Home About Articles Ask the Sheikh
Uchambuzi

Jibu la Swali: Nini Kiko Nyuma ya Ongezeko la Mvutano wa Ukraine na Uchochezi wake dhidi ya Urusi

December 15, 2018
5089

Jibu la Swali

Nini Kiko Nyuma ya Ongezeko la Mvutano wa Ukraine na Uchochezi wake dhidi ya Urusi

Swali: Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alisema: (Urusi ilianzisha vita vya uchokozi dhidi ya nchi yake wakati walinzi wake wa mpaka walipozizuia meli za kivita za Ukraine katika mlango-bahari wa Kerch unaounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov). Haya aliyasema katika mazungumzo yake na chaneli ya Marekani ya Fox News, akiashiria tukio hilo, na kuongeza: ("Bwana Putin, huu ni uchokozi na vita na si mzaha, tukio la bahati mbaya au mgogoro"... Sputnik Arabic 12/12/2018). Urusi ilikuwa imetangaza kuwa walinzi wake wa pwani walizizuia meli tatu za kivita za Ukraine mnamo 25/11/2018 ikidai kuwa zimekiuka maji ya Urusi karibu na mlango-bahari wa Kerch kati ya Bahari Nyeusi na Azov mashariki mwa rasi ya Crimea, na kufuatia tukio hilo Marekani ilitaka kuimarishwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi huku Ulaya ikikataa jambo hilo. Mvutano bado unaendelea kati ya pande hizo. Je, ni nani anayesimama nyuma ya tukio hili? Na kwa nini hali imekuwa ya mvutano upya huko?

Jibu: Tutapitia matukio yaliyotokea na yanayoendelea kutokea huko kuhusiana na mada hii ili jibu liwe wazi, Mwenyezi Mungu akipenda:

1- Urusi, Marekani na Ulaya zilikubaliana mnamo Februari 2014 juu ya kubaki madarakani kwa Rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych, ambaye alikuwa mshirika wa Urusi. Lakini mara tu makubaliano hayo yalipofikiwa, ghasia zilizuka na kugeuka kuwa mapambano ya silaha ambayo yalimfanya Yanukovych kulazimika kutorokea Urusi. Ilibainika kuwa nchi za Magharibi zilikuwa nyuma ya matukio hayo... Urusi ikatambua kuwa Magharibi imeihadaa na imepoteza Ukraine, hivyo ikachukua hatua na kutangaza kuunganisha rasi ya Crimea kwake, na ikawachochea wafuasi wake huko Donbas mashariki mwa Ukraine, ambao walitangaza uhuru wa maeneo yao kwa jina la Jamhuri za Donetsk na Luhansk. Kufuatia hilo, Marekani na Ulaya ziliweka vikwazo dhidi ya Urusi na kuiondoa katika kundi la mataifa saba (G7).

2- Marekani ilitoa wito wa kuipa silaha Ukraine lakini Ulaya ilikataa hilo, kwa sababu inatambua kuwa hatua hiyo italeta mvutano na Urusi na hali ikichochewa itaathiri Ulaya... Hivyo Ufaransa na Ujerumani ziliwasiliana na Urusi ili kupunguza mvutano na kupata suluhisho la kisiasa, na hivyo makubaliano ya Minsk yakasainiwa mnamo 06/02/2015 kati ya nchi hizo tatu bila Marekani. Tuliaashiria hili katika jibu la swali la tarehe 21/02/2015 ambapo tulisema: (Ulaya "Ufaransa na Ujerumani" ilihofia kuwa mabadiliko haya ya moto katika msimamo wa Marekani yangepelekea kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za Urusi dhidi ya Ukraine, na kisha Ulaya kuaibika ikiwa haitasimama upande wa Ukraine, jambo ambalo lingesababisha vita au nusu-vita barani Ulaya wakati ambapo vita hivi haviathiri Marekani. Hilo lilikuwa sababu ya dharura kwa Ulaya kubadili sera yake ya kuikubalia Marekani nchini Ukraine, na kuamua kuwasiliana na Rais wa Urusi ili kupata suluhisho la kisiasa, na kuzuia njia ya ongezeko lolote la mvutano kati ya Ulaya na Urusi. Na hivi ndivyo ilivyokuwa; viongozi wa Ulaya "Ufaransa na Ujerumani" walilijadili jambo hili na kukubaliana mnamo 06/02/2015 bila Marekani, kisha Merkel akaenda Washington mnamo 08/02/2015 kumpa taarifa Obama kuhusu jambo hili na si kumuomba ruhusa... Ilikuwa wazi kuwa kwa mara ya kwanza kwa muda mrefu, Ulaya inafanya maamuzi kabla ya kupata mwanga wa kijani kutoka kwa Marekani. Makubaliano ya kazi yalifikiwa na kuidhinishwa na viongozi watatu Vladimir Putin, Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande mnamo Ijumaa 06/02/2015, na kilichobaki kilikuwa ni kuwaita washirika wa Ukraine "Rais na waasi" ili kuyasaini, kisha Merkel akaenda Washington kumpa taarifa Obama!")

3- Kitendo hiki hakikuifurahisha Marekani, japo baadaye ilitangaza kuunga mkono makubaliano hayo kwa dhahiri, lakini si kwa ajili ya kuyatekeleza bali kwa ajili ya kuyapofua na kufanya kazi ya kuyahujumu. Tulitaja katika jibu la swali hilohilo: (Msimamo huu wa Ufaransa na Ujerumani ulimuathiri sana Obama na utawala wake, na hii ilisababisha mabishano makali katika mkutano wa Munich kati ya Kerry na Merkel, hasa kuhusu matamshi ya Marekani ya kuipa Ukraine silaha wakati Ulaya inakataa hilo). Na tukaongeza: (Ama kinachotarajiwa, Marekani uwezekano mkubwa itatengeneza matatizo mengi kuzuia utekelezaji wake, kwani ina wafuasi nchini Ukraine. Na ingawa Rais Poroshenko yuko karibu na Ulaya, Marekani ina sehemu yake kwake... Hivyo, inaweza kuchochea hali kupitia moja ya mambo matatu au yote kwa pamoja: kuipa Ukraine silaha za kisasa... au mazungumzo ya kuiingiza katika NATO... au kuwachochea baadhi ya watu wake nchini Ukraine. Na hivyo kuvuruga makubaliano hayo, kwa sababu kila moja ya mambo haya matatu yanachochea Urusi na kuathiri matukio, na kupelekea kufeli kwake...) Mwisho wa tulichotaja... Na hili ndilo linalotokea, Marekani inafanya kazi ya kuhujumu makubaliano na kuchochea hali ya mvutano...

4- Kutokana na hapa yamekuja matukio ya hivi karibuni wakati Urusi ilipozizuia meli tatu za kivita za Ukraine pamoja na mabaharia wake... Inaonekana kuwa Ukraine iliichochea Urusi katika jambo hilo... Na haina uthubutu wa kufanya hivyo isipokuwa kwa mwanga wa kijani kutoka kwa Marekani. Shirika la habari la Urusi la TASS liliripoti mnamo 25/11/2018 kuwa (meli tatu za kivita za Ukraine ziliingia katika maji ya Urusi kinyume cha sheria na zilikuwa zikifanya maneva hatari). Kufuatia hilo, Ukraine ilitaka Magharibi iingilie kati. Rais wa Ukraine Petro Poroshenko aliliambia gazeti la Ujerumani la Bild mnamo 29/11/2018 akisema: (Ujerumani ni mmoja wa washirika wetu wa karibu, na tunatumai kuwa kutakuwa na nchi katika NATO zilizo tayari kutuma meli katika Bahari ya Azov kusaidia Ukraine na kuhakikisha usalama huko... Putin hataki chochote isipokuwa kuikalia Bahari ya Azov. Lugha pekee anayoielewa ni umoja wa ulimwengu wa Magharibi. Ujerumani pia inapaswa kujiuliza Putin atafanya nini baadaye ikiwa hatutamsimamisha... Hatuwezi kukubali sera hii ya uchokozi ya Urusi. Kwanza ni rasi ya Crimea, kisha mashariki mwa Ukraine na sasa Putin anataka Bahari ya Azov. Putin anataka kurejesha himaya ya zamani ya Urusi: Crimea, Donbas, anataka nchi nzima). Aliongeza: (Merkel aliokoa nchi yetu mwaka 2015 kupitia mazungumzo aliyoyafanya Minsk. Kwa hivyo tunatumai kupata ulinzi tena kwa washirika wengine kuwa pamoja nasi). Lakini Ujerumani ilikataa hatua ya kijeshi. Kansela wa Ujerumani Merkel alisema: (Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mapambano haya... DPA 29/11/2018) na akamtaka Poroshenko "awe na kiasi" na akataka "hali ibaki kuwa tulivu... na tuweke ukweli mezani na tuone nini kinatokea..." na akaahidi kulijadili jambo hilo na Putin nchini Argentina. Alikataa pia kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas, baada ya kukutana na mwenzake wa Ukraine Pavlo Klimkin nchini Italia katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mnamo 06/12/2018 alisema: ("Berlin haitarajii Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kwa Urusi kutokana na mzozo wake na Ukraine ilimradi juhudi za kupunguza mvutano zinaendelea." Aliongeza, "Kwa sasa nadhani itakuwa ni kosa kuzungumzia vikwazo vipya kwa sababu juhudi zinafanywa kupunguza mvutano. Hakutakuwa na pendekezo kutoka upande wa Ujerumani la vikwazo vipya... Sitarajii muafaka ndani ya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo vipya"... Reuters 07/12/2018). Ujerumani na nchi nyingine nyingi za Ulaya zinatambua hatari ya hali hiyo na madhara yake kwa Ulaya, kwa sababu hiyo hawataki operesheni za kijeshi wala hawataki kuimarisha vikwazo, kwa sababu hiyo ni silaha yenye makali kuwili kwa Urusi na Ulaya.

5- Msimamo wa Marekani unaonekana wazi kuwa uko na uchochezi na kuimarisha vikwazo. Trump alifuta mkutano wake na mwenzake wa Urusi Putin pambizoni mwa mikutano ya G20 nchini Argentina mnamo 30/11/2018 kwa sababu ya kutoridhika kwa utawala wake na kile kilichotokea cha kuzuiliwa kwa meli za Ukraine. Trump aliwaambia waandishi wa habari kabla ya mkutano uliomkutanisha na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe katika mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires, akizungumzia kuzuiliwa kwa meli za Ukraine na Urusi: (Hatupendezwi na kile kilichotokea na haturidhishwi nacho, na hakuna anayeridhika nacho... RT Online 30/11/2018 - Novosti). Mjumbe wa Marekani nchini Ukraine Kurt Volker alikuwa amesema mnamo 27/11/2018: (Uongozi wa Urusi unalenga kuweka udhibiti wa upande mmoja katika bandari hizo ikiwemo Mariupol bila mtu yeyote kuwa na uwezo wa kuzifikia... Na jaribio la Urusi la kudhibiti lenyewe linazua wasiwasi mkubwa, na akasisitiza ulazima wa Urusi kuzingatia makubaliano ya mwaka 2003 yanayohusu usafiri wa majini katika Bahari ya Azov... Haamini kuwa Urusi itafanya shambulio jipya la nchi kavu katika ardhi ya Ukraine, na ikiwa hilo lingetokea lingemshangaza sana... Ukurasa wa Ukraine Arabic 28/11/2018). Makubaliano haya yaliyorejelewa yanathibitisha kuwa Bahari ya Azov na mlango-bahari wa Kerch ni maji ya ndani ya Urusi na Ukraine. Idhaa ya Voice of America iliripoti mnamo 06/12/2018 kuwa (Mjumbe Maalum wa Marekani Kurt Volker atafanya ziara nchini Ukraine katika wiki mbili zijazo na kuitaka Urusi kuwaachilia huru mabaharia wa Ukraine wanaoshikiliwa na kusisitiza kuwa Urusi lazima irejee kushirikiana na Ukraine katika eneo la mlango-bahari wa Kerch na Bahari ya Azov kwa msingi wa makubaliano ya pande mbili yanayohusu jambo hilo yaliyosainiwa mwaka 2003). Kama ilivyo wazi kutokana na tamko hilo, Marekani haichukui hatua kwa haraka, haina haraka, kwani mjumbe wake bingwa wa masuala ya Ukraine anatangaza kuwa ataizuru Ukraine baada ya wiki mbili! Jambo linalomaanisha kuwa hajali suluhisho, bali anataka kubakisha hali katika mvutano; lengo ni uchochezi na kuendelea kwa mvutano na si kutatua tatizo!

6- Inafaa kutaja kuwa Marekani inaipatia Ukraine silaha na vifaa na inalifunza jeshi lake. Mjumbe wa Marekani nchini Ukraine Kurt Volker aliuambia mtandao wa Ujerumani wa Deutsche Welle mnamo 29/11/2018: (Kyiv na Washington zinafungamanishwa na ushirikiano wa kawaida katika sekta ya ulinzi... na nchi yake inaifanyia Ukraine marekebisho ya vikosi vya ulinzi kwa lengo la kuwezesha nchi ya Ukraine kuwa na uwezo wa kisasa na wenye nguvu wa kujihami). Hapa afisa wa Marekani anakiri kuwa nchi yake inaipatia Ukraine silaha. Ukurasa wa Russia Today uliripoti tarehe 09/06/2018 kuwa ("Marekani ilituma ndege 4 katika uwanja wa ndege wa mji wa Lviv magharibi mwa Ukraine kwa ajili ya kuongeza mafuta kwenye ndege zake za kimkakati. Hilo likiwa ni katika mfumo wa ushirikiano na washirika wa Atlantiki ili kuhakikisha usalama wa Mashariki mwa Ulaya kulingana na Washington, na pamoja na ndege hizo walifika Wamarekani 150 kutoka kwa wafanyakazi na wahudumu wa ndege. Ilinukuu ofisi ya habari ya vikosi vya anga vya Marekani barani Ulaya na Afrika ikisema kuwa 'lengo la hatua hii ni kupata usalama zaidi wa Marekani Mashariki mwa Ulaya na ushirikiano zaidi wa kijeshi kati ya wanachama wa NATO na washirika wake'." Ukurasa huo wa Urusi uliongeza: "kwamba ushirikiano kati ya Marekani na Ukraine unaongezeka kwa kasi tangu mapinduzi dhidi ya serikali ya Ukraine mwaka 2014. Ukraine ilianza kupokea magari ya kivita ya Marekani, ndege zisizo na rubani, rada, vifaa, bunduki nzito za kunyatia na mifumo ya kuzuia vifaru, na Wamarekani waliweka sharti la kutozitumia huko Donbas"). Ni wazi kutokana na hilo kuwa Marekani inafanya kazi ya kuchochea hali kwa kuipatia Ukraine silaha na kuishajiisha kuichochea Urusi, hivyo ya mwisho inalazimika kujibu na hili ndilo Marekani inalotaka ili hali ibaki kuwa ya mvutano, na kisha inaendesha kadhia ya Crimea na Ukraine kulingana na maslahi yake... Tunakumbusha tulichokisema katika jibu la swali la tarehe 22/03/2014 baada ya Urusi kutangaza mnamo 18/03/2014 kuunganisha rasi ya Crimea ambayo ilikuwa sehemu ya Ukraine, tulisema: (...hakika Ukraine itabaki kuwa bomu linaloweza kulipuka wakati ambapo mazingira ya kimataifa au ya kikanda yatabadilika kwa ajili ya maslahi ya Urusi au Magharibi, na hapo kila upande utajaribu kuitazama Ukraine yote na kujaribu kuimiliki kulingana na mazingira ya kimataifa wakati huo... kwani Ukraine ni ubavu wa Urusi, na wakati huo huo ni lango la Ulaya...).

7- Marekani inaichochea Ukraine kwa siri ili kuichokoza Urusi kwa kuifanya ichukue hatua ya kurejesha haki yake nchini Crimea na kueneza mamlaka yake katika sehemu yake ya mashariki iliyo chini ya ushawishi wa Urusi, na kutetea haki zake katika Bahari ya Azov na katika mlango-bahari wa Kerch, ambao ni mlango-bahari muhimu sana wa kimkakati kwa nchi zote mbili; hakuna njia nyingine ya kuvuka kutoka Bahari ya Azov upande wa kaskazini kuelekea Bahari Nyeusi upande wa kusini... Inaipatia silaha, na hilo linakinzana na makubaliano ya Minsk. Hivyo Marekani inafanya kazi ya kuyaangusha makubaliano haya ya Ulaya na Urusi, na pia kuongeza mvutano... Wakati Ulaya ikifanya kazi ya kupunguza mvutano kwa sababu hilo limelekezwa dhidi yake. Ndiyo maana tunaona Ulaya inafanya kazi ya kufikia maelewano na Urusi wakati ikifanya kazi ya kujikomboa kutoka kwenye utawala wa Marekani juu yake, hivyo maombi ya Ulaya ya kujenga jeshi huru la Ulaya la kuilinda dhidi ya Urusi na Marekani yanaongezeka... Na hasira ya Marekani juu ya hilo iko wazi kama ilivyotokea katika mkutano wa Rais wa Ufaransa Macron na mwenzake wa Marekani Trump mjini Paris mnamo 09/11/2018, na pia kutangazwa kwa vita vya kibiashara ambavyo vilikuwa vikiilenga Ulaya, na mwito wa Marekani wa kuvunja Umoja wa Ulaya hadharani, na mabishano na kutoelewana kati ya Waulaya na Wamarekani katika mikutano ya NATO na mikutano ya kilele ya G7 mwaka huu na mwaka uliopita, na majaribio ya Waulaya kuipinga Marekani katika baadhi ya masuala ikiwemo Ukraine... Yote hayo yanaifanya Marekani kuchochea hali katika mipaka ya Ulaya nchini Ukraine pamoja na Urusi.

8- Urusi iko katika hali ngumu, bali iko katika mkwamo kuhusiana na Ukraine ambayo kwake ni suala la kufa na kupona. Ikiipoteza, itakuwa wazi mbele ya Magharibi na mji mkuu wake Moscow utakuwa hatarini, hasa baada ya kuipoteza Ulaya Mashariki ambayo ilikuwa ni kina chake cha kimkakati cha kujilinda. Magharibi imeihadaa, hasa Marekani, mara kadhaa kwa kuikubalia kuanguka kwa ukuta wa Berlin na kuikabidhi Ujerumani Mashariki kwa Ujerumani Magharibi na kuiachia Poland na kukubali uhuru wake na uhuru wa nchi za Ulaya Mashariki... Na sasa inaihadaa tena nchini Ukraine, kwani baada ya kukubaliana nayo mwaka 2014 kuwa kibaraka wake Yanukovych abaki madarakani, Magharibi iliwachochea Waukraine kumuangusha. Kisha hadaa nchini Syria! Marekani iliihadaa Urusi kwa kuisukuma kupigana badala yake na kwa maslahi yake nchini Syria, hivyo Urusi ikadhani kuwa Marekani itanyamaza kimya juu ya kuunganisha kwake Crimea na udhibiti wake wa mashariki mwa Ukraine bila ya kupata utambuzi wowote wa Marekani katika udhibiti wake wa maeneo haya! Lau Urusi isingekuwa na upumbavu isingeingilia kati nchini Syria na ingeiacha Marekani iingie kwenye vita na kubaki imekwama humo kama ilivyo hali yake nchini Afghanistan...

9- Muhtasari:

a- Viashiria vya matukio vinaonyesha kuwa Marekani haiko mbali na kuwa ndiyo mchochezi nyuma ya kuzisogeza meli za Ukraine kuelekea Bahari ya Azov bila uratibu na Urusi... Na kwamba Marekani inalenga kupitia hilo kuchochea hali ili kuitumia kwa ajili ya maslahi yake dhidi ya vyombo vitatu: Urusi, Ulaya na Ukraine... Marekani inataka "kuchochea hali" na si kutatua tatizo ili libaki likiendelea na mvutano udumu...!

b- Ulimwengu huu maadamu unatawaliwa na nchi hizo za kibeberu za kisekula, utabaki kuwa jukwaa la njama chafu, jinai za kinyama na kuenea kwa dhuluma za kila namna... Kwani dhana za "ukoloni" zimekita mizizi katika nchi hizo na haziziachi popote zinapofika...

c- Hakika mfumo mtukufu wa Kiislamu ndio pekee utakaouokoa ulimwengu kutokana na maovu ya nchi hizo na mifumo yao ya kutungwa na wanadamu, kwa sababu Uislamu umeteremshwa kutoka kwa Muumba wa mwanadamu, na Muumba ndiye pekee anayejua kile ambacho ni kheri kwa viumbe Wake.

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

"Je! Haelewi aliye umba, naye ndiye Mjuzi wa yaliyofichika, Mwenye habari za kila kitu?" (QS. Al-Mulk [67]: 14)

Hii ndiyo haki inayosimamia uadilifu na kueneza kheri.

فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ

"Basi nini kiko baada ya haki isipokuwa upotovu?" (QS. Yunus [10]: 32)

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

"Hakika katika hayo mna mawaidha kwa mwenye moyo au akatega sikio naye akawa anashuhudia." (QS. Qaf [50]: 37)

7 Rabi’ al-Akhar 1440 H 14/12/2018 M

Share Article

Share this article with your network