(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Jibu la Swali: Ta'zir; Maelezo yake na Hukumu zake
Kwa Nasser Reda Mohamed Osman
Swali:
As-salamu Alaykum. Ubarikiwe ewe Sheikh wangu na Amir wangu, na sisi tubarikiwe kupitia kwako. Katika jibu moja ilikuja ibara isemayo "kwa sababu alitunga sheria ya Ta’zir na akafafanua maelezo ya hukumu zake na aina zake", sasa ni yapi maelezo ya hukumu zake na aina zake?
Jibu:
Swali lako ni kuhusu maandishi yaliyokuja katika jibu la swali la tarehe 02/01/2015, nayo ni:
"Ama adhabu za Ta’zir, nazo ni adhabu kwa maasi ambayo Sharia haikupanga adhabu maalum kwa ajili yake, bali iliacha upangaji wa adhabu hiyo kwa Imam au Qadhi... nazo ni miongoni mwa hukumu za Tariqah (njia ya utekelezaji). Na kitendo cha Sharia kutopanga adhabu hiyo haimaanishi kamwe kuwa haikuweka njia ya kutekeleza hukumu za kisheria ambazo ziliadhibiwa kwa kutozingatiwa kwake kama Ta’zir. Kwani Yeye (Mwenyezi Mungu) alitunga sheria ya Ta’zir na akafafanua maelezo ya hukumu zake na aina zake... na akamwachia Imam pekee kuchagua miongoni mwa aina za adhabu ambazo Sharia ilizibainisha, na kwa kiasi ambacho anakiona kinafaa kwa hali halisi ya maasi na hali ya mwasi. Yaani Sharia ilibainisha namna ya kutekeleza hukumu hizi kwa kuitaka ipatikane adhabu kwa asiyezizingatia, lakini kiasi cha adhabu hii na aina yake... hili ndilo ambalo Sharia imemwachia Imam au naibu wake." Mwisho.
Hatukufafanua kwa kirefu kauli hiyo katika jibu la swali lililotajwa ili kuepuka urefu... na kadhalika katika jibu la swali lako hili, maelezo ya kina hayawezi kutolewa yote kwa sababu maudhui ya Ta’zir ni makubwa na mapana, na mada hiyo imetajwa kwa ukamilifu katika kitabu chetu Nidhamu ya Adhabu (Nizam al-Uqubat)... lakini nitataja baadhi yake:
1- Ta’zir inatofautiana na Hudud na Jinayat. Hudud na Jinayat ni adhabu zilizokadiriwa na kupangwa na Sharia, nazo ni lazima na haijuzu kuzibadilisha wala kuziongeza au kuzipunguza. Ama Ta’zir ni adhabu ambayo haikukadiriwa yenyewe, wala si lazima yenyewe. Kadhalika, Hudud na Jinayat hazikubali msamaha wala kuondolewa na mtawala isipokuwa msamaha kutoka kwa mwenye haki katika Jinayat, na hii ni tofauti na Ta’zir kwani hiyo inakubali msamaha na kuondolewa.
2- Sharia imebainisha aina za adhabu za Ta’zir ambazo anaruhusiwa Qadhi kuadhibu kwazo, na hilo ni kwa nusu (maandishi) za kisheria zilizo wazi, na haijuzu kuadhibu kwa adhabu nyingine yoyote. Kwani adhabu ni kitendo, hivyo ni lazima pawe na dalili ya kujuzu kwake. Na haisemiwi kuwa lazima pawe na dalili ya kumkataza kuadhibu kwa adhabu fulani, haisemwi hivyo kwa sababu asili ni kutokuwepo kwa adhabu. Hivyo, kutoa adhabu fulani ndiko kunakohitaji dalili. Kuhusu asili kuwa ni kutokuwepo kwa adhabu, ni kwa sababu dalili ya jumla imekuja juu ya heshima ya mwanadamu, na kutofanyiwa maudhi, hivyo kutoa adhabu fulani kwake kunahitaji dalili inayoruhusu kuitekeleza. Na ikiwa dalili haijapatikana juu ya kujuzu kwa adhabu fulani, basi haijuzu kuitekeleza.
Wala isisemwe kuwa Ta’zir ameachiwa mtawala kwa ukamilifu bila kikwazo, hivyo anaweza kutoa Ta’zir kwa adhabu anayoiona yeye. Haisemwi hivyo, kwa sababu kilichowekwa kwa mtawala ni kukadiria kiasi cha adhabu, na hakupewa kingine zaidi ya hapo. Sharia imeingilia kati katika adhabu na ikabainisha aina zake, yaani ilibainisha aina za adhabu ambazo mwasi anaadhibiwa kwazo, hivyo Qadhi amekuwa amefungwa na adhabu hizi. Yaani kubainisha kwa Sharia aina za adhabu kumemfunga Qadhi nazo, hivyo si halali kwake kuadhibu kwa nyinginezo, na ana hiari ya kuchagua miongoni mwazo kile anachokiona kuwa ni kizuizi (zajir). Kwa hivyo, ni lazima kwa mtawala anapotoa adhabu ya Ta’zir afuate hukumu za kisheria, asiadhibu isipokuwa kwa adhabu ambazo Sharia imekuja nazo.
3- Sharia imekataza adhabu fulani na ikaruhusu adhabu fulani ambazo ni lazima kufungamana nazo katika adhabu za Ta’zir. Imekataza kuchoma moto, hivyo adhabu ya kuchoma moto haijuzu. Al-Bukhari amepokea kutoka kwa hadith ya Abu Hurairah:
وَإِنَّ النَّارَ لاَ يُعَذِّبُ بِهَا إِلَّا اللَّهُ
"Na hakika moto, hapana anayeuadhibu kwao isipokuwa Mwenyezi Mungu."
Na Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Ikrimah kuwa Mtume ﷺ amesema:
لاَ تُعَذِّبُوا بِعَذَابِ اللَّهِ
"Msidhibu kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu," akimaanisha kuchoma moto. Na Abu Dawood amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Ibn Mas’ud, kutoka kwa Mtume ﷺ kuwa amesema:
إِنَّهُ لَا يَنْبَغِي أَنْ يُعَذِّبَ بِالنَّارِ إِلَّا رَبُّ النَّارِ
"Hakika haipasi kuadhibu kwa moto isipokuwa Mola wa moto."
Haya yote yako wazi katika haramu ya adhabu ya kuchoma moto, na yanajumuisha yale yaliyo katika jinsi yake ambayo yana sifa ya kuunguza kama vile umeme.
4- Sharia imeruhusu adhabu fulani katika Ta’zir ambazo haijuzu kuhukumu kwa nyinginezo, na ilibainisha hilo waziwazi, miongoni mwazo nitataja:
A- Adhabu ya Kuua: Inajuzu kwa Khalifah kufika katika adhabu ya Ta’zir hadi kiwango cha kuua kwa makosa makubwa ambayo hayako katika makosa ya Hudud. Hilo ni kama kosa la kulingania kutenganisha jimbo kutoka katika mwili wa Dola ya Kiislamu, kama ilivyokuja katika hadith tukufu:
مَنْ أَتَاكُمْ وَأَمْرُكُمْ جَمِيعٌ عَلَى رَجُلٍ وَاحِدٍ، يُرِيدُ أَنْ يَشُقَّ عَصَاكُمْ، أَوْ يُفَرِّقَ جَمَاعَتَكُمْ، فَاقْتُلُوهُ
"Yeyote atakayewajia huku mkiwa katika maelewano chini ya mtu mmoja, akitaka kuvunja umoja wenu au kutenganisha jamaa yenu, basi muueni." (Imepokewa na Muslim kutoka kwa Arfajah). Na kwa hiyo, inajuzu kwa Khalifah kuamuru auwawe kama Ta’zir... yaani inajuzu kwa Khalifah kufikia katika Ta’zir kiwango cha kuua.
B- Viboko: Nao ni kupiga kwa mjeledi na vile vinavyofanana nao... isipokuwa kwamba Ta’zir kwa kupiga na viboko haijuzu kuzidi mapigo kumi, au viboko kumi. Hilo limekuja waziwazi katika nusu za hadith; Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Abdulrahman bin Jabir, kutoka kwa aliyemsikia Mtume ﷺ akisema:
لاَ عُقُوبَةَ فَوْقَ عَشْرِ ضَرَبَاتٍ إِلَّا فِي حَدٍّ مِنْ حُدُودِ اللَّهِ
"Hakuna adhabu juu ya mapigo kumi isipokuwa katika adhabu miongoni mwa Hudud za Mwenyezi Mungu."
Hivyo ikiwa hukumu ni viboko, haijuzu kuzidi viboko kumi...
C- Faini (Gharama): Inakubalika faini katika Ta’zir kwa baadhi ya dhambi. Zimekuja nusu kuhusu hilo, miongoni mwazo ni kile alichokitoa Abu Dawood katika Sunan yake kutoka kwa Abu Hurairah akisema: Mtume ﷺ amesema:
ضَالَّةُ الْإِبِلِ الْمَكْتُومَةُ غَرَامَتُهَا وَمِثْلُهَا مَعَهَا
"Ngamia aliyepotea akifichwa, faini yake ni yeye na mfano wake pamoja naye," yaani yeyote anayeficha kuwa ngamia aliyepotea yuko kwake na akamficha mwenye naye, basi anarejeshwa kwa mmiliki wake na mfichaji anapigwa faini ya mfano wake. Kadhalika, kutoa Ta’zir kwa anayekataa kutoa Zaka kwa kuchukua nusu ya mali yake. Haya yote yanaonyesha kuwa Mtume ﷺ aliamuru adhabu ya faini katika Ta’zir.
D- Kifungo: Inajuzu kufunga katika Ta’zir. Kifungo cha kisheria ni kumzuia mtu na kumzuia asijimudu mwenyewe, iwe ni katika mji, au nyumbani, au msikitini, au katika jela iliyoandaliwa kwa ajili ya adhabu au kwingineko. Dalili ya kuwa kifungo ni adhabu miongoni mwa adhabu za Sharia ni kile alichokipokea At-Tirmidhi kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake:
أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حَبَسَ رَجُلًا فِي تُهْمَةٍ ثُمَّ خَلَّى عَنْهُ
"Kwamba Mtume ﷺ alimfunga mtu kwa tuhuma, kisha akamwachia."
Kifungo katika zama za Mtume ﷺ kilikuwa nyumbani, au msikitini, na hali ilikuwa hivyo pia katika zama za Abu Bakr, kwani hakukuwa na jela iliyoandaliwa kwa ajili ya mahasimu. Zilipofika zama za Umar, alinunua nyumba kwa Safwan bin Umayyah kwa dirham elfu nne, na akaifanya kuwa jela. Umar alimfunga Al-Hutaia kwa kashfa (hijo), na akamfunga Sabigh kwa swali lake kuhusu Adh-Dhariyat, Al-Mursalat, An-Nazi’at na mfano wake... Na ni lazima muda wa kifungo uwe maalum, kwani hukumu ya kifungo cha maisha haijuzu kisheria, bali ni lazima kubainisha muda ambao mtu anahukumiwa kifungo.
Na kifungo ni kuzuiliwa, wala si kufanyishwa kazi. Kufanyishwa kazi ni jambo jingine tofauti na kifungo. Kwa hivyo, ikiwa mtu amehukumiwa kifungo haijuzu kufanyishwa kazi, kwa sababu neno kifungo halijumuishi kufanyishwa kazi. Lakini je, inajuzu kuhukumu kwa kifungo na kufanyishwa kazi, au inaishia kwenye hukumu ya kifungo pekee? Jibu la hilo ni kwamba haijakuja nusu ya kisheria ya kuifanya adhabu kuwa ni kufanyishwa kazi, iwe kazi ngumu au zisizo ngumu, na kwa hivyo haadhibiwi kwazo, bali inaishia kwenye kifungo kwa maana ya kuzuiliwa.
E- Mawaidha: Nalo ni kule Qadhi kumpa mawaidha mkosaji kwa kumtisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Dalili ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ
"Na wale ambao mnaogopa uasi wao, basi wapeni mawaidha." (QS. An-Nisa [4]: 34).
Hizi ni baadhi ya aina za adhabu za Ta’zir ambazo zimekuja dalili kutoka katika Sharia juu ya kujuzu kwa mtawala kuadhibu kwazo, na haijuzu kwa mtawala kuadhibu kwa aina yoyote ya adhabu isipokuwa ikiwa imekuja nusu kutoka katika Sharia ya kujuzu kwa aina hiyo.
Natumai katika hili pana utoshelevu.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Facebook wa Amir: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir: Tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Google Plus wa Amir: Google Plus