mungu akurehemu), watu wakanitazama, nikasema: 'Ole wangu, mna nini? Mnanitazama', wakaanza kupiga mikono yao kwenye mapaja yao, nilipoona wananyamazisha nilinyamaza. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipomaliza kuswali - baba na mama yangu wafidiwe kwake - sijaona mwalimu kabla yake wala baada yake mwenye mafundisho mazuri kama yeye. Wallahi, hakunitolea ukali, wala hakunipiga, wala hakunitukana, akasema: إِنَّ هَذِهِ الصَّلَاةَ لَا يَصْلُحُ فِيهَا شَيْءٌ مِنْ كَلَامِ النَّاسِ، إِنَّمَا هُوَ التَّسْبِيحُ وَالتَّكْبِيرُ وَقِرَاءَةُ الْقُرْآنِ "Hakika swala hii haifai ndani yake kitu chochote katika maneno ya watu, hakika hiyo ni tasbihi, takbiri na kusoma Qur'ani." Au kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

An-Nasai ametoa mfano wake. Hivyo, kitendo cha maneno kubatilisha swala kilikuwa ni miongoni mwa mambo ambayo kwa kawaida mfano wa mtu huyo hakuwa anayajua, basi Mtume (saw) akamsamehe na akaichukulia swala yake kuwa sahihi. Na makampuni ya hisa (joint stock companies) kuwa ni haramu kisharia ni miongoni mwa hukumu ambazo mfano wake haujulikani na Waislamu wengi, na kwa sababu hiyo, ujinga (kutojua) unasamehewa. Hivyo, kitendo cha walioshiriki kinakuwa sahihi, hata kama makampuni hayo ni batili. Kama swala ya Muawiyah bin al-Hakam, hakika ilikuwa ni swala sahihi ingawa alifanya ndani yake jambo linalobatilisha swala, lakini alikuwa hajui kuwa maneno yanabatilisha swala.

Bila shaka, wanachuoni na watoa fatwa hawasamehewi kuhusu hisa kwa sababu hukumu hii haifichiki kwa mfano wao ikiwa watajitahidi kufahamu uhalisia wa makampuni ya hisa na dalili za kisharia zinazohusiana ili kutoa hukumu ya kisharia, hivyo wao hawasamehewi. Ama Waislamu wa kawaida, kama tulivyosema, hukumu hii hufichika kwa mfano wao na hivyo wanasamehewa, na wanapojua, ni lazima kwao kuziondoa hisa hizo kwa mujibu wa kile kinachothibitishwa na Sharia katika hilo...

3- Na wajibu unapofika baada ya mtu kujua hukumu ya kisharia katika hisa na kwamba ni batili, ni lazima aziondoe. Hilo ni kwa kumwakilisha anayeziona hisa hizi kuwa halali (yaani kafiri) ili aziuze kwa makafiri, na mwakilishi huyo achukue thamani (pesa) na kumpa mwenye hisa, na thamani hiyo itakuwa halali kwake, kwa sababu alikuwa hajui kuwa hisa ni haramu, na hukumu hii ilikuwa haijulikani kwa mfano wake. Dalili ya hayo ni kwamba wakati kodi ya ardhi (Khiraj) ilipokuwa inawajibika kwa Ahlu Dhimma, walikuwa wakilipa thamani ya kodi hiyo kwa pombe na nguruwe, Waislamu hawakuwa wakivichukua, bali walikuwa wakiwaacha wenyewe wauze na kisha Waislamu wanachukua thamani yake. Abu Ubaid al-Qasim bin Salam ametaja kutoka kwa Suwaid bin Ghaflah, kwamba Bilal alimwambia Umar bin al-Khattab: "Hakika wafanyakazi wako wanachukua pombe na nguruwe katika kodi (Khiraj)", akasema: (Msichukue kutoka kwao, bali waachieni wao wauze, na nyinyi chukueni thamani yake); na hiyo ni kwa sababu pombe na nguruwe ni mali miongoni mwa mali za Ahlu Dhimma, na si mali kwa Waislamu... Kwa hivyo, ikiwa mali katika asili yake ni haramu kwa Muislamu, kisha ikapatikana sababu ya kisharia iliyofanya mali hiyo imilikiwe na Muislamu, basi inajuzu kumwakilisha anayeiona kuwa halali kuiuza kwa anayeiona kuwa halali na Muislamu achukue thamani yake, na itakuwa ni halali kwake mradi tu ameimiliki kwa sababu hiyo ya kisheria.

Hivyo basi, umiliki wa Muislamu wa hisa ikiwa hukumu yake ilikuwa haijulikani kwake, basi thamani yake inakuwa halali kwake ikiwa atamwakilisha anayeiona kuwa halali kuiuza kwa namna ambayo Umar aliamuru kuhusu malipo ya Ahlu Dhimma ya kodi ya ardhi yao kutokana na pombe na nguruwe.

  • Na kwa kuwa ulimwakilisha mama yako naye ni kafiri kuuza hisa kwa benki za kikafiri, basi thamani hiyo ni halali kwako. Hii ni ikiwa ulimwakilisha mama yako katika tarehe hiyo hiyo uliyojua kuwa hisa ni haramu. Na kama mfano wa kuelezea:
  • Ikiwa ulijua kuwa hisa ni haramu mnamo Januari 2015 kwa mfano, na ukamwakilisha mama yako kuziuzia tarehe hiyo hiyo, basi thamani yote itakuwa ni halali kwako.

  • Na ikiwa ulijua kuwa hisa ni haramu mnamo Januari 2015, na ukamwakilisha mama yako kuziuzia mnamo Julai 2015, basi thamani yote itakuwa ni halali kwako isipokuwa faida iliyopatikana na hisa hizo katika miezi ya Februari, Machi, Aprili, Mei, na Juni. Faida za hisa katika miezi hii mitano ni lazima uziondoe kwa kuzitoa kwa ajili ya maslahi ya Uislamu na Waislamu.

  • Hitimisho ni kwamba hisa na faida zake ambazo mama yako alikuwekea ni halali kwako ikiwa ulimwakilisha mama yako kuziuzia tarehe hiyo hiyo uliyojua uharamu wa hisa hizo. Na ikiwa kuna tofauti katika uwakilishi, kama vile ulimwakilisha baada ya miezi miwili au mitatu... tangu ulipojua uharamu wa hisa, basi faida za hisa hizo katika miezi hiyo miwili au mitatu si halali kwako.

Mwishoni, nakutumia salamu na nakupongeza kwa kujali kwako halali na haramu, na nakuombea heri, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network