Swali:
Ni yapi vipimo na maana ya muungano wa kijeshi wa Marekani pamoja na Uingereza na Australia? Je, unalenga China? Au ni pigo la Uingereza na Marekani kwa Ufaransa baada ya (Ufaransa) kubomoa ushawishi wa Uingereza nchini Tunisia, na baada ya mapinduzi ya wafuasi wake dhidi ya vibaraka wa Marekani nchini Guinea, na baada ya juhudi za Ufaransa za kujenga jeshi la Ulaya linalojitegemea na Marekani?
Jibu: Ili kuweka wazi jibu la maswali haya, tunapitia mambo yafuatayo:
1- Katika mkutano wa kilele kupitia video, Rais wa Marekani Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Johnson, na Waziri Mkuu wa Australia Morrison walizungumza katika tangazo la pande hizo tatu kuhusu ushirikiano wa kiulinzi. Kwa mujibu wa Sky News Arabia, 16/09/2021, Biden alisema: ("Sote tunatambua umuhimu mkuu wa kuhakikisha amani na uthabiti katika eneo la Indo-Pasifiki kwa muda mrefu," na Morrison akasema: "Tutaendelea kutimiza ahadi zetu zote chini ya mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia." Ama Johnson akauita uamuzi huo kuwa ni wa umuhimu mkubwa akisema: "Utakuwa mmoja wa miradi tata zaidi duniani.") Nchi hizi ziliuweka maandalizi ya muungano wao kuwa siri kisha zikaishitukiza China na Ufaransa...
2- Wakati Ufaransa ikionyesha hasira kubwa na kuishutumu Marekani na Australia kwa kusema uongo, na kuishutumu Uingereza kwa fursa za kila mara (opportunism) na kusema kuwa muungano huu ni pigo la kisu mgongoni kwa sababu ya Australia kufuta mkataba wa nyambizi kubwa uliotiwa saini na Ufaransa tangu mwaka 2016 wenye thamani ya Euro bilioni 56 (Dola za Marekani bilioni 66 - BBC, 18/09/2021), China nayo ilizungumzia kuanza rasmi kwa Vita Baridi katika bara la Asia. Ilitoa wito kwa Marekani na Uingereza kupitia upya muungano huu na mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia, kwa kuzingatia kuwa kuhamisha teknolojia ya nyambizi za nyuklia kwenda Australia, ikiwa ni nchi isiyo na nyuklia, kunaweza kuwa ni ukiukaji wa mkataba huo. Bila shaka, China itauona muungano huu kuwa hatari kwake, hasa kuhusiana na nyambizi za nyuklia za Australia ambazo zinapinga utawala wa China katika bahari za Asia.
3- Ikiwa Ulaya, mshirika wa jadi wa Marekani, ilichangamka mwishoni mwa zama za Trump nchini Marekani, na uchangamfu huu uliongezeka kwa kilio cha Rais wa Marekani kwamba "America has returned" (Marekani imerejea) na kuifanya kuwa kaulimbiu yake mkabala na kaulimbiu ya Trump "America First" (Marekani kwanza), lakini utekelezaji wa serikali ya Biden wa kujiondoa nchini Afghanistan bila kuzingatia maoni na maslahi ya Ulaya ulionyesha utiifu wa nchi hizo kwa Marekani kwa njia ya kuaibisha kwao. Kujiondoa kwa Marekani nchini Afghanistan kulikuwa kitendo kikubwa zaidi cha kimataifa kilichofanywa na serikali ya Biden katika miezi tisa baada ya kuchukua hatamu za urais kufuatia Trump. Matokeo yake kulizuka ukosoaji mkubwa dhidi ya Marekani barani Ulaya, ambapo maarufu zaidi ulikuwa wito wa Ufaransa wa kuunda na kuimarisha jeshi la Ulaya kando na Marekani. Kisha ukaja muungano huu mpya wa Marekani na Australia na Uingereza, ambayo ilijitoa katika Umoja wa Ulaya (EU), jambo ambalo liliongeza matatizo zaidi! Hilo lilimpelekea Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kusema "ni uamuzi wa ghafla kwa mtindo wa Trump," "pigo la kisu mgongoni," na "pigo chungu," kisha Ufaransa ikamrudisha nyumbani balozi wake kutoka Washington kwa mashauriano!
4- Kwa kutazama kwa kina vipimo vya muungano huu mpya wa kijeshi, tunakuta kuwa ni tukio kubwa katika nyanja ya kimataifa na litakuwa na athari pana ambazo zinaweza kutazamwa katika mfumo wa mkakati wa Marekani wa kuzuia kuongezeka kwa ushawishi wa China na katika mfumo wa "kuadhibu" Marekani na Uingereza kwa Ufaransa kwa tabia yake ya kimataifa inayokiuka (maslahi yao) na athari za hilo kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Hili linaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:
Kwa upande wa China:
Haifichiki tena kwa nchi, hasa China, kwamba malengo ya kimkakati ya Marekani yenye kipaumbele leo ni kupambana na kuongezeka kwa ushawishi wa China na kuzuia hatari zake za kiuchumi za kimataifa na za kijeshi za kikanda. Kwa hiyo, China ilielewa malengo ya muungano huu wa kijeshi tangu wakati wa kutangazwa kwake na ikatangaza kuupinga na kuzungumzia juu ya "fikra za Vita Baridi" na "upendeleo wa kiitikadi" na kwamba makubaliano hayo yanakiuka "kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia" (Msemaji wa Ubalozi wa China mjini Washington Liu Pengyu alisisitiza kuwa nchi hizi hazipaswi kuunda kambi za kibaguzi zinazolenga maslahi ya pande nyingine au kuzidhuru na jambo muhimu zaidi ambalo zinapaswa kufanya ni kuachana na fikra za Vita Baridi na upendeleo wa kiitikadi... Al Jazeera Net 16/09/2021). Hivyo basi, China:
a- Bila shaka inatambua kuwa hatua hii ni kama kiini cha muungano mpya dhidi yake unaoundwa kwa mfano wa NATO ulioundwa dhidi ya Umoja wa Kisovieti. Kama Al Jazeera ilivyonukuu kutoka gazeti la Washington Post (kwamba makubaliano haya yatairuhusu Australia kumiliki na kuendesha nyambizi za kisasa zinazotumia nishati ya nyuklia kuchukua nafasi ya meli za zamani zinazotumia dizeli, jambo ambalo litaipa Australia uwezo wa kushambulia ambao China inahitaji kuupigia hesabu iwapo kutatokea mzozo wowote. Al Jazeera 17/09/2021). Hiyo ni kusema kwamba makubaliano haya yataimarisha uwezo wa kijeshi wa Australia ikiwa ni moja ya mnyororo wa mataifa ya Asia yanayopinga China kupitia kuipatia nyambizi za nyuklia na makombora ya Marekani ya Cruise aina ya Tomahawk...
b- China pia inatambua kuwa mkakati wa Marekani wa kupinga ukuaji wa China ni ule ule, haujabadilika kwa kubadilika kwa serikali huko Washington. Kiini chake ni kuimarisha nchi zinazopinga China katika mazingira yake na kupanda hatari zaidi kuzunguka kwayo. Chini ya anuani ya maeneo ya bahari yaliyo wazi na uhuru wa safari za baharini, Marekani inafanya harakati za kijeshi katika bahari zinazozunguka China, iwe ni kupitia kuhamisha vitengo vya kijeshi vya Marekani moja kwa moja au kwa kutoa msaada wa kijeshi wa moja kwa moja na mkubwa kwa washirika wa Marekani huko Asia wanaopinga China kama vile Japan, Korea Kusini, Australia, India na nyinginezo. Wakati Marekani ikitambua kuwa sera zake za kuzuia ukuaji wa China zimechelewa kwa sababu ya vita vyake nchini Iraq na Afghanistan, China nayo inaona kuwa kuchelewa huku kwa Marekani kunaifanya Washington kujaribu kuzuia ukuaji wa China bila vizuizi, na hii ni hatari sana. Wazo la serikali ya Trump la kuipatia Japan na Korea Kusini silaha za nyuklia na ahadi ya serikali ya Biden leo ya kuipatia Australia nyambizi za nyuklia inaongeza hatari ya sera ya Marekani dhidi ya China na kwamba haijafungwa tena na mikataba ya kimataifa.
Ama kwa upande wa nchi tatu washirika katika "AUKUS", kama ilivyonukuliwa na Al Jazeera mnamo 16/09/2021:
a- (Maafisa wakuu katika serikali ya Marekani walisema: "Ushirikiano huu wa kiulinzi unakuja huku kukiwa na ukuaji wa ushawishi wa China katika eneo hili." Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa mpango wa ulinzi wa AUKUS na Uingereza na Australia utaziwezesha nchi hizi kupata uwezo wa kisasa zaidi wa kufanya manuva na kuzuia vitisho vinavyokua haraka...).
b- Na (Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kuwa kuzinduliwa kwa ushirikiano wa kiulinzi wa nchi tatu na Marekani na Australia kunalenga kufanya kazi bega kwa bega ili kudumisha usalama na uthabiti katika eneo la Indo-Pasifiki. Aliongeza kuwa jukumu la kwanza la ushirikiano huu litakuwa ni kuisaidia Australia kupata nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia...).
c- Na Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison alisema (kwamba nchi yake imevunja mkataba mkubwa ilioingia na Ufaransa mwaka 2016, wa kununua nyambizi za kawaida, kwa sababu inapendelea kujenga nyambizi zinazotumia kani ya nyuklia kwa msaada wa Marekani na Uingereza. Morrison aliongeza kuwa nchi yake haitafuti kumiliki silaha za nyuklia, na itaendelea na ahadi zake za kutoeneza silaha za nyuklia...).
Ama kwa upande wa Ufaransa, kulikuwa na hisia kali za hasira kwani ilishtushwa na kile kilichotokea:
a- (Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alielezea kuvunja kwa Australia mkataba wa kununua nyambizi na nchi yake kama pigo la kisu mgongoni. Aliongeza katika tamko lake kwa redio ya France Info kuwa Ufaransa inahisi kusalitiwa, hasira na uchungu kwa sababu ya Australia kufuta mpango huo, na kuingia ushirikiano na Marekani na Uingereza, ambapo itapata nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia... Al Jazeera 16/09/2021). Pia alisema katika taarifa yake (Kwa ombi la Rais wa Jamhuri, nimeamua kuwaita mara moja mjini Paris kwa mashauriano mabalozi wetu nchini Marekani na Australia. Uamuzi huu wa kipekee unahalalishwa na uzito wa kipekee wa kile kilichotangazwa na Australia na Marekani mnamo Septemba 15. Euro News Arabic, 17/09/2021). Le Drian aliiambia redio ya France Info: "Nina hasira... ni jambo ambalo haliwezi kufanywa kati ya washirika... ni kofi usoni." Deutsche Welle ya Ujerumani, 17/09/2021). Na kabla ya uamuzi wa kuwaita mabalozi: (Mamlaka ya Ufaransa ilifuta hafla iliyopangwa kufanyika jana Ijumaa mjini Washington kuadhimisha kumbukumbu ya mapigano ya baharini yaliyokuwa na maamuzi wakati wa Mapinduzi ya Marekani, ambapo Ufaransa ilichukua jukumu kuu. Al Jazeera Net, 18/09/2021).
b- Waziri wa Majeshi wa Ufaransa Florence Parly aliona (kwamba kuvunjwa kwa Australia kwa mkataba mkubwa wa kununua nyambizi za kawaida kutoka nchi yake ni jambo zito na litakuwa habari mbaya sana... Al Jazeera 16/09/2021).
5- Ama ni kwa nini nchi hizi tatu zikiongozwa na Marekani zilichukua hatua hizi mbali na Ufaransa, bali kwa kile kinachofanana na adhabu kwa Ufaransa, kinachozingatiwa ni yafuatayo:
a- Ufaransa ilikuwa ikikosoa waziwazi na kupinga sera za serikali ya Trump, na hilo lilionekana katika mgogoro wa Mashariki mwa Bahari ya Mediterania kati ya Uturuki na Ugiriki. Wakati serikali ya Biden ilipokuja na kujiondoa nchini Afghanistan kwa njia ile iliyoonyesha kiwango cha utegemezi wa nchi za Ulaya kwa Marekani—nchi ambazo zinataka kuonekana kama washirika na sio wafuasi—Ufaransa ilirejea ndani ya Umoja wa Ulaya ikishinikiza kuundwa kwa jeshi la Ulaya lililotengwa na mwavuli wa Marekani NATO, yaani, ilirejea kupinga uongozi wa kijeshi wa Marekani kwa nchi za Ulaya. Na ujasiri wake uliongezeka dhidi ya ushawishi wa Marekani barani Afrika, jambo ambalo lilionekana baadaye katika mapinduzi ya Guinea na kabla yake katika harakati za kijeshi za Ufaransa katika nchi za Sahel barani Afrika. Haya yote yamejenga chuki ya Marekani dhidi ya Ufaransa.
b- Baada ya mazungumzo ya Brexit ya Uingereza na nchi za Umoja wa Ulaya, ilidhihirika kuwa uhusiano wa Uingereza na Ufaransa ulikuwa umeharibika sana, na hakuna nchi iliyoonyesha dalili za kupungua kwa mvutano. Hilo lilionekana katika msimamo mkali wa Ufaransa na Ulaya katika masharti na makubaliano ya kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja huo. Pengine Ufaransa na nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa zinataka kuzizuia nchi nyingine za Umoja huo kufuata nyayo za Uingereza na kujitoa, jambo ambalo lingesababisha kusambaratika kwa Umoja huo, lakini hilo liliacha uharibifu usio na kifani katika uhusiano wa Ufaransa na Uingereza, na sera zao za kimataifa zilitengana kwa kiasi kikubwa. Wakati Ufaransa ilipoweza kuchukua mamlaka nchini Tunisia kupitia hatua za hivi karibuni za Kais Saied, mbali na kutozingatia maslahi yoyote ya Uingereza, ilianza kuitumia Marekani dhidi ya Uingereza nchini Tunisia, jambo ambalo halikuwa la kawaida katika sera za nchi hizo mbili.
c- Kabla ya hapo, mwanzoni mwa Mei 2021, kulikuwa na mgogoro wa kisiwa cha Jersey, ambacho ni kisiwa kilicho chini ya taji la Uingereza na kipo takriban kilomita 20 kutoka pwani ya Ufaransa, ambapo Uingereza ilituma meli za kivita kuwazuia wavuvi wa Kifaransa kuingia katika maeneo ya uvuvi ya Uingereza baada ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Ufaransa ilitishia kukata umeme katika kisiwa hicho na kutuma boti za polisi na walinzi kulinda wavuvi wa Kifaransa kama jibu kwa hatua za Uingereza. Haya yote yalikuwa ni dalili ya kuongezeka kwa uharibifu wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, jambo ambalo kwa yakini linaisukuma Uingereza kutoa mapigo kwa Ufaransa na kuichochea Marekani dhidi yake. Lakini kwa kawaida ya Uingereza na hila zake, haya yote hufanyika kwa siri... Kwa mujibu wa gazeti la New York Times la Marekani, serikali ya Uingereza (ilicheza jukumu la mapema ili kuunda muungano wa nchi tatu na Marekani na Australia kupeleka nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia katika Bahari ya Pasifiki, kwa mujibu wa maafisa mjini London na Washington. Al Arabiya Net, 19/09/2021).
d- Lakini hatari zaidi kuliko hili na lile, na hasa kwa upande wa Marekani, ni msimamo wa Ufaransa wa kuridhiana na China ambao unapingana na msimamo wa Marekani. (Paris ina wasiwasi mkubwa juu ya washirika wake wa jadi kufuata mkakati wa makabiliano na China ambao kwa hakika utahatarisha maslahi ya Ufaransa katika eneo hilo; kwani utelezi wowote wa kijeshi wa mkakati wa muungano wa nchi tatu katika bahari za Indo-Pasifiki unaweza kusababisha tishio kwa usalama wa raia milioni moja wa Ufaransa katika New Caledonia na French Polynesia, maeneo mawili muhimu ya Ufaransa yanayojulikana kama maeneo ya ng'ambo...) Hivyo, inatarajiwa kuwa Ufaransa itaelekea (kujenga dira ya mkakati wa Ulaya inayojitegemea wakati itakapopokea uenyekiti wa Umoja wa Ulaya mwanzoni mwa mwaka ujao na kuendeleza juhudi zake za kuitoa Ulaya kutoka katika mwavuli wa ulinzi wa Marekani na kuimarisha nafasi ya Umoja wa Ulaya katika nyanja ya kimataifa ili uwe nguvu ya ulimwengu... Al Jazeera 22/09/2021).
6- Hivi ndivyo vipimo na maana ya muungano huu mpya ambao Marekani ikishirikiana na Uingereza ilifanya kazi kuujenga pamoja na Australia ili uwe moja ya mnyororo wa kuizingira China kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kutoa pigo kali kwa Ufaransa kwa kufuta mkataba wake wa nyambizi na Australia na kutoishirikisha katika muungano huu. Muungano huu unasukuma mambo katika bahari zinazozunguka China kuelekea katika harakati zaidi za kijeshi na migogoro na unathibitisha hatari kubwa ambayo Washington inaiona katika umuhimu wa kuzuia ukuaji wa China. Ama Ufaransa yenye sera za kukurupuka, ni dhaifu mno kuweza kuzuia makonde ya Marekani na Uingereza usoni mwake, bali nchi zote za Umoja wa Ulaya zinakabiliwa na udhaifu mkubwa. Kiwango cha jeshi la Ulaya ambalo Ufaransa ilipiga kelele kuliunda kama jeshi la Ulaya linalojitegemea na NATO kilikuwa kidogo sana (askari elfu tano) ili kuonyesha udogo wa uwezo wa kimataifa wa Ulaya, hasa baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
7- Na hivyo ndivyo... hakuna maadili thabiti kwa nchi hizi zinazoitwa kubwa leo:
بَأْسُهُمْ بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعاً وَقُلُوبُهُمْ شَتَّى ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْقِلُونَ
"Uhasama wao baina yao ni mkali. Unawadhania kuwa wako pamoja, lakini nyoyo zao ni mbalimbali. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili." (QS. Al-Hashr [59]: 14)
Ni nchi zinazoliwa na wadudu kutoka ndani na katika uhusiano baina yao. Labda ni habari njema na sunna miongoni mwa sunna za Mwenyezi Mungu ili kurahisisha kudhihirisha Dini Yake. Hivyo ndivyo zilivyokuwa dola mbili za Uajemi (Persia) na Roma wakati wa kusimamishwa kwa Dola ya Kiislamu ya kwanza, na hivyo ndivyo uhusiano kati yao ulivyokuwa, uhusiano wa kupigana na uhasama wa dhahiri:
وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِقَوْمٍ سُوءاً فَلَا مَدَّ لَهُ وَمَا لَهُمْ مِنْ دُونِهِ مِنْ وَالٍ
"Na Mwenyezi Mungu anapoitakia adhabu kaumu yoyote, basi hakuna wa kuizuia, wala hawana mlinzi yeyote badala yake." (QS. Ar-Ra'd [13]: 11)
18 Safar 1443 H 25/09/2021 M