Swali:
Mnamo tarehe 19 na 20/11/2010, mkutano wa kilele ulifanyika mjini Lisbon, mji mkuu wa Ureno, ulioshirikisha nchi kuu na nchi za Muungano wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO). Imetangazwa kuwa nchi hizi zimekubaliana mkakati mpya wa muungano huo uliohusisha mada muhimu, ikiwemo suala la Afghanistan, suala la ngao ya makombora, na uhusiano na Urusi, pamoja na kuidhinisha upanuzi wa mamlaka ya muungano huo ili kuvuka eneo lake hadi mahali popote duniani ambapo muungano huo unaona kuna tishio kwake. Je, Marekani iko siriazi katika suala la kujiondoa Afghanistan? Na inalenga nini katika suala la ngao ya makombora? Kwa nini ilitaka kupanua mamlaka ya NATO? Na nini msimamo wa Urusi kuhusu haya yote? Je, Marekani imeweza kuzishurutisha nchi hizi kwa kile inachotaka? Na je, imeweza kuimarisha msimamo wake wa kimataifa?
Jawabu:
1- Yale yaliyobainika katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo na matamko kuhusu mkakati wa NATO nchini Afghanistan yanabainisha kubaki nchini humo kwa namna ya kudumu, na inahesabu Afghanistan kama suala la kifo na kupona kwa muungano huo. Katibu Mkuu wa NATO, Rasmussen, alitangaza akisema: "Tumekubaliana na Rais Hamid Karzai kuhusu ushirika wa muda mrefu utakaoendelea baada ya kumalizika kwa majukumu yetu ya kivita." Alisema: "Wacha tuseme tu kwa urahisi, ikiwa harakati ya Taliban au wengine wanatumai kuondoka kwetu, basi wasahau jambo hilo, tutabaki ilimradi ni muhimu kwa ajili ya kumaliza kazi." (BBC 20/11/2010). Imeelezwa pia katika taarifa ya mwisho: "Msisitizo kuwa jukumu nchini Afghanistan ni kipaumbele kwa muungano." Obama alikuwa amewataka viongozi wa nchi za NATO waliokutana Lisbon kwamba: "Wasisitize tena kujitolea kwao kwa kudumu nchini Afghanistan." (Gazeti la El Pais la Uhispania 19/11/2010). Shirika la Habari la Ujerumani lilitaja mnamo 20/11/2010 kwamba inatarajiwa kukabidhi mamlaka katika majimbo ya kwanza kwa upande wa Afghanistan ifikapo Julai mwaka ujao, huku vikosi vya muungano vikibaki na udhibiti wa usalama katika maeneo hatari zaidi hadi mwaka 2014, na kufanya kazi ya usaidizi baada ya tarehe hiyo.
Hii inaashiria kuwa Marekani inataka kujidhihirisha kwa kujiondoa katika maeneo salama, yaani ambayo hayana upinzani mkali kutoka kwa Mujahidina, ili kuonyesha kuwa inatimiza ahadi zake ilizojipangia kwa jina la rais wake Obama kwamba kuanza kujiondoa itakuwa mwezi Julai 2011. Hivyo ionekane kwa watu wa Marekani na watu kwa ujumla kuwa imetimiza ahadi zake—kana kwamba Marekani imeshafikia malengo yake na kwamba iko karibu kujiondoa kabisa—lakini uwepo wa vikosi hivi utaendelea hadi mwaka 2014 katika maeneo hatari zaidi. Huu ni ujanja wa kukwepa uamuzi wa kujiondoa Afghanistan na kwamba uvamizi utabaki hadi tarehe hii na baada ya tarehe hii. Marekani inafanya kazi nchini Afghanistan kutekeleza siasa inayofanana na siasa iliyoifuata nchini Iraq kwa kuhakikisha uwepo wake wa kudumu chini ya majina ya makubaliano ya kiusalama, mkakati, ushirika au mengineyo. Katika mkutano huu, Marekani imezishinikiza nchi za Ulaya ili ziendelee kuiunga mkono nchini Afghanistan. Wazungu wengi wanalazimika kubaki kando ya Marekani kwa sababu vita hivi havileti faida yoyote kwao, na faida zote ni za Marekani pekee, huku wao wakiteseka na hali ngumu ya kifedha na wananchi wao hawaoni faida yoyote ya kuendelea kwa vita hivi.
2- Kuhusu mada ya uhusiano wa NATO na Urusi, mkutano wa kilele ulifanyika kati ya nchi za NATO na Urusi chini ya jina la kikao cha (Baraza la Urusi - NATO) kilichojadili uhusiano huu kati ya pande mbili baada ya kuganda kufuatia mzozo wa Georgia mnamo Agosti 2008. Imetangazwa katika mkutano huo kuwa nchi za muungano zimeiondoa Urusi katika kuifikiria kama adui wa muungano na kwamba haionekani kuwa tishio lolote kwake, na hilo linafanyika kwa mara ya kwanza huku ikiwa karibu kutangaza ushirika wa kimkakati na muungano huo. Rais wa Urusi Medvedev alitamka: "Hatua ya baridi na malalamiko ya pande mbili katika mahusiano kati ya Urusi na NATO imekwisha." Alisema: "Tunatazama mustakabali kwa matumaini na tunajaribu kuendeleza uhusiano kati ya Urusi na NATO katika pande zote" (Russia Today 20/11/2010). Lakini aliashiria kuwepo kwa hitilafu ambazo bado hazijatatuliwa kama vile kadhia ya Georgia, akisema: "Kadhia hii isifanywe kuwa kikwazo" na akaashiria hitilafu nyingine bila kuzitaja majina akisema: "Hazipaswi kupelekea kuvunjika kwa mahusiano." (Chanzo hicho hicho).
Alitaja kuwa: "Urusi na nchi za NATO zimekubaliana kuendelea kujadili kadhia ya ngao ya makombora ya Ulaya" na akaongeza kuwa: "Nchi za NATO zenyewe hazioni matokeo yanayoweza kutokana na ngao hii... Pamoja na hayo, ni lazima iwe jumuishi na isiwe kwa ajili ya kuitumikia nchi fulani au kundi fulani la nchi pekee." Aliongeza pia: "Kujitokeza kwa mfumo wa ulinzi wa makombora kunaweza kuangamiza usawa wa nguvu za nyuklia, na hilo lazima liepukwe kwa sababu kubadilisha usawa huu kutapelekea mashindano ya silaha hatimaye." (Chanzo hicho hicho). Chanzo hiki pia kilitaja kauli ya Medvedev kuwa Moscow imeipendekezea NATO kuanzisha kile kinachoitwa mfumo wa (kisekta) wa ulinzi wa makombora bila kufafanua undani wa pendekezo hili.
Inafahamika kutokana na matamko ya Rais wa Urusi kuwa bado hakujafikiwa makubaliano ya mwisho kati ya Urusi na NATO kuhusu mada ya ngao ya makombora na suala la ushirika kati yao. Urusi bado ina wasiwasi na hilo, ambapo alitaja kuwa nchi za NATO zenyewe hazioni matokeo ya kuwekwa kwa ngao ya makombora. Inaonekana anaashiria nchi za Ulaya ambazo hazijui madhara ya jambo hilo kuwa zitaangukia chini ya udhibiti kamili wa Marekani na kwamba hilo litaleta mvutano wa kimataifa na kurejesha hofu za kiusalama kwao. Medvedev anaashiria hofu ya mashindano ya silaha, yaani kwamba nchi nyingine na ikiongozwa na nchi yake zitafanya kazi kuendeleza silaha zao kukabiliana na hali halisi mpya iliyoundwa na Marekani, yaani kwa ajili ya kujilinda na kusimama mbele ya Marekani ambayo itazikandamiza nchi nyingine kwa sababu ulinzi uliowekwa na Marekani umeimarishwa na itafanya kazi ya kuzitisha pande nyingine ili kuzisalimisha kwenye siasa zake.
Obama alikiri kuwa hakujafikiwa makubaliano ya mwisho na Urusi kuhusu mada hii akisema: "Tumeweka juhudi nyingi katika kurekebisha uhusiano kati ya Marekani na Urusi, mchakato ambao umeleta matokeo maalum kwa pande zote mbili. Na sasa tunafanya marekebisho ya mahusiano kati ya NATO na Urusi." Aliongeza: "Tunaiyona Urusi kama mshirika na sio mshindani, tumekubaliana kuimarisha ushirikiano wetu katika nyanja kadhaa na nyanja muhimu zaidi ni ushirikiano katika uwanja wa ulinzi wa makombora." (Russia Today 20/11/2010). Hivyo basi, Urusi haijapata kile inachokitamani, na ndiyo maana makubaliano ya mwisho hayajafikiwa kati yake na NATO, yaani kati yake na Marekani kuhusu ngao ya makombora na suala la ushirika, na inataka kuendelea na mazungumzo hadi ipate kitu muhimu kwake. Urusi ina hamu ya makubaliano na haiyakatai kabisa, na lengo lake kuu ni kuwa mshirika wa Marekani katika kusimamia mambo ya dunia kama ilivyokuwa katika enzi ya Umoja wa Kisovieti ili ihesabiwe kuwa dola kuu. Haitaki kuwa mfuasi wa Marekani, iwe kwa kujiunga na NATO au aina nyingine yoyote ya ufuasi. Inataka kuwa na sifa ya kuwa nchi kubwa yenye siasa ya kimataifa inayojitegemea. Medvedev alitamka akisema: "Ama tushiriki kikamilifu na kubadilishana taarifa na kupewa majukumu ya kutatua masuala haya au yale, au tusishiriki kabisa. Na Urusi haitakubali kuwa nchi iliyopachikwa tu kwenye muungano huo. Na ikiwa hatutashiriki kabisa, basi tutalazimika kujilinda kwa sababu zinazofahamika." (France Presse 21/11/2010). Medvedev alitaja pia: "Kwamba haoni uwezekano wa Urusi kujiunga na muungano wa NATO, lakini hakuondoa fursa ya ushirikiano wa karibu kati ya pande mbili iwapo muungano huo utabadilika na kupata uwazi zaidi katika mahusiano yao." Na alitangaza kuwa "Urusi imekubali kusafirisha shehena kwenda Afghanistan kupitia ardhi yake." (Russia Today 20/11/2010).
Hivyo Urusi imekubali kushirikiana na nchi za muungano kusafirisha vifaa vyake kupitia ardhi yake kwenda Afghanistan. Hii ni huduma ya bure inayotolewa na Urusi kwa Marekani kwa ajili ya kupata baadhi ya maslahi kutoka kwake wakati ambao haijapata chochote kutoka kwa Marekani. Ingawa Urusi inaona kuwa hali nchini Afghanistan inaweza kuitishia ikiwa NATO itashindwa mbele ya Mujahidina huko, lakini ushindi wa Marekani huko utatishia ushawishi wake, yaani ushawishi wa Urusi katika eneo la Asia ya Kati. Hivyo Urusi inapaswa kupiga mahesabu kwa hilo, na kukumbuka kuwa kushindwa kwake katika enzi ya Umoja wa Kisovieti nchini Afghanistan kuliwezesha Marekani kufika katika eneo hili. Hivyo inaonekana kuwa Marekani inataka kuchukua kila kitu kutoka kwa Urusi bila kuipa chochote isipokuwa ahadi tupu. Haitaki kuishirikisha katika kutatua masuala ya dunia bali inataka kuishirikisha katika majukumu yanayohusiana na kuitumikia chini ya jina la ushirika na NATO na wala si pamoja nayo moja kwa moja kwa usawa. Urusi haijaanguka kwenye mtego kikamilifu, ingawa inazunguka chambo za udanganyifu kutokana na utayari wake wa kufanya mazungumzo na hamu yake ya kuwa mshirika kamili!
3- Kuhusu mfumo wa ngao ya makombora, ni kwa ajili ya kuleta utawala kamili wa Marekani juu ya Ulaya ambapo inaiweka chini ya ulinzi wake na kuijazia hofu za kiusalama kila wakati ili kuimarisha udhibiti wake juu yake na kuizuia isiwe nguvu ya kimataifa inayojitegemea na kuishinda Marekani. Inaifanya Ulaya ijipuuze katika kuendeleza nguvu yake ya kijeshi yenyewe, bali inaifanya ipuuze maghala yake ya nyuklia ili yasiwe na thamani yanapoganda na kutofanyiwa kazi ya kuyaendeleza na kuyaboresha. Hiki ndicho Ufaransa ilichohofia na inajaribu kufanya kazi ya kukiepuka. Imefanya makubaliano kati yake na Uingereza kuboresha maghala yao ya nyuklia na kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwao wakati mkutano wa kilele ulifanyika kati ya pande hizo mbili hivi karibuni mwanzoni mwa mwezi huu, yaani tarehe 2/11/2010. Vilevile pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha kikosi cha pamoja cha kijeshi cha kuingilia kati kutokana na vikosi vyao ili kujitegemea katika maamuzi yao mbali na Marekani na kufanya kazi zinazotumikia maslahi yao mbali na utawala wake. Lakini yale yaliyotokana na mkutano wa Lisbon, na kutopinga kwa Uingereza ngao ya makombora inayopendekezwa na Marekani, inaashiria udhaifu wa msimamo wao na kwamba wamekata tamaa ya kufikia chochote katika mkutano huu ambao utawala wa Marekani umeonekana wazi.
Mpango wa ngao ya makombora kwa sura yake ni wa kiulinzi lakini maudhui yake ni ya kishambulizi yakilenga kupambana na kile kinachoitwa ugaidi, nchi kaidi, silaha za maangamizi, tishio la silaha za nyuklia, na makombora ya balestiki. Yaani Marekani kwa jina la NATO imesisitiza siasa iliyoifuata tangu mwanzoni mwa karne hii na hasa baada ya matukio ya Septemba 11, 2001. Baadhi ya nchi ziliipinga ikiwemo Ufaransa na Ujerumani mwanzoni mwa jambo hilo, na bila shaka Urusi pia. Lakini mkutano wa Lisbon umedhibiti msimamo wa Ufaransa na Ujerumani, na kulegeza msimamo wa Urusi, na hii inahesabiwa kuwa ni mafanikio kwa Marekani na idhini kwake kuendelea katika siasa zake za uchokozi. Siasa ya Marekani katika enzi ya Bush ilikuwa bila kuchukua idhini ya wengine, lakini siasa yake ya sasa katika enzi ya Obama ni mwendelezo wa siasa ya mtangulizi wake, lakini inakwenda kwa kuchukua idhini ya wengine.
4- Kuhusu mpango mpya na mkakati mpya unaosema kupanua mamlaka ya NATO na kupanua uwanja wake, huo unaidimisha kuendelea kuwepo kwa NATO ambayo ilipaswa kufutwa baada ya kutoweka kwa sababu iliyoanzishiwa muungano huu, ambayo ni kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti, ukomunisti, na mkataba wa Warsaw. Inaidimisha kuendelea kwake kwa kubuni maadui wapya na kutengeneza vitendo vinavyotishia nchi za NATO. Pamoja na kwamba mkutano huo haukutangaza wazi adui anayekusudiwa kwa muungano wa NATO, wala nini hasa kinachokusudiwa na ngao ya makombora kwa namna maalum, lakini utafiti wa kuifanya ngao ya makombora iwe nchini Uturuki unaonyesha kuwa lengo ni eneo la Kiislamu kuzuia kupata kwake vyanzo vya nguvu au kusimamisha Khilafah ndani yake. Jambo ambalo linabainisha kiwango cha chuki kilichobebwa na makafiri wakoloni kuelekea Uislamu na Waislamu, na pia linafichua ukubwa wa jinai inayofanywa na watawala wa Uturuki wakati Uturuki inapokuwa kituo cha ngao ya makombora!
5- Muhtasari ni kwamba Marekani katika mkutano huu imeweza kulazimisha utawala wake juu ya nchi za NATO na kuzishurutisha kwa matakwa yake, hasa Ulaya Magharibi ili kuiweka chini ya ulinzi wake na kuzuia kujitegemea kwake na kuunda nguvu yake huru. Imepunguza upinzani wa Urusi kwa mipango yake, hivyo hakuna nchi miongoni mwa nchi kuu iliyosimama mbele yake na kuiudhi au kuvuruga mambo au kuchanganya karata upya. Hivyo Marekani kupitia mkutano huu itakuwa imeimarisha hali yake ya kimataifa iliyotikisika kufuatia mgogoro wa kifedha na kufuatia kushindwa kwake nchini Iraq na Afghanistan. Hii ni pamoja na kwamba upanuzi wa mamlaka ya muungano na utafiti wa kuifanya Uturuki kuwa mahali pa ngao ya makombora kumefichua hatari ya mkutano huu kwa Uislamu na Waislamu. Ni wajibu kwa Waislamu kuitambua hatari hii na kuikata mizizi yake kwa kufanya kazi kwa bidii na juhudi kubwa kwa ajili ya kusimamisha Khilafah itakayorejesha vitimbi vya makafiri wakoloni kwenye koo zao, na kufanya mipango yao iwe maangamizi yao.
وَلَيَنصُرَنَّ اللَّهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ
"Na bila shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia yule anayeisaidia (dini) Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda." (QS Al-Hajj [22]: 40)