Alhamdulillah, Swala na Salamu zimshukie Mtume wa Allah, na familia yake, maswahaba zake na waliomfuata, na baada ya hapo.
Nilisimamia matayarisho ya kongamano hili, kuandaa hotuba zake na kusoma mipango yake, hadi tulipofika ukingoni mwa kuanza kwake, Allah Subhaanahu akapenda nisiweze kulifungua kongamano hili kwa neno la sauti au la maandishi “kwa sababu fulani”... kama nilivyozoea kufanya... na Allah amekadiria na alichotaka amekifanya...
Kwa hivyo, kupitia neno hili fupi, ninalipa (qadha) jambo baada ya kuwa halikutekelezwa wakati wake!
Kongamano hili si jambo geni miongoni mwa makongamano yetu ambayo tumeyahutubia kwa Umma wa matabaka yote: watawala na watawaliwa, watu mashuhuri na watu wa kawaida, wanafikra na wanachuoni, na hata masheikh wa masultani! Tukitangaza mbele yao yale yanayowaunganisha baada ya mfarakano, na yanayowapa utukufu baada ya udhalili, na yanayowazindua baada ya usingizi mrefu... tukiwalingania kwenye kadhia mama, Khilafah Rashidah, na tiba yenye mafanikio kwa matatizo yao iliyotelemshwa na Mola wa walimwengu... kukawa na Mwito, na Barua kwa watawala, na kongamano la Khilafah, na kongamano la kiuchumi, na kongamano la wanachuoni, na kongamano la wanawake dawah, kisha likawa kongamano hili la vyombo vya habari...
Naam, si geni miongoni mwa makongamano yale tuliyouhutubia Umma kwayo, lakini lina sifa mbili:
Sifa ya kwanza ni ya kihabari katika wakati ambao habari za kweli zimekuwa adimu... wakati ambao wasema kweli wamekuwa wachache... wakati ambao neno limekuwa biashara, linauzwa na kununuliwa, lengo likiwa ni kuchuma mali, na “kupiga zumari na ngoma” kwa wenye mamlaka na vyeo, hata kama ni kwa gharama ya watu walionyimwa haki na wanaodhulumiwa!
Hii ndiyo sifa ya kwanza ya kongamano hili: limekuja kutangaza neno zito na la kweli katika kutatua masuala ya Umma, bila kuogopa lawama ya mlaumu yeyote katika njia ya Allah... neno la haki ndio silaha yake... silaha kali kuliko upanga mbele ya madhalimu...
Ama sifa yake ya pili ni kuhudhuriwa na watu wa kimataifa, kwani kongamano limekusanya weupe na weusi, wekundu na manjano, wenye lugha za Kiarabu na lugha nyinginezo... rangi zao ni tofauti, na lugha zao kadhalika, lakini wanatamka kwa pamoja, na wanashuhudia kwa pamoja ushuhuda wa haki: La ilaha illa Allah Muhammad Rasulullah... kwayo lugha zao na rangi zao zinaungana, wanapata utukufu kwayo duniani, na wanafaulu kwayo Akhera, wakiwa ndugu kwenye viti vya enzi wakikabiliana...
Hivyo ndivyo ulivyo Uislamu mkuu, ni rehema kwa walimwengu, dawah ya kimataifa, haina nafasi ya ubaguzi wa kikaumu au kizalendo, bali:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ
"Hakika Waumini ni ndugu." (QS. Al-Hujurat [49]: 10)
الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ لا يَظْلِمُهُ وَلا يُسْلِمُه
"Muislamu ni ndugu wa Muislamu, hamdhulumu wala hamuachi aangamie." (Imepokelewa na Al-Bukhari)
Na mwisho, licha ya kila kilichozunguka kongamano hili kutokana na mbinu za madhalimu na wanafiki kwa njama na chuki, na majaribio yao makali ya kuzuia na kukwamisha, lakini lilifanyika kwa neema na fadhila za Allah, na watu wa shari wakarudi na neno na kitendo kibaya... kongamano likafanyika, na hali yake ikiwahutubia madhalimu wenye chuki kwa sauti yenye nguvu na mwangwi:
قُلْ مُوتُوا بِغَيْظِكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ
"Sema: Kufeni kwa hasira yenu! Hakika Allah ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani." (QS. Ali-Imran [3]: 119)
Na mwisho wa yote, matokeo ya kongamano yalikuwa ni kwamba wema na wakweli walituunga mkono na kuwa pamoja nasi, huku madhalimu na wazushi wakituogopa na kusimama dhidi yetu... na kwa kiasi ambacho wa kwanza walitukubali kwa mapenzi na shauku, ndivyo wa mwisho walivyopigana nasi kwa hasira na hofu... lakini mwisho mwema ni wa wachamungu, na sifa njema zote ni za Allah, Mola wa walimwengu.
01-12-2010 M
Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah Amir wa Hizb ut Tahrir