Kwanza: Nilikuwa nimewatumia ujumbe yapata saa nne za usiku kwa saa za Madina jana usiku (usiku wa kuamkia Jumamosi) kwamba mwezi haukuonekana usiku huo, na hiyo ilikuwa ni kwa mujibu wa ripoti za kutafuta mwezi zilizotufikia. Sisi kwa kawaida hatuchelewi zaidi ya saa nne au saa nne na nusu usiku kwa saa za Madina usiku wa kuandama mwezi ili tusichelewe kutoa tangazo kwa ajili ya ndugu zetu walio upande wa Mashariki, kama vile Indonesia na maeneo jirani, ili tangazo liwafikie kabla ya adhana ya Alfajiri. Kwa msingi huo, tangazo lilitolewa kwamba Jumamosi 23/05/2020 itakuwa ni kukamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwamba Eid itakuwa siku ya Jumapili 24/05/2020.
Pili: Kisha habari ikatufikia kwamba mwezi umeonekana na Waislamu watatu nchini Tanzania, pamoja na washuhuda wengine barani Afrika... Hivyo tulituma ujumbe kwa mwakilishi wetu huko ili awatume watu wawili kwa wale walioona mwezi ili kuhakikisha jambo hili, na alifanya hivyo, akatutumia jibu ambalo ni kama ifuatavyo:
5. ]The 3 witnesses saw a very thin crescent ? with the 2 points upwards and the bow facing the sun which had set.
6. They have sworn oaths and declared the shahada before our 3 shabab.[
Tatu: Jibu la mwakilishi lilitufikia mwendo wa saa saba mchana kwa saa za Madina. Hii ina maana kwamba kuonekana kwa mwezi kulikuwa ni sahihi, kwani upinde wa mwezi (The Bow) ulikuwa umeelekea upande wa kuzama kwa jua: (the bow facing the sun which had set), yaani, kilichoonekana ni mwezi mwandamo wa Shawwal, na hilo limethibitishwa kwa ushuhuda wa Waislamu watatu.
Nne: Baada ya kutafakari suala hili na kwa kuegemea hadithi ya Mtume ﷺ iliyopokelewa na Imam Ahmad kutoka kwa Abu 'Umayr bin Anas, amesema: Alinihadithia ami yangu miongoni mwa Ma-Answar katika Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:
غُمَّ عَلَيْنَا هِلَالُ شَوَّالٍ فَأَصْبَحْنَا صِيَامًا فَجَاءَ رَكْبٌ مِنْ آخِرِ النَّهَارِ فَشَهِدُوا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنَّهُمْ رَأَوْا الْهِلَالَ بِالْأَمْسِ فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ يُفْطِرُوا مِنْ يَوْمِهِمْ وَأَنْ يَخْرُجُوا لِعِيدِهِمْ مِنْ الْغَدِ
"Mwezi wa Shawwal ulifichika kwetu (kwa sababu ya mawingu), hivyo tukaamka tukiwa tumefunga. Kisha msafara ukaja mwishoni mwa mchana na wakatoa ushuhuda mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kwamba waliuona mwezi jana yake. Hivyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akaamrisha wafungue katika siku yao hiyo na watoke kwenda kwenye Eid yao kesho yake." (Musnad Ahmad)
Na Al-Bayhaqi ametoa katika As-Sunan al-Kubra kutoka kwa Rib'iy bin Hirash, kutoka kwa mtu mmoja miongoni mwa Maswahaba wa Mtume ﷺ amesema:
اخْتَلَفَ النَّاسُ فِى آخِرِ يَوْمٍ مِنْ رَمَضَانَ فَقَدِمَ أَعْرَابِيَّانِ فَشَهِدَا عِنْدَ النَّبِىِّ صلى الله عليه وسلم بِاللَّهِ لأَهَلاَّ الْهِلاَلَ أَمْسِ عَشِيَّةً فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم النَّاسَ أَنْ يُفْطِرُوا وَأَنْ يَغْدُوا إِلَى مُصَلاَّهُمْ
"Watu walitofautiana kuhusu siku ya mwisho ya Ramadhani, kisha wakaja Mabedui wawili na wakashuhudia mbele ya Mtume ﷺ kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba waliuona mwezi mwandamo jana jioni. Basi Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akawaamuru watu wafungue na waende asubuhi kwenye viwanja vyao vya kuswali." (As-Sunan al-Kubra ya Al-Bayhaqi)
Kwa mujibu wa hayo na kwa kufuata mfano wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ, basi leo Jumamosi 23/05/2020 ndiyo siku ya kwanza ya Eid al-Fitr... Hivyo basi Waislamu wafungue swaumu zao, na kwa kuwa wakati huu ni baada ya jua kuanza kupinduka (adhuhuri), basi waende kesho asubuhi kuswali swala ya Eid... Tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atutakabalie saumu na visimamo vyetu, na aufanye mwezi huu mtukufu kuwa ufunguzi wa kheri na baraka kwa Waislamu wote, na Mwenyezi Mungu (swt) aharakishe kwa Waislamu kusimamishwa kwa Khilafah yao, na awaponye kutokana na kila janga ili wapate utukufu hapa duniani na Akhera, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.
Mwenyezi Mungu atutakabalie ibada zetu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Siku ya Eid al-Fitr, 1 Shawwal 1441 H Inayoendana na 23/05/2020 M
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah