Home About Articles Ask the Sheikh
Siasa

Jibu la Swali: Mkutano wa Kilele wa Erdogan na Putin huko Sochi, Urusi

October 07, 2021
2556

Jibu la Swali

Mkutano wa Kilele wa Erdogan na Putin huko Sochi, Urusi

Swali: Mnamo Jumatano, Septemba 29, 2021, mkutano wa kilele ulifanyika kati ya Erdogan na Putin huko Sochi, Urusi. Rais wa Uturuki alikuwa akiongoza ujumbe uliomjumuisha mkuu wa shirika la ujasusi Hakan Fidan, mkuu wa mawasiliano wa urais Fahrettin Altun, na msemaji wa urais Ibrahim Kalin, bila mjumbe yeyote wa mawaziri wake! (Ilikuwa ya kushangaza kwamba mkutano huo uliodumu kwa saa 3 ulifanyika faragha, na marais hao wawili hawakufanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mwishoni mwake, kinyume na itifaki zinazofuatwa na Kremlin katika ziara kama hizo. Pia, marais hao wawili hawakutoa taarifa ya pamoja ya mwisho... Asharq Al-Awsat, 30/09/2021). Je, ni nini sababu za ziara hii? Na malengo yake ni nini?

Jibu: Ili kujibu maswali yaliyo hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Kutokana na uchunguzi wa maslahi ya sasa ya Marekani, inaeleweka kuwa inaelekeza juhudi zake dhidi ya China na kwamba inapanga kujiondoa katika eneo la Mashariki ya Kati ili kujitolea kwa China, kisha kuwakabidhi vibaraka wake katika eneo hilo kutekeleza jukumu inalotaka. Sera hii ilikuwa mlangoni mwa utawala wa Trump, yaani muda mfupi kabla yake, ambapo mabadiliko katika siasa za Marekani yalitokea; kwani Marekani ilikuwa ikikusanya nguvu zake za kisiasa na kijeshi karibu na China, hivyo ilikimbilia kutumia zaidi nchi zilizo chini yake kama Uturuki. Sehemu ya sera hiyo ilikuwa utawala wa Trump kuipa Uturuki jukumu nchini Syria, Libya, mashariki mwa Mediterania, na maeneo mengine. Kwa jukumu hili jipya la Uturuki, Marekani ilijiondoa kivitendo kutoka katika mazungumzo ya mzozo wa Syria na kuufanya kuwa kati ya Uturuki na Urusi, na yakajitokeza juu mazungumzo ya Uturuki na Urusi huko Astana na Geneva, kisha kuingizwa kwa jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria...

2- Kisha jukumu hili lilipungua mwanzoni mwa enzi ya Biden kutokana na mazingatio ya kisiasa yaliyoonekana na chama cha Democratic. Mawasiliano ya kwanza ya simu kati ya Rais wa Marekani Biden na Erdogan wa Uturuki yalikuwa tarehe 23/04/2021, yakiwa yamechelewa, yaani baada ya miezi mitatu tangu Biden kuchukua madaraka huko Washington. Wakati wa mazungumzo hayo, walikubaliana kufanya kikao kati yao pambizoni mwa mkutano wa kilele wa NATO huko Brussels tarehe 14/06/2021. Katika ishara ya wazi ya tofauti kati yao, Rais wa Marekani alitangaza siku moja baada ya mawasiliano yao kwamba anachokiita mauaji ya Waarmenia nchini Uturuki yanachukuliwa kuwa ni mauaji ya kimbari. Biden alimfahamisha Erdogan nia yake ya kutangaza hilo wakati wa mazungumzo yao ya simu. Uturuki ilipiga kelele na Erdogan akapiga kelele, lakini kelele hizi zote zilibaki ndani ya makelele ya vyombo vya habari. Mkutano wa siri ulipofanyika pambizoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mnamo 14/06/2021 huko Brussels, makubaliano yao kuhusu Afghanistan yalijitokeza, na Erdogan alishangilia jukumu hili. (Erdogan aliashiria kwamba alijadili na Biden hali ya Afghanistan. Alisema: "Tuko tayari, hatuwezi kuwapuuza Taliban nchini Afghanistan, tuko tayari kushughulika nao ikiwa tutapata msaada kutoka Marekani pamoja na nchi nyingine..." CNN Arabic, 14/06/2021). Lakini inaonekana kuwa muhimu zaidi ya hayo lilikuwa suala la kujiondoa nchini Syria, hususan jukumu la Uturuki katika mazungumzo na Urusi kuhusu kujiondoa huko...

3- Kujiondoa kwa utata zaidi kwa Marekani kwa sasa ni Syria kwa sababu suala hilo halihusu Marekani pekee; kwani kuna Iran, chama cha Iran, Uturuki, na muhimu zaidi ya yote ni Urusi, ambayo iliingizwa Syria kwa himizo la Marekani mnamo 29/09/2015 wakati wa mkutano wa Obama na Putin. Mambo haya yote yanahitaji hatua fulani ili Marekani ihakikishe kujiondoa kamili kwa wengine, hususan Urusi, kabla yenyewe haijaondoa vikosi vyake. Hasa kwa kuwa imewapa uhakika Wakurdi kwamba inawaunga mkono na haitawaacha kama ilivyofanya nchini Afghanistan. (Kamanda mkuu wa vikosi vya Syrian Democratic Forces Mazloum Abdi alitaja kuwa Rais wa Marekani Joe Biden aliahidi kuwa Marekani haitawaacha washirika wake Wakurdi nchini Syria baada ya kujiondoa kwake Afghanistan mwezi uliopita... Abdi aliiambia The Times kutoka makao yake makuu karibu na mji wa Hasakah: "Walituhakikishia kuwa hii si Afghanistan. Walisema kuwa sera ya Marekani hapa ni tofauti kabisa." RT, 28/09/2021).

4- Marekani haitaki kujiondoa yenyewe na kuiacha Urusi, hasa kwa kuwa Urusi imeanza kuonyesha kutoridhishwa na sera ya Marekani ya kujitolea kwa China wakati ambapo Urusi inaikaribia China katika msimamo zaidi ya mmoja. Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Marekani wakati wa mkutano wa Rais wa Marekani Biden na Putin wa Urusi huko Geneva mnamo 16/06/2021, ilikuwa ikishinikiza Urusi ijitenge na China na kukaribia msimamo wa Marekani... Ingawa Marekani ilikuwa ikipanga kujiondoa Syria na kuwakabidhi vibaraka wake kusimamia mambo kwa niaba yake, na licha ya kuwa kujiondoa kwa Urusi ni jambo muhimu kwa Marekani kabla ya kuondoa vikosi vyake Syria kabisa na kuwakabidhi vibaraka wake kujaza pengo hilo ili yenyewe ijitolee kwa China; licha ya hayo yote, wakati huo huo haitaki kuifanya Urusi kuwa mshindani wake kulingana naye. Kwa hivyo haikujadili nayo moja kwa moja suala la kujiondoa Syria, bali ilimtwisha Erdogan jukumu la kujadili suala hili nayo kwa kuzingatia kuwa Urusi ina hadhi ya chini kiasi kwamba Marekani haiwezi kujadili nayo moja kwa moja mradi wa kujiondoa Syria. Hasa baada ya Marekani kuhakikisha kuwa kibaraka wake Bashar ameboresha uhusiano wake na nchi za eneo hilo kufuatia mazungumzo ya kufikisha gesi ya Misri kupitia Jordan, Syria, na Lebanon, na ikawa Marekani inaweza kumtegemea hadi itakapopata mbadala anayefaa kwake... Hivyo Marekani ilimtwisha Erdogan jukumu la kujadili na Urusi suala la kujiondoa kwa Urusi nchini Syria... (Erdogan alitangaza kuwa atakutana na Putin mnamo Septemba 29 ili kujadili uhusiano wa pande mbili na maendeleo ya hivi punde katika mkoa wa Idlib nchini Syria. Alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari, "Mkutano wangu na Putin utakuwa wa pande mbili bila kuwepo kwa mtu wa tatu, na hautahusu tu hali ya Idlib, bali tutajadili hali ya jumla nchini Syria, hatua tutakazochukua katika nchi hii, na uhusiano wa pande mbili pia." Erdogan aliashiria kuwa Uturuki na Urusi ni nchi mbili muhimu katika eneo hilo, akibainisha kuwa Putin ni kiongozi wa nchi, na alionyesha hilo katika kutatua mzozo wa Azerbaijan na Armenia. Al Jazeera Net, 28/09/2021). Na Erdogan ambaye aliongozana na Hakan Fidan mkuu wa shirika la ujasusi la kitaifa alisema kabla ya mkutano wake na Rais Putin katika mji wa Sochi, Urusi: (Amani nchini Syria inategemea uhusiano kati ya Uturuki na Urusi, na hatua zinazochukuliwa na nchi hizo mbili kwa pamoja zina umuhimu mkubwa. Anadolu Agency, 29/09/2021).

5- Urusi ilitambua jambo hili na kuliona kuwa ni tusi kwake kwamba Erdogan ajadili nayo suala la kujiondoa Syria badala ya Marekani kujadili nayo jambo hili moja kwa moja, hasa kwa kuwa Marekani ndiyo iliyoingiza Urusi nchini Syria. Vipi sasa isijadili nayo suala la kujiondoa moja kwa moja bali imempa Erdogan jukumu hilo?! Kwa hivyo, Urusi iliona hili kuwa ni tusi kwake, hasa kwa kuwa Putin anajitahidi kuiga Marekani kama nchi kuu yenye ushawishi duniani! Kwa hivyo, Urusi ilichukua msimamo dhidi ya Erdogan ili iwe somo kwa Uturuki na wakati huo huo ujumbe kwa Marekani labda itarejea na kukubali kujadili suala hili, yaani kujiondoa, nayo moja kwa moja, na hilo lilikuwa kupitia:

a- (Rais wa Urusi Vladimir Putin alipuuza kuwasili kwa mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini kwake Jumatano, na badala ya kumpokea uwanja wa ndege, alimtuma meya wa Sochi Alexei Kopaygorodsky, na naibu gavana wa jimbo la Krasnodar Alexander Ruppel... Na Erdogan alipokelewa katika uwanja wa ndege wa Sochi na mkurugenzi mkuu wa itifaki ya nchi katika wizara ya mambo ya nje ya Urusi, Igor Bogdashev, balozi wa Uturuki mjini Moscow, Mehmet Samsar, na konsuli mkuu wa Novorossiysk, Firat Bayar, na wafanyakazi wa ubalozi wa Uturuki... Turkey Now, 29/09/2021).

b- Vilevile, Putin aliielekeza gazeti la Pravda kumrushia matusi Erdogan na kumtaja kama "maskini"! Na inajulikana kuwa Pravda ni gazeti la Urusi ambalo lilikuwa miongoni mwa magazeti makubwa zaidi duniani kwa usambazaji wakati wa kipindi cha Kisovieti, na sasa ni moja ya magazeti kiongozi yaliyo karibu na ikulu ya Kremlin: (Gazeti la Urusi la Pravda, lililo karibu na Kremlin, Jumanne, lilimshambulia Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na kumtaja kama maskini, katika makala yenye maneno makali, kabla ya ziara yake huko Sochi, na katika makala iliyochapishwa katika gazeti la Pravda, mwandishi wa habari wa Urusi, Alexander Shtrom, alisema, "Maskini hana nafasi ya kuchaguliwa tena"... Turkey Now, 29/09/2021).

6- Hivyo basi, mkutano kati ya Putin na Erdogan ulibeba kufeli kwake tangu mwanzo hadi mwisho wake, bali hata kabla haujaanza! Na inaonekana Erdogan alitarajia hilo, na ndiyo maana alijali kuwa wahudhuriaji wa mkutano huo wawe wachache sana, yaani kati yake na Putin pekee, na hivyo mduara wa wanaojua kufeli huko usipanuke, na hivyo ndivyo ilivyokuwa... Hivyo basi hakuna matokeo yoyote chanya yaliyopatikana kutokana na mkutano huo, na alirudi mikono mitupu, na hata mkutano wa kiitifaki ambao hufanywa kawaida baada ya kila mkutano haukufanyika! (Ulihitimishwa katika mji wa Sochi, Urusi, leo Jumatano, mkutano wa Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, bila kufanya mkutano na waandishi wa habari na baada ya mkutano uliodumu kwa saa tatu, pande hizo mbili hazikutoa matokeo au maelewano yoyote, isipokuwa taarifa za kidiplomasia bila taarifa yoyote kuhusu maudhui ya mkutano... Kwa upande wake, mchambuzi wa kisiasa Darwish Khalifa alizingatia katika mazungumzo na tovuti ya Al-Araby Al-Jadeed kwamba kutotoa matokeo yoyote ya mkutano huo kunaashiria kutokuwepo kwa makubaliano kati ya pande hizo mbili na kuwepo kwa tofauti, na kwa kuzingatia hilo hakufanyika mkutano wowote na waandishi wa habari. Khalifa aliongeza kuwa faili la Syria ndio msingi wa mkutano huo na si kama wengine wanavyopigia debe kuhusu Ukraine au Libya... Al-Araby Al-Jadeed, 30/09/2021).

7- Kuhusu mkutano wa Erdogan uliopangwa kufanyika na Biden pambizoni mwa mkutano wa kilele wa G20 mwishoni mwa Oktoba, (Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan atafanya mkutano wa pande mbili na mwenzake wa Marekani Joe Biden wakati wa mkutano wa viongozi wa G20 uliopangwa kufanyika Oktoba ijayo... Vyanzo viliongeza kuwa Erdogan atakutana na mwenzake wa Marekani Biden pambizoni mwa mkutano huo. Anadolu Agency, 28/09/2021), inaonekana kuwa ni kuhusu hatua inayofuata baada ya kufeli kwa mkutano wa Erdogan na Putin!

Inategemewa kuwa Marekani ikiweza kudhibiti msimamo wa Urusi dhidi ya China, yaani kuifanya Urusi iikaribie dhidi ya China, basi wakati huo Marekani haitampa Erdogan thamani yoyote bali itauacha kufeli kwake kumzunguka yeye pekee! Na inaweza kurejea kukubaliana na Urusi ikiwa itahakikisha kuwa itajitenga na China... Kwani hizi nchi za kikoloni hazijali kuwaheshimu vibaraka wao au wale wanaozunguka katika mzunguko wao ikiwa itaona kuwa hilo litaleta maslahi kwake!

8- Na muhtasari wa jambo hili unaweza kujumuishwa katika nukta zifuatazo:

a- Marekani inajiandaa kujiondoa katika Mashariki ya Kati na kukabidhi mambo kwa vibaraka wake na kwa wale wanaozunguka katika mzunguko wake na yenyewe ijitolee kwa China, hata kama hautakuwa mzozo wa moto bali vita baridi kama msemaji wa ubalozi wa China mjini Washington, Liu Pengyu, alivyoituhumu Marekani kwa hilo akizungumzia muungano wa Marekani, Uingereza, na Australia kwa kusema: (Nchi hizi hazipaswi kuunda makundi ya kibaguzi yanayolenga maslahi ya pande nyingine au kuyadhuru, na jambo muhimu zaidi ambalo linapaswa kufanywa ni kuachana na fikra za vita baridi na upendeleo wa kiitikadi... Al Jazeera Net, 16/09/2021).

b- Dola ya Uthmaniyyah ambayo ilikuwa ikiitikisa Urusi kishindo haipo tena, hivyo Urusi na maadui wamepumua, na sasa watawala wa Uturuki kwa mtazamo wa Urusi wamekuwa dhaifu kiasi cha kutoshikika, hivyo haijali kuwapa uzito wowote katika utatuzi wala katika safari!

c- Kuna nukta chanya katika yote yaliyotokea, nayo ni kwamba nchi kafiri za kikoloni zinakaribia kufunga mizigo yao na kuondoka katika nchi za Waislamu, na ni fursa mwafaka kwa wabeba Da'wah na kila anayetaka kufuata ukweli kubashiri kheri kwa kukaribia kupanda kwa daraja ya Uislamu na watu wake, na kudhalilika kwa ukafiri na watu wake:

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

"Hakika katika hayo mna mawaidha kwa mwenye moyo (wa kuzingatia) au anayetega sikio naye awe shahidi (mwenye kuhudhurisha akili)." (QS. Qaf [50]: 37)

Mnamo tarehe 29 Swafar 1443 H 06/10/2021 M

Share Article

Share this article with your network