(Sfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")
Jibu la Swali
Hukumu ya Kumtesa Mtuhumiwa
Kwa Ndugu Juma’a
Swali:
Assalam Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh, Sheikh wetu mtukufu,
Ni nini hukumu ya kutumia kipigo ili mtuhumiwa akiri jambo ambalo anashukiwa nalo bila kuwepo kwa ushahidi madhubuti, bali ni dhana tu, huku ikijulikana kuwa chini ya kipigo hicho mwishowe hukiri kuwa yeye ndiye aliyefanya? Na sehemu ya pili ya swali: Je, inaruhusiwa kutumia sindano za kulevya (hallucination) ili mtuhumiwa akiri yale aliyo nayo, kwa sababu wanahalalisha matumizi yake ili kuepuka kipigo kikali ambacho wakati mwingine hupelekea kifo?
Ndugu yenu Juma’a Barro – Wilayah Syria
Jibu:
Wa Alaikum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Hakika kumtesa mtuhumiwa ni jinai kubwa katika Uislamu ambayo mtendaji wake huadhibiwa adhabu kali kwa mujibu wa hukumu za Sharia. Kadhalika, kutoa maungamo kwa mateso hakuna thamani yoyote katika taratibu za kesi. Si hivyo tu, bali hata kama tuhuma itathibitika dhidi ya mtuhumiwa kupitia kesi sahihi ya kimahakama, hairuhusiwi kwa kadhi kuamua adhabu dhidi ya mtuhumiwa inayohusisha mateso, bali ni adhabu zile tu zilizoelezwa na Sharia... Ili kufafanua hilo tunasema:
1- Tumeshaifafanua amri hii katika Ibara ya 13 ya Muqaddimah al-Dustur (Utangulizi wa Katiba), na matini yake inasema: (Asili ni kutokuwa na hatia, na hakuna yeyote atakayeadhibiwa isipokuwa kwa hukumu ya mahakama, na hairuhusiwi kumtesa mtu yeyote kabisa, na yeyote anayefanya hivyo ataadhibiwa). Na nitanukuu baadhi ya yaliyokuja katika ufafanuzi wake: Muslim amepokea kutoka kwa Wael bin Hujr amesema:
جَاءَ رَجُلٌ مِنْ حَضْرَمَوْتَ وَرَجُلٌ مِنْ كِنْدَةَ إِلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم، فَقَالَ الْحَضْرَمِيُّ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّ هَذَا قَدْ غَلَبَنِي عَلَى أَرْضٍ لِي كَانَتْ لأَبِي، فَقَالَ الْكِنْدِيُّ: هِيَ أَرْضِي فِي يَدِي أَزْرَعُهَا لَيْسَ لَهُ فِيهَا حَقٌّ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم لِلْحَضْرَمِيِّ: أَلَكَ بَيِّنَةٌ؟ قَالَ: لاَ، قَالَ: فَلَكَ يَمِينُهُ، قَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّ الرَّجُلَ فَاجِرٌ لا يُبَالِي عَلَى مَا حَلَفَ عَلَيْهِ وَلَيْسَ يَتَوَرَّعُ مِنْ شَيْءٍ، فَقَالَ: لَيْسَ لَكَ مِنْهُ إِلاَّ ذَلِكَ
"Alikuja mtu mmoja kutoka Hadramaut na mwingine kutoka Kinda kwa Mtume (saw), yule Mhadrami akasema: Ewe Mtume wa Allah, hakika huyu ameninyang'anya ardhi yangu iliyokuwa ya baba yangu. Yule Mkindi akasema: Ni ardhi yangu, iko mikononi mwangu ninailima na yeye hana haki nayo. Mtume wa Allah (saw) akamwambia yule Mhadrami: Je, una ushahidi? Akasema: Hapana. Akasema: Basi una kiapo chake (mtuhumiwa aapie kuwa si yako). Akasema: Ewe Mtume wa Allah, hakika mtu huyu ni muovu, hajali anachoapia na haachi jambo lolote. Akasema: Huna haki kwake isipokuwa hilo tu." (Imepokelewa na Muslim)
Na Al-Bayhaqi amepokea kwa sanad sahihi kuwa Mtume (saw) amesema:
البينة على المدعي، واليمين على من أنكر
"Ushahidi ni juu ya mdai, na kiapo ni kwa anayekataa."
Katika hadithi ya kwanza, Mtume (saw) amemtaka mdai atoe ushahidi, na hii inamaanisha kuwa mshtakiwa hana hatia mpaka ithibitike kinyume chake. Na katika hadithi ya pili, Mtume wa Allah (saw) amebainisha kuwa asili ya wajibu wa ushahidi ni juu ya mdai, jambo ambalo ni ushahidi kuwa mshtakiwa hana hatia mpaka hatia yake ithibitike...
2- Hivyo basi, mtuhumiwa hana hatia mpaka ithibitike, kwa hiyo hairuhusiwi kumtesa kwa njia yoyote ile ili kutoa maungamo kutoka kwake. Kumekuja ushahidi wa kisheria unaokataza hilo kwa uwazi:
a- Hakika Allah (swt) ameharamisha kushambulia nafsi ya Muislamu au sehemu yoyote ya mwili wake, na ameweka adhabu ya kisheria kwa anayeshambulia chochote katika hayo. Allah (swt) anasema:
وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَاناً وَإِثْماً مُبِيناً
"Na wale wanaowaudhi waumini wanaume na waumini wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi iliyo wazi." (QS Al-Ahzab [33]: 58)
b- Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Hisham bin Hakim bin Hizam, amesema: "Hakika nilimsikia Mtume wa Allah (saw) akisema:
إِنَّ اللهَ يُعَذِّبُ الَّذِينَ يُعَذِّبُونَ فِي الدُّنْيَا
"Hakika Allah atawaadhibu wale wanaowaadhibu (wanaowatesa) watu duniani."
c- Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Abu Hurairah, amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:
صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا، قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ...
"Aina mbili za watu wa motoni sijawaona bado; watu walio na mijeledi kama mikia ya ng'ombe wanayowapiga kwayo watu..."
3- Vilevile, kutoa maungamo kwa nguvu (shuruti) hakuna thamani yoyote katika taratibu za kesi wala hakuzingatiwi kwa sababu hayakuchukuliwa kwa hiari:
- Ibn Majah amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Abu Dharr al-Ghifari, amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:
إِنَّ اللَّهَ قَدْ تَجَاوَزَ عَنْ أُمَّتِي الْخَطَأَ، وَالنِّسْيَانَ، وَمَا اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ
"Hakika Allah ameisamehe umma wangu makosa (yasiyo na makusudi), kusahaulika, na lile walilosurutishwa (kulazimishwa) nalo." Basi kile anachosurutishwa nacho mtu hahusiki nacho.
- Al-Hakim amepokea katika Al-Mustadrak 'ala al-Sahihayn kutoka kwa Ibn Abbas (ra), amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:
تَجَاوَزَ اللَّهُ عَنْ أُمَّتِي الْخَطَأَ، وَالنِّسْيَانَ، وَمَا اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ
"Allah ameusamehe umma wangu makosa (yasiyo na makusudi), kusahaulika, na lile walilosurutishwa nalo."
4- Kadhalika, tuhuma ikithibitika kwa ushahidi wa kisheria dhidi ya mtuhumiwa mbele ya kadhi mwenye mamlaka ya mahakama, na katika baraza la mahakama kwa haki na uadilifu, basi hairuhusiwi kuwa na adhabu isipokuwa ile iliyoelezwa na Sharia, na si kwa adhabu ambazo Sharia imeziharamisha au haikuzitaja. Kwa mfano: Hairuhusiwi kuadhibu kwa kile alichokifanya Allah kuwa ni adhabu ya Akhera, na ushahidi wa hilo ni alichopokea Al-Bukhari kutokana na hadithi ya Abu Hurairah kwamba Mtume (saw) amesema:
وَإِنَّ النَّارَ لا يُعَذِّبُ بِهَا إِلاَّ اللَّهُ
"Na hakika moto, haadhibu kwao isipokuwa Allah."
Na Abu Dawood amepokea kutokana na hadithi ya Ibn Mas'ud katika kisa kimoja kwa tamko:
فَإِنَّهُ لا يُعَذِّبُ بِالنَّارِ إِلاَّ رَبُّ النَّارِ
"Kwani hakika haadhibu kwa moto isipokuwa Mola wa moto."
Kwa msingi huu, ikiwa itathibitika dhidi ya mtuhumiwa mbele ya kadhi mwenye mamlaka ya mahakama na katika baraza la mahakama kuwa amefanya jinai aliyoshtakiwa kwayo, hairuhusiwi kuadhibiwa kwa moto wala kwa mfano wake kama vile umeme, wala kwa chochote ambacho Allah huadhibu kwacho. Kadhalika, hairuhusiwi kutekeleza kwake isipokuwa adhabu ambazo Shari' amezitaja. Kwa hiyo, hakuna anayeadhibiwa kwa kuchomwa moto, wala kung’olewa kucha, au nyusi za macho, wala kumpiga kwa umeme, au kumzamisha kwenye maji, au kummwagia maji ya baridi, au kumnyima chakula, au kumuacha bila mahitaji yanayomkinga na baridi, au mengineyo. Bali anaadhibiwa kwa kuishia tu kwenye yale yaliyokuja katika Sharia miongoni mwa adhabu, na kinyume na hivyo ni haramu kwa mtawala kuyafanya kuwa ni adhabu kwa mkosaji...
Kwa sababu hii, hairuhusiwi kumtesa yeyote kabisa, na yeyote anayefanya hivyo amekhalifu Sharia. Na ikithibitika kuwa mtu amemtesa mwenzake, basi ataadhibiwa kwa hilo...
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
27 Safar 1438 H 27/11/2016 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir