Home About Articles Ask the Sheikh
Uchambuzi

Jibu la Swali: Matukio ya Kosovo na Athari Zake kwa Ulaya

June 11, 2023
2197

Jibu la Swali

Matukio ya Kosovo na Athari Zake kwa Ulaya

Swali: Maandamano makali yamezuka kaskazini mwa eneo la Kosovo yakiongozwa na Waserbia wa eneo hilo dhidi ya polisi na vikosi vya NATO. Serbia imeweka vikosi vyake katika hali ya utayari mkubwa kwa uwezekano wa kuingia katika eneo hilo kuwalinda wachache wa Kiserbia. Ripoti iliyochapishwa na tovuti ya National Interest na kunukuliwa na Al Jazeera ilionya kuwa vita ijayo ya Ulaya inaweza kuanzia Kosovo. Ripoti hiyo ilitaja kuwa (kuna kufanana kuliko wazi kati ya hali ya Kosovo na mzozo wa sasa nchini Ukraine, ikiwataka watunga sera wa Magharibi kuzingatia jambo hili. Ilisema kuwa mzozo wa hivi karibuni kaskazini mwa Kosovo uliukumbusha ulimwengu kuwa "vita vya kinyama nchini Ukraine huenda ndio tishio kubwa zaidi kwa utulivu wa Ulaya kwa sasa, lakini si tishio pekee kwa vyovyote vile"... Chanzo: Al Jazeera + National Interest 10/06/2023).

Ni nini kiko nyuma ya matukio haya? Na je, ni hatari kama inavyosikika kutoka kwa matamshi ya maafisa wa kimataifa kuwa yanaweza kulipua eneo la Balkani na kuzishughulisha nchi za Ulaya na vita vya pili mbali na vita vya Ukraine?

Jibu: Ili kufafanua mwelekeo wa mivutano inayotokea leo katika eneo la kaskazini mwa Kosovo, tunapitia mambo yafuatayo:

Kwanza: Mandhari ya Kihistoria:

  1. Baada ya ufunguzi wa Kiislamu wa nchi za Kiothmani (Ottoman) katika eneo la Balkani wakati wa karne ya kumi na tano Miladi, Uislamu ulianza kupenya katika eneo ambalo Dola ya Kirumi ilikuwa imelifanya kuwa eneo la Kikristo tupu. Waalbania walisilimu, nao ndio watu wa Albania ya leo na eneo la Kosovo. Kisha Wabosnia walisilimu baada ya hapo, nao ndio watu wa Bosnia na Herzegovina, ambayo ilijitenga na Yugoslavia mnamo mwaka 1992, na kufuatiwa na vita vya mauaji ya kimbari ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa.

  2. Kosovo ilibaki kuwa sehemu ya Dola ya Kiothmani hadi ilipotoka mnamo mwaka 1912 katika mfumo wa harakati za kitaifa za kujitenga zilizochochewa na Uingereza katika eneo lote la Balkani. Kisha falme nyingi ziling’ang’ania kuitawala Kosovo kama vile Serbia, Montenegro, na ukoloni wa Italia ambao uliiunganisha katika ushawishi wake ndani ya ufalme wa Albania uliokuwa ukiutawala. Kisha mwaka 1946, Rais wa Yugoslavia, Tito, aliiunganisha na nchi yake katika mfumo wa makubaliano ya baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kuipa mamlaka ya ndani (autonomy). Ilibaki ndani ya Yugoslavia hadi hii ya mwisho iliposambaratika mwanzoni mwa miaka ya tisini, na Kosovo ikajipata ikiwa na Serbia, yaani, ikiwa sehemu ya mwisho iliyobaki ya Yugoslavia. Ili isiweze kujitawala, Rais wa Serbia mwenye sifa mbaya, Slobodan Milosevic, aliitawala kwa mkono wa chuma na kufuta hali yake ya mamlaka ya ndani. Machafuko mengi yalizuka baada ya kura ya maoni ya uhuru wake mwaka 1990, na machafuko, ghasia, na mauaji yaliendelea hadi mwaka 1999. Kutokana na mazingira ya kimataifa, muungano wa NATO uliingilia kati na kuanza kuipiga Serbia kwa mabomu hadi ukaishinikiza kuondoka katika eneo la Kosovo. Tangu tarehe hiyo, vikosi vya NATO nchini Kosovo ndivyo nguvu ya kijeshi inayohakikisha amani katika eneo hilo.

  3. Mnamo mwaka 2008, Kosovo ilitangaza rasmi uhuru wake kutoka kwa Serbia na ikatambuliwa na nchi nyingi duniani, ikiongozwa na Amerika na nchi nyingi za Ulaya. Urusi na Serbia zilipinga vikali uhuru huo, na upinzani wa Urusi pamoja na Uchina uliizuia Kosovo kujiunga na mashirika mengi ya kimataifa. Kisha hatimaye tarehe 19/03/2023, katika mfumo wa vishawishi vya kujiunga na Umoja wa Ulaya na kuikabili Urusi baada ya vita vyake dhidi ya Ukraine, Umoja wa Ulaya ulitangaza makubaliano kati ya Serbia na Kosovo ya kurekebisha mahusiano kati yao bila ya kumaanisha kuwa Serbia inatambua uhuru wa Kosovo. Makubaliano haya yalimaanisha kufungua mlango kwa Serbia na Kosovo kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Pili: Mazingira ya ndani na kimataifa yaliyotangulia matukio ya sasa:

  1. Serbia inachukuliwa kuwa ngome ya mwisho ya ushawishi wa Urusi katika Ulaya Mashariki. Urusi imeisaidia katika miaka yote ya mzozo wake na NATO. Hata kuingilia kati kwa NATO mwaka 1999 ili kuikata Kosovo kutoka kwa Serbia kulikuwa pigo kubwa kwa ushawishi wa mwisho wa Urusi katika Balkani, kwani kulionyesha udhaifu wake na kutoweza kuwasaidia wafuasi wake. Lakini Urusi iliendelea kuonyesha uungaji mkono mkubwa kwa Serbia, kuipatia silaha na uungaji mkono wa kisiasa katika mashirika ya kimataifa, na kutangaza upinzani mkali dhidi ya uhuru wa Kosovo. Pia ilitangaza kuanzisha miradi ya kiuchumi kusaidia Waserbia katika Bosnia na Herzegovina, na kuimarisha uhusiano kati ya makanisa ya nchi hizo mbili. Aidha, ilianzisha kituo kikubwa cha habari cha shirika la Sputnik huko Belgrade ambacho kimekuwa kituo cha kuchochea mvutano na kuonyesha uungaji mkono wa Urusi kwa Waserbia. Viongozi wa Serbia wanajitahidi kupigwa picha na Rais wa Urusi Putin ili kupata umaarufu nchini Serbia kabla ya uchaguzi. Kwa ujumla, Urusi ina ushawishi mkubwa ndani ya Serbia na kwa Waserbia wa Kosovo na Bosnia na Herzegovina.

  2. Baada ya Urusi kuanzisha vita nchini Ukraine na kuona muungano wa mataifa ya Magharibi dhidi yake, nchi za Magharibi zimeongeza jitihada za kuishawishi Serbia. Hii ni pamoja na kusimamia makubaliano kati yake na Kosovo ya kurekebisha mahusiano (Machi 2023) na kufungua njia kwa Serbia kujiunga na Umoja wa Ulaya, na labda NATO katika siku zijazo. Hii ni sawa na kujiunga kwa Sweden na Finland katika NATO ili kuongeza hasara za kimataifa za Urusi kutokana na vita vyake nchini Ukraine. Hivyo, kulionekana kukaribiana kukubwa kati ya Serbia na Magharibi. Mnamo Juni 2022, nchi za Ulaya zilizuia ndege ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Lavrov, kupita katika anga zao kutembelea Serbia. Hii iliikasirisha Serbia, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serbia alisema: ("Serbia ndiyo pekee barani Ulaya ambayo haijaweka vikwazo dhidi ya Urusi, na haijajiunga na hali ya wasiwasi dhidi ya Urusi." Youm7, 22/08/2022). Kauli hii inadhihirisha uzito ambao Serbia inahisi kutokana na uhusiano wake na Urusi, hasa kwa kuwa fursa kutoka kwa nchi za Magharibi zimeanza kuifungukia. Hata kuwekwa kwa Serbia katika mkondo wa Magharibi huenda kumepata matokeo zaidi ya hayo, ambapo Sky News Arabia ilichapisha tarehe 04/03/2023: ("Urusi iliitaka Serbia, mshirika wake, kutoa maelezo rasmi siku ya Alhamisi kuhusu ripoti kwamba nchi hiyo ya Balkani imewasilisha maelfu ya makombora kwa Ukraine. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, alielezea 'wasiwasi mkubwa' kuhusu ripoti hizo zilizotajwa kwa mara ya kwanza katika vyombo vya habari vya Urusi vinavyounga mkono serikali mwezi uliopita"). Licha ya Serbia kukanusha kuingilia mzozo wa Ukraine, misimamo hii inaonyesha kuwa Serbia imeanza kupita njia mbali na Urusi hata kama njia hiyo bado ina changamoto au vikwazo.

  3. Mbele ya ukweli huu mpya wa mahusiano kati ya Urusi na Serbia baada ya vita vya Ukraine, Urusi ambayo ina ushawishi mkubwa ndani ya Serbia, imeanza kutumia zana zake za ushawishi ndani ya Waserbia ili kuchochea mvutano na kujaribu kusitisha mchakato wa kuiondoa Serbia kutoka katika ushawishi wake wa kimataifa. (Rais wa Kosovo aliishutumu Urusi kuwa na "maslahi ya uharibifu" katika eneo hilo yanayojumuisha kushambulia Kosovo, Bosnia, na Montenegro. Independent Arabia, 22/12/2022). Kwa mujibu wa chanzo hicho hicho, gazeti la Washington Post liliandika kuwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vimechochea mivutano mipana zaidi katika eneo hilo, likinukuu wachambuzi kuwa matamshi ya utaifa ya Urusi yamepata kukubalika kwa baadhi ya viongozi; akiwemo Rais wa Serbia Aleksandar Vucic. Pia gazeti la Wall Street Journal lilitaja wakati huo kuwa NATO na Umoja wa Ulaya walifanya haraka kutuliza mvutano kati ya Kosovo na Serbia baada ya kuongezeka kwa mivutano hivi karibuni, kukiwa na hofu kwamba Urusi inaweza kutumia mzozo kati ya nchi hizo mbili kuvuruga utulivu wa Ulaya.

  4. Ivana Stradner kutoka Taasisi ya American Enterprise Institute alikuwa ameonya kabla ya kuzuka kwa vita vya Ukraine kwamba Urusi imedhamiria kuleta machafuko katika Balkani. Alisema katika makala yenye kichwa "Urusi Inacheza na Moto katika Balkani" iliyochapishwa na jarida la Foreign Affairs na kunukuliwa na Independent Arabia mnamo 20/04/2023: ("Siondoi uwezekano wa eneo la Balkani kugeuka kuwa uwanja mpya ambapo Urusi itatoa changamoto kwa Umoja wa Ulaya na NATO, ili kuthibitisha kuwa wao ni zimwi la karatasi..." Independent Arabia, 20/02/2022). Kwa hivyo, kinachopewa uzito ni kwamba Urusi ndiyo inayochochea mzozo nchini Kosovo ili kuondoa macho kwenye udhaifu wake ulioonyeshwa na vita vya Ukraine, na ili kuzishughulisha nchi za Ulaya adui zake na vita vingine barani Ulaya, na pia kusitisha mchakato wa kuiondoa Serbia kutoka katika ushawishi wake.

Tatu: Uhakika wa Matukio ya Hivi Karibuni:

  1. Waserbia ndani ya Kosovo hawazidi 120,000 kati ya takriban watu milioni mbili ambao ni wakazi wa eneo hilo. Theluthi moja ya Waserbia wamejilimbikiza katika miji minne ya mpakani na Serbia, ambayo ndiyo kitovu cha mzozo wa hivi karibuni. Katika miji hii minne (yenye watu 50,000) ambapo Waserbia wanashikilia 90% ya wakazi, mamlaka ya serikali ya Pristina (mji mkuu wa Kosovo) imekuwa dhaifu. Polisi hawawezi kushughulikia uhalifu na kukamata wahalifu kwa sababu za kikabila na kushutumiwa kwa kuwalenga Waserbia. Waserbia katika miji hii wameanza kuleta ghasia kwa msingi wa kikabila na kudai kujiunga na Serbia, jambo ambalo linaweka shinikizo kwa upande wa pili wa mpaka mbele ya watu wake kuwalinda Waserbia wa Kosovo.

  2. Ili kuimarisha mamlaka yake katika miji hiyo, serikali ya Kosovo mnamo Agosti 2022 ilitoa sheria za kulazimisha kubeba vitambulisho vyake na namba za magari kaskazini mwa Kosovo. Hii ilisababisha kujiuzulu kwa wingi kwa mameya na polisi wa asili ya Kiserbia mnamo Novemba 2022, na maandamano yalienea kaskazini mwa nchi. Kisha serikali ya Kosovo iliandaa uchaguzi wa mitaa hapo mnamo Aprili 2023 ambao Waserbia walikataa kushiriki, na wagombea Waislamu walitangazwa washindi. Waserbia katika miji hii walikasirika kwa sababu hawataki mameya wao wawe Waislamu Waalbania (Wakosovo). Ghasia zilienea ikiwemo kufungwa kwa barabara hadi serikali ya Kosovo ikajipata ikilazimika kuimarisha usalama. Polisi waliweka usalama kwa ajili ya mchakato wa kuwaapisha mameya wapya, na Waserbia wakajitokeza kutaka kuvamia majengo, wakakuta polisi wa Kosovo wakiwazuia. Rais wa Serbia muda mfupi kabla ya hapo alikuwa ameweka jeshi lake katika hali ya utayari akionyesha uwezekano wa kuingilia kijeshi.

  3. Ama Urusi, ilikuwa ikichochea moto na kuonyesha uungaji mkono mkubwa kwa Waserbia. Msemaji wa Wizara yake ya Mambo ya Nje alisema kabla ya kuzuka kwa maandamano ya tarehe 29/05/2023: ("Urusi inalaani vikali hatua za uchochezi za Kosovo ambazo zimefanya hali kuwa ukingoni mwa 'hatua ya moto', ikiongeza kuwa jukumu la uchochezi dhidi ya Serbia liko kwa Marekani na Umoja wa Ulaya." Youm7, 28/05/2023). Baada ya maandamano, (Sergei Lavrov alisema kuwa mivutano inayoongezeka Kosovo inaweza kusababisha "mlipuko mkubwa" katikati ya Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kuwa hali hiyo "inatisha" na akaonya kuhusu kuzuka kwa volcano kubwa katika Balkani. Sawt Al-Khaleej, 30/05/2023). Vilevile, (Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisisitiza kuwa "Waserbia wanapigania haki zao kaskazini mwa Kosovo", akieleza kuwa jeshi liko katika hali ya tahadhari na "uamuzi utachukuliwa na Rais wa Serbia." Independent Arabia, 30/05/2023).

  4. Kuhusu Amerika, msimamo wake karibu hautofautiani na msimamo wa Ulaya. Taarifa ya pamoja ilitolewa ikisainiwa na Amerika, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, na Italia ikitaka kuchukuliwa hatua za haraka kusitisha mivutano kaskazini mwa eneo hilo. (Tovuti ya Serikali ya Uingereza, 26/05/2023). Uingereza ilikuwa imejitahidi, katika mfumo wa NATO, kuwa na uongozi wa sekta kuu ya kati katika eneo la mji mkuu "Pristina" baada ya kuingilia kati kwa NATO mwaka 1999, na ni nchi ya kwanza katika NATO kuteua balozi wake Pristina baada ya kutangazwa kwa uhuru (Radio Sawa, 21/02/2008). Kisha Amerika ikateua balozi wake miezi mitano baada ya hapo (Youm7, 19/07/2008). Blinken aliona kuwa uamuzi wa mamlaka ya Pristina kutumia nguvu kuhakikisha ufikiaji wa mameya kaskazini mwa eneo hilo katika majengo ya utawala ("ulisababisha ongezeko kubwa na lisilo na sababu la mvutano"... RT, 31/05/2023). Vilevile, (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliwahimiza viongozi wa Serbia na Kosovo kupunguza mvutano, akionya kuwa wanatishia matumaini ya kujiunga na Ulaya. Blinken alisema – kwa waandishi wa habari wakati wa mazungumzo ya NATO huko Oslo Alhamisi iliyopita – "Tunazitaka serikali za Kosovo na Serbia kuchukua hatua za haraka kupunguza mvutano"... Al Jazeera Net, 02/06/2023).

  5. Kutokana na misimamo hii ya Magharibi, inaonekana kuwa hali inaelekea kutulia. Baada ya msimamo mkali ulioonyeshwa na Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti, alianza kuonyesha ulaini. (Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti alisema kuwa anajitahidi kuwalinda Waserbia wote wa Kosovo, akisisitiza kuwa ni haki yao kutoa sauti zao kwa njia za amani, akiongeza kuwa mamlaka nchini Kosovo yanaweza kupatikana kwa uchaguzi na si kwa ghasia. Kurti alipendekeza kufanyika kwa uchaguzi mpya wa mameya katika jaribio la kusitisha ghasia zilizotokea hivi karibuni kaskazini mwa nchi. Al Jazeera Net, 02/06/2023). Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Macron na Kansela wa Ujerumani Scholz walimshinikiza Rais wa Kosovo wakati wa mkutano wa kilele huko Moldova kufanya mkutano na Rais wa Serbia ili kupunguza mvutano.

  6. Kwa haya yote, inabainika kuwa Urusi mbali na kutumia ushawishi wake nchini Serbia, ina uwezo wa kuchochea mvutano katika eneo la Kosovo na ina zana zake nyingi nchini Serbia na kwa Waserbia wa eneo hilo. Inataka kutengeneza kitovu cha mvutano ili kuficha udhaifu wake unaoonekana katika vita vya Ukraine na inataka kuzuia kuondolewa kwa Serbia kutoka katika ushawishi wake. Kauli za maafisa wake kupitia kuonyesha uungaji mkono mkubwa kwa Waserbia zilikuwa zikichochea moto ili kulipua vita nchini Kosovo, lakini nchi za Ulaya pamoja na Amerika zilikuwa zikifanya kazi ya kuzima moto huo mara tu ulipozuka, kwani Amerika na nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa na shauku kubwa ya kuzima moto huo haraka.

Nne: Hitimisho

Hitimisho ni kwamba Urusi haiko mbali na mivutano nchini Kosovo iliyosababishwa na Waserbia wa Kosovo na hivyo kuichochea Serbia. Urusi ilikuwa ikitumaini kutokana na mivutano hii kwamba nchi za Magharibi zitashughulishwa nayo kwa kuzingatia kuwa NATO ipo Kosovo, na kisha moto huu uwake kati ya Waserbia na Kosovo, na hivyo nchi za Magharibi na NATO ziwe katikati yake. Urusi ilitarajia kutokana na hilo kupunguza kuendelea kwa Amerika na NATO katika kuchochea moto wa vita kati ya Urusi na Ukraine. Inaonekana kuwa Amerika na Magharibi walitambua jambo hili, hivyo wakafanya kila jitihada kutuliza mambo kati ya Waserbia na Kosovo, na kuwapa ishara ya uwezekano wa kujiunga na Umoja wa Ulaya na baada ya hapo NATO kwa sharti la kushirikiana katika kuzima mivutano hii. Inaonekana kuwa Amerika na nchi za Magharibi wamefanikiwa katika hilo kama tulivyobainisha kupitia kauli za maafisa, hasa kutoka Amerika na Kosovo.

Hii ndiyo tunayoipa uzito kuhusu mazingira ya matukio haya, mwendo wake na matokeo yake kama tulivyobainisha hapo juu.

Hatimaye, Kosovo kama tulivyotaja ilikuwa ndani ya Dola ya Kiothmani na watu wake walisilimu tangu zamani. Lau si kwamba Waislamu wamekosa Dola ya Khilafah inayowalinda dhidi ya shari za makafiri wakoloni, basi hali ya mambo isingekuwa mikononi mwa nchi hizo kafiri za kikoloni zinazotawala nchi hiyo baada ya bendera ya Uislamu kuwa ikipepea juu ya Balkani na Kosovo...

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) afariji dhiki za Umma wa Kiislamu na urejee kwenye chimbuko la utukufu wake kwa kusimamisha Khilafah upya.

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

"Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu. Yeye humnusuru amtakaye, Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye kurehemu." (Ar-Rum [30]: 4-5)

Tarehe 22 Dhul-Qi'dah 1444 Hijiria
11/06/2023 Miladi

Share Article

Share this article with your network