Home About Articles Ask the Sheikh
Uchambuzi

Jibu la Swali: Ujerumani na Mkakati wa Usalama wa Taifa

June 24, 2023
1942

Jibu la Swali

Swali:

Mnamo tarehe 14/06/2023, serikali ya Ujerumani iliidhinisha, kwa mara ya kwanza tangu mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mkakati wa kitaifa wa usalama wa taifa baada ya mazungumzo yaliyochukua zaidi ya mwaka mmoja kati ya taasisi mbalimbali za Ujerumani. Je, mkakati huu unawakilisha mwisho wa vikwazo vilivyowekwa kwa Ujerumani tangu kushindwa kwake katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia mnamo mwaka 1945? Na nini kinachotarajiwa kutoka kwa Ujerumani baada ya kupitisha mkakati huu katika siasa za Ulaya na kimataifa?

Jibu:

Ujerumani, ikiwa ni nchi iliyoshindwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, iligawanywa katika sehemu nne zilizodhibitiwa na mataifa makubwa yaliyoshinda vita (Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, na Ufaransa). Baadaye, mataifa matatu ya Magharibi yalianzisha Ujerumani Magharibi na Urusi ikaanzisha Ujerumani Mashariki. Kiutendaji, Ujerumani Magharibi ilikuwa ikifuata Marekani kama nchi mfuasi, na hali kadhalika Ujerumani Mashariki kwa Umoja wa Kisovieti (Urusi). Ujerumani Mashariki iliwakilisha kituo cha kijeshi cha mbele kwa Umoja wa Kisovieti kuelekea Magharibi, na vivyo hivyo Ujerumani Magharibi kwa Marekani, ikiwa kiongozi wa kambi ya Magharibi kuelekea Mashariki. Hii ilikuwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia... lakini ukweli huu ulibadilika hatua kwa hatua baada ya hapo:

1- Isipokuwa kwa baadhi ya mambo ya kisherehe, hakuna nchi yoyote kati ya nchi hizo mbili za Ujerumani iliyokuwa na siasa huru mbali na kiongozi wa kambi yake. Hali hii iliendelea hadi Umoja wa Kisovieti ulipodhoofika na kukubali kuunganishwa kwa Ujerumani mnamo mwaka 1990. Hii ina maana kuwa Moscow iliachana na Ujerumani Mashariki kwa faida ya Magharibi. Pamoja na kutiwa saini kwa mkataba wa Maastricht wa umoja wa Ulaya mwaka 1992 licha ya upinzani wa Marekani, na kujikunyata kwa Urusi katika matatizo yake ya ndani baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, Ujerumani ilianza kujitokeza kama nguvu muhimu zaidi ya kiuchumi barani Ulaya. Wajerumani waliona kuwa mazingira ya kimataifa yamebadilika na kwamba kuna fursa ya kuimarisha upande wa kiuchumi kama nguzo ya kwanza ya uhuru wa Ujerumani. Hivyo, Ujerumani ilijitokeza kama nguvu ya kiuchumi inayoshindana na nguvu nyingine za Ulaya bila kuamsha chuki yoyote kwa mataifa mengine ya Ulaya; Uingereza na Ufaransa, au ya kimataifa; kama Urusi na Marekani, hususan kwa vile sera ya ulinzi ya Ujerumani ilikuwa ikizingatia kiwango cha chini kabisa cha kijeshi.

2- Kupitia mafanikio yake ya kiviwanda na kiuchumi na kupanua mahusiano yake ya kibiashara na Urusi, Ujerumani ilifanikiwa kuongoza nchi za Ulaya kiuchumi. Uongozi huu wa Ujerumani uliwekwa na ukweli wa mambo, kama ilivyokuwa katika mgogoro wa Ugiriki mwaka 2010. Kwa ujumla, suala kubwa la kiuchumi haliwezi kuhitimishwa barani Ulaya au katika mahusiano ya nje bila Ujerumani. Ingawa jambo hili halikuwa chanya kwa Ufaransa hususan, lakini udhaifu wa kijeshi wa Ujerumani uliipa Ufaransa hisia ya mara kwa mara kuwa ushindani kati ya nchi hizo mbili bado uko katika mfumo wa amani. Katika vipindi hivyo, Ujerumani ilikuwa ikitoa maoni yake kuhusu changamoto za kiusalama kupitia "Karatasi Nyeupe" (White Papers) zilizokuwa zikitolewa na wizara yake ya ulinzi, ambapo ya kwanza ilikuwa mwaka 1969 na ya mwisho mwaka 2016. Ilikuwa ikizungumzia usalama, ugaidi, na hamu ya kushiriki lakini kupitia Umoja wa Mataifa. Wakati Urusi ilipoitenga rasi ya Crimea kutoka Ukraine na kuimeza mwaka 2014, Ujerumani ilipinga hilo kwa nguvu na kushiriki katika vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi. Lakini maslahi yake ya kibiashara yanayokua na Urusi yaliizuia kuongoza hatua yoyote dhidi ya Urusi. Licha ya mazungumzo kuwa Urusi ilikuwa ikibomoa usawa wa usalama wa Ulaya kupitia kumeza Crimea, kuhusika kwa Ujerumani katika mikataba ya Minsk kuliwapa Wajerumani matumaini ya kusitisha hatari za Urusi kwenye mipaka ya Crimea na Donbas, ambapo Urusi iliwasha moto wa vita mwaka huo na kuwaunga mkono waasi wa Kirusi dhidi ya serikali ya Ukraine.

3- Lakini kwa Urusi kuivamia Ukraine mwaka 2022 na kusadiki kwa Marekani kuwa Urusi inabomoa misingi ya usalama wa kimataifa iliyojengwa na Marekani, mazingira ya Ulaya na kimataifa yalikutana ili kuipa Ujerumani fursa ya dhahabu ya kujenga nguzo nyingine ya kijeshi itakayoongezwa kwenye nguzo yake ya kiuchumi ambayo tayari ni imara. Hii ni kwa sababu Marekani inataka mataifa ya Ulaya yaichukue nafasi yake katika kusimama dhidi ya Urusi ili Marekani ibaki tayari kuzuia kupanda kwa Uchina. Kutokana na hapa, Ujerumani iliona kuwa uwanja wa kimataifa umekuwa wazi kwa Ujerumani kujitokeza kama nchi kubwa kijeshi. Pamoja na kukatwa kwa mahusiano yake ya kibiashara na Urusi, Ujerumani ilitangaza kuanzishwa kwa mfuko mkubwa wa fedha wenye thamani ya euro bilioni 100 kwa ajili ya kuunga mkono jeshi lake na kuliboresha ili liweze kulinda usalama wake. Ilitangaza kuwa vita vya Ukraine vinawakilisha hatua kubwa ya mabadiliko, na hata ilituma ndege zake za kivita mbali hadi kwenye Bahari ya Pasifiki ikiwa ni ishara tosha kuwa nguvu ya kijeshi ya Ujerumani imeanza kujinasua kutoka kwa vikwazo vya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hivyo, hisia za ukuu zimechochewa ndani ya watu wa Ujerumani, na Ujerumani imezungumzia majukumu yake maalum kuelekea Ukraine na hata kuelekea Ulaya Mashariki. Kumekuwa na mazungumzo mengi nchini Ujerumani kuhusu ulazima wa utayari wa kukabiliana na tamaa za kibeberu za Urusi ambazo hazitaishia kwenye mipaka ya Ukraine.

4- Serikali ya Kansela Scholz ilijitahidi wakati wa kuwasilisha Mkakati wa Usalama wa Taifa mnamo 14/06/2023 kuonyesha maelewano ya Wajerumani juu ya mkakati huu. Wawakilishi wa vyama vya Ujerumani katika muungano wa serikali walikuwepo pamoja na Kansela wakati wa kuuwasilisha, ambao ni mawaziri wa chama cha Greens na chama cha FDP, pamoja na chama cha Kansela Scholz (SPD). Hii inaashiria uzito wa mabadiliko haya ndani ya Ujerumani na athari zake katika kuihamisha Ujerumani kutoka nafasi ya kijeshi na kiusalama iliyodumu kwa miongo kadhaa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwenda nafasi mpya, ingawa vyama vya upinzani vimeishutumu serikali kwa kukosekana kwa uwazi katika baadhi ya vipengele vya mkakati huu.

5- Labda kauli ya Kansela wa Ujerumani Scholz inaelezea mabadiliko haya ya kimaendeleo na mapya kwa sera ya Ujerumani:

"Kansela wa Ujerumani alisisitiza kuwa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama ulioidhinishwa na serikali ya Ujerumani leo unachukuliwa kuwa mchango muhimu wa kuhakikisha usalama wa watu nchini Ujerumani kufuatia mazingira yanayobadilika. Mwanasiasa huyo wa SPD alisema kuwa baraza la mawaziri la Ujerumani kwa kuidhinisha mkakati huu limechukua uamuzi usio wa kawaida na muhimu. Scholz alieleza kuwa mazingira ya kisiasa ya kiusalama ya Ujerumani yamebadilika sana kutokana na shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine na kujitokeza kwa uchokozi unaoongezeka wa serikali ya Uchina. Scholz alitaja kuwa kazi kuu ya dola ni kufanya kazi ya kuhakikisha usalama wa raia bila maelewano yoyote, akibainisha kuwa kazi hii itafanywa kupitia mkakati wa usalama unaofuata kanuni elekezi ya usalama jumuishi. Aliongeza kuwa kile kilichokuwa kimezuiliwa katika mipango ya serikali ya Ujerumani huko nyuma kwenye sera ya ulinzi pekee, sasa kitafuata mkabala wa jumla na mpana." (Deutsche Welle ya Ujerumani, 14/06/2023).

6- Waraka wa mkakati wa usalama wa taifa wa Ujerumani unawakilisha misingi inayoelekeza serikali ya Ujerumani kulinda usalama wa watu wake. Moja ya misingi muhimu iliyokuwa ikifuatwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambayo imeondolewa katika waraka huu ni kwamba jeshi la Ujerumani linatekeleza majukumu ya kujihami pekee ili kukabiliana na vitisho vya usalama; sasa limehamia kutekeleza hatua za kina, kumaanisha kwamba zinajumuisha mashambulizi. Huu ni maendeleo makubwa na hatari barani Ulaya. Waraka huo unahimiza uboreshaji wa kina na wa haraka wa jeshi la Ujerumani. Pamoja na kusisitiza kujitolea kwa uamuzi wa muungano wa NATO wa mwaka 2014 wa kutumia angalau 2% ya pato la taifa kwa ajili ya jeshi na usalama, Ujerumani inazitayarisha wizara nyingine kupunguza bajeti zao kwa faida ya jeshi. Huu pia ni mabadiliko makubwa katika kupunguza mtazamo wa ustawi wa Ujerumani. Waziri wa Fedha Christian Lindner alisema: "Kwa miongo mingi Ujerumani 'imeishi kwa faida za amani'. Hii ina maana kwamba kulikuwa na imani kwamba hakuna haja ya kujali sana suala la ulinzi. Waziri huyo wa fedha aliongeza mjini Berlin wakati wa kuwasilisha mkakati huo: 'Hii ina maana kwamba mafungu katika bajeti yatabadilika kwa namna endelevu'." (Deutsche Welle ya Ujerumani, 16/06/2023).

7- Waraka huo pia unawakilisha mtazamo wa serikali ya Ujerumani katika uchambuzi wa hatari. Katika kilele cha hatari za nje ni jeshi la Urusi, au kile walichokiita shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine. Baada ya hapo, kwa kiwango cha chini kidogo, ni kusimama dhidi ya kupanda kwa Uchina na mfumo wake ambao wanauita Magharibi kuwa ni wa kidikteta, kama ilivyoelezwa katika taarifa za Scholz ("kujitokeza kwa uchokozi unaoongezeka wa serikali ya Uchina"). Waraka huo haupuuzi hatari za ndani kama vile usalama wa mtandao, hatari ya kutishia miundombinu ya Ujerumani, na mabadiliko ya hali ya hewa, ingawa masuala haya yana uhusiano wa moja kwa moja na tishio kutoka nje ambapo Urusi inashutumiwa kwa kutekeleza mashambulizi ya mtandao katika nchi za Magharibi, pamoja na uratibu wa kimataifa wa kupunguza hatari za mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ina maana kwamba mkakati huu wa Ujerumani wa usalama wa taifa unawakilisha uhamaji wa Ujerumani kutoka hali moja kwenda hali nyingine katika sera yake ya nje, ingawa baadhi ya shaka na dhana bado vinatawala akili za kisiasa nchini Ujerumani.

8- Kwa kuimarisha jeshi lake na kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuliboresha na kufungua njia mbele ya operesheni za kijeshi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na zile za kishambulizi, Ujerumani itakuwa imeondokana na kizuizi cha kijeshi kilichowekwa kwake katika kile kinachojulikana kama vikwazo vya baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hiyo ina maana kwamba kizuizi hicho kimekuwa ni jambo la kale. Hili linaamsha hitilafu kubwa na za msingi kati yake na Ufaransa, hitilafu ambazo zinaonekana wazi leo, ingawa Ujerumani ambayo ilitia saini mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia bado imejitolea katika hali yake ya kutokuwa na nyuklia, jambo ambalo ililithibitisha mwaka 1990 katika "Mkataba wa Makubaliano ya Mwisho Kuhusu Ujerumani" uliotiwa saini na mataifa makubwa manne wakati wa kuunganishwa kwake mwaka huo huo. Ili kuelewa uzito wa mabadiliko haya nchini Ujerumani, kuimarisha jeshi la Ujerumani kunahitaji kuongeza idadi yake, na hili linapingana na majukumu ya Ujerumani katika "Mkataba wa Makubaliano ya Mwisho Kuhusu Ujerumani" uliotiwa saini na mataifa makubwa mwaka 1990, mkataba ambao uliweka ukomo wa jeshi la Ujerumani kuwa na askari wasiozidi 370,000. Lakini kusukuma kwa Marekani na Uingereza kwa Ujerumani ili icheze nafasi mpya katika kukabiliana na Urusi kutairahisishia Ujerumani kujiondoa kwenye makubaliano haya. Hili litawakilisha kujinasua kwa Ujerumani kutoka kwa vikwazo vyovyote vya Kirusi juu ya nguvu yake ya kijeshi. Ama Ufaransa, msimamo wake unaonekana kuwa dhaifu mbele ya mielekeo ya Marekani na Uingereza ya kuimarisha Ujerumani; bali hitilafu inayoongezeka kati ya Ujerumani na Ufaransa inaweza kufanya kazi ya kudhoofisha Umoja wa Ulaya mzima, jambo ambalo linakaribishwa na Marekani na Uingereza.

9- Ili kupunguza hofu za Ufaransa hususan kutokana na kuongezeka kwa nguvu za kijeshi za Ujerumani, mkakati wa Ujerumani unazungumzia Ujerumani kama sehemu ya Umoja wa Ulaya: "Serikali imebainisha katika mkakati huo seti ya malengo, kama vile ulazima wa kuimarisha ulinzi wa kiteknolojia katika ngazi ya Ulaya, na kuimarisha ukabilianaji na ujasusi, hujuma, na mashambulizi ya mtandao. Pamoja na ulazima wa kuratibu udhibiti wa mauzo ya silaha katika ngazi ya Umoja wa Ulaya." (Deutsche Welle, 16/06/2023). Lakini hili kutoka upande mwingine linaibua hofu za aina nyingine mjini Paris ambayo inaona kuwa mikakati ya Ulaya imeanza kutolewa Berlin. Ujerumani pia inaongoza mradi wa Ulaya wa ulinzi wa anga: "Mkakati mpya unaashiria Ujerumani kama nchi kubwa zaidi barani Ulaya kwa upande wa idadi ya watu na nguvu ya kiuchumi, na hivyo kile kinachohitajika kutoka kwake ili kuimarisha mfumo wa ulinzi wa Ulaya na muungano wa NATO. Inadokeza hamu ya Ujerumani ya kucheza nafasi ya uongozi hapa, hususan kwa vile inatafuta kujenga ngao ya makombora ya Ulaya 'Sky Shield'. Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius alitangaza kuwa nchi 18 zimeonyesha ridhaa yao ya awali ya kushiriki katika mpango huu." (Asharq News, 17/06/2023).

10- Kuhusiana na mtazamo kuelekea Uchina na Urusi kama mifumo ya kidikteta, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Baerbock anasema katika kuelezea mkakati wa usalama wa taifa: "Mkakati huo unategemea 'vipimo vitatu vya msingi' vya sera ya usalama ambavyo ni: Ulinzi, Ustahimilivu, na Udumifu. Eneo la ulinzi linajumuisha kuimarisha jeshi, ulinzi wa raia, na ulinzi wa wananchi. Katika eneo la ustahimilivu, yaani uwezo wa kuhimili, inahusu ulinzi wa 'mfumo wetu wa msingi wa kidemokrasia ulio huru dhidi ya ushawishi haramu wa nje'. Aidha, inapaswa kupunguza 'athari za upande mmoja katika nyanja ya malighafi na usambazaji wa nishati' na kubadilisha vyanzo vya usambazaji." (Deutsche Welle, 16/06/2023). Katika hili kuna ufuasi mkubwa wa Ujerumani nyuma ya sera ya Marekani ya kuzuia minyororo ya usambazaji ya Kichina baada ya Marekani kuilazimisha Ujerumani na Ulaya yote kukata minyororo mingi ya usambazaji wa nishati kutoka Urusi. Jambo hili liko wazi bila shaka katika taarifa za Ujerumani; kwa mujibu wa Kansela Scholz kwa mujibu wa chanzo hicho hicho hapo juu: "Kwetu sisi, ushirikiano na Umoja wa Ulaya na muungano wa kuvuka Atlantiki unabaki kuwa jambo la msingi."

11- Hivyo, vipimo vya mkakati huu wa Ujerumani wa usalama wa taifa vinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

a- Mkakati huu umeweka mwisho kwa kizuizi cha kijeshi cha Ujerumani kilichowekwa kwake tangu mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ujerumani inapiga hatua thabiti kuelekea kuimarisha jeshi lake na kulifanya kuwa mdhamini wa usalama wake, lakini Ujerumani inavunja vikwazo kwa kadiri mazingira ya kimataifa yanavyoruhusu; inabaki kuwa nchi iliyotia saini mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia.

b- Sambamba na mazingira ya kimataifa ya Magharibi, Ujerumani inabainisha maadui zake kulingana na hilo kuwa ni jeshi la Urusi katika daraja la kwanza, na katika daraja la pili ni Uchina ambayo mkakati wa Ujerumani unazungumzia kuwa ni mshirika wa kibiashara na nchi yenye mtazamo wa uchokozi unaoongezeka kuelekea mazingira yake, lakini haufuti ushirikiano nayo katika kutatua matatizo ya kimataifa. Msimamo wake kuhusu hilo unafanana kabisa na msimamo uliotangazwa wa kundi la nchi saba (G7).

c- Ujerumani inabainisha changamoto za kiusalama na kijeshi zinazoizunguka ikiwa ni nchi mwanachama katika Umoja wa Ulaya na mwanachama katika muungano wa NATO. Mkakati wa Ujerumani unasisitiza kujitolea kwa Ujerumani kufanya kazi kupitia taasisi hizi za Ulaya na kimataifa.

d- Ikiwa mkakati huu unasisitiza kuwa Ujerumani ni sehemu ya Ulaya na sehemu ya nchi za NATO na unazungumzia usalama wake kama sehemu ya usalama wa pamoja wa mfumo wa Ulaya na mfumo wa Atlantiki na unasisitiza kuwa inatetea mfumo wa kimataifa unaodhibitiwa na Marekani, hata hivyo yote hayo hayapunguzi uzito wa hatari ya mkakati huu wa Ujerumani. Vile vile haipunguzi ukweli kwamba mkakati huu wa Ujerumani unawakilisha moja ya hasara kubwa za kimataifa kwa Moscow kama ilivyo kujiunga kwa Sweden na Finland katika muungano wa NATO.

e- Ikiwa Ujerumani imetumia miongo mitatu iliyopita nafasi yake ndani ya Umoja wa Ulaya kuonyesha uongozi wake katika masuala ya kiuchumi, hiyo ilikuwa hatua yake ya kwanza kuelekea ukuu. Na sasa inatumia vita vya Ukraine na mazingira ya kimataifa yanayoizunguka kujenga jeshi lenye nguvu na msingi wa kijeshi wa kiviwanda ili iwe hatua yake ya pili kuelekea ukuu. Baada ya hapo inaweza kujinasua kutoka kwa vikwazo vilivyobaki na kujenga mkakati wa Ujerumani uliojitenga na nchi za Ulaya na kujitenga na Marekani. Ingawa hili halitarajiwi katika muda wa karibu, lakini matukio yanaashiria mwenendo wa Ujerumani katika njia hii.

12- Katika kuhitimisha, mataifa makubwa katika ulimwengu wa leo yanashindana kati yao katika kumwaga damu kwa dhuluma na uadui, kueneza ufisadi katika ardhi, na kuangamiza mimea na vizazi. Hali ya watu haitatengemaa isipokuwa ardhi itakapong'ara tena kwa nuru ya Khilafah ili kurejesha amani na usalama si kwa Waislamu pekee, bali kwa kila anayefikiwa na kivuli chake. Na hapo ndipo kauli ya haki itasikika katika kila pembe ya dunia:

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقاً

"Na sema: Kweli imefika, na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka." (QS. Al-Isra [17]: 81)

وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيباً

"Na watasema: Lini hayo? Sema: Huenda yakawa karibu." (QS. Al-Isra [17]: 51)

5 Dhu al-Hijjah 1444 H 23/06/2023 M

Share Article

Share this article with your network