** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)**
Kwa Tamer al-Hajj Muhammad
Swali:
Mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Allah akulinde. Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Baada ya hayo:
Ni nini hukmu ya mali ya haramu baada ya toba, kama vile mali inayotokana na riba, wizi, uimbaji mchafu, au mambo mengineyo?
Je, kuna ufafanuzi maalum au hukmu ni moja?
Ikiwa mali hiyo ni haramu hata kama mmiliki wake ametubu, kuna mtu anayeweza kutaka kutubu lakini anahofia kupoteza mali yake. Je, kuna msamaha kwa hili kwa lengo la kumvutia kwenye toba kama walivyosema baadhi ya masheikh?
Jibu:
Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Allah Subhanahu wa Ta'ala anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَصُوحًا
"Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allah toba ya kweli." (QS At-Tahrim [66]: 8)
Na Anasema Subhanahu:
إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَاعْتَصَمُوا بِاللَّهِ وَأَخْلَصُوا دِينَهُمْ لِلَّهِ فَأُولَئِكَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ وَسَوْفَ يُؤْتِ اللَّهُ الْمُؤْمِنِينَ أَجْرًا عَظِيمًا
"Isipokuwa wale waliotubu, na wakatengeneza, na wakashikamana na Allah, na wakamsafishia Allah dini yao, basi hao watakuwa pamoja na waumini. Na hivi karibuni Allah atawapa waumini malipo makubwa." (QS An-Nisa [4]: 146)
Na At-Tirmidhi amepokea kutoka kwa Anas, kwamba Mtume (saw) amesema:
كُلُّ ابْنِ آدَمَ خَطَّاءٌ وَخَيْرُ الخَطَّائِينَ التَّوَّابُونَ
"Kila mwana wa Adam ni mkosaji, na bora wa wakosaji ni wenye kutubu."
Ili toba iwe sahihi, na Allah Subhanahu amsamehe mwenye kutubu dhambi yake, ni wajibu kwa mwenye kutubu kuacha maasia hayo, ajutie mbele Yake Subhanahu kwa kitendo hicho alichokifanya huko nyuma, na azimie azma ya dhati kutorudia tena mfano wake abadan. Ikiwa maasia yanahusiana na haki ya mwanadamu, basi inashurutishwa kurejesha dhuluma kwa wenyewe au kupata msamaha kutoka kwao. Hivyo, ikiwa ana mali aliyoichukua kutoka kwao kwa njia ya wizi au kunyang'anya (ghasb), ni lazima airejeshe mali hiyo kwa wenyewe, na ajiepushe na mapato hayo maovu kwa njia ya kisheria (shari’ah), kwani kuchuma mali kwa njia ya haramu matokeo yake ni mabaya sana.
Ahmad amepokea kutoka kwa Abdullah bin Mas'ud, amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:
...وَلَا يَكْسِبُ عَبْدٌ مَالًا مِنْ حَرَامٍ... إِلَّا كَانَ زَادَهُ إِلَى النَّارِ
"...Na mja hachumi mali ya haramu... ila itakuwa ni akiba yake kuelekea Motoni."
Na At-Tirmidhi amepokea kutoka kwa Ka'b bin 'Ujrah kwamba Mtume wa Allah (saw) alimwambia:
يَا كَعْبَ بْنَ عُجْرَةَ، إِنَّهُ لَا يَرْبُو لَحْمٌ نَبَتَ مِنْ سُحْتٍ إِلَّا كَانَتِ النَّارُ أَوْلَى بِهِ
"Ee Ka'b bin 'Ujrah, hakika haukui mwili uliotokana na mali ya haramu (suhut) isipokuwa Moto unaufaa zaidi."
Sasa, huyu mtu uliyeulizia anataka vipi kutubu huku akiibakisha mali ya haramu mkononi mwake?! Hiyo siyo toba, bali ni kuendelea katika uovu. Mshauri atubu, na ajiepushe na mapato ya haramu kwa njia ya kisheria, na airejeshe mali ya haramu aliyoiiba au kuinyang'anya kwa wenyewe, na awaombe msamaha, na amtake msamaha Allah Subhanahu mwanzo na mwisho. Allah Subhanahu ndiye Mpaji (Ar-Razzaq) Mwenye nguvu madhubuti, atamfidia akipenda Subhanahu mali nzuri yenye baraka ambayo Allah atamfanyia kuwa na izza kwayo duniani na Akhera. Allah Subhanahu wa Ta'ala anapenda toba ya mja Wake ikiwa ni ya kweli na ya dhati na humlipa malipo yaliyo bora zaidi...
Namuomba Allah Subhanahu amuongoe mtu huyo kwenye uongofu wa jambo lake ili atubu toba ya kweli (nasuha), na Allah Subhanahu ni mwingi wa maghfira.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka kwa tovuti ya Ameer
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Google Plus