S1: Punde tu matokeo ya uchaguzi yalipoonyesha ushindi wa chama cha Congress (Congress Party), uraia wa Kiitaliano wa rais wa chama hicho, Sonia Gandhi, uliibuliwa, ikijulikana kuwa alikuwa ameuacha uraia huo na kuwa raia wa India kisheria na kwa utaratibu sahihi. Kuibuliwa kwa uraia wake wa zamani wa Kiitaliano kulifanywa kwa nguvu sana kiasi kwamba wabunge wa chama cha Janata walitishia kujiondoa katika bunge lililochaguliwa kwa kupinga jambo hilo. Kufuatia hayo, kulikuwa na mivutano iliyopelekea Sonia kujiondoa katika kugombea nafasi ya Uwaziri Mkuu. Je, hii inamaanisha kuwa Marekani ilianza mapema kuleta matatizo kwa chama cha Congress tangu mwanzo wa muhula wake?
J1: Ndiyo, hiyo ni kweli. Si rahisi kwa Marekani kuiacha India irejee kuwa "jikoni" la kisiasa kwa ushawishi wa Uingereza katika bara Hindi (subcontinent) tena. Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa kuna vidole vya Marekani nyuma ya kuchochea suala la uraia wa zamani wa Sonia baada ya kufanikiwa kwake kukiongoza chama cha Congress kushinda uchaguzi.
Ili kuelewa hili vizuri, hebu turejee nyuma kidogo. Chama cha Congress kinajulikana kwa utiifu wake kwa Waingereza, kwani kiliundwa chini ya uangalizi wao. Mmoja wa marais wake wenye bidii zaidi katika kuimarisha siasa za Uingereza na kupinga siasa za Marekani nchini humo alikuwa Nehru, akifuatiwa na familia ya Gandhi (Indira Gandhi, na wanawe Sanjay na Rajiv). Marekani ilikuwa katika mgogoro nao. Kuna uwezekano mkubwa kuwa Marekani ilihusika katika mauaji ya Rajiv Gandhi. Hilo linathibitishwa na ukweli kwamba aliyemfuata katika Uwaziri Mkuu alikuwa (Narasimha Rao), ambaye anatoka upande wa washauri wastani katika chama cha Congress wanaojulikana kwa kuilainishia Marekani, hususan kwa vile alimteua (Manmohan Singh) kama Waziri wa Fedha. Singh ni mtu anayejulikana kwa kuhimiza uwezekaji wa Marekani nchini India, na Waziri huyu wa Fedha alianzisha mahusiano ya kiuchumi na mitaji ya Marekani, hususan katika nyanja ya kielektroniki. Kitendo cha huyu Waziri wa Fedha kuwa ndiye aliyependekezwa kwa Uwaziri Mkuu badala ya Sonia, na kuwa Waziri Mkuu kweli, kinaonyesha kuwa kulikuwa na shinikizo la Marekani nyuma ya hilo.
Vyovyote iwavyo, si rahisi kwa Marekani kukidhibiti chama cha Congress, kwani ni mhimili mmojawapo wa Waingereza. Lakini Marekani haitaiacha India kirahisi baada ya kuingia humo kwa muda wa miaka minane. Itatumia njia iwezavyo kwa ushawishi na vitisho ili kujaribu kukiingilia chama cha Congress, au kukiletea matatizo, au kujaribu kuingilia muungano wa serikali kupitia vyama vidogo vilivyoungana na Congress na kadhalika, kwa sababu chama cha Congress hakimiliki idadi kubwa ya viti peke yake. Lakini hatudhani kama itafanikiwa, kutokana na werevu wa kisiasa wa Uingereza unaokabiliana nayo na ukongwe wa chama cha Congress. Badala yake, Uingereza na chama cha Congress zinaweza kufuata sera ya ulainifu wa kisiasa kuelekea Marekani, kama ilivyo desturi ya vibaraka wa Uingereza katika eneo la Mashariki ya Kati, na hata kama ilivyo desturi ya Uingereza yenyewe katika sera yake kuelekea Marekani; inailainishia kidhahiri huku ikiibana kwa siri. Pamoja na hayo, Uingereza kupitia chama cha Congress haitaacha fursa yoyote inayojitokeza ya kudhoofisha ushawishi wa Marekani katika bara Hindi, hususan nchini Pakistan, bila kuichangamkia, ili kujaribu kuifanya Uingereza ishirikiane na Marekani katika ushawishi katika bara Hindi ikiwa itashindwa kurejesha ushawishi wa Uingereza kama ulivyokuwa hapo awali.
9 Rabi' al-Akhar 1425 AH 28/05/2004 AD